Home Makala Mwarobaini wa Usafiri Ziwa Victoria waja

Mwarobaini wa Usafiri Ziwa Victoria waja

1554
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU

Ukizungumzia maendeleo ya miundombinu katika taifa la Tanzania, hasa katika kipindi cha serikali ya awamu ya Tano, hutaacha kugusia sekta ya usafiri majini hasahasa kwenye ziwa Victoria ambako kwa muda mrefu sasa kumekuwa na kusuasua kwa huduma ya usafiri kulikosababishwa na kuzama kwa Meli ya MV Bukoba ambayo ilikua tegemeo la usafiri  kati ya mikoa ya Mwanza na Kagera, pamoja na kuwepo kwenye ukarabati mkubwa kwa baadhi ya meli zinazotoa huduma katika ziwa hilo.

Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuliona hilo, imewekeza nguvu kubwa katika kutatua tatizo hilo na pia kumaliza kabisa adha ya usafiri wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria pamoja na kurudisha hadhi ya kanda ya ziwa kwa kuanza kujenga Meli mpya kubwa na ya kisasa kwaajili ya kumaliza kabisa shida ya usafiri katika ziwa Victoria.

Akizungumza hilo Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Erick Hamis ambao ndio wenye dhamana kwa niaba ya serikali kusimamia ununuzi, usafirishaji ,ujenzi pamoja na jukumu zima la kuhakikisha meli hiyo Mpya inakamilika kwa wakati na kwa gharama zilizoainishwa amesema ujenzi huo utakamilika kwa wakati na pia watahakikisha ubora na viwango vya kimataifa vinazingatiwa.

Mtendaji Mkuu huyo wa Kampuni ya Huduma za Meli, amesema serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli,  itaandika historia ambayo itaichukua Tanzania miaka mingi sana kuja kufutika kwa jinsi itakavyowarahisishia maisha wakazi wa kanda ya ziwa kutokana na ujenzi wa meli hiyo kubwa.

“Uwekezaji huu mkubwa wa ujenzi wa Meli kubwa katika Ziwa victoria sio tu utafufua matumaini mapya ya wana kanda ya ziwa, bali utatimiza ndoto za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alidhamiria Tanzania iwe kinara wa usafiri kwenye ziwa  Victoria kwa kuwa na Meli za uhakika za abiria, mizigo na hata za uvuvi kwaajili ya maendeleo ya watanzania” Anasema Erick Hamis.

Anasema maono ya Rais Magufuli hayana tofauti na yale ya Baba wa Taifa ndio maana akaamua kuwekeza kwenye ujenzi wa Meli mpya na ya Kisasa ambayo itamaliza kabisa shida ya usafiri na usafirishaji kwenye ziwa victoria.

“Serikali hii haina masihara kitu kinapoanzishwa kinasimamiwa na kinakamilika, kwa sasa baadhi ya vifaa kwaaajili ya ujenzi wa meli hiyo vimekwisha wasili ikiwa ni maandalizi ya awali, aidha ujenzi wa chelezo kwaajili ya kujengea meli hiyo unaendelea kwa kasi chini ya usimamizi wa kampuni ya huduma za meli.

 “Ukitaka kujua ukubwa wa Meli hiyo ni kwamba kwa sasa kontena 300 zimeagizwa kutoka  Korea ya Kusini kwaajili ya kusafirishwa kuja Tanzania, baada ya kufika bandari ya Dar es Salaam vitasafirishwa kwa njia ya reli hadi hapa Mwanza ili kuendelea na ujenzi huo kwa haraka,” anasema Hamis.

Aidha Mtendaji Mkuu huyo wa Kampuni ya Huduma za Meli, anasema meli hiyo itakua na ukubwa wa ghorofa tatu, itakua na uwezo wa kubeba abiria 1200,itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 400 pamoja na magari 20 kwa wakati mmoja hivyo kuwa ya kwanza na ya  kipekee katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Hamis anaweka wazi kwa kusema kuwa meli hiyo licha ya uwezo huo mkubwa wa kubeba abiria na mizigo itakuwa na vyumba maalum vya watu mashuhuri (VIP) pia itakuwa na nafasi ya kutosha kama zilivyo meli nyingi za kisasa, hata kasi yake ni kubwa ikilinganishwa na meli nyingine ambazo kwa safari ya Mwanza hadi Bukoba huchukua kati ya  saa 10 hadi 12, meli mpya itachukua saa6 tu kwa umbali huohuo.

Upekee wa meli hiyo haupo tu kwenye kasi na uwezo wake wa kubeba mizigo, itakuwa pia na lifti kwaajili ya kupanda na kushuka ghorofani pamoja na miundombinu rafiki kwa walemavu, hii itasaidia sana kukuza utalii hasa ukizingatia kwenye ziwa Victoria hakuna meli yenye hadhi ya kitalii.

Mtendaji huyo wa Kampuni ya Meli amewaomba watanzania kuendelea kulipa kodi pamoja na kufanya kazi kwa bidii kwani fedha zote zinazotumika kujengea meli hiyo ambazo ni Bilioni 90 ni fedha za watanzania na hakuna hata senti moja iliyotolewa na wafadhili.

Serikali ya awamu ya tano haijaishia kwenye ujenzi wa meli mpya tu, bali hata meli chakavu na za zamani ziko kwenye ukarabati mkubwa mfano:  Meli ya MV Victoria iko kwenye ukarabati mkubwa wa  zaidi ya shilingi Bilioni 22 ambao unahusisha uondoaji wa vitu vyote chakavu na vya zamani na kuweka mfumo mpya wa rada, injini mpya, viti pamoja na vitanda vipya kadhalika na thamani za kisasa ambavyo kwa ujumla vitaifanya meli hiyo kuwa kama mpya kabisa.

“Wakazi wa Mkoa wa Kagera wakae mkao wa kula kwani Kipenzi chao Meli ya MV.Victoria iko kwenye ukarabati mkubwa na muda sio mrefu itarudi kwenye hali yake , tena nasema itarudi kivingine kwani hata spidi yake itakuwa ni kama ya meli mpya na za kisasa zinazotengenezwa miaka hii,” anasema

Akizungumzia usafiri wa kwenye maziwa makuu kwa ujumla, Hamis anasema serikali pia imewekeza katika ujenzi wa meli mpya katika ziwa Tanganyika ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 pamoja na tani 400 za mizigo, pia ukarabati wa meli kongwe ya MV. Liemba unafanyika na hapo baadaye  kuna mipango ya kujenga Meli ya Mizigo kwaajili ya kurahisisha biashara kati ya Tanzania na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kuimarika kwa usafiri wa meli katika maziwa hapa nchini, kutasaidia sana ukuaji wa uchumi hasa katika maeneo yanayozunguka maziwa hayo pamoja na mikoa ya jirani, aidha nchi zinazotuzunguka zitakua mnufaika mkubwa wa mafanikio hayo, mfano kuimarika kwa usafiri wa meli hasa za mizigo kwenye Ziwa Victoria kutasaidia sana ukuaji wa biashara kwenye nchi ya Uganda kupitia Bandari  ya Portbell.

Anasema kukamilika kwa ujenzi wa meli mpya katika ziwa Victoria, kumalizika kwa ukarabati wa meli kwenye maziwa yote, kutawawezesha kampuni ya huduma za meli kufikiria kujenge meli kubwa pia kwenye Bahari ya Hindi kwani kuna utajiri mkubwa wa maliasili bahari pamoja na utalii.

“Sisi kama Kampuni ya Huduma za Meli tumejipanga kuhakikisha tunamsaidia Mh.Rais kusimamia Meli zote zitakazotengenezwa na kukarabatiwa ili zilete tija kwa taifa na hatimaye nchi yetu ifaidike na rasilimali za Maziwa na Bahari,” anasema Hamis.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mwnza wamepongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Awamu ya Tano hasa kwa kanda ya ziwa  wakiangazia ukarabati wa Meli ya Mv Victoria pamoja na Ujenzi wa Meli Mpya.

Shija Maduhu mkazi wa Nyakahoja Jijini Mwanza anasema kazi zinazoendelea kufanyika kwenye sekta zote hapa nchini zinadhihirisha wazi kuwa Rais Magufuli amedhamiria kuwatumikia watanzania na kuhakikisha wanakuwa na maisha bora.

Tatu Athumani mkazi wa Nansio Ukerewe anasema Ukarabati wa Meli ya MV. Crarias umewafanya wawe na tumaini jipya la usafiri kati ya Mwanza na visiwa hivyo kwani meli hiyo ina kasi zaidi na imekua bora zaidi nan i ya uhakika tofauti na hapo awali.