Home Habari NAIBU WAZIRI: KUTEULIWA NA JPM NI MTIHANI

NAIBU WAZIRI: KUTEULIWA NA JPM NI MTIHANI

4460
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


NAIBU Waziri- Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira, Mussa Sima amesema kuwa kitendo cha kuteuliwa na Rais Dk. John Magufuli ni mtihani mkubwa.

Sima alisema mtihani huo unakuja katika kuitunza heshima ya kuwatumikia wananchi aliyokupatia.

Alisema ugumu zaidi wa uteuzi wa JPM unasababishwa na mwelekeo na aina mpya ya utendaji wake unaowasukuma wasaidizi wake kwenda na kasi anayoihitaji.

Rais Magufuli kwa nyakati tofauti ametoa maagizo kedekede kwa mawaziri wake huku baadhi yao akiwasema hadharani namna wasivyoweza kumvutia katika utendaji wao na hata kuwaasa kuwa huu si wakati wa kubembelezana kwa kuwa uchaguzi umekaribia.

Rais alipata kusema kuwa zipo wizara ambazo bado hazijamshawishi ikiwamo wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya utawala wake, ameshawaondoa mawaziri wawili.

“Wizara ya Mambo ya Ndani ni Wizara ambayo haija ni ‘Impress’ inafanya vibaya vibaya mno. sijawa ‘Impressed’ kabisa lazima niseme ukweli, ” alisema Rais Magufuli wakati akiwaapisha baadhi ya mawaziri.

Sima ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Julai mosi mwaka huu aliteuliwa na Rais Magufuli kushika wadhifa wa Naibu Waziri jambo ambalo anakiri kuwa kitendo cha kuteuliwa na Rais ni heshima kwake na kwamba anajiona anafaa kuwa msaidizi wake katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

Akizungumza na RAI katika mahojiano maalumu yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, pamoja na mambo mengine Sima alisema licha ya kuwa na mtihani wa kuitunza heshima aliyopewa na Rais pia ni mtihani katika kutekeleza maagizo ya serikali na chama tawala kwa kupitia ilani yake kama inavyoelekeza

“Nafasi hii niliyopewa na Rais Magufuli niliipokea vizuri na kwa hali chanya kwa sababu ukishateuliwa maana yake unapewa jukumu la kumsaidia Rais. Hii ni heshima, kwamba unafaa kwa wakati huo. Ila kwa upande wa pili ni mtihani kuitunza hiyo heshima na kutekeleza maagizo ya Rais na chama chetu kwa kupitia ilani yake kama inavyoelekeza,” alisema.

Aidha, alisema baadhi ya maagizo ambayo Rais Magufuli aliyatoa kwa wizara anayoiongoza tayari yameshatekelezwa ikiwamo lile la Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kutoa kibali kwa kiwanda cha betri – Kibaha.

“Ili kutekeleza majukumu yangu kwa umakini na uweledi hasa ikizingatiwa wizara hii ni kubwa, tayari nimekaa na watendaji wote akiwamo Waziri ili kujifunza mambo ambayo wanayatekeleza na changamoto wanazokutana nazo, lakini pia nimeandaa mpango wangu ambao naweza kushauri namna tunavyoweza kufikia malengo yetu kama wizara.

“Rais aligusia mambo mengi ikiwamo suala la NEMC, kwamba inachelewesha kutoa vibali na mfano kile kiwanda cha betri – Kibaha. Nieleze kwamba hili ni jambo la kwanza ambalo nimelifanyia kazi  na wiki iliyopita tayari NEMC wamewapatia kibali,” alisema.

SAKATA LA NAPE

Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri huyo aliwashauri baadhi ya makada na viongozi wa CCM wanaomkosoa Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kwa mienendo yake dhidi Serikali na chama kuwa, wakiachie chama ndicho chenye mamlaka.

Tunaona kuwa kila mtu ana mtazamo wake, mwingine anaweza kuona Nape anakosea au anakosoa, ila mwenye mamlaka ni chama. Sisi watu wa pembeni wote tunaweza kumuangalia kwa mtazamo kwamba labda anadhalilisha, ila chama kinatutazama wote kuwa nani anakwenda kwenye mstari sahihi au si sahihi. Kwa hiyo ataitwa kwenye vikao kama anakosea na chama kina utaratibu wake hivyo sisi hatuwezi kuanza kumshutumu mtu wakati hatuna mamlaka hayo zaidi ya chama,” alisema.