Home Makala Msajili, CAG mmemsikia JPM?

Msajili, CAG mmemsikia JPM?

1356
0
SHARE

 

WAKATI Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akijitokeza na kutetea hotuba ya Rais John Magufuli, akisema alinukuliwa vibaya pindi alipokuwa akizuia wanasiasa kufanya mikutano, maandamano na makongamano sasa Rais ameibuka na kupigilia msumali wa katazo hilo alilosema mwanzo.

Rais Magufuli ameweka wazi kuhusu kauli yake ya kuzuia wanasiasa kutofanya siasa hadi mwaka 2020, kauli hiyo ameitoa kabla Watanzania hawajasahau utetezi uliotolewa na Jaji Mutungi ambaye alisema wananchi waliitafsiri kimakosa kauli ya kwanza ya Rais Magufuli ya katazo la kufanya siasa hadi muda alioupanga kiongozi huyo.

Jaji Mutungi akiwa mlezi wa vyama vyote vya siasa ameushangaza umma kuibuka na kujivika joho la utetezi wa rais.

Katika kauli yake Jaji huyo anayeheshimika alisema Rais Magufuli hakuzuia wanasiasa kufanya siasa badala yake alichokuwa akitaka ni ushirikiano kutoka kwa wanasiasa hao kwa nia ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Jaji Mutungi aligeuka mfafanuzi wa kauli iliyokuwa wazi ya kuwataka wanasiasa kuacha siasa hizo alizoziita za ovyo hadi mwaka 2020 utakapofanyika uchaguzi mkuu mwingine, ili muda uliopo utumike kuijenga nchi.

Akaendelea kumtetea kiongozi huyo wa nchi, kwamba hapingi siasa isipokuwa anapingana na wanasiasa aliowaita pingamizi katika kuleta maendeleo na muda wote wamejikita katika siasa bila kuangalia namna ya kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Hivi karibuni katika uwanja wa Biafra wakati akifungua mpango wa usalama mkoa wa Kinondoni, Rais Magufuli ameonyesha wazi kwamba mtu ambaye hakumuelewa katika tamko lake la kutaka wanasiasa kuacha kufanya siasa hadi mwaka 2020, alikuwa Jaji Mutungi.

Hakumuelewa kwamba Rais Magufuli amezuia hilo kwa hoja nyepesi za kusema kwamba kufanya kwao siasa kutamfanya ashindwe kutimiza ahadi zake katika miaka mitano aliyoomba ridhaa ya kuongoza.

Rais akatoa amri kwa askari kuhakikisha wanawadhibiti wanasiasa wote watakaofanya siasa katika kipindi hiki akiamini kufanya kwao siasa kutamchelewesha kutekeleza ahadi zake.

Dk. Magufuli kafanya hivyo kwa sababu anaamini msajili hana ubavu wa kumnyooshea kidole kwa uamuzi wake wa kwenda kinyume na Kanuni za Maadili ya vyama vya Siasa Mwaka 2007, zilizotungwa chini ya fungu la 22(h) la sheria ya vyama vya siasa (Sura ya 258).

Huenda kwa kuogopa kwake kutumbuliwa Jija Mutungi ameshindwa kabisa kusimamia haki za vyama vya siasa kwa kutumia kanuni ya namba 4(1) (a)-(e) iyosema “Kila chama cha siasa kitakuwa na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa”.

Anajua hana ubavu wa kusimamia kanuni namba 5 (1) (c) inayozungumzia wajibu wa vyama vya siasa kutotumia dola kwa kujinufaisha kisiasa “Kila chama cha siasa kitakuwa na wajibu wa kutunza maadili chini ya kanuni hizi kwa kutotumia vyombo vya dola kukandamiza na kutoa vitisho kwa chama cha siasa kingine kwa manufaa yake”.

Kwa namna ambavyo Magufuli amewajengea woga watendaji wake hali hiyo imekuwa sababu ya msajili kushindwa kusimamia Kanuni ya 5(1)(i).

Kanuni hiyo inasema “Kila chama cha siasa kitakuwa na wajibu wa kutunza maadili chini ya kanuni hizi kwa kuepuka kutumia mamlaka, rasilimali za Serikali, vyombo vya dola au wadhifa wa kiserikali, kisiasa au ufadhili wa nje ama wa ndani kwa namna yoyote ile ili kukandamiza chama kingine”.

Inashangaza kuona msajili anaacha kusimamia wajibu wake kanuni ya 6(1)(a) ya kusimamia maadili ya vyama vya siasa.

Ukitazama nyongeza ya kanuni ya 6(1) (c ), inamuhitaji kuzuia kitendo cha uvunjifu wa kanuni za maadili kisiendelee na kukitaka chama au kumtaka kiongozi wa chama kujirekebisha.

Sasa nimeshangazwa na msajili kushindwa kusimamia kanuni ya 6(1) (d) kwa kushindwa kutoa onyo la maandishi kwa chama au kiongozi wa chama husika.

Nikiachana na upungufu huo uliofanywa na msajili wa vyama vya siasa, mwingine anayestahili kulaumiwa kwa uvunjaji wa haki za kidemokrasia unaofanywa na Dk. Magufuli ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.

Mtendaji mwingine mwenye  dhamana ya kuisaidia serikali katika masuala ya kisheria ni Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG), lakini hadi leo amekuwa kimya akimuacha rais akiteleza katika kauli zake za kuvunja sheria na demokrasia.

Binafsi simlaumu Dk. Magufuli kwa sababu hana utaalamu wa sheria ila lawama nazipeleka kwa AG, kwa sababu ndiye anayestahili kuishauri serikali na Ikulu katika masuala ya kisheria.

Kama rais anaendelea kuvunja sheria na AG anaendelea kukaa kimya sasa atakuwa na faida gani? Kwanini anakula mshahara huku anashindwa kusimamia kazi anayostahili kufanya ya kutoa ushauri wa kisheria kwa Rais na serikali?