Home Makala Kimataifa MSIMUOMBEE MABAYA TRUMP-OBAMA

MSIMUOMBEE MABAYA TRUMP-OBAMA

1147
0
SHARE

LIMA, PERU


Rais wa Marekani Barack Obama, ameiambia dunia akiwa Amerika ya Kusini kuwa, dunia isimtakie mabaya Rais Mteule wa nchi hiyo, Donald Trump, bali impe muda.

Kauli hii ya Obama ni ya muendelezo na alianza kuitoa baada ya kukutana na Rais huyo mteule siku moja baada ya kuchaguliwa kwake katika Ikulu ya Marekani jijini Washington DC.

Obama yupo katika ziara za kuaga na safari hii akiwa nchini Peru, akawataka wananchi wa Latini Amerika, kutojenga mahitimisho mabaya dhidi ya Rais mteule wa Marekani Trump.

Hata hivyo, hata yeye Obama wakati wa kampeni alimtaja Trump kama mtu asiye na uwezo wa kukalia nafasi hiyo ya juu kabisa katika siasa za Dunia.

Akiwa katika nchi za Greece na Ujerumani wiki iliyopita, Obama amekuwa akikutana na swali kuhusu namna alivyoshinda Trump na pia amekutana na watu mbali mbali wakionesha kushangazwa kwao na ushindi wa Trump huku wakiwa na wasiwasi wa moja kwa moja kutokana na kuhisi mabaya kutoka kwa kiongozi huyo. Hali hii inatokana na kauli na misimamo ya Trump kwa nchi nyingine duniani.

“Ujumbe wangu muhimu kwenu ni huu … ni ujumbe ambao pia niliutoa Ulaya, msiweke hitimisho lenu katika kumtabiria mabaya,” Rais Obama alisema akiwa na kundi la vijana katika mkutano wa maswali na majibu nchini Peru.

“Subirini mpaka utawala wake uanze kazi, ni jambo la kuweka sera pamoja na baada ya hapo mnaweza kumhukumu kama kweli yuko pamoja na matakwa ya ulimwengu yaani kuishi na amani na maendeleo ya pamoja,” alisema.

Rais Mteule Trump, alishinda uchaguzi wa Marekani huku akiwa ametoa ahadi ya kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico, kubadili mikataba ya kibiashara na pia kuzuia waislamu kuingia Marekani.

Rais Obama ameamua kupunguza sintofahamu iliyopo kwa kuahidi kuweka masuala sawa katika kipindi hiki cha mpito na amekuwa akiwaambia watu kuwa, Rais huyu mteule ataachana na lugha kali na mbaya alizokuwa akizitoa wakati wa kampeni na hasa atakapokuwa ameona ukweli wa nafasi aliyopewa.

“Litakuwa ni jambo jema kwa wote duniani kutofanya hukumu mapema na kwamba kipindi hiki tumpe rais huyu mteule muda wa kuunda serikali yake, kuangalia sera wanazotaka kuzifanikisha na masuala mengine. Nimekuwa nikisema kuwa namna unavyofanya kampeni sio utakavyotawala,” anasema.

Rais Obama amekuwa akitoa kauli hizi za kutia moyo, ilihali anafahamu kuwa, timu itakayounda serikali ya Rais Mteule Trump, itatumia busara ya kuhakikisha kuwa sera nzuri ambazo Rais huyu kupitia chama cha Democrats alizipitisha katika kipindi cha miaka nane ya utawala wake, zinaachwa ziendelee licha ya kuwa Trump mwenyewe ametangaza mara kadhaa kuwa atahakikisha anazifuta akiingia madarakani.

Baadhi ya mambo ambayo Trump alikuwa akitangaza kuyashughulikia ni pamoja na suala la makubaliano ya kusitisha vikwazo kwa Iran, kwa madai kwmba Iran inatengeneza silaha za nyuklia na sera ya Marekani katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi.

Rais Obama alifanya kampeni kwa mgombea wa chama chake Hillary Clinton katika maeneo mengi na katika mikutano hiyo ya kampeni, alionesha madhaifu mengi ya Trump ambaye baadaye ameibuka mshindi.

Katika mikutano yake ya kuaga, Rais Obama ameendelea kuzungumzia masuala ya ukuzaji demokrasia, masuala ambayo Trump hakuwa shabiki wake.

“Unaweza kuona baadhi ya nchi ambazo zinarudi nyuma badala ya kwenda mbele, hasa katika masuala ya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa mitandao, kuheshimu vyama vya upinzani na asasi za kiraia,” Rais Obama alisema.

Trump alizuia baadhi ya vyombo vya habari kutoandika habari zake wakati wa kampeni, na pia alitishia wakati wa Mdahalo wake na Clinton, akisema iwapo atashinda, atampeleka mahakamani kwa kosa la kutumia barua pepe za serikali kwenye akaunti binafsi wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Japokuwa katika ziara hiyo Obama aliitumia kuonesha nchi za Ualaya kuwa Marekani bado itaheshimu makubaliano yake katika NATO, na kwamba Rais Trump naye atafanya hivyo hivyo.

Sera nyingine ni ile ya Mahusiano ya Marekani na nchi za Amerika Kusini, masuala ambayo hana uhakika nayo sana kama yataenziwa na Trump katika sera zake.

“Katika suala la mahusiano yetu na Latin Amerika, sitegemei mabadiliko makubwa ya kisera kutoka kwa utawala ujao,” alisema huku akifafanua kuhusu suala la Biashara kuwa ni jambo muhimu ambalo huwezi kucheza nalo.