Home Burudani BROTHER K: Nakesha kufikiria namna ya kuwachekesha watu

BROTHER K: Nakesha kufikiria namna ya kuwachekesha watu

5582
0
SHARE

brother-k-wa-futuhiNA EMILIANA CHARLES (TUDARCO)

UKIMTAJA kwa jina la Adrew Ngonyani, unaweza kumtafuta siku nzima bila mafanikio, au unaweza kupelekwa kwa kina Andrew wengi. LAkini ukimtaja kwa jina la Brother K kila mtu atakupleka kwa muigizaji wa kikundi cha Futuhi  linalorusha michezo yake kwenye kituo cha Star Tv.

Brother K ni jina maarufu sana hivi sasa nchini katika sanaa ya vichekesho, staili yake ya uigizaji na vituko vyake vimemfanya kijana huyu kujipatia mashabiki wengi kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Lafudhi yake ya Kiha, inawafanya watu wengi kuamini kwamba msanii huyo ni Muha, lakini jina lake na Ngonyani linaashiria kwamba Brother K ni Mngoni kutoka mkoani Ruvuma.

Hajakaa Ruvuma, alizaliwa mkoani wa Tabora na kukulia katika mikoa hiyo ya kanda ya Maharibi kwa maana ya Tabora na Kigoma, na alikuwa kinara wa maigizo na muziki tangu alipokuwa katika shule ya msingi.

Alitumia muda wake aliokuwa shuleni kuchekesha wanafunzi wenzake  akishirikiana na rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Jose na walikuwa wakipita madarasani kufanya vituko vya aina mbalimbali lakini pamoja na hayo yote hakujua kuwa ana kipaji cha uigizaji hasa katika fani ya vichekesho katika kipindi hicho.

Kwa upande wake wakati akiwa mdogo alikuwa anapenda sana muziki yaani kuimba hii ndio sababu iliyopelekea yeye kushindwa kutambua kipaji chake hicho tangu mdogo ingawaje alikuwa anakitumia mara nyingi wakati akiwa shuleni.

“Usanii wangu ulinipa marafiki wengi na nilijichanganya na kila mtu, nilishiriki kwenye shughuli za vijana kwetu Tabora na hata nipokwenda Kigoma kwa lengo la kutafuta maisha nilikuwa nifanya shughuli nyingi na vijana zikiwemo za usanii katika uimbaji na uigizaji,” anasema.

Licha ya kufanya harakati nyingi za kisanii, katika muziki, hakutoka lakini pia katika uigizaji hakupata nafasi ya kuvuma kwa kuwa kazi nyingi za uigizaji alizifanya katika mlengo wa uelimishaji.

Kama unamfahamu katika uchekeshaji basi kuna wengine wanaomfahamu Brother K kama msanii wa muziki ambapo anaimba mitindo ya R’n’B pamoja na Bongo Fleva ingawa pia anaweza kuimba katika mitindo mingine ya muziki.

Ametoa wimbo mmoja unaokwenda kwa jina la Hadija ambao haijapata umaarufu sana na sasa kuna nyimbo nne katika mtindo wa Bondgo flava  ambazo hivi ataziachia katika siku za hivi karibuni.

Brother K ameliambia RAI kuwa mwaka 2011, ndio ulijenga historia mpya kwa Brother K hasa baada ya kuamua kujiunga na kundi la Futuhi ambalo ndio analifanyia kazi mpaka hivi sasa na watu wengi wamemfahamu kupitia huko.

Akizungumzia maendeleo na mafanikio yake katika sanaa anasema kuwa mwanzo kabla hajaanza maisha alikuwa anaishi nyumbani kwao Tabora lakini pindi alipojiunga na Futuhi alihamia Mkoani Mwanza na kuanza maisha yake na kisha kununua usafiri wake binafsi na ameanza kujenga nyumba yake.

Aliendelea kusema kuwa Futuhi imemsaidia kujulikana sehemu mbalimbali za ndani na nje ya nchi ya Tanzania hii kwake ni moja kati ya maendeleo aliyoyapata.

“Nimeoa n anima mtoto, naiendesha familia yangu bila matatizo yoyote kutokana na kazi hii ya kuchekesha watu, haya ni maendeleo makubwa sana kwangu ingawa yanaweza kuwa si makubwa sana kulingana na watu wanavyoniona kwenye televisheni lakini hiyo ni kutokana na halio halisi ya sanaa hapa kwetu,” anasema.

Anasema kazi za sana bado hazijaanza kuwanufaisha wasanii hasa wale wasanii wa mikoani, kutokana na ukweli kwamba watu wanaoshikilia kazi za wasanii kuwa na nguvu zaidi na kuwa na mwanya wa kunufaika wao kuliko wasanii.

“Nina kila sababu ya kujivunia Futuhi maana imenifikisha hapa nilipo sasa na haya maendeleo yote niliyonayo,” alisema Brother K.

Aliongeza kwa kusema kuwa Futuhi imemkuza kisanii na kuelezea kwamba fani ya uchekeshaji ina mashabiki wengi na inalipa sana ingawa kwa Tanzania bado haijaonyesha kulipa kama nchi zingine.

“Kwa upande wangu ninawashuru sana wenzetu waliotangulia kwenye tasnia hii ya uchekeshaji akiwemo King Majuto, Masanja na kundi zima la ‘Ze Comedy Show’ kwa kuwa wamesababisha sasa hivi uchekeshaji kuwa na chati kubwa,” anasema.

Kuhusu ushindani wa vipindi vya komedi, Brother K anasema ushindani huo unachochea maendeleo ya fani hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza ubunifu kwa wasanii kutokana na ukweli kwamba kila kikundi kinataka kuwa juu.

“Kwanza watu wafahamu kwamba kuchekesha si jambo rahisi, ni kazi ngumu sana kuliko uigizaji wa kawaida, inahitaji mtu ufikirie namna ambayo inaweza kuwachekesha watu kwa ustadi na wasikuchoke, ni kazi inayohitaji ubunifu wa hali ya juu sana. Binafsi huwa nakesha nikifiria namna ya kuwafanya watu wacheke,” anasema.

 

Msanii huyo anasema kuwa hana mpango wa kuacha uchekeshaji na hiyo ni kazi yake ya maisha na anaipenda sana kwa kuwa asipoifanya kazi hiyo anahisi yupo kifungoni au kama mtu ambaye anaumwa.

Malengo ya msanii huyo hapo baadae ni kufungua kampuni yake binafsi na yupo katika maandalizi hayo kwa kuwa katika kipindi hiki yuko chini ya mtu hivyo anafanya kazi za watu na hawezi kukiuka mkataba.

“Nitafungua kampuni yangu,nitakuwa na vijana ambao tutafanya kazi hii, nitatafuta vipaji na kuajiri watu na kampuni hiyo tutajihusisha na uchekeshaji tu,” anasema.

Msanii huyo mbali ya uchekeshaji na muziki pia ni mjasiliamali anayefuga kuku na pia ana bodaboda zake ambazo ameajiri vijana hii ikiwa ni njia nyingine inayomsaidia yeye kuongeza kipato chake na kujikimu kimaisha.

Akizungumzia changamoto anazozipitia Brother K anasema moja ya changamoyo hizo ni kubuni vichekesho kila siku. “Hii ni changamoto kubwa sana, lakini hii ni ya kikazi, changamoto zingine ni pamoja na kukatishwa tamaa na watu ikiwemo watu kuniambia kuwa sina mvuto wa kuwa mchekeshaji,” anasema.

Toka aanze kuchekesha hajawahi kufanya filamu ya kawaida ambayo sio ya kuchekesha na hana mpango wa kufanya hata hapo baadaye kwa kuwa anapenda sana uchekeshaji na kwa upande wa wasanii wenzake wa vichekesho anawaona wanafaa na ni wakali na anatamani siku moja afanye nao kazi kwa kuwa kila mmoja ana staili yake ya uchekeshaji kama Kitale, Kingwendu na wengineo na anawakubaki sana.

Msanii huyo ametoa ushauri kwa wasanii wenzake kwa kusema kutokana na utandawazi uliopo kwasasa umewafanya wasanii wengi kuiga mambo mabaya ikiwemo kutumia madawa ya kulevya na mengineyo hivyo basi amewaomba waache kufanya hivyo kwa kuwa sio kitu kizuri maana wasanii ni kioo cha jamii na mfano wa kuigwa kwa watu.

Brother K alisema kuwa wasanii wakubwa wanaoigiza filamu za kawaida waache kukariri na huku akiwataka kuendelea kuigiza filamu za kwaida balada ya kuanza kuigiza filamu za vichekesho ambazo hawaziwezi na matokeo yake wanaharibu.

Ameiomba Serikali iwasaidie wasanii kwa kuwa sanaa ni moja ya sekta zilizotoa ajira kwa vijana wengi sana hapa nchini. Amesema kuwa pamoja na kuwa Mheshimiwa Nape Nnauye anafanya kazi nzuri sana lakini nguvu inatakiwa iongezeke ili kusaidia wasanii katika suala zima la haki zao za msingi katika kipato chao ambacho kinawasaidia kujikimu katika maisha yao.