Home Makala MUGABE AANDALIWA MKAKATI WA KUMNG’OA

MUGABE AANDALIWA MKAKATI WA KUMNG’OA

779
0
SHARE

HARARE, ZIMBABWE


Mwishoni mwa mwezi uliopita wanasiasa wawili mashuhuri wa upinzani nchini Zimbabwe walikubaliana kuviunganisha vyama vyao ili kumuondoa Rais Robert Mugabe ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 37 sasa.

Hili limejiri wakati uchaguzi mkuu wa mwaka ujao ukikaribia ambapo Waziri Mkuu wa zamani Morgan Tsvangirai na Makamu wa Rais wa zamani Joice Mujuru walitiliana saini makubaliano ya kuunda umoja katika upinzani.

Wawili hao walipeana mikono na kutabasamu kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari. “Tumeamua kuchukua hatua hii ya awali ya kuwaweka Wazimbabwe wote chini ya paa moja kwa lengo kufanya kazi pamoja kuuondoa ukandamizaji na utawala mbovu uliopitiliza, hali ambayo imekuwa ikiliandama taifa letu,” alisema Tsvangirai.

Naye Mujuru alisema: “Ilituchukua miezi sita kuujadili umoja huu. Twafahamu matumaini yenu yako juu sana – sisi tutawaleteeni Zimbabwe mpya.”

Wachunguzi wa mambo wanasema umoja huu ni tukio la kihistoria katika siasa za Zimbabwe. Sababu moja ya mtazamo huo ni kwamba muungano huo unawaleta pamoja watu wawili wenye ushawishi mkubwa, ambao kihistoria walikuwa katika pande mbili za uadui mkubwa.

Akiwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Morgan Tsvangirai alikuwa akitishwa na kukamatwa na vyombo vya dola kwa zaidi ya miongo miwili. Na wakati huo huo, Joice Mujuru, akiwa Makamu wa Rais na swahiba mkubwa wa kisiasa wa Mugabe kwa miaka kumi (2004 – 2014) hadi alipolazimika kujiuzulu, ndiye alikuwa mhusika mkuu wa serikali katika ukandamizaji huo. Hivyo ni tukio kubwa kwa wawili hao kupeana mikono.

Hata hivyo chama cha Tsvangirai cha Movement for Democratic Change (MDC) na kile cha Mujuru cha National People’s Party (NPP) siyo vyama pekee katika umoja huo. Chama cha Movement for Democratic Change-Ncube (MDC-N) cha Welshman Ncube na kile cha People’s Democratic Party (PDP) cha Tendai Biti navyo vimo katika mwavuli huo.

Cha kushangaza zaidi ni kwamba Ncube na Biti wana historia ya mikwaruzano katika MDC, ambapo wote wawili waliwahi kushika nyadhifa za ukatibu mkuu wa chama hicho kwa nyakati tofauti, na wote walikuja kutofautiana na Tsvangirai, hivyo kila mmoja kuondoka kivyake.

Lakini nje ya mfumo wa kisiasa, vikundi vingine vya wanaharakati kama vile ‘This Flag’ na ‘Tajamuka,’ vikundi ambavyo katika miezi ya karibuni vimekuwa vikihamasisha maandamano makubwa dhidi ya Mugabe, navyo vimedhamiria kumng’oa Mugabe.

Vikundi hivi vinasadikiwa kuunga mkono umoja wa upinzani hivyo kuupa umoja huo wigo mpana zaidi wa ki-vuguvugu, na siyo tu muungano wa wanasiasa.

Haya yanayojiri yameibua hamasa kubwa miongoni mwa wale wanaopenda kuona mwisho wa Mugabe na chama chake cha ZANU-PF. Lakini je, hamasa hii ina maana yoyote?

Inaelezwa kwamba upinzani una sababu nzuri tu ya kuwa na hamasa. Wapinzani wa Mugabe wamekuwa wakinyanyaswa mara kwa mara katika chaguzi, na ile almanusra ya ushindi wa MDC mwaka 2008 bado inakumbukwa sana.

Katika uchaguzi huo Tsvangurai alipata asilimia 47.9 za kura za urais na Simba Makoni mgombea mwingine aliibuka wa tatu kwa kupata asilimia 8 za kura, hivyo kisheria kulitakiwa marudio ya wawili wa juu – Migabe na Tsvangirai.

Ghasia kubwa ziliibuka dhidi ya wafuasi wa Tsvangirai kiasi kwamba alisusia kura ya marudio na Mugabe kunyakuwa urais. Lakini waliona kwamba laiti kungekuwapo umoja kati ya Simba Makoni na Tsvangirai, Mugabe angeangushwa asubuhi mapema.

Na baada ya kufanya vibaya katika uchaguzi wa 2013 ambapo kura za Tsvangirai zilishuka hadi asilimia 34, wafuasi wengi wa upinzani walionekana kukata tamaa. Lakini umoja huu wa sasa una nafasi kubwa ya kurudisha matumaini yao.

Aidha wachambuzi wa mambo ya siasa nchini humo wanasema umoja baina ya MDC na NPP unajumuisha maeneo mawili ya ufuasi wa upinzani. Kwa mfano, wanasema, MDC imekuwa na nguvu sana katika kuhamasisha wafuasi hususan katika maeneo ya mijini na sehemu za kusini za nchi, lakini mara nyingi chama hicho kimekuwa kinahangaika sana katika jimbo la Mashonaland ya Kati, eneo ambalo chama tawala kina nguvu.

Hivyo endapo Mujuru, ambaye nyumbani kwake ni jimbo hilo hilo ataweza ‘kuwateka’ wafuasi wengi wa ZANU-PF, basi anaweza kuwa tishio kwa Mugabe.

Lakini kikubwa kuhusu Mujuru ni uhusiano wake na maafisa wengi katika utawala wa Mugabe alikokuwa kama Makamu wa Rais, hasa katika vyombo vya usalama.

Hivyo maafisa hawa muhimu wanaweza kumsaidia Mujuru kuuonda utawala wa Mugabe. Pia inatajwa kwamba huu ndiyo ulikuwa udhaifu mkubwa wa Tsvangirai katika kumuondoa Mugabe katika chaguzi zilizopita, hasa ule wa 2008.

Hata hivyo inaelezwa pia kwamba ingawa Mujuru ana mahusiano na wakuu wa vyombo vya usalama lakini anao uhusiano mdogo na jeshi.