Home Habari Mutungi aiweka njia panda ACT-Wazalendo

Mutungi aiweka njia panda ACT-Wazalendo

370
0
SHARE

Na LEONARD MANG’OHA

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ameendelea kukiweka njia panda chama cha ACT-Wazalendo, kwa kutoweka wazi hatima ya chama hicho baada ya kutekeleza agizo la kukitaka kijieleze. RAI linaripoti.

Machi 25, mwaka huu ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilipeleka kwa uongozi wa ACT-Wazalendo ikieleza nia yake ya kukifutia usajili chama hicho kwa mkadai ya kukiuka sheria ya vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na kuchoma moto bendera ya chama cha Wananchi- CUF.

Ofisi ya Msajili ilitoa siku 14 kwa chama hicho kuhakikisha kinajitetea kabla ya uamuzi huo kuchukuliwa, agizo ambalo lilitekelezwa haraka na uongozi wa ACT-Wazalendo.

Tangu kujibiwa kwa barua hiyo kumekuwa na ukimya unaotafsiriwa kama hatua ya kukiweka njia panda  chama hicho ambacho katika siku za karibuni kimepata idadi kubwa ya wafuasi Zanzibar.

Mwanzoni mwa wiki hii RAI lilizungumza na Msajili wa Vyama  vya Siasa, Jaji Mutungi ili kujua hatma ya ACT-Wazalendo baada ya ofisi yake kuonesha nia ya kukifuta chama hicho.

Akizungumzia suala hilo Jaji Mutungi alisema kamwe ofisi yake haifanyi kazi kwa kushawishiwa ama kushinikizwa na mtu yeyote badala yake wanaangalia namna sahihi ya kushughulikia mambo kwa nia ya kukwepa kufanya makosa katika uamuzi wowote watakaoutoa.

Alisema kitu chohote kinachopokelewa ofisini kwake kinafuatilia, kinachunguzwa na baada ya kujiridhisha na hatua zote hizo ndipo wanatoa taarifa katika muda mwafaka na si kufanya vitu kutokana na  presha ya mtu au vyombo vya habari.

“Sisi tunaendelea na taratibu zetu, bado tunalishughulikia suala hilo, ni ajabu sana kuona vyombo vya habari vinatufuata tutoe maelezo, mimi najitahidi sana kutafuta lugha nyepesi kusudi mnielewe ili isifike mahali muandike vichwa vyenu vya habari ambavyo mnataka nyie.

“Sisi hatutaki tufanye kitu kutokana na  ‘presha’ (shinikizo), najua ninyi mnauliza kwa sababu umma unataka kujua, lakini msubiri, msije mkashangaa uamuzi wa jambo hili  ukachukua hata miezi mitano au sita.

“Nia yetu ni kuepuka kufanya  makosa katika maamuzi tunayoyatoa, hicho  ndicho ninaweza nikasema. Mimi ninaomba mheshimu taratibu zetu kwa sababu sisi bado tunafanyia kazi, wakati mwafaka ukifika sisi wenyewe tutawaita.

“Najua tukiyaingiza kwenye vyombo vya habari mnakaribisha watu kutoa hoja, mnakaribisha pia watu kusema, hatupendi tufike mahala waseme hawa walishawishiwa na vyombo vya habari ndiyo maana wakatoa maamuzi ya namna hii,” alisema Jaji Mutungi.

ZITTO ANENA

Mapema wiki hii Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alioneshwa kushangazwa na ukimya wa ofisi ya Msajili juu ya suala lao.

Alisema pamoja na kuwasilisha barua yao ya utetezi ndani ya muda uliotolewa na ofisi ya Msajili, hakuna majibu yoyote waliyopatiwa.

SABABU YA KUPEWA BARUA

Tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi-CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ajiunge na ACT-Wazalendo, Machi 18 mwaka huu, kumekuwa na kauli,maagizo, maonyo na matamko dhidi ya chama hicho. 

Miongoni mwa hayo ni barua ya Machi 25 mwaka huu iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikionesha nia ya kukifutia usajili usajili wa kudumu chama hicho kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa.

Chama hicho kilitakiwa kujieleza ni kwanini kisifutiwe usajili kutokana na kukosa sifa kwa kukiuka Sheria pamoja na kushindwa kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa fedha ya mwaka 2013/2014, zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Taarifa hiyo ya Msajili ilidai kuwa chama kutowasilisha ripoti kinakiuka sura ya 258 ya sheria ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Barua hiyo ilieleza kuwa: Baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kesi Na. 23 ya mwaka 2016, iliyokuwa inahoji uhalali wa Profesa Ibraimu Lipumba, Machi 18 mwaka huu, kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa sheria ikiwamo kuchoma moto bendera za CUF, uliofanya na mashabiki wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, wanadai sasa ni wanachama wa ACT. Kitendo cha kuchoma bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C, cha sheria ya vyama vya siasa.

“Vile vile katika mitandao ya kijamii imeonekana video watu wakipandisha bendera ya ACT kwa kutumia tamko takatifu la dini ya kiislamu (Takbir), kitendo hiki pia ni kukiuka kifungu cha (9) (1) (c) cha Sheria ya Vyama vya Siasa inayokataza kuwa na ubaguzi wa kidini kwa wanachama wake na kifungu cha (9) (2) (a), kinachokataza katiba, sera au vitendo vya chama cha siasa kuhamasisha au kueneza dini fulani,” imesema taarifa hiyo ya msajili.

“Kutokana na maelezo hayo, vitendo hivyo vinaakisi ukiukwaji wa dhahiri wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambao pia unasababisha chama chenu kupoteza sifa za usajili wa kudumu.

“Hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa anatumia fursa hii kukufahamisha wewe na wanachama wa ACT-Wazalendo nia yake ya kufuta usajili wa kudumu wa chama chenu kwa sababu hizo zilizotajwa,” alisema Msajili katika taarifa yake.

MAJIBU YA ACT-WAZALENDO

Mara baada ya kupokea barua hiyo uongozi wa chama hicho ulikutana na waandishi wa Habari na ndipo hapo, Zitto aliposema kuwa madai ya kutowasilisha hesabu za mwaka 2013/14 hayana ukweli wowote.

Zitto alisema wajibu wa chama cha siasa ni kuwasilisha hesabu zake kwa CAG na kwamba hesabu za mwaka 2013/14 ziliwasilishwa kama walivyotakiwa ila kilichotokea ni kuwa chama hicho kilipata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 ikiwa ni miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha kuisha Juni 30, mwaka huo na kulazimika kuwasilisha taarifa hizo katika taarifa ya ukaguzi ya mwaka 2014/2015.

“Sheria inaruhusu kufanya hivi hata kwa miezi 18 na kabla ya kufanya hivyo tulimwandikia Msajili wa vyama vya siasa barua ya Januari 22 na 29, 2015 na tukajibiwa, barua zote tunazo.

“Msajili angekuwa na nia njema angeweza kuuliza, labda barua zilipotea ofisini kwake tungempa kwa sababu tunazo na sheria ya vyama vya siasa iliyopitishwa hivi karibuni inampa mamlaka ya kuomba nyaraka zozote, tungempa” alisema Zitto.

Kuhusu kuchoma bendera za CUF Kabwe alidai kuwa hata msajili mwenyewe alionyesha hana uhakika kama kweli waliofanya hivyo ni wanachama wa ACT-Wazalendo na kwamba msajili alipaswa  ajiridhishe anaowatuhumu ni wanachama wa ACT-Wazalendo.

Alisema kuhusu matumizi ya neno takbir, kuwa ni jambo lililowashangaza, kwa sababu chama hicho ni chama cha watu wote ikiwamo wenye dini na wasiokuwa na dini na kwamba kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho imeonesha wazi kuwa hawafungamani na dini yoyote ndiyo maana wameruhusiwa kufanya shughuli za siasa.

“Tunafahamu Watanzania wana dini zao, maneno yao ya kawaida kutumika hayana maana ya udini, viongozi wote hufungua hotuba zao kwa kusema bwana Yesu asifiwe, tumsifu Yesu Kristo na Assalam aleykum, hatuamini kama kusema hivyo ni udini” alisema Zitto.