Home Latest News Mrema: Nitapunguza wafungwa

Mrema: Nitapunguza wafungwa

1720
0
SHARE
Augustino Mrema (katikati) akizungumza na Mhariri wa Rai Jimmy Charles (kushoto) na Mwandishi mwandamizi Kulwa Mzee.

NA JIMMY CHARLES,

MOJA ya changamoto kubwa zinazoyakabili Magereza nchini ni mrundikano wa wafungwa na mahabusu.

Kutokana na changamoto hiyo, serikali imekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha inalipunguza ama kulimaza kabisa jambo hilo.

Miongoni mwa mikakati inayofanywa na serikali ni kujenga Magereza na Mahabusu mpya, kutoa adhabu mbadala na wakati mwingine kutoa misamaha kwa wafungwa walionesha kujutia makosa yao na kuwa na utayari wa kujirekebisha.

Utoaji huu wa misamaha kwa wafungwa haufanywi kiholela, badala yako zip[o taratibu stahiki zinazofanikisha suala hilo.

Moja ya taratibu hizo ni uwapo wa Bodi ya Taifa ya Parole, ambayo inajumuisha watu wenye sifa mbalimbali za kitaaluma.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party, Austino Mrema ni miongoni mwa watanzania wachache waliopewa dhamana ya kuiongoza bodi hiyo.

Uteuzi wa Mrema umefanywa na Rais John Pombe Magufuli, baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo Jaji Mstaafu Eusebia Nicholaus Munuo kumaliza muda wake.

Kutokana na umuhimu wa bodi hiyo nchini RAI, liliiona haja ya kufanya mahojiano maalum na Mrema ili kuweka wazi mikakati yake ndani ya wadhifa wake mpya, ambao pamoja na mambo mengine umezua gumzo kutokana na baadhi ya watu kudai kuwa mwanasiasa huyo wa upinzani hakustahili.

Kabla ya kuanza mahojiano hayo, Mrema alionesha kukerwa kwake na madai yanayotolewa na watu wachache kwamba hakustahili na kwamba ni mgonjwa.

“Wapo watu ambao naamini ni wachache, wanasema sikustahili kuteuliwa na kwamba mimi ni mgonjwa, sasa nataka niwaambie mimi nimestahili.

“Nimelitumikia taifa hili kwa muda mrefu nikishika nafasi mbalimbali hadi ya Naibu Waziri Mkuu na hao wanaosema mimi ni mgonjwa, washindwe na walegee, mimi ni mzima niko imara, afya yangu imeimarika sana na ndio maana Rais ameniteua, ningekuwa mgonjwa wala asingeniteua.”

Juu ya kukabiliana na rushwa ndani ya bodi hiyo, Mrema alisema yeye si mtu wa mchezo mchezo na mtu yeyote asithubutu kutaka kumpenyezea rushwa, atamuumbua kwa sababu nia yake ni kusimamia sheria na haki kwa wote wanaostahili.

Mrema alitoa kauli hizo akiwa ndani ya ofisi za wizara ya Ardhi, ambako alilieleza RAI kuwa yupo hapo kwa sababu ya kushughulikia kero za wananchi wake, ambao hakutaka kuwataja ni wa wapi. Sasa fuatilia mahojiano rasmi.

RAI: Watanzania hasa wale waliohukumiwa vifungo vinavyostahili kupata msamaha wa Rais wategemee nini kutoka kwako?

Awali ya yote namshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kuniteua kwenye nafasi hiyo.

Uteuzi wake umeonyesha kwamba yeye ameweka pembeni tofauti za itikadi za vyama vya siasa na kuniteua mimi ingawa sio mwanachama wa CCM, bali ni Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha TLP ambacho kina nia ya siku moja kushika dola.

Namuomba Mhe. Rais aendelee na moyo huo huo kwa kuteua watu wenye uwezo na uzoefu wa kazi husika bila kujali itikadi za vyama kwa sababu nchi hii ni ya watanzania wote.

Kwa kuniteua ametekeleza ahadi yake aliyotoa wakati wa kampeni kwamba yeye atakuwa Rais wa watanzania wote.

Sasa tukija kwenye swali lako, lengo langu ni kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na kuna malalamiko mengi kwamba kuna watu wamefugwa kwa kubambikiziwa kesi, kama vile ujambazi, ubakaji n.k. lengo langu ni kuonana na watu wa aina hiyo kuwasikiliza na kufanya uchunguzi huru na baadae kumshauri Mhe. Rais ikithibitika ni kweli kama wapo magerezani kwa kuonewa, awasamehe kwa sababu yeye anao uwezo huo kikatiba isipokuwa kwa waliohukumiwa na mahakama adhabu ya kifo au kifungo cha maisha.

Unajua Rais wetu ni mtu mwema na mtu wa mungu hapendi watu wake wateseke bila makosa na ndio maana ameniteua mimi niweze kumsaidia kwenye eneo hilo na mimi namuahidi Mhe. Rais pamoja na Watanzania wote kwamba sitawaangusha. Nitatekeleza majukumu yangu kwa juhudi, maarifa, ubunifu na uadilifu wa hali ya juu

RAI: Yapo maneno na minong’ono kwamba Mrema hakustahili kukabidhiwa jukumu hilo kwa sababu ni la kisheria, hili unaliongeleaje?

MREMA: Watu wanaosema hivyo ama hawaelewi au hawakupenda mimi kuteuliwa kushika nafasi hiyo kwa sababu zao binafsi. Nawahakikishia Watanzania kwamba mimi ninazo sifa za kushika nafasi hizo pamoja na sifa za ziada.

Kumbuka kwamba nilikuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi (1990 – 1994) na Naibu waziri Mkuu, enzi zangu uhalifu ulipungua sana, majambazi walisalimisha silaha zao na nilianzisha vituo vidogo vya polisi (police post) nchi nzima.

Pia, nilisaidia mahakama kwa kusikiliza kesi za madai, talaka na mirathi ambazo zilikuwa zimerundikana mahakamani, nyingine zaidi ya miaka 10 bila kutolewa uamuzi.

Kuhusu maneno kwamba sikustahili kupewa nafasi hiyo kwa sababu mimi sio mwanasheria, sheria ya Bodi ya Parole inasema wazi kwamba Mwenyekiti awe mzoefu kwenye mambo ya kisheria au utawala wa masuala ya kijamii.

Mimi kama waziri wa mambo ya ndani mstaafu, ninao uzoefu mkubwa kwenye utawala wa masuala ya kijamii, hivyo natosha kabisa kuvaa viatu hivyo na wala Mhe. Rais hakukosea kuniteua.

RAI: Je, utalazimika kuachia nafasi yako ya Uenyekiti wa chama  cha TLP, ili pengine kuondoa mgongano wa kimaslahi?

MREMA: Hapana, hakuna mgongano wowote wa kimaslahi kwani kazi za chama na kazi za kiserikali haziingiliani. Nitagawa muda kufanya kazi za chama na kufanya kazi za bodi ya Parole. Mbona Kikwete alikuwa Rais na wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM.

Hata Maalimu Seif alikuwa Makamu Mwenyekiti wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF, hoja ya mgongano wa kimaslahi sikuisikia.

RAI: Unatarajia kukabiliana na changamoto zipi kwenye jukumu lako hili jipya?

MREMA: Katika kutekeleza Sheria ya Bodi za Parole changamoto mbalimbali zitakazo jitokeza ambazo ni kikwazo katika utendaji wa shughuli za Parole ni kama ifuatavyo:-

  • Sheria ya Bodi za Parole kuwa na wigo finyu kiasi kwamba haiwanufaishi wafungwa wengi wenye vifungo virefu.  Pamoja na sheria hii kufanyiwa marekebisho kwa Sura 400 ya mwaka 2002 wafungwa wengi wanaotumikia vifungo virefu bado hawapati fursa ya kunufaika kwa kuwa aina ya makosa wanayotumikia yamezuiliwa na sheria hii.
  • Uelewa mdogo kuhusu Parole miongoni mwa jamii (Public awareness).  Ushiriki wa jamii katika kumrekebisha mfungwa ni wa muhimu sana, ili jamii iweze kushiriki vizuri katika jambo hili zinahitajika juhudi za dhati katika kutoa elimu kuhusu Parole. Hasa kwa kuzingatia dhana kwamba uhalifu hufanyika kwenye jamii hivyo na urekebishaji wake ni muhimu ufanyike katika jamii husika.
  • Wafungwa waliopo chini ya utaratibu wa Parole kukosa mitaji ya kuendesha shughuli zao za ujasiriamali pamoja na ugumu wa kupata ajira.  Mara nyingi wafungwa wanapotoka magerezani baada ya kukaa kwa muda mrefu hukuta familia zao zimetawanyika na hata mali zao kutapanywa ovyo, hivyo huhitaji msaada wa kuwezeshwa kuanza maisha upya.
  • Mtizamo hasi wa jamii kuhusu mfungwa. Jamii inashindwa kutambua kwamba, mfungwa anapokuwa gerezani anapitia program mbalimbali za urekebishaji na hivyo anakuwa amerekebika. Badala yake, humnyanyapaa na kumnyooshea vidole na hata kushindwa kumpa ushirikiano ipasavyo.

RAI: Umekuwa waziri wa mambo ya ndani mwenye mafanikio, unadhani nini kinakosekana kwa mawaziri wa wizara hiyo sasa, hasa ukizingatia ndani ya muda mfupi imeshakuwa na mabadiliko kadhaa ya uongozi?

MREMA: Kwa kweli wizara ile ni ngumu ni tofauti na wizara nyingine. Wizara ya mambo ya ndani ya nchi ndio wizara mama, ndiyo inayo simamia amani na utulivu wa nchi nzima. Kumbuka bila ya amani na utulivu hakuna chochote kitakachoweza kufanyika

Hivyo inahitaji waziri mchapa kazi bila kuchoka au kujali muda wa kufanya kazi, pili inahitajika kuongozwa na mtu mwenye hekima na busara ya hali ya juu na vile vile anahitajika mtu mbunifu ili amsaidie Rais kupambana na changamoto mbalimbali zinazokabili taifa.

Hao wanaopelekwa pale na kuondolewa baada ya muda mfupi, ni kwa sababu wamekosa baadhi ya sifa hizo. Nasikia kuna mmoja aliondolewa kutokana na ulevi.

RAI: Unaushauri gani kwa Waziri Mwigulu Nchemba katika kuongoza wizara hiyo, ambayo wakati wa uongozi wako uliifanya kuwa kimbilio la wengi hasa kwa upande wa polisi?

MREMA: Namshauri Mhe. Nchemba awe mfuatiliaji wa mambo kama nilivyokuwa mimi asikae tu ofisini na kusubiri kuletewa taarifa wakati mwingine taarifa zinakuwa za uongo. Pia awe mbunifu kama mimi nilivyokuwa, nilianzisha mpango wa ‘TAJIRIKA NA MREMA’ chini ya mpango huo kila askari polisi aliyekamata rushwa na kusalimisha fedha hizo chafu serikalini, alipewa fedha halali za thamani hiyo hiyo na akikamata mali za magendo anapewa asilimia 10 zinazolingana na thamani ya mali aliyokamata. Hivyo ilisaidia askari polisi kupata ari na motisha wa kufanya kazi. Nilihakikisha wanaofanya kazi vizuri wanapata ‘promotion’ hapo hapo bila kusubiri kwenda mafunzo.

Pia, polisi walio kamata silaha walizawadiwa shilingi 50,000 za wakati huo, fedha ambazo zilisaidia kuinua hali ya maisha kwa polisi na wengine waliweza kumudu na kujenga nyumba za kuishi na kupeleka watoto wao mashuleni.

RAI: Umekuwa ukitajwa kama kinara wa kweli wa upinzani nchini ambaye sasa unadaiwa kuwasaliti wenzako na  kujiegemeza na CCM hilo nalo unalisemaje?

MREMA: Sio kweli, hao wanaosema hivyo ndio wasaliti wa upinzani. Kwa mfano, mimi nilikuwa mbunge wa Vunjo watu wa NCCR Mageuzi badala ya kupeleka nguvu kwenye majimbo mengine yanayokaliwa na CCM na kwenda kulinda majimbo yao manne waliyokuwa nayo Kigoma, wakaelekeza nguvu zao zote kwangu mimi mpinzani mwenzao na kuning’oa, wakaacha majimbo yao yote manne ya mkoa wa Kigoma yakachukuliwa na CCM. Sasa nani msaliti wa upinzani kati ya TLP na NCCR?

Vile vile watanzania tuelewa kwamba maana ya upinzani sio kupinga au kususia kila kitu hata kile chenye maslahi kwa taifa. Kwa mfano, haikuwa sahihi kususia hotuba ya Rais Magufuli alipokuwa akifungua bunge la sasa na vile vile haikuwa sahihi kwa watu wa UKAWA kususia Bunge la bajeti maana wamekosa kuwakilisha mawazo ya wapiga kura wao, hivyo madhara ni makubwa kuliko faida. Kwa hiyo upinzani wa aina hiyo siukubali wala siwezi kuunga mkono.

RAI: Unazungumziaje siasa za nchi hii kwa ujumla hasa katika kipindi hiki ambacho serikali imepiga marufuku mikutano ya hadhara?

MREMA: Kwa hilo wa kulaumiwa ni Ukawa kwa sababu Bunge la bajeti wakati linaendelea wao waliamua kususia wenyewe na wakataka kwenda mitaani kufanya mikutano na maandamano kuelezea mambo yale yale walipaswa kuyasema bungeni. Sasa tujiulize nini maana ya kuwa na Bunge?

Je, kila hoja itapelekwa kwenye mikutano ya hadhara, Bunge litafanya kazi gani? Na hao wabunge wa Ukawa walichaguliwe kufanya kazi gani? Na kama hawataki kukaa bungeni na kutoa hoja ni kwa nini waligombea ubunge?

Hakuna demokrasia isiyokuwa na mipaka, hivyo ni vizuri sheria ya maandamano na mikutano ikawekewa kanuni zake ‘Guidelines’ kwamba ni wakati gani wa kufanya mambo hayo na wakati gani haifai kufanya mambo hayo. Kama tukifanya maandamano na mikutano ya hadhara isiyokwisha kwa kipindi cha miaka mitano wananchi watafanya kazi muda gani?

Demokrasia bila mipaka ni vigumu ‘uncontrolled democracy is Ruinous’ tujiulize nchi gani iliyopata maendeleo kupitia mikutano ya hadhara na maandamano yasiyokwisha kila kukicha? Nchi yetu ni miongoni mwa nchi maskini duniani, hivyo tunahitaji muda mrefu wa kufanya kazi kufikia uchumi wa kati.

Sipingi maandamano na mikutano ya hadhara, lakini iwe na mipaka na itungiwe kanuni ‘Guidelines’ sio kufanya mikutano na maandamano kila kukicha kama wenzetu wa Ukawa kama wanavyotaka, eti kwa sababu tu sheria inaruhusu huko sio kujenga bali ni kubomoa nchi.