Home Makala  Lini maisha yalikuwa laini kwa mvivu!

 Lini maisha yalikuwa laini kwa mvivu!

1478
0
SHARE

NA JIMMY CHARLES

MOJA ya neno lililotawala vijiwe vingi nje na ndani ya mitandao ya kijamii kwa sasa ni ‘maisha magumu’!

“Sasa hivi maisha magumu, serikali mpya imefungia hela”. Hayo ni baadhi ya maneno yanayokazia mjadala huo wa maisha magumu.

Fikra zinazozunguka kichwa changu na kuibua maswali lukuki ni je, lini maisha yalipata kuwa laini kwa mtu mvivu kwenye kutegemea mapato ya ujanjaujanja!!!

Ukifanya uchunguzi mdogo juu ya watoa hoja ya maisha magumu, utabaini mambo makuu mawili  yanayowalazimisha kuyasema hayo.

Mosi. Wengi wao walikuwa ombaomba wanaojipatia fedha bila jasho, tegemezi wenye kuishi mjini kwa kulelewa au wala rushwa kubwa na ndogo, wakwepa kodi ambao walikuwa wakipata zaidi kwenye kila walichokifanya,  kwa maneno mengine ni kwamba ilikuwa jamii ndogo iliyojijengea uhalali wa kupata fedha bila jasho.

Kundi hili lilikuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi isivyo halali, haikuwa tabu kwao kugawa fedha kwa kila aliyewasifia,  walifaidi jasho la wengi, walikuwa na kiburi cha kuponda raha bila mipaka.

Ilikuwa ni jambo la kawaida kwao, kuteketeza kiasi kikubwa cha fedha kwa wakati mmoja ili kutengeneza mazingira ya kupata kikubwa zaidi baadae. Yote haya yaliwezekana bila tatizo.

Pili. Ni kundi linalolalamikia maisha magumu kwa mkumbo, hawa hawana sababu wala hoja  za msingi za malalamiko hayo, wanalalamika kwa sababu kundi la kwanza linalalamika, lakini kwa uhakika hawajaathirika kwa lolote.

Bahati iliyo njema kwa sasa mianya ya ulaji wa jasho la wengi imezibwa, hali inayosababisha malalamiko kwa wale waliokuwa wakilila, huku furaha ikiendelea kutawala kwa wale waliokuwa wakitengeneza mapato yao kihalali.

Inafikirisha kwa mvivu kulalamikia ugumu wa maisha, inashangaza na kustaajabisha. Ni suala lisilowezekana kwa binadamu yeyote duniani kufurahia maisha bila ya kufanya shughuli halali za kujiingizia kipato.

Matajiri wote duniani, pamoja na mambo mengine wanabaki kuwa wachakarikaji wanaojituma na kuhangaika huku na kule.

Kwa sasa fedha za kupeana bila kuvuja jasho hazipo, Rais Dk. John Magufuli amebana mirija ya fedha chafu, dhamira yake ni  kumlisha keki ya Taifa kila raia.

Nia yake ni kuona Mtanzania fukara ambaye hakuwa na thamani mbele ya mabwanyenye anapata kile alichokikosa kwa miaka mingi.

Ameamua kuelekeza nguvu zake zote kwenye huduma za jamii kwa kuhakikisha fedha zote zilizokuwa zikinufaisha wachache zinaelekezwa kwenye matumizi sahihi.

Anafanya hivyo kwa sababu hana deni na mtu, haogopi mtu, hana shuruti kutoka kwa yeyote, urais wake hauna ubia kwa sababu si wa kutafuta kwa mamilioni ya fedha za mafisadi na wahujumu uchumi.

Nafasi aliyonayo ameipata kwa juhudi na bidii zake za kiutendaji kabla na hata baada ya kuingia serikalini, hivyo hana cha kupoteza.

Pamoja na kuwapo kwa kauli kuwa urais wake ni wa bahati, kamwe hataabishwi na hilo, halimsumbui kichwa badala yake unamuongezea hasira ya kutimiza ahadi zake kwa Watanzania wote, bila kujali rangi, kabila, dini na itikadi.

Hali hiyo inampa uwezo wa kuusema ukweli bila haya, anakosoa bila woga, anakataa bila hiyana na anatambua kwa sababu maalum.

Rais anaamini katika kufanya kazi ili kupata pato la halali, haamini katika kubweteka ili upewe na ndio maana hauoni ugumu wa  kuwaeleza watu kufanya kazi kwa bidii ili kuondokana na dhana ya serikali kuwafanyia kila jambo.

Anaamini katika hilo kwa sababu Serikali haiwezi kumpa fedha kila mtu kwa sababu  yapo mambo ya muhimu yanayopaswa kufanywa na serikali kwa manufaa ya wengi.

Ukweli huo wa serikali kufanya jambo kwa maslahi ya wengi unapambwa na uamuzi wake wa kuhalalisha elimu bure kwa wanafunzi wote waliopo shule za msingi na Sekondari.

Bila shaka dhamira yake ni kuhakikisha anapambana na maadui hawa kwa vitendo, kwasababu Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu, Julius Kambarage Nyerere alishasema nchi yetu inakabiliwa na maadui watatu; ujinga, maradhi na umasikini.

Pamoja na kuwatambua maadui hao, bado tumeendelea kuwachekea kwa miaka dahari hali inayotufanya kuwa taifa la walalamikaji miaka nenda miaka rudi, jambo hili bila shaka  halimfurahishi Rais Magufuli.

Kutokufurahishwa na hili kunaonekana wazi kwenye kauli na matendo yake, mara zote amekuwa akihubiri taifa kuondokana na kuombaomba.

Njia pekee ya kutufikisha huko si kulalamikia ugumu wa maisha, bali ni kufanya kazi kwa bidii kwenye kila eneo.

Bila shaka unapopambana na umasiniki kwa vitendo si rahisi kupata muda wa kulalamikia ugumu wa maisha, si rahisi kufikiria kupewa kitu usichokivujia jasho.

Taifa linapokuwa na wachapa kazi  wa kutosha ni rahisi kuondoka kwenye kauli mbiu za ovyo za ‘Maisha magumu’.

Haitatokea hata siku moja maisha kuwa laini kwa mtu mvivu asiyependa kujituma, mwenye kutaka bure kila uchwao.

Fursa za kupata fedha halali ni nyingi zisizo na vikwazo wala masharti ya kibeberu. Tufanye kazi kwa maslahi yetu na maslahi ya Taifa, hakuna maisha laini kwa mvivu.

Mungu Ibariki Tanzania.