Home Michezo Mwakyembe tuanzie kwa Serengeti Boys kwanza

Mwakyembe tuanzie kwa Serengeti Boys kwanza

1561
0
SHARE

NA AYOUB HINJO

KWA kiasi kikubwa mchezo wa soka umekuwa na wafuasi wengi duniani kote pengine kuliko mchezo wowote katika ulimwengu huu.

Pia, mchezo ambao umekuwa ukizalisha fedha nyingi kwa baadhi ya nchi wakiutumia kukuza uchumi na kufanya maendeleo mengine ya msingi ndani yake.

Hata ukifuatilia nchi za Afrika ambazo zimeendelea kiuchumi, mchezo wa soka umechukua nafasi kubwa licha ya mambo hayo kutoonekana moja kwa moja.

Kwa muda mfupi hapa nchini Tanzania, timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys, wamewarudisha mashabiki wa soka kuipenda timu ya taifa.

Miaka ya hivi karibuni Taifa Stars walikuwa hawafanyi vizuri kiasi cha mashabiki kuisusa timu hiyo kwa kutoenda viwanjani kuiunga mkono.

Pamoja na hayo yote, kuna watu wamesimama nyuma ya mafanikio ya kikosi hicho cha vijana ambacho kinafanya vizuri tangu michuano ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika Gabon mwaka juzi.

Shukrani ziende kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, kwa kushirikiana vyema na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na wadau mbalimbali wa michezo na kuonyesha nguvu na mchango katika sekta ya michezo japo ni lazima wao kufanya hivyo.

Mwakyembe umekuwa ukifuatilia kila hatua na kila kona ili kujua wapi tunashindwa na tufanye nini ili kutoka tulipokwama. Nikupe hongera kwa mara nyingine tena.

Pamoja na pongezi nyingi kutoka kwangu na kwa wadau wengine wa michezo mbalimbali naomba tukae chini tuzungumze kuhusu Serengeti Boys.

Tuanzie hapa kwanza. Kama Waziri mwenye dhamana ya michezo umeshirikiana vipi na TFF kuendeleza vipaji vya vijana wetu baada ya michuano ya AFCON kumalizika hapa nchini?

Kuna maisha baada ya michuano hiyo kumalizika. Siamini kama kuna kitu kingine hawa vijana wanakifikiria zaidi ya kuwa wachezaji wakubwa watakaotegemewa na nchi miaka kadhaa ijayo.

Vijana hao wote wanapenda kuwa kama Mbwana Samatta. Wanatamani kufika alipofika Simon Msuva au waende mbele zaidi ya hapo alipo Shaaban Chilunda.

Msingi wao unaanzia hapo ambapo nyie wakuu mpo. Nguvu inayotumika sasa kuwaweka sawa kisaikolojia na kujengwa kiufundi iendelee hadi watapofika kwenye usawa wao.

Nguvu iliyotumika kuunda kamati mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia itumike pia katika kuendeleza maisha yao ya soka baada ya michuano hii inayofanyika hapa Dar es Salaam kumalizika.

Inajulikana hiyo ni kamati ya muda mfupi kwa ajili ya kuwapa morali vijana lakini ushafikiria kuhusu maisha yao baada ya hapa walipo?

Au tunaishi kwa kutegemea kuwa mawakala kutoka maeneo mbalimbali ya dunia watakuwa wakitazama michezo hiyo? Kwanini tusifanye wenyewe? Nimeuliza tu mheshimiwa Mwakyembe.

Fahari yetu iko wapi? Hakuna lisilowezekana katika hili tuwekeze nguvu zaidi baada ya AFCON U17 kumalizika ili kunyanyua morali hata za watoto wengine.

Fahari yetu Watanzania ni kuona vijana wetu wanashiriki kila michuano mpaka ya Kombe la Dunia kwa miaka ijayo. Yote yanawezekana, ndio tunaweza.

Samatta anatazamwa na wengi kama mfano wa kuigwa lakini hata yeye mwenyewe ametumia juhudi zake kufika alipo sasa. Tusiwapitishe vijana njia ngumu aliyotumia staa huyo wa Genk, tuwape njia yenye mtiririko sahihi.

Sina shaka na benchi la ufundi. Wasiwasi wangu ni kuwapotezea muda vijana ambao wanautazama mpira kama ajira yao ya baadaye.

Wapo vijana wengi waliotoka kwenye michuano na mashindano mbalimbali ndoto zao ziliishia kuitwa ndoto kama ilivyo kwa ndoto yenyewe. 

Hawatamani tena kuusikia mpira. Ili kufuta maumivu yao lazima tuonyeshe jinsi gani hawa vijana wa sasa wanatunzwa na kupatiwa kila hitaji lao kufika katika malengo yao na nchi kwa ujumla.

Kwa sasa tunajitahidi kufanya kila lililozuri na jema kwa ajili yao lakini tukifanya mambo mazuri zaidi ya hapa huko mbeleni tutaishi kama wafalme.

Biashara ya wachezaji ni pana mno lakini kwa nchi ni fahari hususan katika kukuza uchumi kama tutawekeza nguvu zetu kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwakyembe, tumejipanga vipi kukuza uchumi kupitia vijana wa Serengeti? Au tumejipanga kuudhoofisha kwa kuwaacha mtaani baada ya kuwatumia sasa?

Tusimame sawasawa kama tunataka kufika mbali zaidi. Maisha ya vijana yapo mikononi mwenu na Watanzania kwa ujumla baada ya michuano hiyo mikubwa kwa vijana Afrika.

Nguvu inayotumika kuwahudumia sasa isije kuwahukumu baada ya michuano ya AFCON U17 hapa nchini kumalizika, bali itumike kama darasa kwao ili kujenga uzoefu wa kupambana na kujua umuhimu na faida wa michezo hiyo.

Vijana hawa bado ni wadogo na inawezekana wengine wamehasi kabisa kwenda shule wakiamini mpira ndio maisha yao. Je, tumejipanga kuwalinda? Naomba nikukumbushe Mheshimiwa Mwakyembe kuwa kuna maisha baada ya michuano ya AFCON U17 kumalizika.