Home Uchambuzi NANI HASA MCHAWI TUMTELEKEZE JANGWANI?

NANI HASA MCHAWI TUMTELEKEZE JANGWANI?

2496
0
SHARE

NA BOLLEN NGETTI

BUSARA inanitaka kutumia parandesi ya maneno kutambulisha safu hii mpya katika gazeti kongwe ikiwa ni kutaka kumfahamisha msomaji nini hasa shabaha ya kuwepo kwa safu hii.

Naam. Mtu anaweza kujiuliza ni kwa nini safu hii ibatizwe/isilimishwe jina la “Safari ya Kaanani?” Ninatambua uwepo wa dini nyingi tu hapa nchini lakini ukweli uliobayana ni kwamba dini kuu zinazochomoza kama pembe za ng’ombe ni Ukristu na Uislamu. Hilo si la kubishania hadi kuku warejee bandani. Ndio, ni Ukristu na Uislamu!

Katika dini hizi kuu mbili tunasadikishwa kupitia misaafu yao (Kuran na Biblia) kwamba wana wa Israeli waliokamatwa na kufanywa watumwa Afrika (Misri) kwa miaka mia nne walifikia hatua ya kutoroka kutoka katika makucha ya dikteta Farao wa Misri kwenda nchi ya ahadi kama walivyoahidiwa na Mungu wao chini ya uongozi mahiri na makini wa Nabii Musa, yaani Kanaani. Kwamba baada ya mateso makali ya kazi za suruba, kudhalilishwa, kubezwa, kuvunjiwa haki za kibinadamu, kukosa uhuru wa kujieleza na kusikilizwa, kunyanyaswa kwa kila namna, hatimaye Mungu wao alifanikiwa kuwatorosha kutoka Misri kwenda Palestina iliko nchi hiyo ya ahadi.

Kwa mujibu wa historia ya maandiko matakatifu na teolojia ni kwamba watu hawa walitakiwa kutumia siku arobaini (40) kutoka Misri hadi Kaanani lakini cha ajabu ni kwamba wana hawa wa Kiebrania walitumia miaka 400 kufika Kaanani. Lakini pamoja na yote hata kiongozi wao Musa hakuweza kufika Kaanani bali alioneshwa kwa mbali kabla ya kufa na Joshua na Kalebu kuchukua usukani kuwavusha Waisraeli.

Historia inatueleza kuwa safari hii ilikuwa ngumu mno jangwani iliyojaa mabonde, milima, miiba, taabu kiasi kwamba wakati mwingine ilibidi wananchi hawa wa Israeli kumuasi Mungu wa Musa na kujiundia mungu wa kuchonga, mungu ndama wa dhahabu. Lakini kinachofurahisha ni kwamba pamoja na uasi huu wa kudai demokrasia na uhuru wa kuabudu, Musa hakuamuru FFU wala Polisi kuwapiga ama kuwatawanya kwa maji ya kuwasha bali alitumia hekima na busara alizojaaliwa na Muumbaji kutuliza “munkari” yao huku akiwatangulia mbele na fimbo iwakayo moto nyakati za usiku hadi walipofika nchi ya ahadi kwa kuchelewa.

Lakujiuliza ni kwa nini wananchi hawa wa Israeli walikawia kufika Kaanani? Nini hasa vilikuwa vikwazo? Hata hivyo, hatimaye walifika katika nchi ya babu zao waliyoahidiwa na Mungu wao (hata kama wamepora ardhi ya Palestina) wakijulikana kama “wazururaji”.

Msomaji wa safu hii mpya, mwaka 1961 nchi yetu ya Tanganyika kisha Tanzania ilijipatia uhuru wake kutoka katika makucha ya wakoloni yaani Waarabu, Wajerumani na mwisho Waingereza. Tukiwa utumwani chini ya mbawa na kwapa chafu za wakoloni tulinyanyaswa, tuliteswa, tulibezwa na kudharauliwa kuanzia na tamaduni zetu, dini zetu, uafrika wetu, elimu yetu. Tuliuzwa kama mbuzi wa shughuli mnadani. Hatukuruhusiwa kuwahoji watawala juu ya ukatili wao kwetu maana hiyo ilikuwa ni dhambi ya mauti. Mkoloni alikuwa ni katili mno kwetu kiasi kwamba udhalilishaji kwa wanawake ulionekana burudani kwa wakoloni. Hakika kilikuwa ni kipindi kigumu mno kwa babu zetu ambao hatimaye waliamua “kujitoa ufahamu” na kuanza kupambana na wakoloni iwe ni kwa silaha (Chifu Mkwawa) iwe ni kwa diplomasia (Mwalimu Nyerere) lakini mwisho tulishinda tisho. Hatimaye tulipata uhuru na kupandisha bendera yetu ya Uhuru Desemba 9, 1961 saa 6:00 usiku huku wananchi wakibubujikwa machozi ya furaha.

Katika kusherehekea siku hii ya kuachiwa huru ili sasa tujiamulie mambo yetu wenyewe kwa uhuru wetu, yapo mambo kadhaa ambayo wapigania uhuru kama viongozi wetu walituahidi kwamba sasa Tanzania inaanza safari kuelekea nchi ya ahadi kama tulivyoahidiwa katika uwanja wa Uhuru. Kiongozi wetu, Musa (Nyerere) na wenzake walituahidi mambo kadhaa tutakayoyakuta katika nchi ya ahadi. Hata kama Mwalimu alifariki kabla ya kufika katika nchi hiyo ya ahadi lakini alifanya kazi ya kutukuka yenye heshima kubwa kupigania uhuru wetu. Narudia, kupigania uhuru wetu.

Kwamba hatimaye Watanzania nao watafika katika nchi ambayo hakuna mtoto chini ya miaka mitano atakayepoteza maisha yake kwa ugonjwa wa malaria, nchi ambayo kila mama atafungua bomba la maji mita tatu kutoka mlangoni kwake kuchota maji safi na salama, nchi ambayo hakuna mtu atakayepoteza maisha yake kwa kula kinyesi cha binadamu (kipindupindu), nchi ambayo hakuna mkulima atashindwa kufikisha mazao yake sokoni kisa eti barabara mbovu, nchi ambayo hakuna mwanafunzi wa chuo kikuu atakayezurura mitaani na bahasha ya kaki kusaka ajira hewa, nchi ambayo kina mama wajawazito watakuwa na usalama wa kujifungua salama asilimia 100 na kila aina ya “asali”. Hakika ni nchi iliyojaa maendeleo ya kwelu.

Walituambia tunakwenda na watoto wetu, wake/waume zetu, tunakwenda na mali zetu katika nchi ambayo hakuna mwananchi atakayepoteza maisha kwa kukosa chakula, nchi ambayo barabara za lami zitatandazwa kila kijiji, nchi ambayo hata mwenye nyumba ya tembe au nyasi atakuwa na uhakika wa umeme, itakuwa ni nchi iliyojaa kijani kila mahali, nchi ambayo uhuru wa kujieleza na demokrasia pana utakuwa umetamalaki kwa kiwango cha juu. Nchi ambayo Katiba na Sheria za nchi zitaheshimika na kila mtu bila kuangalia cheo chake ama hadhi yake katika jamii. Kwa kifupi itakuwa ni nchi iliyojaa wazalendo, wachapa kazi, hodari, wenye kuheshimiana isiyo na ubaguzi wa rangi, kabila, kanda, dini, jinsia, yaani jamhuri ya waungwana. Nani asiyetamani kufika katika nchi hiyo?

Akiwaaga wakoloni wa Kiingereza usiku ule wa Desemba 9, Mwalimu alisema; “natamani wakoloni hawa warudi hapa nchini Tanganyika baada ya miaka kumi wajionee tutakavyokuwa tumepiga hatua kwa mambo waliyoshindwa kwa miaka zaidi ya arobaini ya kukutawala.” Kwa maneno mengine ni kwamba Mwalimu alikuwa akiwaalika wakoloni waje kuona nchi hiyo aliyotuahidi baada tu ya kuanza safari ya kujitawala tukiwa nchi huru. Yaani kuyafikia mema hayo niliyoorodhesha hapo juu, Safari ya Kaanani ambayo ingetuchukua miaka kumi tu.

Maswali ya kujiuliza ni: kwa nini hatujafika katika nchi hiyo? Nini hasa ni vikwazo? Kina nani wanatukwaza njiani tusifike nchi ya ahadi? Ni taasisi gani inatukwaza tusifike Kaanani ya Mwalimu Nyerere na wenzake? Nani hasa ni mchawi katika safari hii? Nani anayechonga mungu wa ndama? Nini kifanyike ili tuweze kufika katika nchi hiyo ya ahadi?

Joshua wetu (Rais Magufuli) amekuwa akirudia-rudia kauli; “tumechelewa sana, tumechezewa sana, hatukutakiwa kuwa hapa ni lazima tukimbie.” Kauli hii inaashiria kuwa tulipofikia hatufanani na watu waliosafiri miaka zaidi ya 50. Kwamba Mwalimu alitaka tufike nchi ya ahadi baada ya miaka 10 lakini matokeo yake sasa ni zaidi ya nusu karne bado tunazungumzia barabara za juu na treni ya umeme. Ndio maana Rais Magufuli anachanja mbuga huku koti lake likipeperushwa na upepo huku ametushikilia mikono tukimbie naye ili walau tupunguze vikwazo tufike nchi ya ahadi, maendeleo ya kweli.

Msomaji wangu, hii ndio sababu ya safu hii kubatizwa jina la “Safari ya Kaanani.” Katika safu hii kila wiki tutajadili vikwazo vinavyotuzinga kama miiba inayotuzuia kufika nchi ya ahadi. Tutavichambua kwa kina moja baada ya nyingine na kutoa suluhisho nini kifanyike. Ninajua vikwazo ni vingi lakini kupitia safu hii hakuna jiwe hata moja litakaloachwa bila kung’olewa isipokuwa lile moja tu la pembeni walilokataa waashi. Tutajadili masuala ya uchumi, siasa, sayansi ya jamii na maendeleo alimradi tu, tuvijue vikwazo njiani ili tuepukane navyo.

Kwa leo na kwa ufupi sana tunaweza kuona moja ya vikwazo katika safari yetu. Nalo ni baadhi ya wateule wa Rais Magufuli ambao hujifanya vichwa ngumu kutotaka kujua nini Rais alimaanisha aliposema “elimu bure” kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne! Kwamba baada ya kuona ada imefutwa rasmi katika shule zote za Serikali sasa baadhi ya wateule hao wa Mkuu wa nchi wamerudisha ada hiyo kwa mlango wa nyuma. Kwamba sasa inaitwa michango mara ya ujenzi, madawati, chakula, ulinzi, mitihani na majaribio, sare nakadhalika. Hali hii imefanya baadhi ya wanafunzi kushindwa kufika shuleni baada ya shule hizo kufunguliwa Januari 8 mwaka huu.

Hata hivyo tayari “Joshua” kaliona na kuwaketisha Mawaziri wenye dhamana katika sekta ya Elimu yaani TAMISEMI (Suleiman Jaffo) na Elimu (Prof. Joyce Ndalichako) na kuwaagiza kuhakikisha hakuna mwanafunzi hata mmoja atakayerudishwa nyumbani eti kwa sababu ya michango hiyo ya hovyo hovyo. Na kwamba Mkurugenzi yeyote ambaye hili litatokea katika wilaya yake aanze tu safari ya kurudi Misri kabla jua halijazama juu yake: hana kazi!

Hata hivyo, wazazi nao wanapaswa kutobweteka mno na “msamaha” huu. Tukumbuke kwamba kinachoitwa “elimu bure” ni katika ada tu. Lakini wazazi bado wanao wajibu wa kushirikiana na Serikali ya CCM kutekeleza azma hiyo. Mathalan, kumnunulia mwanao vitabu vya ziada ili kumpanua maarifa, kalamu, madaftari na nyongeza nyinge katika kumfanya mtoto kusoma kwa bidii. Kumhimiza kusoma kwa juhudi na maarifa. Tutambue kuwa ili mtoto aweze kufaulu mitihani yake vyema anahitahi ushirikiano wa Mwalimu, Yeye Mwanafunzi na Mzazi. Kila mmoja afanye sehemu yake kwa umakini unaotakiwa. Serikali imefanya sehemu yake, epuka kuwa kikwazo katika safari yetu kuelekea maendeleo ya kweli, Kaanani! Alamsiki!

*Mwanasafu ni Mwandishi, Mchanganuzi na Mtafiti katika masuala ya Siasa na Maendeleo ya Jamii. Anapatikana kwa simu namba 0786 791 229