Home Latest News MUSA SIMA: BUNGE LA BAJETI LILIKUWA LA MOTO

MUSA SIMA: BUNGE LA BAJETI LILIKUWA LA MOTO

4557
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


JULAI mosi mwaka huu, Rais John Magufuli alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na katika taasisi mbalimbali za Serikali kwa kuteua viongozi 16. Mojawapo ya viongozi ambao waliangukiwa na ngekewa hiyo ni Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima (CCM).

Mabadiliko hayo yalikuja siku chache baada ya Bunge la Bajeti kuhitimisha shughuli zake Juni 29, mwaka huu, jina la Sima likasikika katika mabadiliko hayo baada ya kupewa nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania Muungano na Mazingira.

Hata hivyo, ni mara ya kwanza kwa Sima kuwa Mbunge. Amechaguliwa 2015, na ameteuliwa kuwa Naibu Waziri kwa mara ya kwanza.

Yapo mambo mbalimbali ambayo RAI limepata wasaa wa kuzungumza naye na kudadavua kinaga ubaga, jinsi alivyojipanga kutekeleza majukumu yake kwa uweledi ili asimkwaze Rais Magufuli kama ambavyo amekuwa akisema mara kwa mara kuwa baadhi ya wateule wake bado hawaja mwi-‘impress’.

RAI: Hii ni mara ya kwanza kuteuliwa kushika wadhifa wa Naibu Waziri, je umeupokea vipi uteuzi huo?

SIMA: Niliupokea vizuri na kwa hali chanya kwa sababu ukishateuliwa maana yake unapewa jukumu la kumsaidia Rais. Hii ni heshima kwamba unafaa kwa wakati huo. Ila kwa upande wa pili ni mtihani kuitunza hiyo heshima na kutekeleza maagizo ya Rais na chama chetu kwa kupitia ilani yake kama inavyoelekeza.

RAI: Moja ya mambo ambayo Rais Magufuli aliwashauri wateule wake, ni kufanya kazi kwa bidii ili kujitangaza (kuji ‘promote’), Je, umejipanga vipi kuongeza jitihada katika hilo?

SIMA: Kweli hili ni jambo alilotueleza wazi kwa kuwa na yeye alipitia katika nafasi hizi. Kwa kuzingatia kuwa nimekwenda kwenye wizara kubwa mbili, ambayo ni muungano na mazingira. Hususani mazingira yenyewe ni eneo pana sana kwa sababu tunazungumzia mazingira yote yanayomzunguka mwanadamu.

Kwanza ni nimekaa karibu na watendaji wote akiwamo waziri ili kujifunza mambo ambayo wanayatekeleza na changamoto wanazokutana nazo lakini pia nimeandaa mpango wangu ambao naweza kushauri namna tunavyoweza kufikia malengo yetu kama wizara.

Aidha, Rais aligusia mambo mengi ikiwamo suala la NEMC, kwamba inachelewesha kutoa vibali na mfano kile kiwanda cha betri – Kibaha. Nieleze kwamba hili ni jambo la kwanza ambalo nimelifanyia kazi  na wiki iliyopita tayari NEMC wamewapatia kibali.

Nilienda mwenyewe Kibaha kwenye kiwanda hicho cha China board Group na kuzungumza nao na walifuata taratibu zote ila hoja ya msingi kwanini NEMC wachelewe kutoa kibali?

Licha ya kukutana na mambo mengi ila kubwa nililokubaliana na waziri ni kubadilisha utaratibu ambapo sasa provisional permit (kibali cha awali) inatolewa kwanza ndipo cheti kamili baadaye, lakini pia maeneo yote au mikoa yote ambayo haijatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji tumeagiza itenge maeneo hayo na kufanya mpango wa tathmini ya mazingira, ili kurahisisha kazi pindi mwekezaji anapokuja apewe kibali cha awali na baadae kibali kamili. Hivyo ndivyo tulivyokubaliana kwa utaratibu huo mpya.

BUNGE

RAI: Bunge la Bajeti limekwisha na Bajeti Kuu ya Serikali imepita, ni nini maoni yako kwa Bunge na Serikali?

SIMA: Kwa kweli lile Bunge tangu na mimi niingie bungeni lilikuwa Bunge la aina yake. Hoja nyingi ziliibuka na si korosho tu hata mifugo, viwanda na kilimo. Ni Bunge ambalo wabunge tulipata fursa ya kusema wazi ila kwa lengo la kuisaidia serikali, na serikali iliyapokea mengi. Ni mategemeo yangu kuwa serikali tutafanyia kazi yale yaliyoyasemwa.

Ni Bunge ambalo lilitoa fursa  ya kutosha kwa wabunge kusema mpaka wanasema ‘nisipojibiwa vizuri sitaungwa mkono na chama changu’, lakini wengi walitanguliza busara mbele, kwa sababu  wasingetanguliza busara tusingefikia pazuri. Spika naye alitoa fursa ya kutosha kwa wabunge, na tulifikia hitimisho ajenda ikapita na yapo mambo yameanza kufanyiwa kazi sasa. Na tukirudi inawezekana tusikutane na changamoto ya hayo yaliyosemwa awali.

RAI: Wapo baadhi ya wabunge wa CCM ambao walisimama kidete kutetea masilahi ya wapiga kura wao hatua iliyowafanya kuonekana ni wasaliti, Je, ni kweli wanastahili kupewa sifa ya usaliti?

SIMA: Hapana…kila mbunge ni mwakilishi wa eneo lake, kwa hiyo anaangalia masilahi ya wananchi wake, pili chama na tatu serikali. Hivyo lazima aangalie kwa mfumo huo. Kama wapo ambao tumekubaliana kwa mfumo huo na mtu akaenda kinyume na hayo huyo tutamuita msaliti ila kama amekubaliana na hayo na baadae akatoa ushauri huyo si msaliti. Kwa sababu amekubali, ila tuitamuita msaliti kama kwenye bajeti mwishoni anasema hapana, huyo tutamuita msaliti ila hakuna mwanaCCM aliyesema hapana.

SERIKALI

RAI: Ni miaka miwili na nusu sasa tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, je, imefanikiwa wapi na wapi pengine unaona imekwama na inapaswa kupatilia mkazo?

SIMA: Serikali imefanikiwa kwenye maeneo mengi, tukigusa kwenye sekta ya miundombinu na uchukuzi, imefanikiwa kuliko ilivyokuwa huko mwanzo. Lakini hata kwenye eneo la uwajibika kwa watumishi wa umma vilevile rushwa imepungua kwa kiasi kubwa.

Pia serilkali imeanzisha miradi mikubwa ambayo inatambulika kimataifa kwa mfano Stigler’s Gorge, ni mradi mkubwa ambao unaenda kumaliza tatizo la umeme, zaidi Megawati 2100 zitazalishwa, ujenzi wa barabara za fly over. Tutakapokamilisha miradi hii nchi yetu inaweza kufikia mahali na kupunguza utegemezi.

Kuna miradi mingi katika sekta ya kilimo, maliasili, uvuvi na mifugo ambazo tayari serikali imeshatoa maelekezo ambayo hata sasa hali inaonesha wazi kuwa yanatekelezwa kikamilifu.

RAI: Kumekuwa na kauli kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, wasomi na hata wananchi wa kawaida kuwa miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege haina tija ya moja kwa moja kwa wananchi kama ilivyo kwa miradi ya elimu, maji na afya,  hili unalizungumziaje?

SIMA: Lazima waangalie nchi zilizoendelea walifanyaje. Lakini hata sasa kwenye afya na elimu huwezi kuona malalamiko mengi kama ilivyokuwa awali vivyo hivyo kwenye maji, tunaendelea kutekeleza miradi mingi.

Kiujumla niseme hatuwezi kuendelea kujikita kwenye eneo ambalo tunaweza kulimudu kisa linagusa wananchi moja kwa moja.  Lakini ukiangalia Stigler’s Gorge ni kwamba China walikuwa na mradi mkubwa kama huu, wao walitaka kuangalia kimataifa, kwani ukiwa na mradi kama huu au ndege haya yote ikiwamo hivyo vipaumbele vitatekelezwa kwa kupitia hii miradi mikubwa.

Niwaombe Watanzania wote tuungane, tukianza kukwamisha miradi hii kwa masilahi ya kisiasa hatutafika. Tumuunge mkono Rais wetu ili aweze kufikia malengo mazuri ya kuwaletea wananchi maendeleo.

JIMBO

RAI: Mara nyingi mawaziri au naibu waziri wakishatoka kwenye nafasi hizo, hurudi majimboni mwao na kueleza wapiga kura wao kuwa walikuwa wamebanwa na sasa wanao muda wa kutosha kuwatumikia tena. Je, umejipanga vipi kutumikia wapiga kura wako na nafasi uliyopewa sasa ya Naibu waziri?

SIMA: Kuteuliwa waziri huku ukiwa una jimbo, ni fursa mojawapo ya kushirikiana na wenzako vizuri. Ila licha ya kuteuliwa waziri au naibu waziri una siku 14 zinazotambulika kiserikali kwenye wizara ambazo utaona ni lini inafaa kwenda kufanya kazi za jimbo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi wako. Baada ya hapo awamu nyingine tena unazo siku 14. Ninachoona ni sawa na wabunge tu kwa sababu nao wanamwezi mmoja wa kufanya kazi jimboni muda mwingi ni masuala ya kibunge.

RAI: Kwa kuwa ni mmoja wa wadau wa zao la alizeti hasa ikizingatiwa linalimwa kwa wingi mkoa wa Singida, unafikiri nini kinasababisha zao hili lisiendelee kunufaisha wakulima wake?

SIMA: Ukiitazama Tanzania tuna mahitaji ya mafuta ya kula zaidi ya tani 400,000 ila tunachozalisha hakizidi tani 150,000 kwa mwaka. Hii ina maana nakisi yote hiyo inatoka nje.

Mafuta ya alizeti yana Cholesterol ndogo ukilinganisha na mengine, changamoto iliyopo katika zao hili ni uzalishaji mdogo ambao unasababishwa na mambo mengi, kubwa ikiwa ni pamoja na ushindani mdogo wa viwanda au wanunuzi, pili ukosefu wa pembejeo na bei yenye mvuto kwa wakulima.

Ni kwamba Singida kuna kiwanda cha Mount Meru ambacho pekee ndio kikubwa na kinanunua alizeti kwa bei ndogo kwa sababu kipo chenyewe hakuna mshindani wake, kwa hiyo bei wanayonunua alizeti kwa wakulima ni ndogo jambo linalosababisha wakulima kutokuwa na hamasa ya kutosha kulima zao hili kwa wingi.

Lakini pia kuna uhaba wa pembejeo, kuanzia kwenye mbegu bora, dawa na vifaa, ndio maana tunatoa wito kwa wawekezaji kuwekeza zaidi kama ilivyo kwenye zao la shayiri, wawekezaji wamewekeza na kuwawezesha wakulima kila kitu ila sisi hatuna hicho kitu, mkulima anajilimia tu.

RAI: Ni changamoto gani ambayo bado unaona ni pasua kichwa na huuoni uwezekano wa kuitatua haraka?

SIMA: Ni eneo moja ni la maji, ingawa si pasua kichwa kwa sababu mwanzo miradi ilipokuja haikusimamiwa vizuri, hata fedha zilipokuja kulikuwa na changamoto ya kuelewa namna ya kuzisimamia.

Ndio maana nilipochangia bungeni nilishauri hii idara ya maji iliyokuwa chini halshamauri ipelekewe wizarani jambo ambalo nashukuru waziri amelisikia na amepeleka wizarani. Kwa maana hiyo mipango tunaona ni mizuri na tatizo hili litaisha, vivyo hivyo kwenye umeme baadhi ya maeneo huku mjini hakuna miradi ya umeme, ukichilia mbali miradi ya REA vijijini. Hili nalo nililisema na nikaonana na waziri husika akanihakikisha miradi wa umeme mjini unakuja.

RAI: Unazungumziaje chaguzi ndogo za marudio zinazoendelea katika kata 79 na jimbo la Buyungu?

SIMA: Uchaguzi ni uchaguzi tu, unapoingia vitani huwa unapaswa kushindana pamoja na kwamba sasa hali halisi iliyopo nchini inatubeba CCM kutokana na uchapakazi unaofanywa na Rais Magufuli, kwamba kwenye ilani mengi yanaonekana tunavyotekeleza.

Wenzetu hawana cha kusema, mfano nina kata moja ya Unyambwa, ni imani yangu kuwa hata ukiangalia kwenye chaguzi zote tangu tuingie madarakani 2015 tumeshinda zote na hata hizi tutashinda zote. Ninatoa wito kwa wanaCCM tufanye kazi kwa sababu uchaguzi huu ndio unaonesha picha ya uchaguzi wa mwakani 2019.

RAI: Tangu alipoondolewa kwenye nafasi ya uwaziri, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), amekuwa akitoa kauli kwenye mitandao ya kijamii na hata bungeni, ambazo zinatafsiriwa kuikosoa serikali. Kwa kuwa wapo wanaounga mkono hatua hiyo na wapo wanaokosoa, kwa upande wake unafikiri ni sahihi anayoyafanya?

SIMA: Kuzungumza hilo ni ngumu kwa sababu kila mtu ana mtazamo wake, mwingine anaweza kuona anakosea au anakosoa, ila mwenye mamlaka ni chama. Sisi watu wa pembeni wote tunaweza kumuangalia kwa mtazamo kwamba labda anadhalilisha na mengine, ila chama kinatutazama wote kuwa nani anakwenda kwenye mstari sahihi au si sahihi. Kwa hiyo ataitwa kwenye vikao kama anakosea na chama kina utaratibu wake hivyo sisi hatuwezi kuanza kumshutumu mtu wakati hatuna mamlaka hayo zaidi ya chama.

RAI: Ni upi ujumbe wako kwa watanzania kwa ujumla?

SIMA: Ninaomba Watanzania kuwa tunapozungumzia mazingira na usafi ni jukumu la kila mmoja wetu na si la viongozi, kunaweza kuwa na siku ya usafi Jumatano au Jumamosi, ila siku ya usafi ni kila siku na kila mmoja atekeleze wajibu wake na watupatie ushirikiano.  Kwa sababu sasa mazingira ni ajenda ya kudumu hivyo tuchukulie mazingira kama ndio maisha yetu.