Home Michezo Ndayiragije kumfuta machozi Mzee Bakhresa?

Ndayiragije kumfuta machozi Mzee Bakhresa?

1529
0
SHARE

NA FAUDHIA RAMADHAN

AZAM FC msimu ujao inatarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni mara yao ya tano kufanya hivyo tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 2007.

Japo Azam FC ilianzishwa kama timu ya wafanyakazi wa Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) kama sehemu ya kujifurahisha na kuimarisha afya zao, lakini baadaye lilikuja wazo la kuifanya kuwa klabu rasmi ili iweze kushiriki michuano mbalimbali.

Ni kutokana na wazo hilo, hatimaye msimu wa mwaka 2008/2009, ilipanda daraja na kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na tangu wakati huo, haijawahi kushuka.

Ndani ya kipindi hicho, Azam yenye maskani yake Chamazi Complex, Dar es Salaam, imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja tu, ikifanya hivyo msimu wa 2012/13, chini ya kocha Mwingereza, Stewart Hall.

Kwa upande wa kimataifa, Azam FC imefanikiwa kushiriki michuano hiyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mara nne.

Mwaka wao wa kwanza kushiriki michuano hiyo ya CAF, ilikuwa ni 2013 walipopata nafasi ya kuonyesha umwamba wao Kombe la Shirikisho Afrika, kabla ya kufanya hivyo tena mwaka uliofuata, 2014.

Azam ilishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2015, huku miaka ya 2016 na 2017, ikikata tiketi ya Kombe la Shirikisho.

Klabu hiyo ilipata tiketi hizo kutokana na kushika nafasi mbili za juu katika Ligi Kuu Bara, ikichuana vilivyo na wakongwe wa soka hapa nchini, Simba na Yanga.

Katika vipindi vyote ambavyo Azam imeshiriki michuano hiyo ya CAF, haijawahi kufika mbali zaidi ya kukaribia hatua ya makundi msimu wake wa kwanza, yaani 2013.

Na sasa wakati Azam ikiwa imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho msimu ujao, wapenzi wa soka nchini wamekuwa na shauku kuona timu hiyo itafanya nini.

Ifahamike kuwa tangu imepanda daraja, wapenzi wa soka walikuwa na matumaini makubwa na Azam kutamba katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla kutokana na uwekezaji uliofanywa na S.S Bakhresa.

Pamoja na uchanga wake kulinganisha na Simba na Yanga zilizoanzishwa miaka ya 1930 mwanzoni, Azam ndiyo klabu inayoonekana kuendeshwa kisasa kutokana na uwekezaji uliofanywa.

Klabu hiyo ina viwanja viwili, ukiwamo wa kisasa unaofaa kwa mechi za ligi hadi za kimataifa, ‘gym’ yenye vifaa vya kisasa vya mazoezi, hosteli ya kiwango cha juu, bwawa la kuogelea na vitu vinginevyo vinavyostahili kuwapo katika klabu ya kisasa.

Katika kuifanya klabu hiyo kuwa ya ushindani hasa, S.S Bakhresa, alihakikisha anaunda mfumo sahihi wa uongozi, huku benchi la ufundi likiwa na watu wenye taalum ya soka.

Ni kutokana na hilo, klabu hiyo ilifanikiwa kuajiri makocha sita tofauti wa kigeni wa kiwango cha juu, kuanzia Mbrazil Nider dos Santos (2008-09), Mbrazil Itamar Amorim (2009–10), Mwingereza Hall (2010-12, 2012-13, 2015-2016), Mcameroon Joseph Omog (2013-14), Mhispania Zeben Hernandez (2016), Mromania Aristca Cioaba (2017-18) na Mholanzi Hans van der Pluijm (2018-19).

Pia, ilifanikiwa kusajili wachezaji nyota kutoka hapa nchini na nje ya Tanzania, tena ikifanya hivyo kwa gharama kubwa, lakini mafanikio yake yaliishia kushika nafasi mbili za juu Ligi Kuu Bara, huku ikiishia hatua za awali michuano ya kimataifa.

Baadhi ya wachezaji hao ni Kipre Tchetche, Michael Balou na Pascal Wawa (Ivory Coast), Allan Wanga na Brian Majwega (Uganda), Yakubu Mohammed na Daniel Amoah (Ghana), Jean Baptiste Mugiraneza(Rwanda), Didier Kavumbagu (Burundi), Donald Ngoma na Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe), Obrey Chirwa (Zambia) na wengineo.

Wazawa ni Gaudence Mwaikimba, John Bocco, Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Hamisi Mcha, Shomari Kapombe, Himid Mao, Gadiel Michael na wengineo wengi.

Na kwa sasa inapojiandaa kushiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao, ikitwaa tiketi hiyo kama mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC2019), wapenzi wa soka nchini wanasubiri kuona iwapo wakali hao wa Chamazi wanaweza kufika mbali.

Tofauti na misimu iliyopita, Azam safari hii itakiwasha katika michuano hiyo, ikiwa chini ya kocha anayetajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha, Ettienne Ndayiragije raia wa Burundi.

Kocha huyo aliyewahi kuinoa Mbao FC ya Mwanza, amejijengea jina kutokana na kandanda la timu yake hiyo hadi alipotua KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam, aliyoiwezesha kukata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika nafasi ya nne katika msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara.

Kwa timu iliyopanda daraja msimu huo huo na kushika nafasi ya juu hadi kukata tiketi ya kukipiga michuano ya kimataifa, ni jambo kubwa mno lililochangia kuwashawishi mabosi wa Azam kumtwaa kocha huyo.

Inapojiandaa kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ni wazi Azam ya Ndayiragije inasubiriwa kuona iwapo inaweza kumfuta machozi Mzee S.S Bakhresa, wakiwamo wapenzi na wachambuzi wa soka hapa nchini ambao wameonekana kutoridhishwa na mafanikio ya klabu hiyo tangu ilipoanzishwa kulinganisha na uwekezaji uliofanywa.

Inafahamika kuwa Mzee Bakhresa ametumia fedha nyingi mno kuifikisha Azam ilipo sasa, hivyo njia pekee ya kumfariji mfanyabiashara huyo, ni timu hiyo kufika mbali Kombe la Shirikisho Afrika msimu unaotarajiwa kuanza Agosti mwaka huu na hata kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Hata hivyo, ili Ndayiragije aweze kufanya mambo makubwa Azam, ni wazi atahitaji uhuru wa kufanya kazi bila kuingiliwa na siasa za ‘usimba’ na ‘uyanga’ ambao umekuwa ukiziathiri klabu nyingi hapa nchini.

Pia, kocha huyo atahitaji kuwezeshwa kusajili wachezaji anaoona wanalingana na hadhi ya klabu hiyo na michuano ya kimataifa kwa ujumla, jambo ambalo si tatizo kwa wamiliki wa Azam FC.

Hebu tusubiri kuona nini kitatokea ndani ya Azam ya mtaalam Ndayiragije. Je, itafanya kweli msimu ujao na kuzitoa jasho Simba na Yanga na hata kufika mbali Kombe la Shirikisho Afrika? Tusubiri tuone.