Home Michezo MWAKINYO AMEWAKILISHA MABONDIA WANAOLAZIMISHWA KUPENDA SOKA

MWAKINYO AMEWAKILISHA MABONDIA WANAOLAZIMISHWA KUPENDA SOKA

4426
0
SHARE

NA HASSAN DAUDI


Wiki iliyopita, medani ya masumbwi ilipambwa na taarifa ya bondia mzaliwa wa jijini Tanga, Hassan Mwakinyo. Ndiye aliyekuwa gumzo katika mijadala mbalimbali iliyohusu mchezo wa ndondi.

Kilichomfanya kuwa ‘habari ya mjini’ ni ushindi wake wa pambano la uzito wa Welter Weight, akimtembezea kichapo mwenyeji wake nchini Uingereza, Sam Egginton.

Huenda kumchapa Egginton kusingetosha kuwashangaza wengi, lakini ushindi wa ‘TKO’, tena ugenini, halikuwa jambo la kawaida.

Na ikizingatiwa kuwa kwa miaka mingi mabondia wa Tanzania wamekuwa wakipoteza mapambano yao ya nje, hakuna ubishi kuwa alichokifanya Mwakinyo kilipaswa kupewa uzito ule.

Ushindi wake haukuishia kuwaduwaza mashabiki wa masumbwi pekee kwani Ijumaa ya wiki iliyopita alialikwa kuhudhuria kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma.

Ukiliweka kando hilo la kwenda bungeni, ni ukweli usiopingika kuwa safari ya mafanikio ya Mwakinyo haikuwa nyepesi. Kwamba haikutosha kumpongeza kwa maneno na mwishowe kumchangia kiasi cha fedha.

Ni kweli tulimwandaa Mwakinyo kwenda kutuchukulia ubingwa huko Uingereza au kwetu imekuwa ‘surprise’?

Si kwamba hili ni bezo kwa wabunge waliojitolea 20,000 kila mmoja ili kumpa kifuta jasho Mwakinyo. Hakika wanastahili pongezi pia kwa moyo wao huo.

Hata hivyo, hakuna namna unayoweza kuficha mazingira mabovu ya mchezo wa ngumi nchini. Ni kama unavyoweza kusema bondia anahitaji ‘roho ya paka’ kufikia walau nusu ya mafanikio aliyorudi nayo kijana huyo.

Kuakisi hilo, katika mahojiano yake na moja kati ya magazeti ya michezo, Mwakinyo alisema: “Siasa ipo kila mahali. Niliondoka nikiwa kama mkimbizi. Sasa hivi kila mmoja anasema amenisaidia…”

Alichokisema hakitofautiani na kilio cha mabondia wengi nchini, ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakipelekwa nje ya nchi wakiwa hawajaandaliwa, hivyo kukumbana na vichapo vinavyoitia aibu Tanzania mbele ya mataifa mengine.

Huku mamlaka husika zikiwepo, likiwamo Baraza la Michezo (BMT), mara kadhaa imeshuhudiwa timu ya taifa ya ngumi ikienda katika michuano ya kimataifa, nikitolea mfano ile ya Jumuhiya ya Madola, ikiwa imeshafeli.

Ndiyo, kabla ya kukwea pipa kwenda kushiriki mashindano hayo makubwa, tayari mabondia na makocha wao huwa wameshavurugwa kisaikolojia, sababu ikiwa ni ile ile ya miaka yote, ukata.

Cha kushangaza sasa, siku ya kuagwa na kukabidhiwa bendera ya taifa tayari kwa safari, utasikia wakiombwa kurejea na medali!

Kwa bahati mbaya, nguvu kubwa imekuwa ikiwekezwa katika soka, mchezo ambao hata hivyo hakuna ulichowahi kuifanyia bendera ya Tanzania licha ya uwekezaji unaofanywa kila uchwao.

Wakati klabu zikibaki kuwa wasindikizaji katika michuano ya Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf)-Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, Taifa Stars haijazigusa fainali za Afcon tangu mwaka 1980.

Ukimtazama Mwakinyo na mabondia wengine waliowahi kufanya vizuri nje ya nchi, ndipo unapoweza kujiuliza, nusu ya ufadhili uliopo Stars, Simba SC na Yanga SC, ungehamishiwa kwenye ndondi, tungekuwa wapi leo hii?

Huku wachezaji, makocha na wafanyakazi wengine wa benchi la ufundi katika timu hizo wakiishi kifalme, wenzao wa timu ya taifa ya ngumi hujiandaa na mashindano wakiwa na msongo wa mawazo.

Mbali ya uhaba wa vifaa, pia hufika hatua ya kutembeza bakuli kwa ajili ya mahitaji muhimu kama chakula.

Aidha, kutokana na nguvu kubwa iliyoelekezwa katika kandanda, ikiwa ni pamoja na fedha nyingi zinazomwagwa katika usajili wa mastaa wa nje ‘maproo’, hatari iliyopo ni kuliona kundi la mabondia chipukuzi likivutiwa huko.

Ikifikia huko, ina maana hatutawaona tena akina Mwakinyo, ingawa pia hakuna uhakika kama katika soka tutakuwa tumemaliza ‘adhabu’ tuliyojipa tangu mwaka 1980 ya kutoshiriki fainali za Afcon.