Home Latest News MUGABE NA ASANTE ISIYO NA UHALISIA

MUGABE NA ASANTE ISIYO NA UHALISIA

841
0
SHARE

NA RUTH FERNANDO

HABARI ya dunia kwa sasa ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ‘Jongwe’ ambaye anatajwa kushikilia rekodi ya kuwa Rais mkongwe Afrika na dunia kwa ujumla.

Kwa sasa Jongwe anapitishwa kwenye tanuru la moto, linalokolezwa na kuchochewa na baadhi ya watu wake wa karibu.

Makamu wa Rais aliyetimuliwa na Mugabe Emmerson Mnangangwa pamoja na Mkuu wa majeshi wa nchi hiyo Generali Constatino Chiwenga wanaonekana kuwa nyuma ya mkakati wa kumwondoa Rais huyo wa muda mrefu wa Zimbabwe.

Vuguvugu la wawili hao na viongozi wengine wa serikali, linaonekana kuungwa mkono na viongozi wa umoja wa maveterani wa Zimbabwe wanaoongozwa na  Chris Mutsvangwa, Douglas Mahiya na Victor Matemadanda.

Muungano huo wenye lengo la kukomesha utawala wa miaka mingi wa Mugabe sasa unaungwa mkono na idadi kubwa ya wananchi wa Zimbabwe.

Hii inaashirisha wazi kuwa sasa utawala wa Jongwe umefikia tamati, kwa maana hauwezi kuendelea zaidi, badala yake unaweza kukoma kwa kutimuliwa au kwa hiyari yake.

Hata hivyo, dalili za ‘babu’ kukubali kung’oka kwa hiyari zinaanza kutoweka siku baada ya siku hasa baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kutoa hotuba ambayo dunia ilidhani ni ya kutangaza kujiuzulu, lakini haikuwa hivyo.

Katika hotuba yake hiyo iliyotazamwa na mamilioni ya watu duniani Jongwe aliapa kuendelea kuongoza taifa hilo kwa wiki kadha, licha ya shinikizo la kumtaka aachie madaraka.

Katika hotuba yake ambayo wachambuzi wa mambo wanaiita ya kuonesha umoja na kukubaliana na kile kilichofanywa na jeshi, Mugabe aliihitimisha kwa kutumia maneno mawili ya Kiswahili ambayo ni asante sana.

Kwa kawaida neno asante hutolewa kwa kumaanisha shukrani baada ya kutendewa jambo lililojema. Asante inayotolewa mbele ya ubaya mara nyingi haibebi maana halisi kama ile inayotolewa mbele ya uzuri.

Kwa muktadha huo ni wazi asante ya Mugabe haikumaanisha kile ambacho wengi walikitamani kukipata kutoka kwake badala yake alitoa asante iliyoibua mtazamo na mipango mipya ya uasi dhidi yake.

Katika hotuba yake hiyo ya moja kwa moja iliyorushwa na kituo cha runinga cha Taifa hilo Mugabe alikwenda kinyume na matakwa ya wengi kwa kusema kuwa anapanga kuongoza mkutano mkuu wa chama mwezi Desemba.

Ikumbukwe kuwa Mugabe ameyasema hayo wakati tayari maofisa wakuu wa chama cha Zanu-PF walikuwa wameidhinisha hatua ya kumvua uongozi wa chama hicho na kumpatia saa 24 ajiuzulu la sivyo wamuondoe madarakani.

Hatua ya ZANU-PF ilikuja baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa serikali wiki iliyopita, huku mzozo kuhusu nani atamrithi ukizidi kutokota hatua inayoonesha wazi kuwa Mugabe ameshapoteza ushawishi na udhibiti wa chama chake.

Kwa kiwango kikubwa Mugabe anaelekea kuvuna alichokipanda kwani mzozo wa sasa ulianza mara baada ya kumtimua  makamu wake Mnangagwa wiki mbili zilizopita.

Hatua hiyo ililikera jeshi ambalo lilitazama hatua hiyo kama jaribio la kumteua mke wake Grace ambaye amekimbia nje ya nchi hiyo kuwa makamu wa rais na mwisho kuwa mrithi wake.

Mapema Jumapili iliyopita, Mnangagwa alitawazwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha Zanu-PF na mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2018.

Katika mkutano huo pia, Grace Mugabe, mwenye umri wa miaka 52, alivuliwa uanachama wa chama hicho pamoja na maafisa wengine wakuu.

“Mkutano mkuu wa chama (cha Zanu-PF) utafanyika wiki chache zijazo na nitauongoza na kusimamia shughuli zake,” Rais Mugabe ameliambia taifa kupitia runinga, akiwa ameandamana na majenerali kadha wakuu jeshini.

Hata hivyo, Jongwe ameonesha ukomavu kwa kukiri ukosoaji dhidi yake kutoka kwa Zanu-PF, jeshi na umma, na kusisitiza kwamba ipo haja ya hali ya kawaida kurejea.

“Bila kujali faida au madhara ya jinsi (jeshi) walitekeleza operesheni yao, mimi, kama amiri jeshi mkuu, nakiri kwamba kuna matatizo,” amesema, akirejelea hatua ya jeshi ya kuchukua udhibiti wa runinga ya taifa wiki iliyopita.

Raia wengi nchini Zimbabwe wameonekana kushangazwa na hotuba ya  Mugabe ambaye alitarajiwa na baadhi yao kujiuzulu.

Hatua ya Mugabe ya kugoma kutangaza kujiuzulu imeonekana kumkwaza kiongozi wa chama chenye ushawishi cha maveterani wa vita vya ukombozi wa Zimbabwe Chris Mutsvangwa, ambaye ameweka wazi kuwa sasa Robert Mugabe huenda akaondolewa madarakani kwa hiyari baada ya yeye mwenyewe kushindwa kuchukua uamuzi sahihi.

Mutsvangwa alisema hotuba ya kiongozi ambaye alikuwa chaguo la kwanza la maveterani hao haijazingatia uhalisia.

“Tutafuata njia ya kumuondoa madarakani na tunawataka watu warejee tena barabarani kuandamana.”

Ikumbukwe kuwa maveterani hao walikuwa wafuasi safi na watiifu wa Mugabe na wao waliwahi kuongoza uvamizi wa mashamba yaliyomilikiwa na Wazungu mwaka 2000 na wametuhumiwa kwa kutumia ghasia na fujo kwenye uchaguzi ili  kumsaidia Mugabe kusalia madarakani.

Hata hivyo mwaka jana, maveterani hao waliacha kumuunga mkono Jongwe kwa sababu mbalimbali kubwa ikiiwa ni kumpa nafasi zaidi mke wake.

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai ambaye aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu katika serikali ya umoja wa taifa na chinbi ya Rais Mugabe nae alionesha kushangzwa na hotuba ya ‘babu’.

Kiongozi huyo wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) alikuwa akimtarajia Mugabe, mwenye umri wa miaka  93, ajiuzulu baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa serikali wiki iliyopita.

“Nimeshangaa sana. Si mimi pekee, bali taifa lote. Anacheza mchezo fulani. Amevunja matarajio ya taifa lote.”

Wafuatiliaji wa mambo wanahoji kuwa ni vipi Rais Mugabe anaweza kuongoza mkutano huo mkuu wa chama cha Zanu-PF mwezi ujao, ikiwa ameshavuliwa uongozi.

Mugabe ameongoza Zimbabwe kwa miaka 37 tangu taifa hilo lilipojipatia uhuru mwaka 1980 kutoka kwa Uingereza.

Hotuba yake hiyo ilikuwa mara yake ya pili kuonekana hadharani tangu jeshi lilipotangaza kuchukua udhibiti wa taifa hilo katika kile walichosema ni juhudi za kuondoa “wahalifu” ambao wamemzingira rais.

Ijumaa, alihudhuria mahafali katika chuo kikuu wazi cha Zimbabwe, lakini hakutoa tamko lolote wakati huo.