Home Makala MRUDISHENI AZORY, IMETOSHA

MRUDISHENI AZORY, IMETOSHA

768
0
SHARE

NA JIMMY CHARLES

NI zaidi ya miezi miwili sasa, haijulikani roho na mwili vya mwandishi wa habari Azory Gwanda viko wapi.

Haijulikani kama yuko hai ama amekufa, haijulikani kama huko aliko kama anafurahia maisha ama anasulubiwa na kuteswa kutwa kucha.

Kama amekufa hata mabaki ya mwili wake hayajulikani yaliko, kama yuko hai hata sauti yake haipai angani kuomba msaada.

Azory hajaonekana machoni pa jamii yake kwa siku 66 hadi kufikia leo, wengi tunajiaminisha na kuaminishana kwa kutumia lugha nyepesi na laini kuwa eti, amepotea!

Amepoteaje kiumbe huyu mwenye akili timamu aliyekuwa anaongoza familia yake yenye mke na watoto timamu na madhubuti!

Katika masimulizi na maelezo yanayotolewa dhidi ya Azory sikuwahi kusikia kama ana uhaba wa akili kichwani mwake. Sikusikia ama hata kuambiwa.

Azory ni timamu, ni timamu wa akili na mwili, kama hiyo haitoshi Azory ni mtu anayejulikana kwenye eneo analoishi, si mtu wa kutopata msaada hata kama amepandwa na uchizi ama wendawazimu wa ghafla utatakaomsukuma kupotea nyumbani kwake.

Ukweli huo unathibitisha dhahiri kuwa kamwe hawezi kushindwa kuijua njia ya nyumbani kwake, hawezi kupotea kwa siku 60 bila ya kupata msaada uwe wa ndugu, jamaa, rafiki na hata majirani zake.

Taarifa rasmi za kupotea kwa Azory zilianza kuibuka mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, wakati huo tayari alikuwa hajulikani alipo kwa siku.

Mazingira ya kupotea kwake yananasibishwa na kufuatwa kwake na watu wasiojulikana katika maeneo yake ya kazi.

Watu hao walimchukua haielezwi kuwa ni kwa lazima ama kwa hiyari na kwenda nae nyumbani kwake.

Ilielezwa kuwa kwa akili ya haraka Azory alikwenda alikokuwa mkewe (shambani) bila shaka lengo lilikuwa ni kutaka kumuonesha  kuwa yuko na watu ambao huenda hata yeye hakuwa akiwafahamu.

Bila shaka haikuwa rahisi kumweleza mwenzi wake kuwa siko kwenye mikono salama, badala yake wasimualiaji wanasema alimwomba mkewe ufunguo wa nyumbani kwao.

Mke wake Anna Pinoni, alilithibitisha hili kwa kusema kuwa Novemba 21, mwaka jana asubuhi watu waliokadiriwa kuwa ni wanne wakiwa ndani ya gari aina ya Toyata Land Cruiser nyeupe walifika katikati ya mji wa Kibiti sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara na kumchukua.

Kwa maelezo ya Pinoni alibainisha kuwa baada ya watu hao kumchukua Azory, gari lilielekea shambani kwake wakati huo ikiwa inapata saa nne asubuhi.

Azory na watu wake hao walimkuta mkewe shambani hapo wakati huo akiwa amekaa kistaarabu kabisa kwenye kiti cha nyuma.

Haraka alimuita mkewe akiwa ndani ya hilo gari na kumuulizia kuhusu alipoiweka funguo ya nyumbani kwao.

Mkewe bila hofu alilisogelea gari hilo na kuzungumza na mumewe kutokea dirishani na kumweleza alipokuwa ameweka ufunguo huo uliokuwa ukiuliziwa na Azory.

Azory alimwambia mkewe kuwa amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo basi angerejea siku inayofuata kwa maana ya Novemba 22, mwaka jana.

Inadaiwa gari iliondoka shambani hapo kinyume nyume hadi njia panda na kuelekea nyumbani kwa Azory, kilichofanyika huko anakijua mwandishi huyo na watu aliokuwa nao.

Hata hivyo, mkewe alisema aliporudi nyumbani kwake aligundua kufanyika kwa upekuzi ndani ya nyumba yao kwani vitu vyake vilikuwa shaghalabhaghala.

Tangu siku hiyo ya Novemba 21, mwaka jana hadi leo Azory haijulikani yuko wapi kwani hata simu zake hazipatikani.

Kupotea kwa Azory ni mwendelezo wa matukio ya hovyo ya kupotea kwa baadhi ya watu akiwemo Ben Saanane.

Kama ilivyo kwa Ben ndivyo ilivyo kwa Azory,  kila mmoja kwa nafasi yake ameacha simanzi na majonzi kwa familia zao.

Ni ukweli usiopingika familia ya mwandishi huyo inakosa furaha na amani kwenye mioyo yao, haijui nini kimemfika mwenzi wao.

Hali kama hiyo bila shaka inawakumba pia wanahabari, maana hawajui ni nani anafuata baada ya Azory, ingawa kiza na msitu wa kusahau umeanza kuitawala mioyo yetu.

Hata hivyo, hili la Azory si la kulisahau hata kidogo, ni suala gumu linalopaswa kukumbukwa kila uchwao.

Binafsi yangu nafarijika na hatua ya kampuni ya MCL, hakika wao wameamua na kudhamiria kupaza sauti ya haki.

Ni wakati mwafaka kwa vyombo vyote vya habari kuendelea kushirikiana na MCL ili kuongeza kasi ya kupaza sauti itakayosaidia kufikisha tamati suala hili.

Kitendo cha kukaribisha roho wa kusahau kwenye suala hili, kunadhihirisha kuwapa uhalali wahusika waliopandwa na roho za kifedhuli na kuamua kuudhulumu uhuru wa Azory kwa sababu ambazo hazijapata kuwekwa wazi.

Kama ilivyofanyika awali, ndivyo iendelee kufanyika sasa katika kuvitumia vyombo vya habari kumsemea Azory, kuwacha MCL peke yake ni kubariki utengano hasa kwenye masuala ya msingi kama haya, ambayo yanahitaji sauti ya wengi.

Ukweli ni kwamba awali wengi tulilia na kupaza sauti za uchungu juu ya tukio hili, lakini ghafla tumesahau, hatukumbuki tena, hatusemi tena, hatushirikiani tena kwenye hili.

Kwa kushirikiana na vyombo vya dola upo uwezekano mkubwa wa vyombo vya habari kusaidia kutatua suala hili kwa haraka.

Kwakuwa dhamira ni kutaka kurejeshwa kwa Azory upo uwezekano wa kusimama pamoja na kupaza sauti zitakazochochea kupata majibu sahihi ya suala hili.

Amepotea  Ben Sanane, sidhani kama kuna majibu sahihi yameshawahi kupatikana. Majibu hakuna na  jamii inaonekana kusahau.

Ni vema wanahabari tukatambua kuwa lililomfika Azory linaweza kumfika yoyote yule bila kujali yuko wapi na anafanya nini.

Pigo alilopigwa Azory halimaanishi ndio mwisho wa mapigo kwa wanahabari na wanataaluma wengine.

Kama ni kusema, kulia ama kupiga kelele ni sasa. Tunapaswa kulia na kusema pamoja, hakuna wakati mwingine utakaofaa kusimama imara katika kuupigania uhai wa mwanataaluma mwenzetu.

Hadi leo sababu za Azory kutoweshwa katika mazingira tatanishi hazijulikani na hakuna wa kuzisema kwa sababu anaepaswa kusema hajulikani alipo.

Si wakati sahihi kwa vyombo vya habari kudhani suala hili ni la upande mmoja, ni muda sahihi kwa vyama vyote vya kitaaluma, vyombo vya habari na wanahabari kusimama pamoja.

Kama tunaweza kusimama pamoja katika kumhudumia mwanahabari mwenzetu aliyekumbwa na ugonjwa ama kushiriki kikamilifu katika misiba ya wanataaluma wenzetu, iweje tushindwe leo kutumia kalamu zetu kumsemea Azory.

Ifike mahali kwa pamoja  tuombe kurejeshwa kwa Azory kwani imetosha, miezi miwili ni mingi sana.

Mungu Ibariki Tanzania.