Home Makala MWECO YAWATOA USINGIZINI WANAWAKE MBARALI

MWECO YAWATOA USINGIZINI WANAWAKE MBARALI

625
0
SHARE

NA JIMY CHARLES


MOJA ya changamoto kubwa inayowakabili wanawake nchini hususani wa maeneo ya vijijini, ni mfumo dume ambao umetumika kukandamiza haki zao hata kama zimetajwa kisheria.

Jambo kubwa ambalo ni tatizo sana vijijini ni haki ya kumiliki ardhi kwa wanawake/ wasichana, ambalo tangu kufanyika marekebisho ya sheria ya ardhi, sasa  jinsia zote zinaruhusiwa kumiliki.

Sadala Mbella, Mkazi wa Lujewa wilayani Mbarali, anasema kwa mila za makabila mengi mwanamke hastahili kupewa ardhi kwa kuwa inaaminika mwanamke si mkaaji wa kwao, bali ataolewa na kwenda kuanza mji wake chini ya usimamizi wa mumewe na hivyo ardhi aliyonayo mzazi wake hugawanywa kwa watoto wa kiume pekee.

“Kwa baadhi ya makabila ikitokea mwanamke husika hakuolewa au aliolewa na kurudi nyumbani kwao baada ya maisha ya kwa mume kuwa magumu, akifariki huzikwa mpakani na si kama ambavyo mwanamume hutendewa.

“Wazazi hugawanya ardhi kwa watoto wote wa kiume hata wenye umri mdogo na kwa makabila kama ya ukanda wa kaskazini, mtoto wa kiume wa mwisho ndiye mwenye haki ya kupewa ardhi ya eneo la nyumbani na kuishi na wazazi wake hadi siku zao za kuishi duniani zitakapoisha,” alisema.

Gelmana Tahya anabainisha kuwa hali ya mwanamke kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi inasababisha changamoto nyingi hata anapoolewa, huko nako hukutana na unyanyapaa kama aliouacha kwao.

“Mwanamke wa kijijini huwekwa katika mtazamo wa kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi na hata ikitokea mume wake amefariki, bado ukoo huamua hatma ya ardhi husika licha ya mwanamke kuwa sehemu ya washiriki wa utafutaji wa ardhi hiyo.

“Ni kawaida kama mwanamume aliandika wosia, mgao wa mali huuelekeza kwa watoto wa kiume na mkewe huishi kwa mwavuli wa watoto wake na si kuwa na haki ya chochote na wakati mwingine msimamizi wa mirathi kuwa shemeji au ndugu mwingine kwenye ukoo,” anasema.

Asasi ya kiraia ya Mbarali Water Sanitation and Environmental Conservation Organization (MWECO) chini ya udhamini wa Taasisi ya Foundation for Civil Society (FCS) pamoja na kukabiliwa na jukumu la kuwajengea uwezo wanawake na wasichana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali, wamefanikiwa kuwatoa usingizini wanawake kwenye eneo la ardhi.

MWECO imejitahidi kuwajengea uwezo wanawake na wasichana juu ya kuzitambua haki zao kwenye masuala ya ardhi wilayani Mbarali.

Kipengele muhimu kinachotazamwa na MWECO ni haki ya wanawake kumiliki ardhi na wajibu wa wananchi kwa ardhi ya kijiji pamoja na kuwa na mabaraza ya ardhi kwa ajili ya kushughulikia migogoro mbalimbali inapojitokeza.

Ingawa kumekuwa na taasisi nyingi zilizofanya kazi ya kuwajengea uwezo wanawake na wasichana juu ya kujua haki ya kumiliki ardhi, MWECO imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ufahamu huo juu ya masuala ya ardhi unakuwa na tija kubwa kwa kila mwanamke wilayani Mbarali.

Kabla ya kuenezwa kwa ufahamu huo ilikuwa ni jambo gumu kwa mwanamke kumiliki ardhi. Mwanamke aliruhusiwa kufanya shughuli za uzalishaji juu ya ardhi ya wazazi au familia yake, lakini si kumiliki na kuwa na maamuzi nayo.

Mwanamke na mtoto wa kike walitumika kama nguvu kazi ya kuzalisha mazao ambayo mwanamume ndiye mwenye maamuzi nayo na mwanamke haruhusiwi kuhoji jambo lolote.

Mwanamke alidunishwa na kutumika kama ‘Trekta’ la kuzalisha mali na manufaa kwenda kwingine, kwa kuwa mwanamume ndiye mwenye hiari ya mazao yaliyozalishwa kwa pamoja na fedha husika na wakati mwingine huzitumia kufanya anasa au kuongeza mke mwingine bila kuboresha mahitaji ya msingi ya familia iliyohusika katika uzalishaji.

Katika wilaya hiyo, pia kuna Jukwaa la  Wakulima ambalo linasaidia kuelimisha wanavijiji sheria ya ardhi na kufuatilia kwa karibu masuala yanayohusu umiliki wa ardhi kwa wanawake na sasa mwanamke anaruhusiwa kupeleka maombi ya ardhi na kujadiliwa na wajumbe wa Serikali ya kijiji naye kugawiwa ardhi kwa kadiri alivyoomba kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Mwenyekiti wa MWECO, Nikumwitika Ngondo, anasema pamoja na kuwa na majukumu mengine, wameona haja ya kumjengea uwezo mwanamke katika masuala ya kujua haki yake katika kumiliki ardhi.

“Tunayo miradi maalumu tunayoifanya chini ya ufadhili wa FCS, lakini hatufungwi kuwajengea uwezo wanawake na wasichana kwenye masuala ya ardhi.

“Tumeamua kuliangalia eneo hili kwa sababu ya umuhimu wake, tunakutana na changamoto, hasa ukosefu wa fedha na umbali wa kijiji na kijiji, lakini kamwe hatukati tamaa,” alisema Ngondo.