Home Habari MWINYI: WASHINDANI NI MUHIMU KWA ATCL

MWINYI: WASHINDANI NI MUHIMU KWA ATCL

2640
0
SHARE
Abbas Hassan Mwinyi

NA GABRIE MUSHI

Mbunge wa Fuoni, Abbas Hassan Mwinyi (CCM) amesema washindani ni muhimu katika biashara ya usafiri wa anga ili kuongeza wigo kwa serikali kukusanya mapato.

Mwinyi ambaye ni rubani aliyewahi kulitumikia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), amesema shirika hilo linapaswa kuwa na washindani ili kuongeza morali kwa watendaji na viongozi wake kujiimarisha.

Akizungumza na RAI katika mahojiano maalumu, pia alisema ndege za ATCL hazitumiki ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali ambazo serikali inapaswa kuzifanyia kazi haraka.

“Ushindani unatakiwa kuhamasishwa na serikali yenyewe kwa sababu yale mashirika yanalipa kodi. Tusikamue ng’ombe mmoja tu tukikamua ng’ombe wengi ndio faida. Kwa hiyo ushindani wa kibiashara una afya na naamini serikali inatambua hilo,” alisema.

Akizungumzia kuhusu hali ya usafiri wa anga nchini hasa baada ya ATCL kupatiwa ndege tano, Capt. Mwinyi alisema kuna pande mbili ambazo zinapaswa kuwajibika.

“Serikali ina wajibu wake na shirika vilevile. Wajibu wa shirika ni kwamba baada ya kupata ndege hizo tano, wawe wanazitumia vema, kwamba kusiwe na ubadhirifu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ila naamini chini ya uongozi wa sasa, shirika litakwenda. Ila tahadhari ni kwamba wasiruhusu wajanja wanaochezea kompyuta kuiba mapato ya shirika kwa kuwa sasa vijana wajanja sana.

“Pia kusiwe na hujuma kama kusema ndege imejaa kumbe ndege ipo wazi. Waboreshe utendaji kiteknolojia, si wakati wa kwenda dirishani kununua tiketi, ni wakati wa kwenda kufanya booking online,” alisema.

Alisema serikali nayo ina wajibu kwani, kitaalamu ni kwamba ndege haitakiwi itulie kwenye ardhi, inachotakiwa ni kufanya kazi saa 24, ina maana kwamba wanabadilisha tu crew (timu).

“Inatoka pair moja ya crew baada ya muda kumalizika inaingia pair nyingine ili ndege ifanye kazi saa 24. Hiyo ndio inaitwa ‘full utilization’ (matumizi sahihi) ya ndege, kwa hali ilivyo sasa hivi, tunafanya under utilization,  kwa sababu bado viwanja vingi vya ndege nchini havikidhi viwango vya ndege kufanya kazi kwa saa 24, kwingine taa hakuna, wahudumu hakuna. Sasa serikali kwa sehemu kama hizo iboreshe kama njia ya kurukia ndege ni fupi, zirefushwe ili ndege itumike kwa asilimia 100.

“Ingawa serikali imefanya maboresho ya viwanja vingi vya ndege ila bado sehemu nyingi hakuna viwango vya kutosha. Tukumbuke ndege zimenunuliwa kwa fedha nyingi, hivyo zikitumika vizuri ule uwekezaji uliowekwa utarudishwa mapema. Ila zikiwa usiku zinalala hakutafikia malengo mapema,” alisema.

Aidha aliongeza kuwa ni dhahiri soko lipo —la nje na la ndani, kwa sababu kuna kampuni kubwa za KLM na British Airways ambazo kila ndege zinapokuja zimejaa abiria.

“Wapo Watanzania wengi wanasafiri kibiashara. Wapo ambao wangependa kupanda ndege zetu kuliko za nje. Kwa hiyo soko lipo la nje na ndani,” alisema

Mwinyi ambaye pia ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alizungumza mambo mbalimbali ya kisiasa katika mtiririko wa mahoajino yafuatayo.

RAI: Kwa kuwa historia yako inaonesha ulikuwa rubani na umebobea zaidi kwenye fani hiyo zaidi ya siasa, unaelezeaje tofauti ulioiona tangu uchaguliwa kuwa mbunge kulingana na uzoefu wako?

MWINYI: Tofauti ni kubwa sana kwa sababu wahenga wanasema ‘ukitaka kujua utamu wa ngoma, shurti uingie ucheze’, lakini ukiwa unasikia tu kwa wenzio ni tofauti kabisa unavyodhani. Kwa hiyo tofauti kubwa ninayoiona ni kwamba ubunge ni kazi kubwa ambayo ina lawama nyingi na nzito, hasa sisi ambao majimbo yetu yapo nje ya miji mikuu yaani vijijini.

Kuna changamoto nyingi tofauti na mijini. Mfano barabara hazipo, njia hazipitiki, umeme hakuna, maji upatikanaji wake ni wa shida, kwa hiyo changamoto ni nyingi.

Licha ya Mbunge kupewa mfuko wa kuchochea maendeleo katika jimbo lake, lakini fedha zinazotolewa ni kama mkia wa mbuzi, kwa maana kuwa fedha ni kidogo sana kulingana na mahitaji ya jimbo husika. Kwa hiyo wakati mwingine hali inakuwa ngumu sana kwa kuwa wananchi wanakuwa na matarajio mengi kwako tofauti na Wabunge wa mijini ambako umeme upo, maji yapo na barabara zipo. Hizo ndio changamoto ambazo bado tunapambana nazo.

RAI: Kutokana na hali hiyo, umejipanga vipi kukabiliana na changamoto hizo?

MWINYI: Upatikanaji wa umeme ndio ilikuwa changamoto kubwa, ila tumeanza kuitatua, tumeshatoa fedha kwenye Shirika la Umeme Zanzibar na baada ya miezi kadhaa umeme utapatikana katika maeneo ambayo hayakuwa na umeme. Upande wa barabara tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwani toka tuingie tumerekebisha baadhi ya barabara na sasa zinapitika, ingawa nyingi si kwa kiwango cha lami. Pia wiki iliyopita Rais Ali Mohamed Shein amefungua barabara ya Kijitoupele. Hata hivyo changamoto bado zipo tunaendelea kutatua hatua kwa hatua.

Hali ya kisiasa Zanzibar

RAI:  Kwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kulikuwa na mvurugano uliotokea na kusababisha kufutwa kwa matokeo ya Rais na Baraza la Wawakilishi, unafikiri hali hiyo imeathiri ukuaji wa maendeleo ya Zanzibar, hasa ikizingatiwa baadhi ya nchi wahisani zimepunguza au kukata misaada yao?

MWINYI: Ni kweli, kumekuwa na athari kidogo kwa sababu yale mataifa ambayo tulikuwa tunayategemea katika misaada, ni mataifa ambayo hayatoi misaada bure, yanakusaidia kwa masilahi yao ili yashinikize yanayotaka uyafanye kama vile mambo ya ushoga. Sisi kwetu utamaduni huo hatuna. Sasa unapoukataa kwa tafsiri yao, unaikandamiza demokrasia.

Hivyo lazima tuwe na heshima na nchi yetu kuliko kupewa misaada yenye mashinikizo yaliyo nje na utaratibu wetu. Kwa kiasi fulani, imetuathiri, ila pia imetujenga kuwa tumeonesha msimamo kuwa si watu wa kusukumwa sukumwa.

RAI: Unaizungumziaje hali ya kisiasa Zanzibar, hasa ikizingatiwa Rais aliyepo madarakani, Dk. Ali Mohamed Shein anamalizia ngwe yake ya mwisho?

MWINYI: Kwa kweli kiongozi wetu yupo makini sana, kuna baadhi ya mambo hana masihara nayo… ni wale ambao wanaanza kufanya kampeni kabla ya wakati, makundi kweli yalijitokeza na bado yapo chini kwa chini, lakini uongozi wa juu wa chama ukiongozwa na Rais John Magufuli, wamekemea kwa nguvu zote. Pia ameonya walioanza mchakato anawafahamu na huenda wakakatwa kabisa. Kwa hiyo, muda wa kampeni bado, Rais yupo madarakani, ni muda wa kutekeleza ahadi za mwaka 2015, ili tukishatekeleza tutapata heshima na ridhaa ya madaraka 2020.

Utendaji wa JPM

RAI: Baadhi ya Watanzania wanatazama utendaji wa Rais Magufuli kuwa unaogofya wasaidizi wake ndani ya chama au serikali, kwa upande wako unautathmini vipi?

MWINYI: Wahenga wanasema ‘ujana maji ya moto’, huyu ni rais wa tano, hata ukitazama umri wake huyu ni kijana kuliko watangulizi wake. Huyu ana uthubutu, yupo makini na yale anayotaka kuyatekeleza. Na mambo yalivyokuwa yanaenda huko serikalini bila kuwapo kwa mtu kama Magufuli yangekuwa yanalala.

Ile kumuogopa wanamuogopa kwa sababu za msingi kwa kuwa hamuonei mtu, usipotimiza wajibu wako ipasavyo lazima uende na maji. Kwa mfano, rais wa awamu ya kwanza alisema tutahamia Dodoma, ila wamepita marais wanne hawajahamia, ila yeye amethubutu. Kwa hiyo ana uthubutu mkubwa.

Ukitazama miundombinu, sasa kuna mradi mkubwa sana wa SGR, na fedha nyingi ni za ndani kwa sababu yupo makini katika ukusanyaji wa kodi. Kwa kuwa bila ukusanyaji wa kodi ni ngumu kuendesha nchi. Kwa hiyo wanamuona mkali na ni vizuri kuwa mkali, kwa sababu utamuona mkali pale ambapo hutekekelezi wajibu wako.

Jambo la msingi tuendelee kumuunga mkono Rais Magufuli kwa jitihada za makusudi anazofanya, wananchi tupende kulipa kodi, ili tumsaidie rais. Rais ana mipango na miradi mikubwa ambayo yote ina manufaa kwa nchi yetu, tulipe kodi tusifanye ujanjaujanja.

RAI: Kutokana na uwingi wa Wabunge wa CCM kupitisha miswada ya sheria zisizo na tija kwa jamii kwa kupiga kura ya ndiyo, unafikiri umefika wakati sasa wa kubadili mfumo na kupiga kura ya siri, ili kunusuru Wabunge wanaopenda kupinga jambo husika wasichukuliwe hatua?

MWINYI: Kila chama kina utaratibu wake wa kufanya shughuli zake, na Wabunge wa CCM wakati fulani tulienda kwa wananchi kuomba ridhaa tukanadi sera zetu na wapinzani wakanadi za kwao. Kwa hiyo, wana CCM ndio waliopata ridhaa, ndio maana wapo wengi ndani ya Bunge na demokrasia inasema wengi wape.

Kwa hiyo, sioni haja ya kubadilisha utaratibu, kwani hata sasa wapinzani wameongezeka bungeni, na wao sasa wajitahidi wanadi sera zao. Kwa mfano, CCM kuna demokrasia, ila ukiangalia CUF tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza ni mgombea mmoja tu wa urais anayesimamishwa mpaka sasa. Kwao kuna ufinyu wa demokrasia tofauti na kwetu CCM.

Hata viongozi wa juu hawataki kuachia madaraka, ukitaka kuchukua fomu ili kumpa changamoto kiongozi wako, yanakukuta kama yaliyotokea kwa Zitto Kabwe na Chadema.

Kero za Muungano

RAI: Kwa kuwa ni Mbunge unayetokea Zanzibar, umechukua hatua gani kushirikiana na wenzako kutatua kero za Muungano ambazo zimekuwa zikilalamikiwa sana na Wazanzibari?

MWINYI: Ni kweli kulikuwa na malalamiko mengi, kero za Muungano zilikuwa nyingi kuliko sasa. Nchi mbili ambazo zimeungana kuna mambo ambayo lazima yafanyiwe kazi, hata mimi nimeoa miaka 17 iliyopita, kuna tofauti nyingi tu, ila tunazimaliza ndani ya chumba chetu.

Kwa hiyo, kero za Muungano nyingi zimetatuliwa kama vile tozo ya umeme, tumelalamika na malalamiko yamekwenda sehemu husika na sasa mchakato upo katika majadiliano, kwamba viongozi waandamizi wanafanya majadiliano ili tuje na pendekezo zuri kwa manufaa ya pande zote mbili.

RAI: Kwa kuwa wewe ni mtoto wa Mzee Mwinyi, Rais wa awamu ya pili na katika familia umefanikiwa kushika hatamu nyingi za kisiasa ndani ya serikali za awamu mbali mbali, nini siri ya mafanikio hayo na umejifunza nini kwa Mzee Mwinyi?

MWINYI: Kwa kawaida mtoto humfuata Baba yake, hata familia ya daktari mtoto unapomuona baba kila siku anakwenda kutibu wagonjwa, naye atakuwa na shauku ya kuwa kama baba yake. Na sisi tangu utoto tumemuona baba katika siasa, limetuvutia… ila kubwa pia tumeliona kwake ni kule kujishusha, amejijengea heshima ndani ya jamii, hamuudhi mtu, nafikiri tabia ileile na sisi tumeiga kutoka kwake — kwamba  tunapokaa na watu vizuri, wakajua rekodi zetu, pengine ndio chanzo cha sisi kufanikiwa katika chaguzi mbali mbali za kisiasa.