Home Makala Kimataifa MTO NILE NA SIASA ZINAZOGONGANISHA MATAIFA YA UKANDA

MTO NILE NA SIASA ZINAZOGONGANISHA MATAIFA YA UKANDA

1663
0
SHARE

NA HILAL K SUED

WIKI iliyopita Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, alifanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania na moja kati ya mazungumzo yake na mwenyeji wake, Rais John Magufuli, aligusia suala la matumizi ya Mto Nile unaochukua maji yake kutoka Ziwa Victoria ambalo sehemu kubwa yake liko upande wa Tanzania.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Magufuli aliwaambia waandishi wa habari kwamba, kila upande umekubali kuendelea na mazungumzo kuhusu suala hilo ambalo limekuwa nyeti kwa miongo mingi.

Lakini si wengi wanaofahamu historia ya siasa za mto huu ambao ni mrefu zaidi duniani (kilomita 6,700), unaopita katika nchi tisa za Afrika ya Kati, Mashariki na Kaskazini Mashariki, historia ya mizozo mikubwa ya kisiasa baina ya nchi hizo na Misri. Nchi hizo ni Misri yenyewe, Burundi, Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia,  Sudan na Sudan ya Kusini, Sudan na Misri ambazo zote zina tabia nchi tofauti.

Mto huo unaotoa maji yake mengi kutoka Ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, unajazwa maji yake kutoka mito mitatu inayotokea milima ya Ethiopia – Blue Nile, Sobat na Atbara. Aidha, tunaweza pia tukataja mito mingine kwa upande wa Tanzania kama vile Mto Mara na Mto Kagera. Vyanzo vya Mto Kagera ni milima iliyopo kwenye mpaka wa Burundi na Rwanda.

Aidha, inaelezwa kwamba Misri hutoa misaada ya kifedha kwa Serikali za nchi hizo mbili ili kutunza vyanzo vya mto huo.

Lakini historia ya miongo ya karibuni ya Bonde la Ziwa Victoria na matumizi ya Mto Nile, imekuwa tata sana kwani imeingiliwa sana na masuala ya kisiasa katika eneo hilo na nje pia.

Kuna madai kwamba Misri tangu enzi za ustaarabu wake wa kale takriban miaka 5,000 iliyopita, imejijengea haki ya asili ya matumizi ya mto huo na kwamba misingi ya haki hiyo ndiyo imekuwa kiini cha majadiliano yake kadha na mikataba liyofikiwa na inayoendelea baina yake na nchi zinakoanzia au zinazokopitia maji mto huo.

Na takribani mikataba yote ilitambua umuhimu wa maji ya Mto Nile kwa uhai wa nchi ya Misri na hivyo, kuipa upendeleo wa pekee nchi hiyo.

Kwa mfano, mkataba wa kikoloni wa mwaka 1929, Misri imekuwa ikipewa upendeleo wa kutumia maji hayo kwa shughuli mbalimbali zikiwamo kilimo, nishati na maji safi.

Lakini miaka ilivyokuwa ikienda, mabadiliko ya tabia nchi na matakwa ya maendeleo kama vile mahitaji ya nishati ya umeme, miundombinu na kilimo cha umwagiliaji, kumekuwapo na msukumo mpya kuhusu nchi nyingine za ukanda huo kuwa na udhibiti mkubwa zaidi wa maji ya Ziwa Victoria kwa mahitaji yao ya maendeleo.

Mwaka 2010 makubaliano ya Entebbe, Uganda yalifikiwa kuhusu matumizi sawa ya mto huo, lakini Sudan na Misri hawakusaini mkataba huo hadi sasa.

Hivyo basi, kwa kuwa “haki” hii ya Misri ipo, ina maana kwamba upunguzwaji wowote wa maji ya mto huo unaingilia masuala ya usalama wa taifa la Misri na hivyo kunaweza kuanzisha mifarakano baina yake na nchi hizo.

Julai 2014, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, aliendelea kuweka msimamo kuwa Tanzania itaendelea kuitetea Misri kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile.

Membe aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Waziri wa Uingereza wa Masuala ya Afrika, Mark Simmonds, kwamba Misri ina chanzo kimoja tu cha maji na kuongeza matumizi ya maji ya mto huo ni kuiangamiza.

Alisema kitendo cha baadhi ya wabunge kutaka maji ya mto huo yatumike sawasawa na nchi nyingine si cha kibinadamu na kilikuwa na lengo baya hasa kwa nchi ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa Tanzania.

Kauli hii ya Membe ni ya mara ya pili baada ya aliyekuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mahadhi Maalim, kujibu bungeni swali la aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mwadau (CUF) mapema Mei mwaka huo aliyetaka kujua iwapo mabadiliko ya kisiasa nchini Misri yangeathiri makubaliano ya matumizi ya Mto Nile. Mabadiliko ya kisiasa yaliyotajwa ni yale yaliyomwondoa kupitia mapinduzi ya kijeshi aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mohammed Morsi.

Membe alisema inapaswa majadiliano yaende pole pole na nchi husika zikubali kuipendelea Misri katika mikataba ijayo ili kuiokoa nchi hiyo iliyopo jangwani.

Aliongeza kuwa Tanzania ni wakombozi na heshima ya nchi hii ni kumsaidia mnyonge na hivyo, kuilinda na kuitetea Misri ni uwakala mzuri.

Kumekuwapo nyakati ambapo Misri imetishia kuingia vitani kuhusu maji ya Mto Nile. Mfano mzuri ni miaka ya karibuni tu.

Miaka mitano iliyopita aliyekuwa Rais wa Misri, Mohamed Morsi, alitoa onyo kwamba nchi yake haitaki vita na Ethiopia lakini pia iko tayari kwa lolote lile.

Kauli ile ilizidisha maradufu joto la mtafaruku mkubwa uliokuwapo kwa muda kuhusu mradi wa ujenzi nchini Ethiopia wa bwawa kubwa la kuhifadhia maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, mradi wa Grand Renaissance katika mkondo wa Blue Nile karibu na mpaka na Sudan uliokuwa unajengwa na kampuni moja ya Italia wa kuzalisha umeme tu, umeme ambao utauzwa pia kwa nchi jirani. Mradi huo sasa umekamilika.

Aidha, Ethiopia ilisema kwamba mradi huo usingepunguza kasi ya mkondo wa Nile, hasa baada ya bwawa lake kubwa likisha kujaa na kamwe isingetumia maji hayo katika shughuli za umwagiliaji mashamba.

Mto Nile ambao mkondo wake mwingine – White Nile – unaanzia Ziwa Victoria kupitia Uganda, Sudan ya Kusini na Sudan (ambako unaungana na Mkondo wa Blue Nile), unaingia Misri na kukatisha katikati ya nchi hiyo na kuishia katika Bahari ya Mediterranean.

Katika hotuba yake kupitia luninga, Morsi alisema kwamba anafahamu fika mahitaji ya kimaendeleo ya nchi masikini zinazozunguuka vyanzo vya mto huo, lakini alisisitiza kwamba nchi yake kamwe haiwezi kukubali kuona kasi ya mkondo wa Mto Nile unapungua, kwani maji yake yamekuwa ni uhai ya Wamisri kwa milenia kadhaa.

Aidha, alikumbushia wimbo mmoja wa kale wa Kimisri kuhusu Mto Nile unaosema: “Mto ukipungua angalau kwa tone moja la maji basi jibu lake ni damu yetu.”

Kauli hiyo pamoja na nyingine kali za wanasiasa wa Misri zilizidisha hofu ya kuwapo ‘Vita ya Maji” baina ya nchi ya kwanza na ya pili kwa idadi ya watu barani Afrika – yaani Ethiopia na Misri. Kuna baadhi ya wanasiasa walitoa pendekezo kwamba iwapo Ethiopia itahatarisha maji ya Mto Nile, basi Serikali ya Misri ichukue hatua ya kuwapa misaada makundi ya waasi wanaopigana na Serikali ya Ethiopia.

Lakini ingawa mgogoro huu pia ulionekana kumpa Rais Morsi fursa ya kuwahamasisha Wamisri kumuunga mkono baada ya mwaka wake wa kwanza wa migogoro mikubwa nchini mwake tangu ashike madaraka, pia ulikuwa unampa fursa ya kutafuta mwafaka wa suala la matumizi ya Mto Nile, suala nyeti na ambalo kama ilivyoelezwa hapo juu limedumu kwa miongo kadhaa.

Misri hutumia karibu maji ya Mto Nile yanayoingia nchini humo kwa ajili ya matumizi yake yote mbali mbali na kwamba, bila Mto Nile basi hakuna Misri kama taifa. Mara kadhaa, katika kusisitiza uhalali wa madai yake, Serikali ya Misri imekuwa ikitaja mikataba ya tangu enzi za wakoloni, mikataba ambayo imekuwa inaihakikishia nchi hiyo sehemu kubwa ya maji hayo.

Kwa upande wake, Ethiopia ambayo ni ya pili kwa uwingi wa watu (91 milioni) barani Afrika (ya kwanza ikiwa Nigeria), inadai kwamba mikataba hii imepitwa na wakati.

Nchi nyingine kusini mwa nchi hizo na ambazo pia ni wahusika wa maji ya Mto Nile ikiwamo Tanzania, nazo pia zinataka kujiendeleza kutokana na maliasili hiyo ya maji ya Mto Nile na vyanzo vyake.

Tanzania kwa mfano kwa takribani miaka kumi sasa imekuwa ikiyatumia maji ya Mto Victoria kwa matumizi yake ya majumbani katika mikoa ya Shinyanga na mipango iko mbioni kuyafikisha maji hayo Mkoa wa Tabora.

Uganda nayo iliamua kutumia maji ya Ziwa hilo kuzalishia umeme baada ya kuongeza mitambo mingine ya kufulia nishati hiyo pale Bujagali.

Sudan ambayo pia inayo mabwawa yake ya kuzalisha umeme na umwagiliaji katika Mto Nile unaopita nchini humo, iliunga mkono mradi wa Ethiopia, ikisema kwamba inatarajia kunufaika na umeme unaotarajiwa kuzalishwa.

Misri nayo imekuwa na mradi wake wa umeme katika bwawa la Aswan, inalalamika kuhusu uwezekano wa kupunguka kwa maji kutokana na mradi wa Ethiopia. Serikali ya Misri ilisema utafiti wa wataalamu wake ulikuwa unaonyesha kwamba, nchi yake itaathirika sana kutokana na mradi wa Ethiopia.