Home Habari kuu Mtatiro umekunywa mvinyo gani uliokulewesha?

Mtatiro umekunywa mvinyo gani uliokulewesha?

807
0
SHARE

HASSAN DAUDI

KWAKO Julius Mtatiro, mmoja kati watu makini kuwahi kuwashuhudia tangu nilipoanza kufuatilia siasa za Tanzania miaka michache iliyopita.

Nilianza kuvutiwa na utendaji wako ukiwa kijana machachari wa Chama cha Wanachi (CUF). Ulianza kuwa sehemu ya wanasiasa niwapendao kwa uwezo wao wa hali ya juu katika kujenga hoja tangu mwaka 2008.

Nakizungumzia kipindi ulipojiunga na CUF ukiwa umetoka kuhitimu Shahada ya kwanza pale UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).

Kama ilivyo kwangu, naamini hakuna mwanachama wa CUF aliyesahau namna ulivyokuwa ukiiweka kwenye wakati mgumu Serikali.

Ukiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya CUF, nakumbuka ulivyokuwa mwiba mchungu, hasa kwa upande wa Bara, ambako hukuacha kunyooshea mkono kila ulichoona si sahihi chini ya Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakata Kikwete.

Niseme ulikuwa bora kwenye ubora wako wa kusimamia kile ulichokiamini. Kama si jukwaani, basi kwa kutumia taarifa za CUF kwa vyombo vya habari, na endapo kusingekuwa kote huko, basi ‘ungeipapasa’ Serikali kwa makala zako zilizojaa ufundi wa kujenga hoja.

Kwa ujumla wake, itoshe kusema Mtatiro ulikuwa alama muhimu ya upinzani, ukiwakilisha vema ile dhana ya upande huo kuwa na haki ya kukosoa utendaji wa Serikali.

Wakati nazisikia taarifa za kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), Agosti, mwaka jana, nikiri wazi kwako kwamba mambo mawili makubwa yaliyokuja akilini mwangu.

Mosi, niliamini upinzani umepoteza silaha muhimu katika mapambano yake ya kidemokrasia dhidi ya CCM. Kilichonijia akilini ni kwamba CCM wamepata, upinzani umepoteza.

Pili, sikuwa na shaka kuwa haitachukua muda mrefu kabla ya kupewa kazi ya kufanya ndani ya CCM. Hatimaye ukachaguliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Unaweza kudhani nilikuwa muumini wa ile dhana ya CCM kununua wapinzani kwa ahadi za kuwapa vyeo lakini wala sikuwa huko na wala sitarajii.

Nataka niamini ulikwenda CCM kwa mapenzi yako. Kilichonifanya niwe na imani ya wewe kutosota kupata kazi ya kufanya ukiwa CCM ni umakini wako, ambao hakika ulihitajika mno kwa kasi Rais John Magufuli.

Labda sitaeleweka vizuri lakini niseme tu ukweli, kwamba tukiweka kando siasa, si tu wananchi wa Tunduru, bali kila Mtanzania alitakiwa kushukuru kuona Serikali imepata mtu wa aina yako. Wewe ni ‘jembe’.

Nitakuwa nimekosea kusema upinzani ulipoteza kwa masilahi ya taifa? Bila shaka hapana, nitakuwa sahihi, japo sitasita kukubaliana na watakaokuwa na mtazamo tofauti. Wakati mwingine, tunapaswa kukubali kutokubaliana.

Hata hivyo, nikiamini bado wewe ni mwanasiasa mwenye weledi mkubwa, hivi karibuni nilishangazwa na kauli uliyoitoa katika mahojiano yako na chombo cha habari (jina nitalihifadhi).

Kwamba wakati unajiunga CUF miaka 10 iliyopita, chaguo bora lilikuwa CCM lakini hukutaka kujiunga nacho kwa kuwa ulikiona ni chama kikubwa na kilichojengeka. Kwa kifupi, hukuiona nafasi yako huko.

Binafsi nilikwazika na kauli yako hiyo na si kwamba kwa kuwa umeitoa ukiwa CCM, bali sikutarajia kuwa ingetoka kinywani mwako, nikitambua una weledi wa kutosha.

Aidha, sikutegemea kukusikia ukilisema hilo hata kwa bahati mbaya kwa kuwa natambua kwa umri ulionao, nategemea kukuona kwa muda mrefu katika medani ya siasa.

Kusema ulikuwa na mapenzi na CCM tangu ukiwa upinzani inakufanya uichafue taswira yako, hivyo kutishia uhai wako kisiasa katika miaka michache ijayo.

Mtatiro unafahamu hakuna mwanasiasa aijuaye kesho yake ndani ya chama anachokiwakilisha leo na katika hilo nitakutolea mfano wa watu wawili.

Kumbuka kilichotokea kabla ya mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Nani angeweza hata kutabiri kuwa Edward Lowasa na Frederick Sumaye wangehamia upinzani?

Nikikukumbusha kuwa huenda hilo likakukuta, vigogo hao, ambao ukweli ulivyo ni kwamba wamekuacha mbali kiuzoefu ndani ya CCM na siasa kwa ujumla, walikiacha chama hicho na kwenda upinzani.

Nakukumbusha tu, mwandishi nguli wa vitabu, Will Rogers, aliwahi kusema: “Kadiri unavyofuatilia siasa, unabaini kuwa kila chama kina matatizo kuliko kingine.”

Sasa hapo najaribu kujiuliza tu, itakuwaje kwako Mtatiro endapo utaona kila kitu kikienda tofauti na matarajio yako kule CCM?  Jibu linaweza kuwa kuacha siasa au kurudi upinzani. Tujadili hapo kidogo.

Ukiacha siasa utakuwa umewakatilia walio wengi, nikiwamo pia, ambao mara nyingi wamekuwa wakiamini katika uwezo wako.

Wakati huo huo, huenda utakuwa umejikatili, kwa kushindwa kutimiza ndoto nyingi, ambazo unazo katika maisha ya siasa.

Lakini je, utawaambia nini wapinzani wakati tayari umeshasema CCM ilikuwa chaguo bora kwako tangu ulipoingia CUF mwaka 2008?

Wasiwasi wangu ni kwamba kauli yako hiyo itakuwa karata nzuri kwa mahasimu wako kukuzuia kuingia upinzani, jambo ambalo linaweza kukuathiri kisiasa.

Hiyo ni kwa upande mmoja na sasa tugeukia mwingine, ambao hakika nao umenifanya nikufikirie mara mbili, hata sasa nianze kutilia shaka kila kauli nitakayoisikia kutoka kwako.

Hivi, wakati unasema ulikuwa upinzani, huku ukiamini CCM ndiyo chama bora kuliko vyote huoni kama inakuvua moja kwa moja sifa za kuwa kiongozi?

Kana kwamba hukuwa Mtatiro niliyekutambua kwa misimamo yako, ambayo mara zote ulijitaja kuwa ni mkweli, ulisema hata maoni yako juu ya Katiba Mpya yalikuja tu kwa kuwa ulikuwa mpinzani.

Unachotaka kusema ni kwamba kila ulichokuwa ukishauri kipindi cha mchakato huo kiliandaliwa na upinzani na wewe ulikuwa mtekelezaji tu.

Je, kama ulipindisha ukweli, tena katika suala la msingi kama lile, ambalo utekelezaji wake uligharimu mamilio ya fedha zitokanazo na kodi za wananchi, huoni hustahili kuwa kiongozi?

Pia, niendelee kukuuliza tu, ndani ya muda mfupi tangu ujiunge na CCM, ina maana umebadilika na kuacha tabia ya kufuata mkumbo, hata unapohisi unawaumiza walio wengi?

Nikisema ulichowaaminisha wananchi ni kwamba hata katika wadhifa ulionao sasa, Mkuu wa Wilaya, utafanya kile utakachoona kinalinda masilahi ya mamlaka nitakuwa nje ya ukweli kwa kiasi gani?

Ikiwa umekiri maoni yako ya juu ya Katiba Mpya yalitokana na nafasi yako katika upinzani, unaturuhusu kuamini yapo mengi uliyowahi kuwadanganya wananchama na wapenzi wa CUF?

Kwamba uliposema Ilani ya Ukawa ndiyo suluhisho la kero za wananchi wakati unagombea Ubunge pale Segerea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 haukuwa ukimaanisha?

Vipi kauli yako kwamba Rais Magufuli hafai kuiongoza Tanzania kwa sababu akiwa wizara ya ujenzi alishindwa kutengeneza barabara za Segerea, hivyo asingeweza kufanya lolote Ikulu?

Aidha, kwa kile ulichokisema kuwa usingeweza kuingia CCM wakati ule (2008), bado sina shaka kuwa unaendelea kuuheshimu upinzani, kwa kuwa ulikupa nafasi ya kujijenga kisiasa kupitia nyadhifa mbalimbali ulizoshika ndani ya CUF.

Mwisho, nikuage kwa kukung’ata sikio, nikitarajia kukuona Mtatiro ukiomba radhi, ikizingatiwa kuwa viongozi, wanachama na wapenzi wake walikuamini na kukupatia fursa ya kukomaa kisiasa.

Kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yako wilayani Tunduru.