Home Makala Mwaka 2019 nanyanja ya siasa

Mwaka 2019 nanyanja ya siasa

862
0
SHARE

Na FARAJA MASINDE

MWAKA 2019 uko ukingoni kwani umebakiza siku chache tu kuingia mwaka mpya wa 2020. Hata hivyo niwazi kuwa mwaka huu utasalia kukumbukwa kwa matukio mengi ya kisiasa katika pemmbe zote za dunia.

RAI limekuchambulia baadhi ya matukio hayo ambayo kwa mwaka huu yameweza kutikisa kwa kiwango cha juu nyanja hii ya siasa ndani na nje ya Tanzania.

Kwa kuanzia Tanzania kwa ufupi kubwa ni kufanyika kwa Mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Agosti 17 na 18 utaendelea kubaki kama kumbukumbu muhimu za mwaka huu ulipowakutanisha viongozi wakuu wa mataifa 16 yanayounda jumuiya hiyo.

Licha ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo pia ilishawishi kupitishwa kwa lugha ya Kiswahili kupitishwa kuwa miongoni mwa lugha rasmi zitakazotumika katika jumuiya hiyo.

Rais Dk. John Magufuli aliyepokea uenyekiti wa SADC alisema kitendo cha kukifanya Kiwashili kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo ni heshima kubwa hasa kwa mwasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyejitolea upendo wake si tu kwa Watanzania bali hata watu wa nchi jirani na Afrika kwa jumla.

Mbali ya mkutano wa SADC, mwaka huu pia Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 34 zikiwamo tano zinazounda jumuiya ya Nordic inayojumuisha Sweden, Norway, Finland, Denmark na Iceland ukiwa ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika.

Katika mkutano wa mwaka huu nchi hizo zijadili namna ya kuimarisha uhusiano wenye tija kwa maendeleo ya nchi washiriki hususani katika sekta ya biashara na uwekezaji kwa maendeleo pamoja na kukuza ushirikiani katika masuala ya ulinzi na usalama.

ZIARA ZA VIONGOZI   

Pia Tanzania iliwapokea wageni mbalimbali kwa ziara za kikari na kirafikiwa ambapo Mnamo Julai mwaka huu Rais Dk. John Magufuli alimpokea Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alimpomtembelea mapumzikoni nyumbani kwake Chato mkoani Geita ikiwa ni ziara ya kihistoria kwa marais walio madarakani kutembeleana nyumbani.

Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine wawili hao walihimiza kuendeleza kushirikiana na kulinda uhusiano wenye historia kubwa baina ya nchi hizo na kuwataka wananchi wa mataifa hayo kutokubali kulaghaiwa na kupotoshwa kwa maneno yasiyofaa yanayolenga kuwatenganisha. 

Ziara hiyo ilifanyika kipindi ambacho Mbunge wa Starehe Kenya, Charles Njagua maarufu kama Jaguar, alitoa kauli za kuwataka Watazania wanaoishi na kufanya biashara nchini humo kuondoka ndani ya saa 24 la sivyo watachukuliwa hatua jambo lililozua mvutano.

Mwaka huu pia Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, alifanya ziara ya siku mbili nchini  akisema ina lengo la kuzungumza na Rais Magufuli juu ya kufikia amani ya kudumu nchini DRC. 

Pia aliwashukuru walinda amani wa Tanzania wanaohudumu nchi yake chini ya mpango wa kikosi cha Umoja wa mataifa Monusco.

Rais Magufuli alimuhakikishia Rais Tshisekedi kuwa Tanzania itayaondoa majeshi yake ya walinda amani kutoka DRC mara amani ya kudumu itakapopatika na katika nchi hiyo.

Aidha, Agosti 14 na 15 Tanzania ilimpokea Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliyekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mwaliko wa mwemyeji wake Rais Dk. Magufuli. 

Ziara hiyo ya Ramaphosa ililenga kukuza ushirikiano katika masuala ya uchumi, siasa, utamaduni na kijamii kati ya nchi hizo. 

Ziara hiyo iliambatana na kuhudhuria mkutano wa 39 SADC uliofanyika nchini siku tatu baadaye. 

LOWASSA AREJEA CCM

Machi Mosi mwaka huu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alichukua nasafi katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania pale alipotangaza kurudi rasmi CCM baada ya kuwa nje ya chama hicho karibu miaka minne tangu alipokihama na kujiunga na Chadema.

Lowassa alihama CCM baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kupitisha mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015, katika Uchaguzi Mkuu uliomweka madarakani Dk. John Magufuli.

RAIS ZUMA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Mwaka huu pia imeshuhudiwa kufikishwa katika Mahakama ya Juu ya Afrika Kusini Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma, kutoa utetezi wake dhidi ya tuhuma za rushwa na ufisadi zinazomkabili.

Tuhuma hizo zinadaiwa kutendwa na Zuma alipokuwa Rais wa Taifa hilo lenye uchumi imara zaidi barani Afrika, tuhuma ambazo yeye mwenyewe anadai kuwa ni njama zilizokuwa na lengo la kumwondoa katika ulimwengu wa siasa.

Zuma anakabiliwa na mashtaka dhidi ya rushwa, udanganyifu na kujitajirisha kinyume cha sheria kwa kufanya biashara ya mauzo ya silaha akiwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo katika miaka ya 1990, ambapo anashutumiwa kupokea rushwa kutoka katika kampuni moja ya Ufaransa ya Thales ili kuipa mkataba wa mauzo ya silaha uliokamilishwa mwaka 1999.

Zuma anatuhumiwa kushawishi baraza la mawaziri kumpatia mkataba huo wenye faida kubwa unaohusiha familia ya Gupta. 

vilevile kiongozi huyo anatuhumiwa kupokea rushwa katika kampuni inayoendeshwa na familia ya Watson.

Tuhuma hizo ndizo zilizotoa msukumo kwa Zuma kujiuzulu wadhifa wake wa urais Februari mwaka jana, na nafasi hiyo kuchukuliwa na Cyril Ramaphosa.

Zuma Anadai kuwa shirika la upelelezi la kigeni liko nyuma ya sakata hilo kwa lengo la kumtoa kumchafua na kwamba amejihakikishia kuwa anatuhumiwa yeye ni mfalme wa rushwa. Anadai kuwa licha ya kupewa majina ya watu waliopanga njama hizo ingawa hakufuatilia zaidi kuhusu sakata hilo.

KUONDOKA IKULU BOUTEFLIKA 

Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika

Mapema mwanzoni mwa mwaka huu Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika, alilazimika kujiuzulu wadhifa wake wa urais baada ya kuhudumu kwa miaka 20 kuanzia mwaka 1999.

Uamuzi huo wa kujiuzulu ulitokana na maandamano ya  wiki kadhaa ambapo Makundi ya vijana waliandamana kupinga utawala wake wakitaka mfumo mpya wa Serikali huku kukiwa na madai kuwa kiongozi huyo alikuwa anatumiwa na makundi vya kisiasa, biashara na maofisa wa jeshi.

Msukumo mwingine wa kumtaka kuondoka madarakani ulitoka kwa jeshi la nchi hiyo Jeshi la lililomtaka kiongozi huyo mwenye miaka 82 kutangaza kuwa hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya uongozi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa Kiharusi kwa muda mrefu huku akiojitokeza hadharani mara chache.

KAULI YA KIBAGUZI YA JAGUAR

MBUNGE WA Jimbo la Starehe nchini Kenya, Charles Njagua

Julai mwaka huu MBUNGE WA Jimbo la Starehe nchini Kenya, Charles Njagua maarufu kama Jaguar, alitoa kauli ya kibagizi kwa wafanyabiashara wa kigeni wakiwamo Watanzania kuondoka nchini humo vinginevyo wataondolewa kwa kipigo jambo lililochochea hisia miongoni wa nchi zenye raia wake nchini humo ikiwamo Tanzania.

Mbunge huyo aliipa serikali ya nchi hiyo muda wa saa 24 kuhakikisha inawaondoa na kuwarudisha kwao wafanyabiashara wote wa kigeni waliopo kwenye jimbo lake, wakiwemo Watanzania.

Njagua alisema kama Serikali ya Kenya itashindwa kufanya hivyo, atashirikiana na wananchi wa jimbo hilo kuvamia maduka ya wafanyabiashara hao na kuwatoa kwa nguvu, ikiwemo kipigo na kuwapeleka uwanja wa ndege ili serikali iwarudishe kwao. Moja ya sababu zilizomfanya mbunge huyo kutoa kauli za chuki dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni ni kwamba wananchi wa jimbo lake hawana uwezo wa kushindana kibiashara na wafanyabiashara hao kutoka Tanzania, Uganda, China na mataifa mengine.

Baadaye Serikali ya Kenya kupitia kwa Msemaji wake, Kanali mstaafu Cyrus Oguna, ilisema inalaani matamshi ya mbunge huyo na kuwataka wafanyabiashara wa kigeni kuwa watulivu na kuendelea kufanya biashara zao, kwa kuwa serikali inawahakikishia usalama wao na wa biashara zao. 

Oguna kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema kauli za kibaguzi hazina nafasi katika mazingira huru ya utandawazi, lakini pia ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Kenya.

“Mara nyingi Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akisisitiza kuhusu dhana ya uwazi na ukaribishaji kwa Waafrika wenzetu na jumuiya ya kimataifa kuitembelea nchi yetu, kushirikiana na Wakenya na kuwekeza kwa uhuru nchini mwetu,” ilieleza taarifa hiyo.

Kutokana na kauli hiyo mbunge huyo alikamatwa na polisi na kuwekwa rumande kwa siku kadhaa akituhumiwa kwa kauli hiyo ya chuki na ya kibaguzi.

UCHAGUZI AFRIKA KUSINI

Mei 8, mwaka huu Afrika Kusini ilifanya uchaguzi wake Mkuu ambapo Rais Cyril Ramphosa aliibuka kidedea nachama chake cha African National Congress (ANC), licha ya kwamba alikuwa akikabiliwa na ushindani mkali kufuatia changamoto zinazolikabili taifa ahilo ambazo zilitumika kama fimbo na wapinznai wake.

Baadhi ya changamoto hizo zilikuwa ni, ukosefu wa ajira, umiliki wa ardhi,  kukosekana kwa usawa.

KIFO CHA MUGABE

Robert Mugabe

Septemba 6, mwaka huu, Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe alifariki dunia akiwa na umri w amiaka 95.

Mugabe alikuwa nchini Singapore akipokea matibabu kwa muda mrefu.

Kiongozi huyo aliiongoza Zimbabwe kutoka 1980 mpaka 2017, alipong’olewa madarakani na makamo wake kwa msaada wa Jeshi.

UCHAGUZI MKUU UINGEREZA

Desemba 12, mwaka huu Uingereza ilifanya uchaguzi wake mkuu wa Waziri Mkuu pamoja na wabunge ambapo katika uchaguzi huo, Kiongozi wa chama cha Conservative, Boris Johnson alirejea kwenye wadhfa wake baada ya kumshinda mpanzani wake,Jeremy Corbyn wa chama cha Labour.

Katika uchaguzi huo Chama cha Johnson kilipata viti zaidi ya 364 vya wabunge.

KURA YA BREXIT

Aidha, Johnson alisema kuwa uamuzi huo unampatia jukumu la kufanikisha Brexit na kuiondoa Uingereza katika muungano wa Ulaya.

”Zaidi ya yote nataka kuwashukuru watu wa taifa hili kwa kujitokeza kupiga kura ya Disemba ambayo imebadilika na kuwa ya kihistoria, ambayo inatupatia sisi kama serikali mpya fursa ya kuheshimu uamuzi wa kidemokarsia wa raia wa kulibadilisha taifa hili na kuonyesha uwezo wa raia wa taifa hili’,” alinukuliwa Johnson.

Alisema kuwa ni jukumu lake kuindoa Uingereza katika muungano wa EU .

“Raia wanataka mabadiliko” , alisema, ”hatuwezi kuwavunja moyo na hatutawavunja,” anasema.

RAIS WA ZAMANI WA PAKISTAN AHUKUMIWA KIFO KWA UHAINI

Desemba 17, wmaka huu, Jenerali Pervez Musharraf(76), kiongozi wa zamani wa kijeshi nchini Pakistan alihukumiwa kifo katika mahakama maalum mjini Islamabad.

Mahakama hiyo ya watu watatu ilimuhukumu kwa kesi ya kiwango cha juu cha uhaini baada ya kuahirishwa tangu 2013.

Jenerali Musharraf alichukuwa mamlaka katika mapinduzi ya kijeshi 1999 na akahudumu kama rais wa taifa hilo kutokea mwaka 2001 hadi 2008.

Kwa sasa anaishi Dubai baada ya kuruhusiwa kuondoka nchini humo kwa matibabu 2016.

Mashtaka hayo yanahusiana na hatua ya jenerali Musharraf ya kuiahirisha katiba 2007, wakati alipoweka utawala wa dharura uliolenga kuongeza muhula wake.

WAUAJI WA JAMAL KHAHOGGI WAHUKUMIWA KIFO

JAMAL KHAHOGGI

Mahakama nchini Saudia imefahamisha kuwa watu watano wamehukumiwa adhabu ya kifo kufuatia mauaji ya mwanahabari Jamal Khahoggi , mwanahabari alieuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul nchini Uturuki.

Taarifa zilizotolewa na mahakama zimefahamisha kwamba watu watatu wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 24 kufuatia sakata la mauaji ya mwanahari huyo.

Mahakama  haikumfungulia kesi yeyote Suud al Kahtani , mshukiwa ambae  anatajwa kama kiongozi wa mauaji ya Jamal Khashoggi.

Mshukiwa huyo ameachwa huru.
Balozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Mohammed al Otaybi pia hakushtumiwa  kuhusika na mauaji hayo .

Mkurugenzi msaidi wa idara ya upelelezi wa Saudia Ahmed sseri ameachwa huru licha ya kuwa alikuwa akihusishwa na mauaji ya Jamal Khashoggi.

Jamal Khashoggi aliuawa Oktoba 2 mwaka  2018 katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul kwa kukosoa serikali ya kifalme ya Saudia.

RAIS TRUMP AFUNGULIWA MASHTAKA

Desemba 19, mwaka huu, Baraza la Wawakilishi lilimkuta makosa Rais Donald Trump kwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kujinufaisha yeye mwenyewe na pia kuzuia juhudi za bunge kuchunguza vitendo vyake.

Katika kura ambapo kila upande wa chama uliegemea upande wake, Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na Wademokrat lilipitisha vifungu viwili vya kumshtaki Trump, Mrepublikan, na hivyo kufanya awe rais wa tatu wa Marekani kufunguliwa mashtaka katika historia ya miaka 243 ya nchi hii.

Trump ambaye amekejeli tuhuma za mashtaka yaliyo funguliwa kumuondoa madarakani na kuwashambulia Wademokrat kwa kushinikiza hilo, hivi sasa kuna uwezekano wakukabiliwa na kesi mwezi Januari 2020, katika Baraza la Seneti.

Lakini Warepublikan waliowengi katika Baraza la Seneti inatarajiwa zaidi kutomuondoa madarakani, na hivyo kuwaachia wapiga kura kuamua juu ya hatma yake Trump wakati akiomba muhula wa pili kurejea White House katika uchaguzi mkuu Novemba inayokuja.

RAIS WA SUDAN AHUKUMIWA

Omar al Bashir

Desemba 14, mwaka huu, Rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir amehukumiwa kifungo cha miaka miwili katika kituo cha kijamii baada ya kupatikana na kosa la ufisadi.

Kwa mujibu wa sheria za Sudan watu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 hawahutumikii kifungo cha jela hivyo kongozi huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 75 atapelekwa katika kituo cha jamii.

Bashir alikuwa akikabiliwa na kesi ya ufisadi ambako alidaiwa kuficha fedha za kigeni zenye thamani ya dola milioni 25, zilizopatikana katika nyumba yake muda mfupi baada kung’olewa madarakani mwezi Aprili, mwaka huu.

Hata hivyo, pamoja na hukumu hiyo, Rais Bashir bado anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Muda mfupi kabla ya kusomwa kwa hukumu dhidi yake, baadhi ya wafuasi wa Rais huyo wa zamani walianza kushangilia kwa sauti ya juu wakisema kesi ilikuwa ni ya kisiasa kabla ya hakimu kuwaamuru watoke nje ya mahakama.

BOBI WINNE NA URAIS

Aprili 11, mwaka huu, Mbunge wa Kyadondo nchini Uganda, Robert Kyagulani  maarufu Bobi Wine ametangaza kuwania urais wa nchi hiyo mwaka 2021.

Kauli ya mwanamuziki huyo ni ishara kuwa atapambana na rais wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni anayeliongoza Taifa hilo kwa miaka 33 sasa.

Februari, 2019 chama tawala Uganda  cha National Resistance Movement (NRM) kilimpitisha Museveni  kuwania urais mwaka 2021.

Hatua hiyo ya NRM ilitangulia na uamuzi uliofanywa mwaka 2017 na wabunge wa Uganda waliopitisha mabadiliko ya katiba ya kuondoa ukomo wa umri wa miaka 75 ya kuwania urais na kumpa nafasi Museveni.

Katika mahojiano na kituo cha matangazo  cha ‘The Associated Press’ Bob Wine alisema atapambana na Museveni kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi.

“Nitapambana na Rais Museveni kwa niaba ya watu, ”amesema Bobi Wine.

Hayo ni baadhi tu ya matukio ya kisiasa ambayo RAI limekukusanyia kwa mwaka 2019.