Home Latest News Nani alishuhudia ‘magaidi’ wakiteka ndege?

Nani alishuhudia ‘magaidi’ wakiteka ndege?

1438
0
SHARE

airportNa William Shao

KATIKA mfululizo wa makala zangu katika toleo lililopita, nilionyesha kile kinachonifanya nisiamini hata kidogo—kwa mujibu wa vyanzo vingi vya habari—kuwa Mohamed Atta anayedaiwa kuwa kiongozi wa ugaidi ndiye aliyeshiriki katika ugaidi huo.

Hiyo inanipa sababu ya kuamini kuwa Atta hakuwa gaidi kama ilivyodaiwa. Lakini kama hakushiriki, inawezekana pia hata wanaodaiwa kushirikiana naye nao hawakushiriki pia. Kama hivyo ndivyo, ni nani basi aliteka ndege zile Septemba 11, 2001?

Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) waliiambia dunia kuwa siku ile ya Septemba 11, 2001 ndege zote nne zilitekwa na Waarabu 19, kila kundi likiwa na marubani wake ambao baada ya kuziteka walizirusha na kuzibamiza kama walivyokusudia.

Lakini kikwazo cha uwezekano wa kukubaliana na madai hayo ni kwamba majina ya watekaji hao hayakuwa katika orodha ya abiria wa ndege hizo.

Tatizo jingine ni kwamba taarifa hiyo ya FBI, au tuseme taarifa rasmi ya Serikali ya Marekani, ni kwamba, ingawa tunaambiwa kuwa watekaji wanne au watano walikuwa kwenye kila ndege katika zile nne zilizotekwa siku hiyo, hakuna ushahidi wowote wa madai haya uliowahi kutolewa.

Kama wale wanaodaiwa kuwa ni watekaji walikuwa katika ndege hizo, bila shaka hawakutumia mabavu wakati wakipanda ndege hizo. Walipanda wakiwa na tiketi zao kama abiria wengine, na hivyo ni lazima wangekuwa kwenye orodha ya abiria wa ndege hizo sawasawa na abiria wengine.

Kama walitumia njia za kawaida kabisa kupanda ndege hizo, basi ni lazima majina yao yangekuwa kwenye orodha iliyotolewa na mashirika ya ndege. Lakini orodha iliyotolewa haikuwa na jina hata moja la wale waliotajwa kuwa watekaji.

Madai ya kwamba majina ya abiria wengine hayakuwekwa kwenye orodha kwa sababu ndugu zao wa karibu walikuwa hawajaarifiwa hayana msingi wowote. Huwezi kuficha jina la mtu ambaye tayari umeshamtaja.

Kwa mujibu wa taarifa za FBI, kulikuwa na zaidi ya gaidi mmoja katika kila ndege iliyohusika katika tukio la Septemba 11. Lakini FBI hawakusema kama ‘watekaji’ hao walitumia ‘njia za panya’ kupanda ndege hizo au walitumia njia halali kama wale abiria wengine.

Kama walitumia njia haramu, kwanini hawakugunduliwa, au angalau kutiliwa shaka? Na kama walitumia njia haramu, walifanya hivyo kwa ndege zote nne ndani ya muda wa saa moja tu?

Tuchukulie kwamba waliingia ndani ya ndege hiyo bila kugunduliwa. Kama hivyo ndivyo, basi kulikuwa na watu wa ziada katika kila ndege. Hawakuwaona kabla ndege hazijapaa? Tunaweza kukubali kuwa katika ndege zote nne watu hao hawakugunduliwa, lakini tukubali kwamba wafanyakazi wa ndege waliona watu wengine wa ziada katika ndege hiyo ambao hawakuwa katika orodha ya abiria na bado hawakufanya lolote kabla ndege hazijapaa?

Hakukuwa na ukaguzi wowote kabla ndege haijaondoka uwanjani? Ingelikuwa ni ndege moja tu iliyokumbwa na zahama hiyo tungeweza kusema ‘sawa’, lakini tuamini tu kwamba katika ndege zote nne hakuna mfanyakazi hata mmoja, awe wa uwanja wa ndege au mhudumu yeyote katika ndege, aliyeshtuka mapema kwamba kuna hali isiyo ya kawaida?

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, mkaguzi wa tiketi za abiria katika Uwanja wa Ndege wa Boston Logan, Gismond Pepin, alipohojiwa aliwaambia wapelelezi wa FBI kuwa hakuona jambo lolote lisilo la kawaida, “Vinginevyo ningewapasha habari wakuu wangu wa kazi,” alisema Gismond.

“Waliniuliza kama niliona jambo lolote ambalo halikuwa la kawaida,” alisema, “lakini ningeliona ningemwambia meneja wangu kama ningekuwa nimeliona kwa wakati huo, lakini kwa bahati mbaya, hakukuwa na jambo lolote la kutiliwa shaka.”

Hakuna kidokezo chochote cha serikali ya Marekani kinachosema ndege hizo zilitekwa zingali ardhini. Ingekuwa ndivyo, zisingepaa angani, au angalau amri ya ‘magaidi’ ya kupaisha ndege ingesikika kutoka kwa watekaji.

Haijulikana kama iliwahi kutolewa orodha iliyokamilika inayoonesha idadi ya abiria wote na majina yao, wakiwamo Waarabu 19 wanaodaiwa na FBI kuwa walitekeleza ugaidi wa Septemba 11.

Turudi pale pale mwanzoni. Kama kweli yule anayedaiwa kuwa alikuwa kiongozi wa watekaji siku hiyo, yaani Mohamed Atta, alikuwa kwenye ndege Flight 11, kwanini jina lake halikuwamo katika orodha ya abiria waliopanda ndege hiyo na wakati tuliambiwa kuwa alikuwa na tiketi?

Kama alikuwa katika ndege hiyo, na bado jina lake halikuwamo, aliingiaje katika ndege hiyo? Kwa waliofuatilia kwa makini habari za abiria wa ndege zile watakuwa wanajua kuwa orodha ya abiria hao iliyotolewa na Shirika la Habari la Marekani, Associated Press (AP), Septemba 17, 2001 ilitegemea habari zilizotolewa na “wanafamilia, marafiki, wafanyakazi wenza na mawakala wa serikali.”

Kwanini mawakala wa serikali ya Marekani, kama mashirika ya ndege, hawakuweza kuyaweka katika orodha hiyo majina ya wale wanaodaiwa kuwa ni Waarabu 19 walioteka ndege zile?

Ingawa hakukuwa na majina ya Waarabu katika orodha zote za abiria wote waliokuwa katika ndege zile, Septemba 28, 2001—siku 17 baada ya mashambulizi hayo—FBI ilidai kuwa ilikuta wosia na maelekezo ya maziko katika mkoba wa Mohamed Atta aliouacha katika Uwanja wa Ndege wa Logan.

Huo ni mkoba unaodaiwa kuwa ni wa kiongozi wa watekaji ambaye yeye mwenyewe anadaiwa kuiteka ndege ‘Flight 11’ iliyopaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Boston kwenda Los Angeles na kisha kuibamiza kwenye moja ya minara miwili ya majengo ya WTC.

Kwa kuwa jina la Mohamed Atta halikuwa katika orodha ya abiria wa ndege ile, je, tuamini kwamba mkoba wake ulikuwa na jina lake lakini tiketi yake ikawa na jina jingine? Kama hivyo ndivyo, hilo jina jingine lilikuwa la nani? Na kama alitumia jina lake, kwanini halikuwa katika orodha ya majina ya abiria waliopanda ndege hiyo?

Zaidi ya hilo, kama mkoba huo haukuwa na jina la Kiarabu, ambalo lingeshukiwa kuwa mojawapo ya majina ya watekaji, kwanini FBI waliufungua mkoba huo badala ya kuurudisha kwa anuani iliyoandikwa juu yake?

Taarifa ya kurasa 585 ya The 9/11 Commission ya Serikali ya Marekani haikuzungumzia sana suala hilo, pengine kwa sababu haikuwa na majibu. Njia pekee ambayo mashirika ya ndege yangeitumia kuijua idadi ya abiria wote waliokuwa katika ndege zake ni kwa kutumia orodha ya majina ya abiria waliopanda ndege siku hiyo ya tukio. Lakini hawajatoa sababu ya msingi ni kwanini hawakutoa orodha ya majina yote na badala yake wakatoa sehemu yake tu.

Sababu ya kwanza ya kutotoa majina yote kwenye orodha ya abiria ilidaiwa kuwa “ndugu wa karibu walikuwa hawajafahamishwa”. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu moja, lakini haikuwa sababu pekee. Pengine ilikuwa ya kwanza, lakini haikuwa ya mwisho.

Mashirika ya ndege yalipobanwa na waandishi wa habari ikapatikana sababu nyingine. Wakadai kuwa baadhi ya familia za waliokufa katika ndege hizo ziliomba majina ya wanafamilia hao yasitajwe.

Kwa mchambuzi aliyesoma habari hizo ataona majibu hayo ni kituko, hususan unapochukua sababu ya kwanza ukaioanisha na sababu ya pili. Walitaka tuamini nini? Kwamba ndugu wale wale ambao hawakuwa wamefahamishwa kuhusu ndugu zao kufia kwenye ndege zilizotekwa ndio ndugu hao hao walioomba majina ya ndugu zao waliokufa yasitajwe?

Yaani ndugu ambao hawakufahamishwa kuhusu ndugu zao kufia katika ndege ndio hao hao wanaomba ndugu zao hao wasitajwe? Hicho ndicho walitaka tukiamini?

Msemaji wa Shirika la Ndege la ‘American Airlines’, Tim Kincaid, alipohojiwa na David Icke, mwandishi wa kitabu ‘Alice in Wonderland’ © 2002, kueleza kwanini kuna baadhi ya majina ambayo hayakuwamo katika orodha, alijibu kwa mkato: “Waulize FBI.”

Ingawa FBI hawakuwako wakati shirika hilo likiandaa orodha ya abiria wa ndege zake, sasa ikaonekana kana kwamba FBI ndio ambao wangeweza kulisemea. Kwanini?

Msemaji wa shirika la ndege la ‘United Airlines’, Rich Nelson, alipohojiwa kuhusu suala hilo, alimwambia mwandishi wa ‘Alice in Wonderland’ kuwa waliruhusu tu kuchapishwa kwa majina ya watu ambao wanafamilia waliruhusu yachapishwe. Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa.

Hayo ndiyo majibu ya tikitaka. Tukutane toleo lijalo.