Home kitaifa MUHEZA VINARA WA WIZI WA UMEME TANGA

MUHEZA VINARA WA WIZI WA UMEME TANGA

1066
0
SHARE
Mmoja wa wakaguzi wa mifumo ya umeme Oktavian Mmunyi, akiangalia nyaya zilizounganishwa chini kwa chini kwaajili ya kuba umeme wa Tanesco

Na Amina Omari, TANGA

SHIRIKA la umeme nchini Tanzania Tanesco ndio shirika pekee hapa nchini lililopewa dhamana ya kusambaza huduma ya umeme katika maeneo yote hapa nchini.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, shirika hilo limekuwa katika utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo unakuwa wa uhakika nchi nzima.

Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa ambayo imeunganishwa katika kupata huduma hiyo kupitia gridi ya taifa kutoka na kuwa na kituo cha kuzalisha umeme kilichopo Hale.

Mhandisi Abdulrahman Nyenye ni meneja wa shirika hilo mkoa wa Tanga anasema kuwa, wamefanikiwa kupeleka huduma hiyo katika wilaya zote nane zilizopo mkoani hapa. Anasema kuwa katika maeneo ya wilaya hizo hususani makao makuu ya kila wilaya husika yamefanikiwa kupata kwa ukaribu huduma hiyo kwa kiasi
kikubwa .

“Changamoto tunayokabiliana nayo kwa sasa ni kupeleka umeme kwenye maeneo ya pembezoni ambayo hapo awali yalichelewa kupata maendeleo ya haraka”anasema Mhandisi Nyenye.

Anasema kuwa, lengo la mkoa ni kuhakikisha wanasogeza huduma karibu na wananchi hususani wale wa maeneo ya pembezo ili kuhakikisha wanapata huduma hiyo ili kuweza kujiletea maendeleo yao. Pia, katika kuhakikisha wanatoa huduma bora wamejitahidi kuboresha kitengo cha dharura ili kiweze kufanyakazi kwa ufanisi mkubwa wa kushughulikia dharula kwa wakati muafaka.

Vile vile kutokana mkoa huo kuanza kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda, shirika hilo nalo halikuwa nyuma katika kuhakikisha wanaboresha huduma zake ili kwenda sambamba na sera hiyo.

Katika kituo chake cha Majani Mapana ambacho kinahusika na kuhudumia maeneo ya viwanda wameweza kufunga transifoma mpya yenye ukubwa wa 45 MVA.

“Kufungwa kwa transifoma hiyo kutasaidia kumaliza changamoto iliyokuwepo awali ya umeme mdogo ambao ilikuwa ni mmoja ya kilio kikubwa cha wenye viwanda vingi katika maeneo hayo,” anafafanua Meneja
huyo.

Hata hivyo Mhandisi huyo amesema kuwa licha ya mafanikio ya kuboresha huduma shirika hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha juhudi hizo.
Anasema moja ya changamoto hizo ni wananchi waliowengi kuhusika na uchomaji wa nguzo za umeme zinazobabaisha shirika kupata hasara kubwa ya miundombinu yake kuharibika.

Anazitaja wilaya za Pangani na Lushoto, kuwa ndizo zinazoongoza kwa kuhusika na matukio hayo ya uchomaji wa nguzo za umeme hivyo kupelekea maeneo hayo kukosa umeme mara kwa mara.

“Tumekuwa tukipata hasara mara kwa mara kutoka na miundombinu yetu kupita katika maeneo yenye mashamba hivyo wananchi wakati wa kusafisha
mashamba wanachoma moto karibu na nguzo hivyo kuungua na kuleta hitilafu ya kukatika kwa huduma,”anasema.
Meneja huyo anasema kuwa, wamekuwa wakitoa taarifa za kuwepo kwa matukio hayo kwa polisi ili waweze kuchukuwa hatua za kisheria pamoja na kudhibiti vitendo hivyo.

“Tumekuwa tukiwashirikisha viongozi wa vijiji katika changamoto hiyo ili nao waweze kutoa elimu kwa wananchi wao kuhusu athari za uchomaji wa nguzo hizo na pia katika kuthibiti vitendo hivyo,” anasema Nyenye.

Wizi wa umeme ni aina nyingine ya changamoto inayolikabili shirikahilo sio kwa mkoa wa Tanga pekee bali katika maeneo mengine nchi nzima.Kwa mkoa wa Tanga, wilaya ya Muheza ndio inaongoza kwa kuwa na wizi wa umeme ambao umekuwa ukisababisha hasara kwa shirika kwa kiasi kikubwa.

“Uunganishaji wa umeme kwa kutumia njia zisizo rasmi  unaofanywa na vishoka umekuwa ni tatizo kubwa lakini tumekuwa tukikabilina nalo kwa kufanya oparesheni za mara kwa mara,” anabainisha Meneja huyo.

Aidha, amewaasa wananchi kuacha tabia hiyo kwani pale mtu unapokamatwa unalazimika kulipa fedha nyingi ambapo kama ungepitia njia rasmi wangeweza kupunguza fedha hizo. Vile vile wizi wa nyaya za umeme unaofanywa na wananchi umekuwa ni sehemu ya changamoto hususani katika maeneo ya yenye mapori katika wilaya za Korongwe.

“Wizi wa nyaya umekidhiri sana katika eneo la Magoma lililopo wilayani Korogwe lakini kwa sasa tupo kwenye utekelezaji wa kubadilisha nyaya za copper ambazo zimeoneka zinaibiwa sana na kuweka za silver”anasema
Meneja wa mkoa.

Hata hivyo shirika hilo licha ya kutoa huduma hiyo lakini wananchi pamoja na taasisi zimekuwa zikichangia kuzorotesha utoaji wa huduma bora kutoka na kushindwa kulipa madeni kwa wakati. Mhandisi Nyenye anasema kuwa kwa mwaka huu wamejipanga kuhakikisha wadaiwa sugu wote wanawaunganisha kwenye huduma ya mita za LUKU badala ya huduma iliyopo hapo awali.

Asema kuwa ili waweze kufanikiwa kukusanya madeni hayo wameweka utaratibu maaluma wa kuwaingiza kwenye mikataba ya namna ya kulipa malimbikizo ya madeni yao  kabla ya kuwaingiza kwenye huduma ya LUKU .