Home Makala Mtaji wa mwanasiasa ni umma si uma

Mtaji wa mwanasiasa ni umma si uma

1339
0
SHARE

NA NDAHANI N. MWENDA

JULIUS Malema Sello ni mmoja ya wanasiasa vijana wanaofanya vizuri katika siasa ngumu za Afrika zenye kutawaliwa na ghiriba nyingi kila mahala na kila uchwao, walau yeye nchi aliyepo inaheshimu Uhuru wa maoni na Uhuru wa kujieleza kwa raia wake tofauti na nchi nyingine za Afrika.

Si yeye tu bali wapo vijana wengine wengi wanaofanya vema katika siasa za Afrika licha ya mazingira ya wanasiasa wa Upinzani kufanya siasa ni magumu kwa Afrika, tena hasa wanasiasa vijana. Tanzania tumebahatika kuwa na vijana wengi wanaojiingiza kwenye siasa tangu mwaka 2005 kwenye Uchaguzi Mkuu wa tatu tangu tuingie katika mfumo vyama vingi.

Kwa mara ya kwanza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipata mwakilishi wa kuchaguliwa (Mbunge) mwenye umri chini ya miaka 30 ambaye alikuwa ni Zitto Zuber Kabwe ‘Ruyagwa’ (CHADEMA), Pia palikuwemo Wabunge wengine vijana kama Amina Chifupa (Vitimaalum) ambaye hata hivyo alifariki kabla ya muda wake wa uwakilishi haujaisha.

Hapo ndiyo ukawa mwanzo wa vijana wengi kujiingiza katika siasa mara baada ya muda mrefu kuonekana kuwa siasa ni za wazee tu na si vijana.

Mwaka 2010 tulishuhudia pia idadi kubwa ya vijana wengi wakigombea nafasi za uwakilishi kwanzia Udiwani hadi Ubunge, hiyo ilidhihirisha kuwa siasa kumbe yaweza kufanywa na watu wa rika zote wenye vigezo vya kugombea nafasi za uwakilishi.

Si tu Tanzania bali hata nchi zingine za Afrika tumekuwa tukiona vijana wakigombae nafasi mbalimbali za uwakilishi tofauti na zamani, hata nchi jirani za Kenya na Uganda tumekuwa tukishuhudia vijana wakigombea nafasi hizo, kwa ujumla siasa haichagui umri, uwe kijana ama mzee kikubwa tu ni uwe na vigezo vinavyokidhi matakwa ya kisheria.

Licha ya idadi kubwa ya vijana kujingiza katika siasa barani Afrika, bado wengi hawatambui umuhimu wa nafasi hizo na nani wanayetakiwa kumtumikia. Bado vijana wengi hawajui nini maana ya uwakilishi, si wote lakini walio wengi bado hilo hawalijui ndiyo maana wengi wamekuwa hawadumu kwenye nafasi zao. Wengi hawadumu kwasababu huamua kusimama na watawala si wananchi hasa katika kukemea uminywaji wa demokrasia, ufisadi na uminyaji wa Uhuru wa kujieleza.

Hapo awali nimeeleza kuhusu Julius Malema ambaye kwa sasa ni Kiongozi wa chama cha upinzani huko Afrika Kusini, nimemuleza Julius Malema kama mfano wa kuigwa kwa vijana wa kiafrika hasa wanaotaka kupaa kisiasa, pia Tanzania tunaye Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo. Hawa wawili historia zao kwa mbali ‘zinataka kufanana’ kwani hapo awali walikuwa wanachama wa vyama vingine na sasa ni wanachama wa vyama vingine tena vyote vikiwa vya upinzani, na lakuvutia zaidi ni kuwa hawa wote ni viongozi wakuu wa vyama vyao vya sasa, na kikubwa zaidi wote bado hawajapoteza mvuto kwa wapiga kura wao wazamani na wa sasa.

Julius Malema amekuwa mwanachama wa chama tawala nchini Afrika Kusini ANC tangu akiwa na miaka 9 hadi alipofukuzwa mwaka 2012 akiwa kama Rais wa Baraza la Vijana Taifa la chama [ANC-Youth League] hicho kikongwe duniani. Kabla ya hapo Julius Malema alishika nafasi nyingi ndani ya chama hicho kabla ya kushika nafasi hiyo ya juu kabisa.

Kilichomfanya afukuzwe ndani ya ANC ni kitendo cha yeye kuikosoa Serikali ya chama chake pale ilipoenda kinyume cha matakwa ya Umma, aliwashambulia baadhi ya Mawaziri ambao walitoka ndani ya ANC kitendo ambacho kiliwakera watawala. Hata Baba yake mlezi kisiasa Jacob Zuma alishambuliwa na Julius Malema alipokwenda kinyuma na matakwa ya Umma.

Hivyo baada ya kufukuzwa ndani ya ANC, mwaka 2013 alianzisha chama chake kinachojulikana kama “Economic Freedom Fighter” (EFF) ambacho kimekuwa tishio kwa chama tawala (ANC) na chama cha kingine cha Upinzani cha “Democratic Alliance” ambacho kimekuwa kikituhumiwa kuingia fungate na watawala na hivyo kuacha kazi ya kutetea Umma.

Mwaka 2015  Julius Malema  alituhumiwa kutoa kauli za kibaguzi ama za kichochezi kama hapa kwetu Tanzania ilivyozoeleka, haikuishia hapo tu watawala walimpa kesi ya utakatishaji fedha, lakini kesi zote hizo Mahakama ilitupilia mbali baada ya mkurugenzi wa mashitaka (DPP) kuchelewesha kuwasilisha ushahidi, na hivyo Mahakama kudai kesi hizo zilikuwa na mlengo wa kisiasa.

Vile vile tumeshuhudia jinsi Zitto Kabwe ambavyo ameweza kudumu katika siasa takribani inakaribia miaka 15 sasa tangu aijingize kwenye siasa za majukwaani. Kitu kinachomtofautisha Zitto Kabwe na wanasiasa wengine vijana ni kitendo cha yeye kusimama na Umma, Zitto Kabwe si Mbunge wa Jimbo lake tu bali ni Mbunge wa Tanzania nzima, anawasema wananchi wa Bulyahulu, anawasemea wananchi wa Tandahimba, anawasemea wananchi wa Uvinza anawasemea wananchi wa Pemba na Watanzania wote kwa ujumla, hapa ndipo ulipo utofauti kati yake na wanasiasa wengine vijana. Zitto Kabwe, Julius Malema na Robert Ssentamu [Bobi Wine] ni wanasiasa vijana wa kupigiwa mfano Afrika, kwani wameweza kuzishinda changamoto za kutumiwa na watawala katika kuendeleza kukandamiza masilahi ya Umma.

Sote tumeshuhudia Zitto Kabwe alivyosimama kidete kwenye sakata la mgodi wa Buzwagi, sakata lililopelekea Mawaziri wawili kujiuluzu, pia tulishuhudia Zitto Kabwe akisimama kidete kwenye sakata la Mchuchuma na Liganga, Zitto Kabwe hakuishia hapo alisimama kidete kwenye sakata la Escrow akiwa na rafiki yake marehemu Deo Filikunjombe aliyekuwa Mbunge wa Ludewa. Zitto Kabwe ndiyo sababu ya kutungwa kwa sheria mpya ya madini ya mwaka 2010.

Hivi karibuni tumeona Zitto Kabwe alivyosimama na wananchi wa Mtwara na Lindi na mikoa yote inayozalisha zao la korosho mara baada ya Serikali kuvuruga soko la korosho, zao ambalo limekuwa mkombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo. Zitto Kabwe ni mwanasiasa ambao Tanzania inawahitaji kwasasa, anafanya siasa kila anapoona panastahili, Zitto Kabwe anajua wapi aongee, nini aongee na muda gani akae kimya. Zitto Kabwe, Julius Malema na Bobi Wine ni vielelezo vya wanasaiasa vijana wakipewa nafasi ya kutetea wananchi wanaweza, hawayumbishwi licha ya kupewa kesi mbalimbali za kuwakatisha tamaa.

Mwaka 2018 tulishuhudia jinsi Bobi Wine alivyoutikisa utawala wa kiimla wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, licha ya kuteswa na kupigwa pamoja na kushikiliwa katika kambi ya kijeshi kwa siku kadhaa bado Bobi Wine hakurudi nyuma katika kudai haki za Waganda kutoka kwa serikali isiyoambilika ya Yoweri Museveni, Rais ambaye amedumu madarakani kwa miongo mitatu. Jeshi la Polisi la Uganda lilimua dereva wake na baadae yeye akawekwa kizuizini. Hivyo ndiyo vijana wa Kitanzania na Afrika wanapaswa kujua jinsi ya kudumu kwenye siasa kuwa ni kusimama na Umma, mtaji wa mwanasiasa yoyote dunuani ni watu na watu siyo wanaompa nafasi agombee Ubunge ama Udiwani bali wale wanaohalalisha Udiwani ama Ubunge wake ama Urais ambao kimsingi ni wananchi.

Tunahitaji wanasiasa wasioweka matumbo yao mbele kuliko masilahi ya waliowaweka madarakani. Tumeona jinsi Julius Malema anavyopambana juu ya suala la watu weusi ndani ya Afrika Kusini kukosa ardhi huku radhi kubwa ikihodhiwa na wazungu wachache ambao wamepewa na watawala.

Julius Malema amekuwa akipambana watu weusi kupata ardhi ya kulima, pia hivi karibuni tumeona akikemea kitendo cha Waafrika Kusini wanaowashambulia watu kutoka mataifa mengine (hasa ya Afrika) wakidai kuwa wanachukua nafasi za kazi ambazo wao wamekuwa wakizikosa kwa muda mrefu.

Tuna lundo la wanasaisa vijana ambao wameishia njiani kutokana na kutotambua nafasi zao, wengi wanapenda mafanikio ya haraka (Uwaziri/Ubunge) kuliko yale ya kuyatafuta kwa jasho na damu.

Kwasasa Zitto Kabwe anaweza kugombea Ubunge mahala popote pale Tanzania na akashinda tofauti na Mbunge yoyote yule Tanzania.

Vilevile Julius Malema anaweza akagombea mahala popote ndani ya Afrika Kusini iwe Johannesburg, KwaZulu Natal, Limpopo na akashinda kwa kishindo.

Wanasiasa wetu lazima watambue kuwa ili ufanikiwe kisiasa inahitaji nguvu na akili kama wanavyofanya Malema na Zitto, tunahitaji siasa za masuala siyo za kushambulia watu. Siasa za masuala zinazogusa maisha ya watu, siasa zenye tija siyo za kupakana matope. Katika hili, hakuna mwanasiasa aliyewahi kusimama na Umma akaangushwa, vijana lazima wajifunze hili maana wao ndiyo hatma ya nchi yetu, huwezi kupewa Ubunge ili uwatumikie watu wewe unakuwa ‘busy’ na mambo yako. Wanasiasa vijana ili wadumu lazima waepuke anasa na mteremko.