Home Habari MTI HUSHIKILIWA NA MIZIZI

MTI HUSHIKILIWA NA MIZIZI

4820
0
SHARE

Na MUDHIHIR MUDHIHIR


MTI ni jamii ya mimea inayoota ardhini. Naam, ipo mimea inayoota juu ya maji. Hujapata kusikia habari ya magugu maji! Kwa wenye taaluma ya elimu ya mimea, maelezo yao juu ya mti ni kitu gani huwa ni yenye kina cha kutosha. Lakini maelezo yangu na ya kwako katika kuuchambua mti yataanza na kuishia mizizi, shina, matawi, majani, maua na matunda. Na hata haya yatakuwa ni maelezo ya juu juu tu bali kwa muktadha wa mjadala wetu huu, yatatosheleza haja.

Twende zetu ardhini, mti hushikiliwa na mizizi ambayo pia hufyonza  virutubisho mbalimbali vya kuunawirisha mti. Lipo shina ambalo ni njia ya kusambaza virutubisho na chakula, na ni ghala la kuhifadhia chakula cha mti. Yapo matawi yenye kuhimili uzito wa majani, maua na matunda. Ndiyo! Maua yakifumba kisha hufumbuka yakazaliwa matunda. Majani huyalinda matunda kwa kuota rangi yake ya kijani kibichi hadi yanapobadilika rangi na harufu tayari kwa kuliwa. Majani pia huleta kivuli na mandhari ya kuvutia.

Unacheka nini! Nimepatia ee! Hayo yote kwa ujumla wake ndiyo mti.  Niliyokusudia kuyaleta hapa siyo haya kwani kwa haya tu hata wewe unayatambua vyema. Msaada ninaouhitaji hapa barazani  unahusu hulka za majani, matawi na mizizi. Tunalo sisi wanadamu la kujifunza kutokana na hulka hizi?

Mshikamano wa majani na mtu hunawiri vizuri katika neema za misimu ya mvua. Mitihani ya jua la kiangazi ikishika kasi uswahiba wa majani hunyauka yakapukutika chini na matawi yakabakia uchi. Bali na ukame ukipamba moto zaidi na matawi husaliti mti kwa kukauka na kuishia kuwa kuni jikoni. Juu ya ardhi mti hubaki na upweke wenye nyoyo wakachora milizamu ya mchozi kwa huruma, na wenye nyongo wakaangua vicheko vya kipo wapi!

Chini ya ardhi, mti hauna upweke. Ipo mizizi ambayo kwa asili na maumbile yake haionekani kwa macho. Mizizi huwa ikisema kuwa hatutakuacha mti na ikibidi kuanguka  tutang’oka na wewe. Nakuona umekunja uso ghafla. Unao watu unaotaka kuwafananisha na majani au matawi ambao sasa ni wenza wako na karibu kwa sababu ya neema tele tele zilizokuzunguka? Au watu hao sasa wameusaliti uswahiba kwako kwa sababu umegubikwa na dhiki za jua la kiangazi?

Ukitamani kuyapa nafasi ndani ya moyo wako maswali ya hapo juu, basi utambue kuwa unakaribia kuufufumaa utu wako nawe uwe mti. Nawe utakuja kunyauka na kupukutika kama majani. Nawe utakuja kukauka na kuunguzwa kama kuni. Wewe ni mtu si mti. Ndani ya utu wako hakuna majani, matawi wala mizizi. Ndani ya mtu kuna utu, kujitambua na dhamira.

Sijasema humu wala sitadiriki kusema popote kuwa ni jambo baya kuwafananisha baadhi ya watu na majani au matawi. Hata kidogo! Kwani ni kweli si uongo kuwa wapo wanaozikimbia ndoa zao, wanaowakimbia rafiki zao na kadhalika kwa sababu ya ukata. Ila ninalolisisitiza mimi ni umuhimu wa mtu kuuthamini utu wake, kujitambua kuwa yeye ndiye mvuta kasia na upondo katika safari yake, na kuhakikisha kuwa anajiandaa vya kutosha katika kutekeleza dhamira yake.

Kalamu ya Muungwana inashauri kuwa ikiwa yupo unayetamani kujifananisha na mti basi kwanza ajiulize, yeye anataka kuwa nani. Majani, matawi au mizizi.