Home kitaifa MUSSA SIMA: Haikuwa kazi rahisi kumbwaga Msindai

MUSSA SIMA: Haikuwa kazi rahisi kumbwaga Msindai

2936
0
SHARE

mussaNA GABRIEL MUSHI

SINGIDA Mjini ni jimbo mojawapo lililopata bahati ya kuongozwa na mmoja wa vijana matajiri Afrika, Mohamed Dewji. Hata hivyo baada Dewji kutangaza kutogombea tena jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hali ilikuwa ngumu kwa mgombea aliyeteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Ramadhani Sima kuwaaminisha wapiga kura wa jimbo hilo kuwa sasa wapo chini ya kiongozi wa kawaida asiyekuwa tajiri kama ilivyokuwa awali.

Sima ni mmoja wa makada wa chama hicho aliyechukua nafasi ya Dewji baada ya kumbwaga mpinzani wake kutoka Chadema, Mgana Msindai.

Ikumbukwe kuwa Msindai alikuwa kada wa CCM kindakindaki na mpaka anahamia Chadema katika dakika za lala salama mwaka jana, alikuwa Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM nchi nzima.

Hata hivyo katika hali ambayo haikutarajiwa, Sima ambaye pia alikuwa Katibu wa itikadi na uenezi mkoa, alifanikiwa kumshinda bosi wake huyo ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida.

Ili kupata uhondo wa mpambano wa kisiasa katika mkoa huo pamoja na mambo mengine, RAI lilifanya mahojiano maalumu na Mbunge huyo wa CCM kama ifuatavyo.

RAI: Umefanikiwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza, nini ulichojifunza katika harakati za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana?

SIMA: Nimebaini changamoto za uchaguzi ni nyingi, lakini kwa jimbo la Singida mjini ambalo limeongozwa kwa miaka 10 na Mohamed Dewji – mtu tajiri lakini demokrasia ya nchi hii haingailii vigezo hivyo inaangalia namna gani unaweza kuperfom. Kwa kuwa demokrasia ilikuwa inaniruhusu yapo mambo ambayo nimedhamiria kuwafanyia wanaSingida ndio maana imeniwia rahisi baada ya Dewji kuamua kukaa pembeni.

Katika kura za maoni tulikuwa wagombea sita changamoto nyingine ikaibuka kwenye matokeo ambayo nilishinda kwa kura zaidi ya 6,000, mwenzangu alikuwa na kura 3000 lakini bahati mbaya sana matokeo yakatangazwa batili kuwa yule wa pili akatangazwa mshindi kwa madai kuwa naye alipata zaidi ya kura 6,000. Hali hii iliibua taharuki ndipo nikasimamia haki yangu nikaonesha ushahidi halisi ambao niliupeleka CCM mkoa hadi Taifa, ndipo wakaona ukweli wenyewe.

Nawashukuru viongozi wa juu wa CCM wakiwamo Jakaya Kikwete ambao kwa pamoja walibaini ubatili wa matokeo yaliyotangazwa na kukubaliana na ushahidi nilioupeleka pamoja na ushahidi walioupata kutoka kwa wachunguzi waliotumwa jimboni.

Pia tuliitwa sekretarieti yote tukahojiwa wakabaini kuwa ni kweli matokeo yalikuwa batili ndipo Halmashauri kuu ikanipa ushindi wangu. Kwa hiyo katika kinyang’anyiro cha kura za maoni kulikuwa na changamoto zake.

Tulipoenda kwenye uchaguzi mkuu hali ilikuwa ngumu sana kwa sababu tayari kulikuwa na makundi ambayo sasa kulikuwa na kazi ya kuyaunganisha hayo makundi.

Wenzetu Chadema walikuwa wamemsimamisha Mgana Msindai ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa, kwanza alikwenda kugombea wilaya ya Mkarama akashindwa akaamua kuhama chama akaenda Chadema ndipo akaja kugombea Singida mjini, ikumbukwe kuwa alikuwa pia Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM Tanzania.

Kwa hiyo alikuwa mtu mzito na wenzetu Chadema waliamini wameweka mtu mzito, hivyo kupambana na mtu kama yule nikaona hii ni changamoto ya tatu sasa, nikajipanga nikakaa chini kuandaa mbinu namna ya kupambana naye.

RAI: Tueleze kwa undani ni mbinu gani zilizofanikisha kumwangusha aliyekuwa Mwenyekiti wako licha ya uzoefu wake ndani ya siasa?

MSIMA: Nilijipanga kuelezea wananchi kile nitakachowafanyia… nilikaa chini nikaangalia mapungufu yake mzee wangu huyu na uwezo wake upo wapi, hivyo nikajikita kimbinu kuwaelezea nitawafanyia nini wanaSingida. Zaidi ya mikutano 70 nilihudhuria yote sikumtukana mzee yule wala kumfanyia chochote kibaya.

Matokeo yalikuwa chanya sana, sikuamini kwa sababu katika vituo 223 niliongoza vyote na katika matokeo yote 36,000 nilimpita mze wangu huyu kwani alikuwa na kura 16,000 hivyo tofauti ilikuwa zaidi ya 20,000 hakuna liyetarajia. Kimsingi tulimaliza salama mzee akakubali matokeo na sasa tumeendelea kufanya kazi.

RAI: Wananchi wa jimbo lako walikuwa na historia ya kuongozwa na kijana tajiri zaidi barani Afrika, Mohamed Dewji, licha ya umaarufu huo, unatarajia kufanya nini ili wasiione tofauti kubwa kati ya uongozi wake na wako?

SIMA: Hii ni changamoto ambayo sasa watu walizoea ni jimbo ambalo liliongozwa na mmoja wa matajiri vijana Afrika, ilikuwa ni kazi yangu sasa kuwaondoa watu wenye hali hiyo na kuwarudisha kwenye hali ya kawaida kuwa mimi si tajiri. Nikaanza kuhudhuria vikao vyote vya baraza, nikakaa na watendaji wa idara mbalimbali, serikali, manispaa, hivyo nikajifunza nikajua wapi sasa napaswa kuanzia.

Baada ya hapo nikaanza kufanya ziara kuwapa watu majibu kwenye matatizo ya maji, umeme huduma zote za kijamii, nikaandika barua Tanesco wakanijibu ambapo walinieleza namna watakavyomaliza tatizo la umeme. Walinieleza kuwa kuna umeme ambao utapitishwa na REA, vipo vijiji ambavyo vitapitiwa mradi mkubwa wa umeme wenye volti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga, pia nikawandikia barua Mkurugenzi wa SUWASA, akanielezea changamoto zilizopo. Kwa maana hiyo niliweza kutambua matatizo ni yapi na wapi tuanzie na mimi nifanye kitu gani nikiwa kama msimamizi wa wananchi.

Kwa namna ya utumishi nilikuwa nafanya kazi yangu kama inavyotakiwa, kwa sababu utumishi si kwenda Bungeni tu, lazima tuanzie kusimamia yale yaliyopo pale na yale yaliyopo ndani ya uwezo wa serikali ndipo tusimamie huko.

RAI: sasa umekuwa mbunge wao, unawaahidi nini wananchi wako wa jimbo la Singida Mjini?

SIMA: Kimsingi wananchi wangu wa Singida mjini, nawaahidi utumishi uliotukuka, mengi tumewaahidi na sasa utekelezaji wake umeanza kwa usahihi. Nilizungumza mengi na kazi yangu sasa ni kuanza kusimamia, hivyo ninaahidi utumishi uliotukuka si utukufu.

RAI: Katika chaguzi ndani ya CCM kumekuwapo na malalamiko ya rushwa, Je, unafikiri hali hii inafifisha demokrasia ndani ya chama?

SIMA: Nilikuwa Katibu wa CCM mwenezi mkoa, katika uongozi wangu nilikuwa napingana na rushwa sana kwa kuzingatia kanuni namba nne ya chama kuwa sitatoa rushwa wala kupokea. Kwenye kazi yangu ya uenezi nilitumia muda mwingi sana kuelimisha hili, kwenye wilaya zote.

Kwenye kura ya maoni haya yalijitokeza kwani baadhi ya wachache waligeuza yale matokeo kwa sababu ya rushwa. Ndiyo maana hata chama pale kwangu kiligundua hilo na kugeuza matokeo. Kwa hivyo rushwa bado ipo huku chini ndio maana ilipofikia mkoa wakagundua hilo na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na uhuru bila rushwa.

RAI: Rais Magufuli akikabidhiwa uenyekiti ataweza kumaliza tatizo hilo ndani ya CCM?

SIMA: Ninatamani hata leo apewe kwa sababu ni mtu mwenye dhamira ya dhati kuwatumikia wananchi kwani pamoja na nafasi ya urais bado anakwenda kwenye zile wizara kukagua na kugundua uchafu na ubadhirifu mbalimbali. Tunaiona dhamira na dira ya serikali kwa kile anachoonesha, anaandaa mahakama ya mafisadi, pia mirija mingi ya mfisadi imezibwa hivyo tunatarajia haya yaje kwenye chama.

Kwa hiyo ni imani yangu sasa kuwa akirudi kwenye CCM kitu cha kwanza ni kuhakikisha kuwa chama anakisafisha kama ambavyo sasa anasafisha serikali, hivyo tunatarajia ili aweze kuwa na serikali imara lazima awe na chama imara. Kama unataka kukomesha rushwa serikali lazima aanze kwenye chama chake, hivyo ni imani yangu kuwa alichokionesha huko serikali akirudi kwenye chama afanye mara tatu yake, tuwe na chama safi ambacho kitakuwa na waadilifu, naamini kutakuwa na transformation kubwa sana ya kuajiri vijana waadilifu na Magufuli atafanya hivyo.

RAI: lipo suala la utumbuaji wa majipu linalofanywa na Rais Magufuli, unafikiri lina tija kwa Taifa au linachochea hofu kwa watumishi wa serikali?

SIMA: Naunga mkono sera hii na hofu inakuja kwa watumishi kwa sababu tuliishi kwa mfumo wa kupiga dili, kutoheshimu viongozi au kuheshimu yule tu. Hofu hii inawajaa lakini kama kweli unafanya kazi kwa uadilifu huwezi kuwa na hofu, kama mtu unafanya kazi bila urasimu, bila kupiga dili huwezi kuwa na hofu. Sasa ukienda serikali unahudumiwa vizuri, mfano viongozi wa mitaa na vijiji sasa wanaheshimika.

Kwa hiyo hofu ile inawajaa kwa sababu ni watu ambao hawakutarajia hayo, lakini imani yangu ni kwamba mageuzi yoyote lazima yaache changamoto yapo makundi yatakayoumia kwa sababu walizoea kupiga ‘dili’, mfano wapo wapinzani ambao lazima wapinge chochote anachofanya vizuri lakini sasa tunaona hata wao wanamsifia Rais Magufuli.

RAI: Hivi karibuni kuliibuka vurugu Bungeni, nini ulijifunza katika mikutano ya aina ile?

SIMA: Tulikuwa bado hatujaelewa mwelekeo wa serikali, mwelekeo wa Magufuli upo vipi, ndiyo maana wale wapinzani walitoka nje alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi ila tuliporudi kujadili hotuba walirudi na tukawa wamoja, kwa sababu aligusia vitu vinavyoigusa jamii.

Kwa mara ya kwanza nilipigwa na butwaa baada ya kuona sasa wanazomea na mambo mengine, kwa kuwa sikutaka kujiingiza katika yale mazingira kwani ninasimamia kile wananchi walichonituma.

Ila wapinzani wanataka kuiaminisha jamii kuwa wao ndio wazuri siku zote wakati sisi sote ni wamoja, bado ni imani yangu kuwa tunaporudi kwenye Bunge la bajeti kama tuna dhamira ya kuinua uchumi wa Tanzania sasa tuwe wamoja.

RAI: Mschi 20, mwaka huu kulifanyika marudio ya uchaguzi Zanzibar, unadhani utasaidia kutatua mgogoro wa kisiasa Visiwani humo?

SIMA: Kimsingi kama mwanasiasa suala la Zanzibar, kwa jinsi ninavyoelewa kwanza huwa ninawaamini sana huwa sishawishiki kuingilia kwa sababu mpaka kuamua kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa walikubaliana wenyewe. Kwa miaka mitano hapakuwa na lakini baada ya uchaguzi mkuu pakawepo na mgogoro sasa wameipata serikali mpya ni imani yangu wazanzibar kwa namna wanavyokwenda mpaka kuendelea watakuwa wamoja na serikali yao nzuri kwa masilahi ya watanzania wote… bado naamini Wazanzibar watarudi na kuendelea kwa pamoja, tuwaombee waendelee kuishi kwa amani.

RAI: Wewe ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na mazingira, umejipanga vipi kumsaidia Rais Magufuli atimize lengo la kuwa Tanzania ya viwanda?

SIMA: Ni kweli tuna malengo ya kufikia nchi yenye uchumi wa kati au viwanda. Tumeanza kazi hii kwa muda mfupi sasa tunasikia presentation za mashirika mbalimbali. Kazi wanazofanya tuna kila sababu ya mashirika haya kubadilika kwani Magufuli anategemea tumsaidie kufikia malengo haya ambayo watanzania wanaamini. Mfano Kituo cha Uwekezaji (TIC) inabidi wakae sawa kwa sababu katika taarifa waliyotoa inaonesha miradi zaidi 1,500 lakini inayofanya kazi ni mitano tu kwa miaka 10, hivyo lazima wajipange upya na mkurugenzi Julieth Kairuki alikiri hivyo ameenda kuiandaa taarifa upya.