Home Latest News MZEE WA UPAKO: Wanaotupinga kushikiri siasa ni mbumbumbu, limbukeni

MZEE WA UPAKO: Wanaotupinga kushikiri siasa ni mbumbumbu, limbukeni

963
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI,

Hivi karibuni kumeibuka mijadala mbalimbali kuhusu hali ya kisiasa nchini. Mijadala hiyo baadhi huibuliwa na viongozi wa dini ambao kwa namna moja au nyingine wana nguvu ya ushawishi kwa jamii kwa kuwa na waumini wengi katika makanisa yao.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya wasomi na wanasiasa wakongwe kukemea baadhi ya viongozi wa dini kujihusisha na masuala ya siasa ambapo mmoja wa kiongozi wa dini anayetajwa kuibua mijadala ya aina hiyo kila mara ni Askofu wa Kanisa la Ufufua na Uzima, Joseph Gwajima.

Ingawa Askofu Gwajima amekuwa akiwapuuza wanaomtuhumu katika masuala hayo, Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo maarufu kama ‘Mzee wa upako’  naye amesema watu hao ni mbumbumbu na wanapaswa kupuuzwa.

Akizungumza na RAI mapema wiki hii pamoja na mambo mengine alizungumzia hali ya kisiasa nchini na kutoa tahadhari kwa Watanzania katika kulinda amani na utulivu uliopo nchini.

RAI: Unazungumziaje uongozi wa Rais Magufuli ukilinganisha na awamu zilizopita?

LUSEKELO: Utawala wa Rais Magufuli una kasi kubwa, licha ya wananchi kulia ukata, watacheka baada ya mwaka mmoja wataona mafanikio yake, kwa sababu amekuwa ni kiongozi mtekelezaji, kila kona ya nchi sasa kazi zinafanyika. Na sasa ameijenga taswira nzuri ya Tanzania.

Nashangaa kuona watu wanamsema vibaya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, nadhani waache mara moja kwa sababu amefanya kazi kubwa. Kikwete alikuwa Rais mpole na mwenye huruma ambaye aliendesha nchi katika hali ya utulivu mpaka anamaliza muda wake.

Ni jambo la ajabu iwapo Watanzania watampuuza kiongozi huyo.

Huwezi kusema kuwa Kikwete kasababisha watumishi hewa, ukwepaji wa kodi maana inawezekana ndiye aliyemkabidhi Rais Magufuli haya anayoshughulikia leo.

Ni vema Taifa likaepuka siasa za maji taka kwani hazifai katika kuendesha nchi.

RAI: Unafikiri mtindo wake wa utumbuaji majipu ambao kwa sasa amekuwa kimya na ule wa kubana matumizi zitamfikisha katika malengo yake?

LUSEKELO: Tumempata Rais anayetafsiri mawazo ya wananchi kwa vitendo, kupambana na rushwa, ufisadi na anakusanya kodi. Si rahisi kumfukuza kazi mke wa makamu wa Rais mstaafu, lakini yeye anaefanya hilo. Rais ambaye hatamani kwenda Ulaya. Nawaambia subiri baada ya mwaka matokeo mtayaona la maana mpeni ushirikiano.  Sizungumzi haya kwa ajili ya kujipendekeza, sihitaji ukuu wa wilaya.

RAI: Nini kifanyike ili kurudisha hali ya utulivu wa kisiasa nchini kwa kuwa wabunge wa upinzani hawakushiriki baadhi ya vikao vya Bunge na baadhi yao wamesimamishwa kutoshiriki.

LUSEKELO: Ule ni mchezo sawa na Tom na Jerry, wote wamekosea, si vizuri kuendeleza huo ulevi wa madaraka. Dk. Tulia bado hajapevuka katika uongozi wa Bunge na ubunge kapewa.. hakugombea, lakini wabunge nao wanaongozwa na kanuni na taratibu.

Mtanzania anayejua historia ya nchi yake hawezi kufumbia macho suala hilo. Binafsi nawalaumu waliotoka (wabunge wa upinzani) na waliobaki (wabunge wa CCM). Kushindana si kuzuri. Mbatia (James Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na wenzake wanapaswa kujua kuwa naibu spika ni mchanga katika siasa waende naye taratibu maana kapewa ubunge tu na kuwa naibu spika.

Nashangaa wazee kama Salim (Ahmed Salim – Waziri Mkuu mstaafu), Pinda (Mizengo – Waziri Mkuu mstaafu) na Warioba. Sijui walishindwa nini kukaa na wabunge hawa ili kumaliza tofauti zao.

Ila katika suala la Bunge kurushwa ‘Live’ hata mimi kwa kweli nimefedheshwa, hivyo viongozi wanapaswa kuepuka kukomoana katika masuala yahusuyo Taifa.

Kwa hatua tuliyokuwa tumefikia Bunge hilo kuwa ‘live’ lilikuwa linaleta afya katika siasa. Si lazima kujifananisha na mabunge ya nchi nyingine eti hayarushi live.. kwani ni lazima kuiga kila kitu? Sisi tuanze kurusha ‘Live’ na wao wataiga kwetu kwa sababu wabunge waliokuwa wakilala bungeni tumewaona hawajarudi.

RAI: Unazungumziaje watu wanaodai kuwa Rais Magufuli ni ‘dikteta uchwara’ kwa kuwa amepiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa na mambo mengine?

LUSEKELO: Rais si dekiteta uchwara kama wanavyodai, ingawa ni kweli amepewa madaraka makubwa ndiyo maana Mapendekezo ya Katiba ya Warioba yalitaka Rais apunguziwe madaraka.

Leo mtawala akitaka mkutano polisi atamzuia vipi wakati mkuu wa jeshi hilo ameteuliwa na Rais? Rais pia ni amiri jeshi mkuu.

Rais ana madaraka makubwa lakini huwezi kujua pengine hali hiyo ndiyo inasababisha amani na utulivu wa Taifa miaka yote.

Kama utaruhusu watu kufanya mikutano huku kuna dhana ya kuibiwa kura hali inaweza kuwa mbaya hivyo ni vema viongozi wa vyama vya siasa wakatumia nafasi hiyo kufanya  siasa za utawala zaidi badala ya maandamano na mikutano ya hadhara.

Hivi watu 10,000 wakiandamana na kusema Magufuli aliiba kura itakuwaje? Tuna askari wa kuwazuia! Nadhani wanasiasa wafanye kazi ya utawala katika vyama vyao. Tutulie kwanza tutibu majeraha. Hakuna jambo baya kama kuwaongoza watu wenye njaa maana hawana la kupoteza

Kenya kuzuia maandamano ni ngumu sana lakini hapa kwetu hadi Zitto (Kabwe-Kiongozi wa ACT-Wazalendo) alizuiwa kufanya mkutano wa ndani. Kwetu rais ana madaraka makubwa sana hivyo umefika wakati wa polisi kutekeleza wajibu wao vyema, wakumbuke kuwa nao ni binadamu pia.

RAI: Unatoa wito gani kwa Watanzania kurudisha hali ya utulivu wa kisiasa nchini?

LUSEKELO: Katika mchakato uchaguzi mkuu kwa chama tawala kupata mgombea wake wa urais kulikuwa na watu wenye majina makubwa, akiwamo Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.

Niliwaambia CCM, Membe huwezi kumpuuza, Lowassa naye huwezi kumpuuza maana wanataka madaraka na kwa vyovyote lazima mtapata mtikisiko. Nikawaomba waahirishe suala la kupata Katiba Mpya maana wasingelimaliza na muda ulikuwa mfupi…Kama mwaka huu hautatumika kutibu majeraha yaliyotokea huko nyuma, tutaharibikiwa sana.

Mchakato wowote wa uchaguzi na kura ya maoni ndani ya vyama huacha mpasuko na watu hutumia dini na ukabila kubaguana, hivyo lazima baada ya uchaguzi mambo hayo yamalizwe.

Tunapaswa kukumbuka kuwa wote ni Watanzania tusahau uchaguzi. Sasa ni wakati wa kuijenga nchi. Amani inatengenezwa, na Mungu huwapa hekima maana kujenga ni kazi na kubomoa ni rahisi, huu ni mwaka wa uponyaji na kurejesha Taifa pamoja.

Kuanza kubagua watu kwa sababu walitoka CCM kwenda Chadema au kutoka Chadema kwenda chama tawala si jambo sahihi kwani tunaona yanatokea kwa nchi ya Sudani kusini, imevurugika kwa kuendekeza siasa za chuki na uhasama. Nawaambia ile nchi itakuwa kama Somalia, itawachukua muda mrefu sana kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.

RAI: Unafikiri ni sahihi viongozi wa dini kujihusisha na majibizano ya kisiasa na kuonesha wazi hisia zao kwa mwanasiasa fulani?

LUSEKELO: Ukienda mahali ukimsikia mtu anasema usilete siasa hapa huyo atakuwa ni mbumbumbu na limbukeni kwani hata vitabu vya Mungu mambo ya siasa yalizungumzwa.

Siasa ni maisha ya watu kama kuna mtu anayedhani haitakiwi kwa viongozi wa dini kuzungumzia siasa atakuwa na tatizo la nufahamu kwani siasa ni kila kitu, ni afya na ni eneo linalotoa maamuzi mbalimbali.

RAI: Katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM ulifanikisha kumteua Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, ulighubikwa na makada waliokuwa wakiwataja na kuwatupia vijembe mara kwa mara mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Sumaye kuwa, unafikiri hatua hiyo inaleta afya gani katika siasa?

LUSEKELO: Nani! Lowassa… jina lake kutajwa sana katika vikao vya CCM. Hiyo inaashiria kuwa ni mtu tishio… Ndiyo ni tishio.

Hilo lilidhihirika hata katika mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa urais, kutokana na Lowassa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa. Kitendo Lowassa kuzua mjadala katika mkutano huo sambamba na wimbi la makada wanaohama vyama vyao, niseme tu kwamba haya si mambo yanayopaswa kuwa mjadala kwa sababu uchaguzi ulishapita.

Lakini nisema jambo moja kuwa kuna fununu za Nabii maarufu wa Bara la Afrika, Temitope Belgun Joshua (TB) wa kanisa la Kimataifa la The Synagoge Church of All Nations (SCOAN) kwamba anatarajia kuja nchini hivyo ni vema akaja yeye  binafsi na si kwa mwaliko wa Ikulu.

Kwa sababu iwapo ikulu itamkaribisha kiongozi huyo basi Rais Magufuli ajiandae kupata laana zikiwamo mvua zisizokwisha.