Home Makala Muujiza wa Mohamed Atta—5

Muujiza wa Mohamed Atta—5

1217
0
SHARE

Na William Shao

WTCKATIKA mfululizo ma makala hizi, tumeona kuwa aliyedaiwa kuwa kiongozi wa ugaidi wa Septemba 11, 2001, Mohamed Atta, huenda hakushiriki kwa namna yoyote katiia ugaidi ule. Uchambuzi makini unaweza kuonesha jambo hilo.

Turudi pale ilipoanzia sura hii. Mashirika ya ndege ya American Airlines na United Airlines ambayo ndege zake zilihusika katika mashambulizi ya ‘kigaidi’ nchini Marekani Septemba 11, 2001 yalitoa orodha ya abiria wa kila ndege iliyotekwa siku hiyo.

Hakuna orodha hata moja kati ya zilizotolewa na mashirika hayo iliyokuwa na hata moja ya majina yaliyokuwa katika orodha ya ‘magaidi’ iliyotolewa na FBI. Isitoshe, katika orodha hizo, hakukuwa na hata jina moja la Kiarabu.

Kama hakukuwa na hata jina moja la Kiarabu, basi hakukuwa na Mwarabu hata mmoja katika ndege zile. Inashangaza kusikia kuwa walioteka ndege zile ni Waarabu.

Ukweli unabaki wazi. Tazama! Ndege nne zinatekwa katika ardhi ya Marekani, katika muda wa ndani ya saa moja, kutoka katika viwanja vitatu vya kimataifa vya nchi hiyo, zikasababisha madhara makubwa kiasi kile, na bado hakuna chochote kilichofanywa na Mamlaka ya Anga ya Marekani (FAA—Federal Aviation Administration) na Mamlaka ya Ulinzi wa Anga la Amerika ya Kaskazini (NORAD), ambazo zina mfumo wa kuitika haraka na kutenda kazi haraka sana mara inapogundulika kuwa mambo si shwari katika anga ya Marekani?

Ni kweli kwamba The Pentagon au serikali yenyewe ya Marekani ilishtukizwa sana kiasi kwamba haikuweza kufanya lolote? Zaidi ya yote hayo, hakuna usahidi wowote unaothibitisha kuwa “watekaji 19 wa Kiarabu” wanaodaiwa kuteka ndege zile walikuwa katika ndege hizo. Huenda “watekaji 19” ni utunzi ulioandaliwa vyema lakini ukakosa viungo muhimu vya kuufanya uaminike.

Kuamini jambo lolote unaloambiwa kunategemea mambo mengi—miongoni mwa hayo ni yule anayekuambia, jinsi anavyokuambia na namna unavyolipokea.

Kama nilivyoeleza mwanzoni mwa mfululizo wa makala haya, mwanadamu aliyenivutia zaidi katika hadithi ya Septemba 11 si Osama bin Laden, George W. Bush, Collin Powell, Condoleeza Rise wala Robert Mueller, bali ni Mohamed el-Amir Awad el-Sayed Atta, ambaye FBI waliiambia dunia kuwa ndiye aliyekuwa kiongozi wa utekaji na ugaidi wa Septemba 11.

Siku moja baada ya Atta kudaiwa kuonekana akiwa baa mjini Florida, ilidaiwa kuwa mwanadamu mmoja anayefanana na mtu wa kutoka Mashariki ya Kati, yaani Mwarabu, aliingia katika mnara wa kuongozea ndege wa Uwanja wa Ndege wa Logan ulioko Boston, Marekani, kisha akazungumza maneno fulani. Iliaminika—na hii iliaminika tu—kuwa mtu huyo ni Atta. Haukuwahi kutolewa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai hayo. Hata kama hujawahi kufika Marekani, ukichunguza sana madai hayo, muda unaotajwa, jiografia ya Marekani na matukio mengine, utaishuku taarifa hiyo.

Ikiwa  mtu huyo “wa kutoka Mashariki ya Kati” alikuwa Mohamed Atta, aina yoyote ya usafiri aliotumia kutoka Florida, alikokuwa baa akinywa vodka, hadi Boston—iwe ni wa ndege au wa gari—ulikuwa na kasi ya ajabu sana.

Kama ni kweli alikuwa Florida hadi saa moja jioni, kwa mujibu wa Tony Amos, meneja wa baa ya Shuckums Oyster, na bado kesho yake akawa Boston, basi haiwezekani kwamba alitumia gari, bali ndege, jambo ambalo nalo linatia shaka.

Lakini kama kweli alitumia ndege, maelezo ya tiketi yake hayajawahi kutolewa kama ushahidi wa madai hayo. Pia inadaiwa kuwa gari alilolikodisha kutoka kampuni ya Warrick Rent-A-Car alilirudisha kesho yake, Septemba 9, 2001.

Kwa hiyo kama huyo anayetajwa ni Atta, lazima iwe kwamba alikuwa Florida (baa) Septemba 7 hadi saa moja jioni, kisha akasafiri kwa ndege kutoka Florida kwenda Boston kesho yake, Septemba 8, akaenda kwenye mnara wa kuongozea ndege wa Uwanja wa Ndege wa Logan, Boston, akasema maneno aliyosema, kisha akapanda ndege na kurudi Florida siku hiyo hiyo au labda kesho yake, Septemba 9, na siku hiyo hiyo akarejesha gari alilokodi.

Baada ya hapo akapanda tena ndege na kwenda Boston kwa mara nyingine na kukodi gari jingine ambalo alilitumia kwenda Portland, Maine. Kama yote haya yalifanyika, basi anayetajwa ni Atta. Lakini ni vigumu sana kukubali kwa sababu hii si hadithi inayokaribia kufanana na jambo lisilowezekana, bali ni jambo lisilowezekana.

Saa chache kabla ya mtu huyu “wa kutoka Mashariki ya Kati” aliyedhaniwa kuwa ni Atta kuonekana katika mnara wa kuongozea ndege katika uwanja huo, ilisemekana kuwa watu wanne wanaofanana na watu “wa kutoka Mashariki ya Kati” walimuuliza mwongoza ndege mmoja namna ambavyo wangeweza kuingia katika mnara huo.

Haijulikani wangepata nini kwenye mnara huo kama watu hao wangeingia, au kama waliingia. Kama hilo ni la kweli, haijulikani watu hao “wa kutoka Mashariki ya Kati” wangefaidikaje na kuingia kwao katika mnara huo, na pia haijulikani hiyo ingewasaidiaje katika kuteka ndege siku chache tu baadaye.

Kama kweli walikuwa ni watu “wa kutoka Mashariki ya Kati”—pengine akiwamo Atta—hakuna faida yoyote ambayo wangeipata kwa kutaka kuingia kwenye mnara huo. Sana sana kitendo hicho kingewafanya watu wawashuku na hivyo kuharibu mpango mzima wa utekaji wao ambao inadaiwa waliuandaa kwa miaka kadhaa.

Watekaji makini wasingefanya kosa kama hilo. Lakini kwa kuwa hadithi hiyo ilitumiwa ili kuonesha kuwa ni kweli kulikuwa na watu “wa kutoka Mashariki ya Kati” walioonekana wakifanya kama FBI walivyosema, basi ingesaidia zaidi kuwafanya watu waamini kuwa ni kweli waliofanya kitendo hicho ni watu “wa kutoka Mashariki ya Kati”.

Katika watu hao, Atta, ambaye alitumiwa katika hadithi hiyo kuwa ndiye aliyekuwa kiongozi wa ‘ugaidi’ huo, alihusishwa katika kila kitendo kiovu kilichoweza kupatikana au kudhaniwa ili ikubalike katika akili za watu kwamba kweli yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa watekaji wale. Jambo lolote ambalo ‘watekaji’ hawangetaka liwatokee ni kutiliwa shaka kabla hawajatekeleza mipango yao.

Kwa hiyo kama ungetaka hadithi yako iaminike kuwa Waarabu ndio waliofanya kitendo kile, ungeanza kutengeneza hadithi nyingine zikiwa na dondoo ambazo zikiunganishwa pamoja zitaweza kumfanya mtu asadiki kuwa watu “wa kutoka Mashariki ya Kati”, ambao ni Waarabu, ndio waliohusika.

Na kwamba kitendo cha kutaka kuingia katika mnara wa kuongozea ndege kilifanyika katika uwanja ule ule ambao ndege mbili zilizotekwa siku ile zilipaa ni mojawapo ya dondoo ambazo baadaye zingesaidia kuifanya hadithi ya watu “wa kutoka Mashariki ya Kati” iaminike.