Home kitaifa MSEKWA: Magufuli hamwonei mtu

MSEKWA: Magufuli hamwonei mtu

1939
0
SHARE

msekwaGABRIEL MUSHI NA SHABAN MATUTU

ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Pius Msekwa amesema Rais John Magufuli hamwonei mtu katika hatua anazochukua dhidi ya watumishi wabadhirifu na wazembe serikalini.

Msekwa ambaye pia alikuwa Spika wa Bunge kuanzia mwaka 1994 hadi 2005, alisema mtindo anaotumia Rais Magufuli katika kutekeleza majukumu yake, haudhalilishi mfumo wa uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Katika mahojiano maalumu yalifanyika hivi karibuni nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam, Msekwa anazungumzia mambo mbalimbali yakiwamo mwenendo wa Bunge.

RAI: Unazungumziaje uongozi wa Rais John Magufuli katika kipindi kifupi alichokaa madarakani?

MSEKWA: Ningependa kusema kwamba tofauti ya uongozi wa Rais Magufuli na wengine ni namna anavyoshughulikia majukumu yake, yaani style (mtindo) ya uongozi, usimamizi wake wa mambo, ukaribu wake na utekelezaji wa ahadi alizozitoa. Kwa jumla ufuatiliaji wa mambo yeye mwenyewe hiyo ndiyo tofauti yake na wenzake, kwa sababu hajatunga sheria yoyote mpya, anatekeleza zilezile. Hivyo tutambue kuwa uongozi ni usimamizi, ametuonyesha njia ya jinsi kiongozi anavyopaswa kuwa.

RAI: Katika kipindi kifupi alichokaa madarakani pia amekuwa akiwasimamisha kazi watumishi wabadhirifu kwa mtindo maarufu wa kutumbua majipu unadhani ni hatua sahihi anazochukua?

MSEKWA: Anakidhi mategemeo ya waliomchagua, kwani kiongozi sahihi ni yule anayefuata miiko ya uongozi wa sheria, anatumbua majipu hamuonei mtu, kwani mwenyewe mamlaka ya kuteua ndiye mwenye mamlaka ya kutengua, ametoa mfano mzuri wa uongozi wa sheria na jinsi watu wanavyozungumzia uongozi wake, hayo ndiyo maoni ya wananchi

RAI: Huoni kuwa kitendo cha kuwatumbua majipu wateule wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ni sawa na kuuvua nguo utawala wa Serikali ya awamu ya nne?

MSEKWA: Rais ni rais, anatengua uteuzi wake, au wa rais, kwa sababu urais ni taasisi si mtu, ingawa waliteuliwa na rais mwingine, alitumia mamlaka ya rais na huyu Magufuli anatumia mamlaka ya rais, suala la kumvua nguo Kikwete hayo ni maoni yenye nia mbaya na waliomtangulia, tutazame rais kama taasisi.

RAI: Pamoja na hayo baadhi ya wananchi wanautafsiri uamuzi wake wa kutumbua majipu kuwa unaweza kuleta utata kwani watumishi wanasimamishwa ndipo uchunguzi ufanyike, huoni kuwa hiyo si njia sahihi ya utawala bora?

MSEKWA: Mtindo huo ni mzuri, hakuna haja ya kulea uovu, kwa kuwa tayari mtu ameshatuhumiwa anatakiwa kusimamishwa ndipo uchunguzi ufanyike, hivyo ndivyo sheria zetu zinavyosema, hivyo watambue kuwa kusimamisha mtumishi ili uchunguzi ufanyike ni utekelezaji wa sheria, kama uchunguzi ukionesha hana kosa atarudishwa.

RAI: Rais Magufuli alipoingia madarakani alitangaza kusitisha safari zote za nje kwa watumishi wa Serikali isipokuwa kwa kibali maalumu, na yeye hajasafiri mpaka sasa, unadhani uamuzi huo ulikuwa na tija kwa Taifa?

MSEKWA: Kwanza tutambue kuwa si kwamba Rais hatatoka, tumempa kipindi cha miaka mitano, si lazima atoke kwa kipindi cha miezi mitatu, lazima aunde serikali yake aipe mwelekeo ndipo aangalie mahusiano na nchi nyingine, kwa sababu tumemchagua atutumikie sisi, si kwamba hatakwenda hapana, ni kipaumbele kwamba anaanza na nini.

RAI: Unawazungumziaje baadhi ya wanasiasa walioukosoa uamuzi wake huo kama vile Bernard Membe?

MSEKWA: Inapaswa kufahamu kwamba huo ni mtindo wake wa uongozi, kuchaguliwa leo kesho ukatoka ni style (mtindo) yako, huyu anastyle yake tofauti, lazima Membe akubali hii tofauti si kama ile aliyoizoea, ndani ya miaka mitano anapanga majukumu yake kwa kutoa kipambuele kwa kitu fulani.

RAI: Katika kipindi chake cha kampeni, Rais Magufuli aliahidi kuunda serikali ndogo, baada ya uteuzi wa Baraza la Mawaziri pamoja na makatibu wakuu, wapo baadhi ya wachambuzi wanaombeza kwa kuunda serikali kubwa, unadhani wapo sahihi?

MSEKWA: Haya ni mambo ya Katiba, serikali maana yake mawaziri, si makatibu wakuu au wakurugenzi, hivyo aliposema anaunda serikali ndogo maana yake ni mawaziri. Kifungu cha katiba kinaeleza baraza la mawaziri, Magufuli anatekeleza Katiba si maneno ya watu, serikali ni mawaziri watasaidiwa na idadi yoyote ya wasaidizi wao.

RAI: Kuna tofauti gani kati ya Bunge la sasa na lile la kipindi ulipokuwa Spika wa Bunge?

MSEKWA: Ni uelewa tu hasa mambo ya kikatiba, sheria zinafundishwa chuo kikuu hivyo si wengi waliofika huko. Niseme tu hakuna tofauti ya Bunge hili na lile lililotangulia, kwa maana majukumu ya Bunge, wakati wangu na hata baada yangu, wanapitisha sheria, bajeti hayo ni majukumu ya kikatiba kifungu cha 63, hayo hayajabadilika.

Tofauti iliyopo ni style (mtindo) tu namna wanavyotekeleza majukumu yao. Lakini pia kila zama na kitabu chake, hivyo kizazi hiki kimeleta wabunge machachari, wanabishana na spika, kinyume cha kanuni, kanuni ni zilezile, wakati wangu walitii sasa hawatii hivyo kila zama na kitabu chake.

RAI: Katika vikao vya Bunge hivi karibuni kulizuka vurugu ambazo vililazimu askari kuwatoa baadhi ya wabunge wa upinzani bungeni, unafikiri hatua ya kuwaingiza askari bungeni ilikuwa sahihi?

MSEKWA: Ni sahihi kuingiza askari kuwatoa wabunge bungeni, hata Afrika Kusini kanuni zinaruhusiwa, popote ulipo ukivunja sheria vyombo vya dola vinakushughulikia, ikumbukwe kuwa askari polisi hawavamii kuingia bungeni wanaitwa na Spika, kawaida hawaitwi kuingia kwenye Bunge, hapana anasitisha shughuli ndipo anawaita. Hapo askari wanaalikwa kuingia, baada ya kusitisha Bunge na kuacha kuwa Bunge.

Kitendo cha kuwatoa wabunge wasiotii amri ya spika, kila Bunge linafanya hivyo, mimi sikufanya hivyo kwa sababu haikutokea.

RAI: Je, CCM iko imara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliosheheni ushindani?

MSEKWA: CCM iko imara sana, watu wanasema CCM hii imebadilika, nisema haijabadilika chochote, nyie mnaokimbia ndio mmebadilika,

RAI: Wapo wanaosema uchaguzi huu umeleta mpasuko ndani ya chama, unazungumziaje hilo?

MSEKWA: Uchaguzi haukuleta mpasuko, umeboresha demokrasia, kwa mtazamo hasi wanasema imepasuka, ila mtazamo chanya ni kwamba uchaguzi uliopita umeimarisha demokrasia na umedhihirisha nguvu ya CCM. Kwa sababu demokrasia ni ushindani na unanoga pale timu zinazoshindana nguvu zinapokaribia kuwa sawa, kwa mfano kwa ngazi ya Rais timu za ushindani yaani Magufuli na Lowassa ilionekana kana kwamba nguvu zinakuwa sawa, lakini pili kwa CCM kushinda katika hali ile CCM imedhihirisha nguvu yake. Kuanzia ubunge hadi urais. Ni safi kabisa, kwa sababu ushindi wa asilimia 58 siku hizi hakuna anaezidi 70.

RAI: Kwa kuwa hadi sasa Rais mstaafu hajamuachia uenyekiti wa CCM Rais Magufuli, unafikiri anakiuka utaratibu wa chama?

MSEKWA: Rais mstaafu Kikwete ameshatangaza kuwa mwaka huu atamwachia Rais Magufuli, hawezi kukiuka, ni utamaduni wetu, ndani ya mwaka mmoja tangu Mkapa, Mwinyi.

RAI: Kwa ushindani uliojitokeza mwaka jana, unafikiri CCM itaweza kufanya maajabu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020?

MSEKWA: Hatutaki maajabu, lakini tunataka serikali ya CCM iwatumikie wananchi waridhike kuwa inafaa kupewa madaraka tena. Ndiyo maana Nape (Katibu wa Itikadi na Uenezi), aliposema CCM itashinda hata kwa goli la mkono nikamkosoa kuwa CCM ni chama kikongwe kitashinda kwa uhalali, alipotosha umma.

RAI: Kwa tathmini za kiuchaguzi huoni kuwa CCM inazidi kuporomoka na ni dalili mbaya kuelekea 2020?

MSEKWA: CCM inapanda na kuporomoka, Mkapa kwa mara ya kwanza alishinda asilimia 61 na mara ya pili alishinda wa asilimia 71, Kikwete kwa mara ya kwanza alishinda kwa asilimia 82 na 2010 akashuka kwa mazingira yaliyokuwapo.

Magufuli ameshuka kidogo na kupata asilimia 58, huyu ni mtu tofauti, 2020 Magufuli kwa kasi anayoenda nayo tutaona, hapana haja ya kupiga ramli, mambo anayofanya anafanya ndani ya Serikali, hatupo kwenye chama kushika hatamu, sasa ni chama cha siasa kushiriki uchaguzi na kushinda.

RAI: Zipo taarifa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana anatarajia kuachia ngazi muda wowote, unafikiri uamuzi wake huo utaathiri chama?

MSEKWA: Ni uamuzi wa mtu kupumzika, aliteuliwa ana haki ya kusema sasa napumzika, mfano mimi niliamua mwenyewe kupumzika kwa umri wangu, haya ni maamuzi ya mtu.

RAI: Unazungumziaje mgogoro wa kisiasa Visiwani Zanzibar?

MSEKWA: Watu wasichanganye sheria na siasa, tatizo la Zanzibar msingi wake upo katika Katiba ya Zanzibar, wanaosimama upande wa Rais Shein, wanasema Katiba ya Zanzibar kifungu cha 28 i) kinasema Rais aliyepo ataendelea kuwa Rais mpaka Rais mwingine atakapoapishwa, hata Bara inasema hivyo, sasa hana mrithi, hivyo wanasema ni halali.

Maalimu Seif (CUF) na wenzake, wanasema kuna kifungu cha 28 ii) kwamba hakuna atakayekaa madarakani zaidi ya miaka mitano tangu alipoapishwa, katiba hiyo hiyo, sasa ukitaka kujua ni yupi sahihi, tafsiri hizo ni mahakama tu si mwanasiasa, hicho ndiyo kiini cha tatizo, sasa mkibadilishana na kuweka siasa mtavutana bila kufikia mwisho.

RAI: Wapo wanaodai kuwa uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha ni wa kwake binafsi hakuwashirikisha wajumbe wa tume, hili unazungumziaje?

MSEKWA: Kuna mkanganyiko kwa sababu hatujui wala hatuna uhakika wa kilichotokea, kama ni kweli hapakuwa na kikao, hatujui, na kama hakufanya hivyo ni kosa la kisheria, si la kisiasa, kama alivunja sheria adhabu yake ipo mahakamani, lakini hatujui kama kweli. Katiba ya Zanzibar inasema ZEC ni mwenyekiti, makamu wake na wajumbe wanne, kosa lenyewe ni la kisheria, haliwezi kuamuliwa kisiasa, haliwezi kumalizwa kisiasa wakati jambo la kisheria, walikaa mara nane walishindwa.

RAI: Rais Magufuli amelaumiwa kwamba anakwepa kutatua mgogoro wa Zanzibar,  unadhani ni sahihi kwake kufanya hivyo?

MSEKWA: Magufuli hawezi kwa sababu ni utawala wa sheria, Katiba yetu ina serikali mbili kuna mambo ya Muungano na ambayo si ya Muungano, kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano, Rais hana mamlaka yoyote, ni mambo yaliyo nje ya mamlaka yake, yale yapo chini ya mamlaka ya Zanzibar.

Ni kwamba uchaguzi wa baraza la wawakilishi au urais Zanzibar, si mambo ya Muungano hawezi kuingilia kwani utawala wa sheria haumpi mamlaka ya kuingilia haya, tusimtwishe mzigo ambao si wake, Ni katiba hiyo na sisi tunazungumzia utawala wa kikatiba, ataliingiliaje sasa?

RAI: Nini suluhu la mgogoro huo?

MSEKWA: Uchaguzi ndio suluhu ya matatizo. Nimeishi kwenye siasa za uchaguzi tangu 1965, hivyo nina imani ya uchaguzi kuwa ndio suluhu, katika siasa uchaguzi ndio suluhu sasa hilo ni tatizo maalumu. Hivyo tunaona marudio inaweza kuleta tatizo zaidi, kwani nusu ya Wazanzibar ndio watashiriki, inaweza kuwa tatizo wakinyamaza, wasiponyamaza itakuwa tatizo, au tuseme wakiridhika haitakuwa tatizo, wasiporidhika ni tatizo.

RAI: Kuna ukweli gani kuwa historia ya Pemba ndio tatizo la mgogoro wa kisiasa Zanzibar?

MSEKWA: Zanzibar ni kama nchi, lakini hata Mwalimu Nyerere alisema, tukivunja Muungano kutakuwa na Pemba na Wazanzibar, hilo ni tatizo la kihistoria, matatizo hayo yanatokana na tofauti za kihistoria kati ya sehemu hizo. Kwani Sultani alitawala kote, Unguja na Pemba lakini zaidi ni Unguja, na hata alipopinduliwa hakukimbilia Pemba, angeweza kukimbilia Pemba akaomba msaada, kwa hiyo hiyo ni historia,

RAI: Unautazamaje upinzani wa sasa ukilinganisha na miaka iliyopita?

MSEKWA: Vyama vya upinzani vimeimarika, jambo kubwa ni ule muungano wa Ukawa, umoja ni nguvu siku zote.

Kila wakati na tukio au majukumu yao, wale wana majukumu yao ya kisiasa. Wanashiriki ili siku moja washinde.

RAI: Baadhi ya walioshiriki uchaguzi mkuu ndani ya CCM, walilalamikia mchakato ulivyofanywa, unazungumziaje hilo?

MSEKWA: Kingunge alizoea kusema hayo malalamiko, lakini niseme kuwa sasa yameshapita, utaratibu ni uleule lazima yaje majina matano. Hakijabadilika kitu, Kingunge anakumbukia kanuni za zamani, alitoka kwenye uongozi wa CCM muda mrefu,  baada ya hapo tulitunga kanuni za maadili, kwamba lazima maadili ya wagombea yatazamwe, kiwe kigezo cha kupata hao watano, sasa ni utekelezaji wa kanuni zetu. Tulishafika hatua tukasema matumizi ya fedha, rushwa sasa lazima kuangalia maadili yao.

RAI: Rais Magufuli bado hajateua wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, unamshauri nini katika kujaza nafasi hizo?

MSEKWA: Wale anaoona yeye wanaweza kumsaidia, ila hajaniomba ushauri siwezi kumpa.