Home Makala Kimataifa MTIFUANO WA MAREKANI, CHINA WAFIKIA PABAYA

MTIFUANO WA MAREKANI, CHINA WAFIKIA PABAYA

4032
0
SHARE

MAREKANI

Misingi ya siasa za Kimataifa baina ya nchi mbili za Marekani na China imeonekana kuchukua sura mpya baada ya China kumuwajibisha Balozi wa Marekani katika nchi hiyo.

Kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya China,nchi hiyo imekiri kumuwajibisha kwa kuwasilisha malalamiko kwa Balozi wa Marekani nchini humo, ikiwa kama moja ya kupinga vitendo vya Marekani dhidi ya China.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Geng Shuang’s, alisema kuwa vitendo vya Marekani dhidi ya taifa hilo, ni vitendo vyenye kuashiria wazi kabisa uvunjifu wa misingi ya siasa za kimataifa za nchi mbili hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya wiki moja tangu Marekani ilipotangaza kuliwekea vikwazo Jeshi la China kutokana na hatua zake za kununua ndege za jeshi kutoka Urusi, pamoja na makombora ya kurushwa kutoka ardhini. China ilinunua ndege 10 za Sukhoi Su-35 na makombora ya S-400.

Serikali ya Marekani ilisema ununuzi kama huo unakiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi, tabia ya Urusi nchini Ukraine na madai ya kuingilia kati uchaguzi wa Marekani.

China haijajiunga kwenye vikwazo ilivyowekewa Urusi na Marekani na washirika wake tangu mwaka 2014. Uhusiano kati ya Marekani na Urusi ulidorora kwa haraka baada ya Urusi kulimega eneo la Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014.

Aidha, kufutwa kwa mazungumzo ya kijeshi kati ya Marekani na China, ni hatua nyingine inayoashiria uhasama wa mataifa hayo mawili yenye nguvu ya kiuchumi duniani kufikia pabaya

Itakumbukwa kuwa mapema wiki hii, Wizara ya Ulinzi ya China ilifuta mazungumzo ya kijeshi kati yake na Marekani,  ikiwa ni wiki chache baada ya nchi hiyo kufuta mazungumzo ya kibiashara baina ya pande hizo mbili.

Mazungumzo hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika mapema wiki hii mjini Beijing, lakini sasa duru za habari zimebainisha kuwa serikali ya China imemrejesha nyumbani Kamanda wa Jeshi la Majini aliyekuwa safarini nchini Marekani, kwa ajili ya kushiriki mkutano wa 23 wa kimataifa wa makamanda wa majeshi ya majini.

Hatua hiyo ya Marekani inaonyesha kwamba, mgogoro kati ya nchi hizo mbili umeongezeka, kama ambavyo pia Marekani inakusudia kuwalenga washirika wa kiuchumi na kijeshi wa Beijing.

Japokuwa kisingizio kinachotumiwa na Marekani katika kadhia hii ni kuzidisha vikwazo dhidi ya China, lakini ukweli ni kwamba Marekani pia imeilenga Urusi na inafanya jitihada kuibana nchi hiyo katika ngazi ya kijeshi.

Aidha, kushadidishwa vikwazo vya Marekani dhidi ya China kunaonyesha kwamba, Marekani ina wasiwasi wa kuongezeka zaidi uwezo wa kiuchumi na kijeshi wa nchi hiyo ya Asia na kuwa nguvu kubwa duniani, na hata siasa za kuipandishia ushuru wa bidhaa kutoka China hazikuweza kuzuia ustawi wa kiuchumi wa nchi hiyo.

China ilisema italipiza kisasi kwa kutoza ushuru wa Dola za Kimarekani bilioni 60 kwa bidhaa kutoka Marekani, baada ya Rais Donald Trump kutangaza kiwango cha ushuru wa ziada kwa bidhaa zinazoingia kutoka China. China ilitangaza hivyo baada ya kutangazwa kuwa ushuru wa ziada kuwa Dola bilioni 200.

Mvutano huu ni matokeo ya vita ya kibiashara kati ya nchi hizi mbili. Katika kudhihirisha uhasama kati ya pande hizo mbili,  Wizara ya Fedha ya China, ilisema inalipiza kile alichokiita ajenda ya Marekani ya kutazama upande mmoja na biashara yenye ushindani usio sawa.

Hata hivyo, Rais Trump alitahadharisha kuwa atalipiza kisasi ikiwa wakulima, wafugaji na wafanyakazi wa Kimarekani watalengwa kwenye maamuzi ya China.

” Tumekuwa na biashara isiyo na uwiano sawa na China, mwaka jana tulipoteza kiasi cha zaidi ya Dola bilioni 500 kwa China, hatuwezi kufanya hivyo” alisema.

Kwa msingi huo, iwapo China na Urusi, ambazo ni wanachama muhimu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hazitasimama imara kuzuia sera hizo za Marekani, huwenda hapo baadaye mahusiano ya Urusi na China yakakumbwa na changamoto kubwa na matatizo zaidi kutoka Marekani.