Home Makala MUDA WA KUCHANGAMKIA FURSA NI SASA

MUDA WA KUCHANGAMKIA FURSA NI SASA

594
0
SHARE

NA SUSAN UHINGA, TANGA


WATANZANIA tulio wengi tumekuwa na utamaduni wa kutekeleza mambo yetu kwa mfumo wa zimamoto.

Hatuna maandalizi ya kutosha ya mambo tunayotaka kuyafanya sasa au hata baadaye, hatuna malengo, hatujali muda, tunaamini kila kitu kitafanyika tu bila hata kupanga.

Hali hii ndiyo inaweza kuwagharimu wakazi wengi wa Tanga kwenye mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi linalotokea nchini Uganda hadi Chongoleani.

Bomba litapita katika mikoa minane ya Tanzania, wilaya 24 na vijiji 80. Mikoa itakayonufaika ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Tanga ambako bomba hili litaishia ndiyo utakaofaidika zaidi, kwa sababu ndiko visima vikubwa vya kuhifadhia mafuta vitajengwa, lakini pia ndiko kwenye bandari itakayotumika kusafirishia mafuta hayo kwenda nje ya nchi.

Wilaya tano kati ya nane za Mkoa wa Tanga zitanufaika na mradi huo, wilaya hizo ni Korogwe, Kilindi, Handeni, Muheza na Tanga yenyewe, hii inamaanisha zaidi ya vijiji 50 vitapitiwa na mradi huu.

Ni wazi kuwa sasa Tanga kama mkoa uliokuwa na neema katika miaka ya 1970-80, si tu kwa kilimo bali pia viwanda, unaweza kurejea kwenye kilele chake cha ubora wa uchumi kupitia bomba hili.

Bomba linatarajiwa kutoa ajira 10,000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya utafiti, upimaji na ujenzi na ajira 1,000 za kuendelea.

Uwapo wa mradi huo mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla unafungua fursa kwa kila sekta kama vile makampuni ya usafirishaji, ulinzi, taasisi za kifedha, huduma za kiafya, kampuni za chakula na hoteli, makampuni ya wataalamu (wanasheria, wahasibu, wahandisi, wataalamu elekezi na kadhalika), wakulima, wafugaji, wavuvi hadi mama lishe na bodaboda.

Mradi wa bomba hilo utahamasisha ujenzi wa miundombinu kama barabara, reli, uwanja wa ndege na bandari.

Katika eneo la mradi, kilomita 200 za barabara zitajengwa na kilomita 150 kuboreshwa, lakini pia kupitia kanuni ya wajibu wa kampuni zinazoendesha miradi kutoa huduma za kijamii, maeneo mengi ambayo bomba litapita watapata huduma za umeme, maji, shule, barabara na kadhalika.

Kama wananchi wa maeneo ambayo mradi huo utapita hawataanza maandalizi ya kuchangamkia fursa zitakazoambatana na mradi huo, bila shaka watajikuta wanakuwa watazamaji na huenda wakaishia kulalamika na kuisukumia lawama Serikali.

Hakuna sababu ya wakazi wa Tanga kusubiri kuambiwa nini cha kufanya, badala yake wanatakiwa kuanza sasa kuchungulia fursa.

Hakuna sababu yoyote ya wakazi wa Tanga wa maeneo yatakayopitiwa na mradi kufikiria zaidi ajira za moja kwa moja za mradi huo, ukweli ni kwamba wengi wa watakaoajiriwa ni wale wenye utaalamu aidha wa kuendesha mitambo au shughuli nyingine zinazohitaji watalaamu.

Hii inadhihirisha ajira rasmi zinaweza kuwagusa watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na pengine hata nje ya nchi. Kwa kulitambua hili ni vema wakazi wa Tanga wakajiandaa kuchangamkia fursa zitakazotokana na mradi huo kama nilivyotangulia kusema hapo juu.

Labda maswali yataibuka kuwa watachangamkiaje? Ni kweli ipo hofu kuwa ili ufanye jambo na likuletee tija ni lazima uwe na mtaji mkubwa. Hii ni dhana inayopaswa kupingwa na kutokomezwa.

Tukumbuke ujio wa mradi wa bomba la mafuta utagusa watu wa kada na rika mbalimbali. Wapo maofisa wa ngazi za juu watakaohitaji mahitaji ya juu kulingana na hadhi zao.

Lakini pia watakuwepo watumishi wa ngazi za chini ambao wao nao watahitaji kufanya matumizi yanayolingana na vipato vyao, hawa ndio wengi na kundi hili ndilo linaloweza kuchangia pato kubwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo kuliko kundi la kwanza la maofisa ambalo linajumuisha watu wachache sana.

Jambo muhimu kwa wakazi wa Tanga watakaopitiwa na mradi huu ni kuwa tayari kubadilika kulingana na mazingira, kuwa na utayari wa kuboresha biashara zao ili kuondoka kwenye ufanyaji wa biashara wa kimazoea.

Kutofanya maandalizi ya kupokea fursa za mradi huo sasa ni sawa na kujimaliza wenyewe hali itakayotufanya tuwe wasindikizaji wa wageni watakaotoka China kuja kuwauzia chai wachimba mitaro wa mradi.

Litakuwa ni jambo la ajabu kama wanavijiji watakuwa wanasubiri kulipwa fidia za mimea yao zaidi badala ya kuelekeza nguvu kwenye kuwekeza hata kwa mgahawa tu.

Napenda kuwafahamisha kuwa bomba hilo litapita katika eneo kubwa la Mkoa wa Tanga, lakini wataalamu wameshajipanga kuhakikisha linaepuka maeneo yenye shughuli za binadamu kadiri inavyowezekana, hali ambayo itapunguza migogoro.

Mradi huu utajengwa kwa haraka na unatazamiwa kuchukua miezi 24, sawa na miaka miwili, zabuni za ujenzi zinatazamiwa kutangazwa mwishoni mwa mwaka huu na hivyo ujenzi wa bomba utaanza katikati ya 2018 na kukamilika katikati ya mwaka 2020.

Mradi unatazamiwa kudumu kwa miaka 25 hadi 30, kwa sababu mafuta yaliyogunduliwa Uganda ni mapipa bilioni 6 na mapipa yatakayokuwa yanasafirishwa kwa siku kupitia bomba hilo ni 216,000 kwa siku.

Muda wa kuchangamkia fursa za bomba la mafuta kwa Watanzania ni sasa.

0767414185