Home Makala MZAZI NA MWANA, MOTO HUZAA JIVU

MZAZI NA MWANA, MOTO HUZAA JIVU

5035
0
SHARE

Mudhihiri Mudhihiri


KUJAALIWA mtoto ndani ya ndoa ni faraja na furaha kwa wanandoa. Nimeanza na neno kujaaliwa kwa sababu uzazi hautokani na ubingwa wa wanandoa bali ni fadhila yake Mwenyezi Mungu. Wapo wanaokumbwa na mtihani wa kuvunjika ndoa zao kwa sababu ya kukosa watoto. Labda ni kwa sababu ya imani haba, Mungu atuepushie mbali. Sio siri kujaaliwa watoto ni faraja na furaha. Wanandoa hufurahia kuimarisha ndoa yao na wazazi wao hufurahia kupata wajukuu, watani wao.

Kwa wazazi wengi kama siyo wote mtoto kwao ni mkongojo wao wa uzeeni mwao. Huwalea watoto wao upeo wa malezi. Na wengine husomesha wana wao elimu za dunia na akhera kwa viwango vya  kutajika. Wengi wao huyafanya haya kwa kujikalifu taklifu kubwa ajabu. Yote haya ni maandalizi ya kutengeneza mkongojo utakaokuja kuwasaidia uzeeni. Basi kufuzu au kufeli kuna Mungu, chambilecho moto huzaa jivu.

Kulea mwana si jambo rahisi na jepesi. Kumkuza mwana hadi awe mume au mke kuna shira na shubiri zake. Hujapata kusikia watu wakisema kuwa kuzaa si kazi ila kazi ni kulea! Kuengaenga mwana kama yai, fimbo za asubuhi na jioni, na kuongoa mwana kwa wimbo mui havilei mwana. Uzito wa mtoto  ukizidi uzito wa mbeleko mtue asote na mwenyewe atatambaa. Kudondoka na vilio anaposimama dede na kutembea tete ndiyo kukuwa huko. Hakika mchelea mwana kulia hulia yeye.

Tunaona namna wazazi walivyozama katika mshughuliko wa malezi ya watoto wao. Gharama za kusomesha, matibabu na kadhalika hazikadiriki. Zipo nyakati huwa natamani walau kuwaza tu iwapo wazazi ndani ya huba ya watoto wao huwapitia ndani ya fikra zao mapenzi waliyokuwa wanapewa na wazazi wao. Huwa natamani pia kujua iwapo wanandoa hawa hukumbuka shida walizokuwa wanawasababishia wazazi wao walipokuwa watoto.

Kila ninapojaribu kufumbua midomo ili niwakabili wazazi kwa maswali haya, ulimi wangu hujikomelea kooni sauti isitoke. Husemwa  kuwa jana, leo na kesho ni mduara muhimu katika maisha ya mwanadamu mwenye nadhari. Hapana ubishi kuwa nadhari ni mwenza muhimu kwa maisha yetu maana asiye nadhari ng’ombe. Jana tulikuwa watoto na kuishi kwa kutegemea wazazi. Leo tumekuwa wazazi na kutumia kila tupatacho kulea wenetu. Mkongojo wa shaibu na ajuza uwapi?

Wenetu wanaopukutisha kila tunachokichuna leo kwa matarajio ya kuwa wasaidizi wetu kesho uzeeni, wakati huo nao watakuwa ni wazazi wenye kushughulika na watoto wao. Huo utakuwa ni wakati wao wa kujiandalia maisha kama vile kujijengea nyumba na kukabiliana na changamoto kadha wa kadha za maisha. Hakika ya wakati huo ni kuwa mkongojo wako wa kweli ni fimbo ya kutembelea na siyo mkono wa mwana.

Kwa hayo niliyoyasikia kutoka kwa waliyonyewa na mvua nami nikayaandika kama ulivyoyasoma, kichwa changu hakiishi kuwaza na kuwazua. Je! Nimejiandaa vya kutosha ili kujinusuru na kadhia ya kuja kulazwa katika chumba cha wajukuu? Je! Nimejiandaa vya kutosha katika masurufu yangu ya safari ya uzeeni ili nisije kugombea ziwa na wajukuu wangu? Je! Nimejiandaa vya kutosha ili wajukuu na vitukuu waone fahari kunizunguka badala ya kuninyanyapaa na kunikimbia?

Kalamu ya Muungwana ingependa kumuona kila shaibu na ajuza wanakuwa na raha na furaha badala ya kuwa kinyaa na karaha. Haya yote huandaliwa leo na siyo kesho.