Home Tukumbushane Nchi za Kiafrika haziwezi kufundishana kuendesha uchaguzi

Nchi za Kiafrika haziwezi kufundishana kuendesha uchaguzi

2135
0
SHARE

Rais anayeondoka madarakani Joseph Kabila akipiga kura yake katika uchaguzi desemba 39 2018.

HILAL K. SUED

Zaidi ya wiki mbili zilizopita Congo (DRC) ilifanya uchaguzi ambao kama ilivyo ada kwa nchi nyingi Barani Afrika haukukosa mizengwe na figisu tele.

Kwanza kabisa uchaguzi wenyewe ulicheleweshwa kwa miaka miwili bila shaka kumuewesha rais aliyepo madarakani kwa miaka 17 Joseph Kabila, kutafuta upenyo – kupitia katiba na njia nyinginezo – wa kuendelea kubakia madarakani kama vile wenzake katika nchi jirani za Burundi, Rwanda, Uganda, Afrika ya Kati na Congo Brazzavile.

Wengi wanashangaa kwa nini alishindwa. Inawezekana upinzani ulikuwa mkubwa sana, au nchi za nje ziliweka msukumo mkubwa. Lakini kama alikuwa anacheza na muda, basi inaonekana kafanikiwa kwa kiasi, angalau hadi sasa, kwani uchaguzi umefanyika, na mgombea wa upinzani Felix Thishekedi kaibuka na ushindi.

Pamoja na ushindi wa mgombea wa upinzani chama cha Kabila kimeshinda viti vingi Bungeni na hivyo kitatoa Waziri Mkuu. Kwa maana hii Kabila bado atakuwa na mkono na hivyo ushawishi mkubwa katika serikali mpya. Lakini kuna kingine zaidi ya hapo – inadaiwa Tume ya Uchaguzi, kwa niaba ya Kabila, ilicheza na matokeo kumpa ushindi Tshishekedi ambaye inadaiwa alikuwa tayari amekubaliana na Kabila ili aje amlinde.

Hata hivyo mgombea aliyeibuka wa pili Martin Fayulu amepinga matokeo hayo kwa kutaja hizo sababu na tayari katangaza kwenda mahakamani. Hivyo mambo ni bado kabisa nchini DRC na huenda hali iliyopo nchini ya kukosekana umoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe itaendelea – sababu kubwa ni kutaka mtu mmoja alindwe kutokana na makosa ya utawala wake.  

Mimi huwa sikubaliani na wazo kwamba nchi za Kiafrika zinaweza kujifunza kutoka nchi nyingine katika Bara hili kuhusu masuala ya demokrasia, hususan namna ya kuendesha chaguzi zilizo huru.

Napata ugumu sana kusema nchi fulani ndiyo mfano bora wa kuiga kwa sababu demokrasia na uendeshaji wa chaguzi katika nchi nyingi Barani humu ni kiini macho na hufanyika kwa ghilba na udanganyifu mkubwa.

Kuna baadhi ya nchi angalau unaweza ukataja kwamba ni mfano mzuri wa kujifunza – kama vile Arika ya Kusini, Ghana, Botswana na labda Liberia. Lakini hata nchi hizi kuna kasoro nyingi tu hujitokeza.

Nakubali kwamba duniani pote, hakuna chaguzi zinazoendeshwa kwa uhuru na haki kwa asilimia 100 – hata katika nchi inayodaiwa imeendelea sana katika demokrasia – yaani Marekani.

Sote twakumbuka mwaka 2000 jinsi nchi hiyo ilipoushangaza ulimwengu baada ya kuibuka kwa mgogoro mkubwa uliyotokana na uchaguzi wa rais uliowapambanisha George W. Bush wa chama cha Republicans na na Al Gore wa Democratic.

Mgogoro huo ulitokana katika uhesabuji kura katika jimbo la Florida na ulimalizwa tu na uamuzi wa Mahakama ya Juu kabisa nchini humo (Supreme Court), baada ya karibu miezi miwili ya vuta nikuvute katika mahakama za ngazi mbali mbali. Ndiyo maana nchi za wenzetu rais mteule hukaa muda mrefu kabla ya kuapishwa ili kutoa fursa ya kushughulikia mambo kama hayo.

Mahakama hiyo iliamua (kwa kura 5 kwa 4 za Majaji) kumpa ushindi Bush, ingawa wengi waliona kuwa uamuzi huo ulitokana na nia ya kulimaliza tu suala hilo lilikowa linaliletea picha mbaya nchi hiyo mbele ya uso wa ulimwengu.

Kumbukeni Marekani haina Tume ya Uchaguzi kama ilivyo hapa kwetu na nchi nyingine nyingi. Usimamizi wa chaguzi zote hufanywa na mamlaka za serikali za majimbo. Hivyo hakuna siku ambayo ‘Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi’ kwa muda mfupi hujifanya ‘mungu mtu’ kwa kuwaweka wananchi roho juu na katika shauku kubwa kungojea kumtangaza mshindi wa kiti cha urais, kwani kule Marekani mshindi hujulikana hata kabla ya kura zote kuhesabiwa.

Hali hii kwa mfano ilitokea katika uchaguzi wa mwaka 2012 ambapo Barack Obama alijulikana mshindi hata kabla ya jimbo la Florida kukamilisha zoezi la kuhesabu, zoezi ambalo lilikuja kukamilika wiki mbili baadaye.

Nchi pekee duniani ambayo naikubali kuwa na chaguzi huru na zisizo na migogoro ya kiuendeshaji ni Uingereza. Nimekuwa nafuatilia chaguzi za nchi hiyo tangu miaka ya 60 lakini sikumbuki lini kulizuka vuta nikuvute kutokana na maamuzi ya matokeo ya chaguzi zake.

Migogoro huzuka pale tu chama kimoja kinaposhindwa kupata idadi ya viti bungeni kukiwezesha kuunda serikali, lakini hii haitokani na maamuzi mabovu ya matokeo.

Hata hivyo kuna baadhi ya vitu tunaweza kujifunza kuhusu chaguzi za kidemokrasia kutoka nchi nyingine barani Afrika – hususan uteuzi wa Tume ya Uchaguzi na muundo wake. Hapa kwetu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Makamishna wa Tume na Mkurugenzi wake huteuliwa na Rais ambaye pia ni kiongozi wa chama tawala ambaye si mara moja au mbili hugombea pia nafasi ya urais katka chaguzi.

Uteuzi huo unakinzana na ule msingi mkuu na maarufu wa utoaji wa haki usemao: “Si kwamba haki itendeke tu, bali pia ni lazima ionekane inatendeka” (justice must not not only be done but must also seen to be done).

Haingilii akilini kwamba aliyebuni ulazima kwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kuwa na sifa za jaji wa Mahakama Kuu pia aliyafikiria masuala mbali mbali likiwemo hili la msingi mkuu wa kutoa haki.

Nchi za Kenya na Afrika ya Kusini kwa mfano mchakato wa kumchagua mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ni mrefu na una muonekano kwamba haki inaweza kutendeka, hachaguliwi na mtu mmoja.

Na hata, pamoja na uhuru wake, inaweza kuingiliwa na dola katika maamuzi yake na kupindisha matokeo kama ilivyokuwa kwa uchaguzi wa Agosti 2017, njia za haki za kimahakama zilikuwa wazi kabisa.