Home Makala Kimataifa NANI MWENYE HAKI YA KUMILIKI ZANA ZA NYUKLIA?

NANI MWENYE HAKI YA KUMILIKI ZANA ZA NYUKLIA?

1675
0
SHARE
Kituo cha nyuklia cha Israel.

NA HILAL K SUED

Wakati dunia inashuhudia hali ya kutishiana misuli kati ya nchi ndogo ya Korea ya Kaskazini na Marekani, hali ambayo imeleta hofu ya kutumika kwa zana za kinyuklia, swali moja kubwa limekuwa likiulizwa ni nani hasa mwenye hati miliki ya zana hizo.

Kwa mfano propaganda za muda mrefu za nchi za Magharibi kupitia vyombo vyao vya habari zimekuwa mstari wa mbele kuuambia ulimwengu kwamba Israel ama haina zana za kinyuklia, na kama inazo basi zana hizo ziko katika mikono salama, kuliko zile ambazo Iran ingeachiwa kuzitengeneza.

Lakini kutokana na vyanzo vya kuaminika vya nchi hizo hizo za Magharibi, Israel inamiliki mabomu ya nyuklia kati 80 hadi 400 katika ghala yake iliyoko Dimona katika Jangwa la Negev. Nchi hiyo ilikuwa ya sita duniani katika kutengeneza zana hizo kwa ushirikiano na wanasayansi wa Ufaransa na zana ya kwanza ya nyuklia ilikamilishwa mwaka 1966.

Wachunguzi wa mambo wamekuwa wakisema iwapo Iran itatuma mabomu yake (yaani iwapo itakuwa nayo hapo baadaye) kulitekeleza taifa la Israel, nyambizi za kinyuklia za Israel zilizoko katika Bahari ya Mediterranean zina uwezo wa kuteketeza sehemu kubwa ya Iran.

Kuacha idadi ya mabomu ya nyuklia ambayo Israel inamiliki, mnyumbuliko huu wa mashambulizi ya kiangamizi ni wa kufikirika zaidi kuliko kiuhalisia.

Mahmoud Ahmedimanajd, aliyekuwa rais wa Iran kabla ya huyu wa sasa, aliwahi kusema anashangaa Israel na maswahiba wake wa Magharibi wanavyopaza propaganda kwamba Iran ina nia ya kuifuta kabisa Israel kutoka ramani ya dunia. Alihoji: “Mbona hampigi kelele taifa la Palestina ambalo tayari lilishafutwa kutoka ramani ya dunia?”

Mapema mwaka jana Iran ilitiliana saini na mataifa sita ya nchi za Magharibi katika suala la mradi wa nishati ya nyuklia wa Iran, lengo ni kwamba katika mradi huo Iran iangalie isizidishe virutubisho vinavyowezesha kutengeneza zana za nyuklia. Kwa maneno mengine ni kuhakikisha nchi hiyo ya Mashariki ya Kati haitamiliki zana za nyuklia –

Tofauti na miradi ya nyuklia ya nchi za India, Pakistan, Korea ya Kaskazini na Israel yenyewe, ambayo hairatibiwi na Umoja wa Taifa chini ya taasisi yake ya kuratibu nguvu za atomiki (IAEA), mradi wa Iran, kama ili katika nchi za Magharibi na nyingine kama Urusi unaratibiwa na taasisi hiyo.

Na hapo ndipo nchi za magharibi zimekuwa zikipata mwanya wa kuibana Iran kutokana na uhasama uliopo baina yao, uhasama wa miaka mingi tangu mapinduzi ya Kiisilamu ya mwaka 1979.

Mradi wa Iran uliingizwa katika uratibu wa IAEA mwaka 1976 wakati wa utawala wa Rais Gerald Ford wa Marekani, wakati huo Iran ikitawaliwa na Mfalme Shah Reza, swahiba mkubwa wa Marekani (na wa Israel pia). Na lengo lilikuwa ni kuipa sapoti Israel dhidi ya harakati za nchi za Kiarabu dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi.

Lakini baada ya mapinduzi ya Ayatollah Khomeini ya 1979, mradi huo wa iran ukageuka kuwa chungu kubwa kwa Marekani na Israel, hasa wakati wa urais wa Ahmedinajad ambaye alionekana kuhoji: “Mbona Israel wana mradi huo, na pia zana za nyuklia na haiulizwi chochote?”

Majibu ya Marekani yalikuwa ni kwamba nyuklia za Israel (na hata zile za Pakistan na India) ziko katika mikono salama. Kwa maneno mengine nyuklia za Iran haziko katika mikono salama – bila shaka kwa sababu ya usalama wa Israel.

Lakini pia kuna uhasama baina ya India na Pakistan kuhusu jimbo la Kashmiri, uhasama ambao siyo tu uliibua nchi hizo mbili kupigana mara kadha, bali pia kuanzisha miradi yao nyuklia.

Pakistan kwa mfano ni nchi ya Kiisilamu na ambayo kuna harakati nyingi za wapiganaji wenye itikadi kali, lakini bado Marekani inasisitiza zana zake za nyuklia ziko katika mikono salama.

Kwa upande wao viongozi wa Israel wanawaona wale wa Iran kama siyo watu wa kawaida – ni machizi, wakereketwa wakubwa wa udini, na kwamba wanaweza kuiangamiza nchi yao wenyewe (Iran) kwa uchu wao wa kuliangamiza taifa la Israel. Mitazamo ya aina hii inatokana na miongo mingi ya chuki dhidi ya Iran, hususaan viongozi wao.

Lakini ukweli ni kinyume kabisa – kwamba viongozi wa Iran ni watulivu, na huyapima sana masuala ya kisiasa kabla ya kuchukuwa hatua. Si viongozi wanaokurupuka na kuliweka taifa lao rehani. Haya  yamesemwa na mwandishi mmoja maarufu, raia wa Israel, Yuri Avnery katika makala yake katika gazeti la Jerusalem Post miezi kadha iluiyopita.

Avnery ambaye pia ni mwanasiasa na mswanaharakati mkubwa wa upatanishi baina ya Israel na Wapalestina, aliwahi kuwa mwanachama wa kikundi cha Irgun katika miaka ya 1940 kilichokuwa kinadai taifa la Israel kutoka koloni la Palestina lililokuwa linakaliwa na Uingereza.

Alishiriki sana katika ulipuaji mabomu miundombinu, mahoteli na majengo mengine ya wakoloni hao katika vitendo ambavyo sasa hivi vingeitwa ugaidi tu.

Avnery anasema jazba za Iran za kimapinduzi za wakati wa Ayatollah Khomeini zimepungua nchini Iran, na hata Khomeini mwenyewe, angelikuwa bado hai, asingefanya mambo ya kuhatarisha taifa lake mwenyewe.

Pamoja na hayo, historia pia inatuambia kwamba kabla ya mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979 mahusiano baina ya Wayahudi na Wairani yalikuwa mzuri sana tena kwa miaka mingi. Wakati taifa la Israel lilipoanzishwa, Iran ilitambuliwa rasmi kama ni swahiba wa ki-asili wa Israel, kwani Waziri wake Mkuu wa kwanza, David Ben Gurion aliiona Iran kama ni nchi muhimu kwa usalama wake katika dunia ya nchi nyingi hasimu za Kiarabu.

Mfalme Shah wa Iran, aliyesimikwa na Wamarekani mwaka 1941 alizidisha biashara na Israel na pia shirika la makachero la Mossad la Israel na lile la Iran la Savak yalishirikiana na CIA ya Marekani kuratibu harakati za Wakurdi waliokuwa wakipambana na utawala wa Sadam Hussein wa Iraq.

Hata baada ya mapinduzi ya mwaka 1979, Israel iliiunga mkono Iran katika ile vita yake dhidi ya Iraq katika miaka ya 80.

Hivyo basi iwapo mambo yataharibika kabisa nchi hizi mbili zinaweza kujikuta zikivumiliana katika uwiano wa kutishiana. Hivyo ni vyema nchi hizo zikatumia muda uliopo kurekebisha mambo kupata muafaka katika mgogoro kati yao.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, katika kutafuta kura katika uchaguzi uliopita wa 2015, alitumia ubabe, lugha ya vitisho na kadhalika dhidi ya Iran wakati majadiliano ya mradi wake wa nyuklia yakiendelea huko Uswisi.

Aidha inafahamika wazi kwamba ‘uhasama’ wa Iran kwa Israel unatokana na hatima ya watu wa Palestina. Hali ya undugu iliyopo kupinga maonevu ya Wapalestina yamejikita ndani ya damu ya Waisilamu duniani kote, hivyo Iran haiko peke yake. Hivyo hakuna kitu kingine kinachochochea uhasama huu wa sasa isipokuwa suala la Wapalestina.

Yuri Avnery anasema iwapo suala la Wapalestina litatatuliwa, hakuna kiongozi yoyote wa Iran atakayeweza kuamsha uhasama wowote kwa wananchi wake dhidi ya Israel.