Home Makala Mvutano baina ya Boris, EU unavyokwamisha mchakato wa Brexit

Mvutano baina ya Boris, EU unavyokwamisha mchakato wa Brexit

429
0
SHARE

FARAJA MASINDE NA MASHIRIKA

MPANGO wa nchi ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) sasa ni kama umekwaa kisiki, hii ni baada ya EU kusogeza muda wa hadi Januari mwaka 2020.

Mapema wiki hii, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson alijaribu tena kurusha karata yake ya kusaka uungwaji mkono kuhusu uchaguzi wa Desemba mwaka huu ili kuokoa mchakato wa nchi hiyo kujiondoa EU ambao umeahirishwa kwa mara ya tatu sasa.

Baada ya nakala inayoitisha uchaguzi wa wabunge Desemba 12 mwaka huu,  kukataliwa na Baraza la Wawakilishi, Boris alitangaza kwamba anaandaa kura mpya kuhusu kufanyika kwa uchaguzi wa mapema. 

Kiongozi huyo aliyerithi mikoba ya Theresa May, ana imani kwamba kupitia uchaguzi huo atakuwa na wabunge wengi ambao watamwezesha kutimiza ahadi yake ya kutekeleza mchakato wa Brexit, ikiwa ni miaka mitatu na nusu baada ya kura ya maoni ya mwaka 2016.

Shinikizo hilo la Boris la kutaka kuiona Uingereza ikijiondoa katika umoja huo wa Ulaya limekuwa na presha kubwa kwake, hatua ambayo imemfanya ajiapize kuwa yuko tayari kujitoa uhai iwapo mchakato huo utashindwa kukamilika.

Katika moja ya kauli zake za hivi karibuni, Boris aliahidi kuwa ni lazima ataiondoa nchi hiyo kwenye umoja huo huku akisisitiza kuwa atafanya hivyo ‘kwa mbinu yoyote ile’ na kwamba heri afe chini ya shimo kuliko kuomba kusitishwa kwa mchakato huo.

MSIMAMO WA EU

Hata hivyo upande wa EU, Jumatatu ya wiki hii umekubali kuchelewesha kwa muda wa miezi mitatu Uingereza kujitoa kutoka Umoja huo hadi Januari 31, mwakani.

Kauli hiyo ya EU ilikuja ikiwa ni siku chache tu kabla ya kufikia leo Oktoba 31  ambayo ndiyo ilikuwa tarehe ya mwisho ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya, hata hivyo kwa maneno mengine unaweza kusema kwamba mchakato wa Brexit bado haujulikani mwelekeo wake.

Hayo yanajiri wakati wanasiasa wa Uingereza wakiwa hawako karibu ya kufikia muafaka juu ya vipi, lini na hata iwapo hatua ya kuachana na EU itawezekana. 

Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yamefikia makubaliano Jumatatu wiki hii kuchelewesha Brexit hadi Januari 31, mwakani pamoja na uwezekano wa Uingereza kujitoa mapema iwapo Bunge la Uingereza litaidhinisha makubaliano ya kujitoa.

Awali kabla ya uamuzi huo wa EU kuipa miezi mitatu Uingereza, mabalozi kutoka mataifa ya EU wamekutana Jumanne hii, kujadili hatima ya Uingereza katika umoja huo na kuamua nchi hiyo iongezewe muda gani, ili wabunge wapitishe mapendekezo mapya ya kujiondoa kwenye umoja huo.

Hata hivyo ripoti za awali tayari zilishaonyesha kuwa baadhi ya mabalozi hao, wanataka Uingereza ipewe muda wa miezi mitatu fununu ambazo hatimaye zilikwa kweli.

Kauli ya Boris kuhusu uchaguzi, alisema iwapo wataongezewa muda hadi Januari mwaka 2020, ataitisha Uchaguzi Mkuu wa mapema.

Boris bado anaendelea kusisitiza kuwa anataka Uingereza iondoke kwenye umoja huo ifikapo Oktoba 31 mwaka huu.

Boris alisema uchaguzi unaweza ukahitajika kama kuondoa mkwamo wa Brexit, lakini chama cha upinzani cha Labour kilitaka kujadiliwa kwanza kwa tarehe ya mwisho ya Brexit ambayo ni Oktoba 31.

Sasa ni wazi kuwa Boris atashinikiza kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu baada ya mapendekezo hayo.

Hata hivyo hali bado ni tete kwa waziri huyo kwani wabunge wamekuwa wakigomea mapendekezo yake ya kutaka mkataba mpya kujadiliwa haraka na kutiwa saini baada ya siku tatu, huku yeye akiwalaumu wabunge kama chanzo cha kukwamisha mpango huo.

“Nasikitika kuwa wabunge wamepiga kura kuchelewesha kujiondoa kufikia Oktoba 31 na mkataba, sasa lazima serikali iendelee kuweka mikakati ili kuwa tayari iwapo hakutakuwa na mkataba.

“Lakini pia nitazungumza na wakuu wa EU kusikia wanavyowaza, lakini niseme kuwa sera yetu ni kuwa tusichelewe na tuondoke ifikapo tarehe 31,”alisema Boris.

ONYO LA EU

Awali, Rais wa Halmashauri Kuu ya EU, Jean-Claude Juncker, alionya juu ya kutokea hali tata zaidi iwapo wabunge wa Uingereza watashindwa kupigia kura mkataba wa Brexit uliopatikana kwa njia ngumu. 

Makubaliano hayo yamepatikana baada ya takribani miaka mitatu ya kuvutana na wiki kadhaa kabla ya muda, uliokuwa umewekwa kama wa mwisho wa Oktoba 31 kwa Uingereza kujiondoa katika EU Ulaya. 

Hayo yalijiri huku viongozi wa EU wakiwa mbioni kuidhinisha bajeti ya muda mrefu ya umoja huo katika siku ya pili ya mkutano wao wa kilele mjini Brussels, huku kukiwa na hali ya kutoelewana kuhusu jinsi ya kushughulikia ufadhili unaohusiana na suala la Brexit huku kukiwa na masuala mapya yanayopaswa kupewa kipaumbele kama uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi.

Ikumbukwe kuwa katikati ya mwezi huu, Boris, alituma barua tatu kwa EU baada ya Bunge la Uingereza kupiga kura ya kuchelewesha kuufanyia uamuzi mpango wake wa Brexit. 

Barua ya kwanza kutoka kwa Boris ilitumwa kwa Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk. 

Barua hiyo ambayo haikutiwa saini na Boris ilikuwa ni nakala ya rasimu iliyomo katika sheria za Uingereza inayomlazimu waziri mkuu kuomba kurefushwa muda wa mchakato wa Brexit.

Barua ya pili iliyopelekwa kwa EU ni kuhusu pingamizi la waziri mkuu huyo wa Uingereza dhidi ya kurefushwa muda wa Brexit. 

Boris alisema katika barua hiyo kuwa kurefushwa muda wa mazungumzo ya mchakato wa Brexit litakuwa ni kosa kubwa, huku barua ya tatu ikitoka kwa Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, Tim Barrow na kupelekwa kwa jumuiya hiyo ya EU kwa niaba ya Boris. 

Ujumbe wa Boris uliomo kwenye barua hiyo iliyochapishwa kwenye Twitter na mwandishi mmoja wa gazeti la Financial Times mjini Brussels ulisomeka kuwa;

“Nimeweka wazi tangu nilipochukua madaraka ya Uwaziri Mkuu na nimerudia hayo kwa wabunge siku ya Jumamosi kwamba maoni yangu na msimamo wa serikali yangu, kuhusu kuongeza muda zaidi wa mchakato wa Brexit kutaharibu masilahi ya Uingereza na ya washirika wetu wa EU na kwamba hatua hiyo itavuruga uhusiano kati yetu,”ilisema sehemu ya barua hiyo.

Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk alithibitisha kupokea barua ya maombi ya kurefushwa mchakato wa Brexit na kusema kuwa ataanza kujadili suala hilo na viongozi wa EU. 

Lakini wakati mambo yakiwa hivyo, maelfu ya watu wameandamana mwezi huu mjini London, wakitaka kura nyingine ya maoni kuhusu nchi hiyo kujitoa kwenye EU. 

Waandamanaji hao walisherehekea pia hatua ya bunge la nchi hiyo, kupiga kura ya kuahirisha kwa muda mchakato wa Brexit. 

Wengi wa waandamanaji hao walisafiri umbali mrefu kutoka maeneo mbalimbali ya Uingereza hadi jijini London kushiriki kwenye maandamano hayo. 

Uingereza ilitangaza mchakato huo wa kujitoa kwenye umoja huo wa Ulaya Machi mwaka 2017, huku ikitoa sababu mbalimbali.

Hata hivyo kupitia mchakato huo tayari viongozi mbalimbali wameachia ngazi wakiwamo viongozi wa juu wa Serikali kwa maana ya Waziri Mkuu, David Cameroon na Theresa May.

Mwisho