Home Makala NDELE:  MTAJI WA MWANASIASA NI WATU NA ELIMU

NDELE:  MTAJI WA MWANASIASA NI WATU NA ELIMU

931
0
SHARE

NA PENDO FUNDISHA-MBEYA.


WANASIASA wengi wamekuwa na mtazamo hasi kwenye suala zima la siasa, wengi wao wamekuwa wakiamini na kudhani kwamba ili uwe mwanasiasa mzuri ni lazima uwe na mtaji wa watu.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alipata kuifafanua dhana hii kwa kusema kuwa ili mwanasiasa aweze kuwa na siasa safi ni lazima awe na uwezo wa  kusoma vitabu.

Mwanasiasa asiye na uwezo wa kuchanganua mambo ni sawa na mtu anayesomewa barua kutokana na kutojua kusoma.

Mwalimu Nyerere alipata kusema kuwa usomaji wa vitabu na kuapata nafasi ya kusafiri kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ndio nguzo pekee inayoweza kumjenga mwanasiasa makini.

Ndele Mwaselela, ni miongoni mwa wadau wa maendeleo katika mkoa wa Mbeya na Jimbo la Mbeya mjini, pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shule ya Patrick Mission ya Jijini Dar es Salaam.

Mdau huyu, ni miongoni mwa Watanzania wachache walioamua kuwekeza kwenye elimu kwa kusaidia zaidi ya shule 10 za msingi za jijini Mbeya kwa kujenga vyumba vya madarasa na kupeleka vifaa mbalimbali zikiwemo kompyuta.

Licha ya jitihada hizo, Ndele anaeleza kuwa kukosekana kwa elimu bora ndiko kunakozalisha idadi kubwa ya wanasiasa kufanya siasa zisizo na mashiko.

Amesema wanasiasa wasio na uelewa wamekuwa ni wafuata upepo na wasio na dira ya maendeleo wala huruma kwa wananchi wanaowaongoza.

“Watu wengi hawakumwelewa Hayati Mwalimu, hasa pale alipokuwa akiielezea siasa  safi, alikuwa akimaanisha kwamba ili mwanasiasa aweze kuwa na siasa safi ni lazima ajiwekeze kwenye usomaji wa vitabu.”

Anasema, kama  mtu anataka kuwaongoza watu lazima kuna vitu ambavyo vitakuwa ni tofauti, hivyo unaposoma na kutembelea maeneo tofauti utapata ufahamu wa kutambua na kujua kuwa wewe unautumishi uliotukuka na wa maono, huku akimtolea mfano Rais Dk. John Magufuli kuwa ni kiongozi mwenye maono kwa Watanzania.

Maono ya Rais ndio silaha tosha ya maendeleo huru ya nchi hii tangu kupatikana kwa uhuru na ndio yatasaidia nchi kuwa sehemu ya maendeleo  na Rais huyu si kwamba alikurupuka.

Ukimfuatilia kwa undani lazima utabaini kwamba alikuwa ni mtu wa kusoma vitabu na kutembelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya kujifunza, hivyo ni Rais mwenye maono na Tanzania.

“Ukiwa mtumishi utaheshimu watu, utasikiliza watu utawapeleka watu katika hali itakayojenga ustawi wa maendeleo, watu watatulia, watu wataweza kuwekeza kwenye maendeleo lakini pia  kiongozi yoyote ambaye hana maono ni ngumu kuongoza watu,”anasema.

Maandiko ya dini yameeleza kwamba, viongozi wote walikuwa na maono, hivyo ukimchukua mtu ambaye hana maono na kumpa madaraka ya uongozi ni tatizo, ukiangalia nchi zilizoendelea, watawala wote walikuwa na ndoto ambayo walipeleka chini kwa jamii waliyoiongoza na wakafanikiwa.

Ukiangalia hivi sasa Rais anatekeleza maono aliyokuwa nayo kwa ajili ya watu wake na ndio sababu ameweza kufanya kazi kwa kutomuogopa mtu, kubwa analoangalia ni jinsi gani ataweza kufanikisha maono ya maendeleo aliyokuwa nayo kwa nchi yake.

Anasema, watu wanapochukua fomu za uongozi wanapaswa kuwa na maono wasikurupuke tu, wala wasifanye kwa kufurahisha watu wala kwa malengo ya jambo fulani kama biashara na hili ningewaeleza wafanyabiashara kwamba kama waligombea nafasi za uongozi kwa minajili ya biashara zao basi hawawezi kufika mbali.

Ukisoma kwenye historia unaona viongozi waliotaka kuingiza biashara hawakufika mbali, kwani walikuwa wakitaka kutumia biashara kuwa siasa na siasa kuwa biashara, vitu ambavyo haviendani kwani ni lazima upande mmoja utaelemewa.

Anasema, uongozi si jambo la kukimbilia ni lazima ujipime sana na uwe na uvumulivu wa kutosha, kwani unatakiwa kufanya kazi pasipo kuangalia sura za watu, hasa Tanzania ambako siasa zimetaliwa na makundi na kama tunavyofahamu kwamba makundi  hayawezi leta maendeleo ya nchi zaidi ni kwa watu fulani.

“Kuna usemi usemao , mtu ukitaka kuendelea sharti usiwe na makundi, kwanza hamuwezi kuwaza wote sawa na haiwezekani mkawa na maono sawa, aliyechaguliwa ni mmoja tu, hivyo ni lazima atekeleza maono yake kutokana na kuweka pembeni makundi kama Magufuli alivyofanya, amekuwa na uthubutu wa kutekeleza mambo ambayo viongozi waliopita walikuwa wakiyaogopa,”anasema.

Anasema, ili amefanikiwa kutokana kwamba wakati wa siasa zake hakwenda na makundi, hivyo anatosha kuwa ni mwalimu wa wanasiasa wengine, ngazi ya uwenyekiti, udiwani hadi ubunge hasa ngazi ya ubunge ambako kunahitaji  msasa wa hali ya juu.

Wabunge na madiwani wengi wao ni fuata upepo, wakati fulani mtu unajiuuliza hivi hawa wabunge wanaramani ya maendeleo, haiwezekani eneo kubwa la jimbo liwe na changamoto, ambazo gharama yake haizidi milioni 200 lakini kiongozi hana mkakati wowote.

“Mbunge ukimuuliza nini mkakati wake, atakuambia nimejipanga we usajali utaona tu, haiwezekani kiongozi asiye na kipaumbele, kiongozi hafahamu watanzania wanataka nini kwa sasa, hivi sasa watanzania wengi wanataka kulima na kusomesha watoto wao suala la kula kwao si tatizo,”anasema.

Kiongozi wa kisiasa huwezi kuwatafutia pesa utakuwa unawadanganya, huwezi kuwatafutia, chakula utakuwa muongo, watanzania wanataka watoto wao wasome shule, wanajua uwezo wao ni wakutafuta milo mitatu, hivyo serikali inavyotoa elimu bure basi wasaidizi wa serikali, wakiwemo wabunge wawe na ramani ya maendeleo kwenye jimbo lake.

Wawe na uwepesi wakutaka kuhudumia wananchi, mfano ningekuwa mimi, kwanza niseme ubunge si kazi ni lazima mbunge awe na kazi yake, ukienda na ubunge ndio ukupe fedha hapo ndipo unapokosana na wananchi kwani zile fedha unazopewa jaribu kuzirejesha kwa wananchi.

Wapo wabunge wachache walifanya hivyo na walifanikiwa lakini ukiingia na mawazo kwamba ubunge ukulipe, ukujenge na ukutoe kuwa tajiri ni lazima wananchi waumie na hapo ndiko suala la watoto kulundikana darasa moja na kujisaidia vichakani linatokea.

Kiongozi lazima awe mbunifu, asiwe na muda wa kusafiri safari za starehe lazima utulie ili kutafakari maendeleo ya wananchi wake na mbunge unapaswa kutulia jimboni, rais ni mwalimu mzuri sana, mimi binafsi nimeiga mambo matano na wala sijajilaumu.

Mimi si kiongozi lakini nimetulia siku tatu Mbeya ila nimebaini changamoto nyingi za jimbo la mbeya, mkuu wa mkoa ameenda kwa speed hivyo wenyeviti, madiwani lazima waende kwa speedi waachane na siasa za uhanaharakati kwani muda umepita zile zilikuwa siasa za kutafuta madaraka sasa tunataka maendeleo.

Anasema, Tanzania si masikini ni tajiri sana, kinachohitajika ni uongozi unaojali watu.

Mkoa wa Mbeya, elimu imeshuka sababu kubwa ni siasa za harakati, siasa za hamsha hamsha, kila siku ni kifika hapa nakutana na vijana utawaonea  huruma sababu kubwa walipotoshwa na ahadi hewa za wanasiasa.

Vijana wenyenguvu za kilimo lakini wamepotea kutokana na kununuliwa na wanasiasa, kupandishwa kwenye majukwaa lakini hali zao ni shida kwa sasa, wakipewa elfu 10 wananyang’anyana kama nyama.

Akizungumzia nini mikakati yake: ndele anasema kuwa mkakati wake ni kuwekeza kwenye elimu, anatarajia kuanzisha taasisi kubwa ya maendeleo lengo ni kuwakomboa wanambeya hususani vijana.

Anasema, pia kazi kubwa itakayofanyika ni kuwaelimisha wazazi wangu kwani wakielimika wataleta faida kubwa kwa watoto pili ni kukaa na vijana, nataka wajikite kwenye shughuli za uzalishaji, kuwaondoa kwenye mabano, lazima watoke na kufanya kazi, tutachora ramani ya mwelekeo ya Mbeya mpya, na hili litagusa wengi na hatutahitaji  wanasiasa watuunge mkono wala fedha zao hatuzihitaji.

Kuhakikisha shule zetu zinaungana na kuwa na sauti moja ya kumtoa mtoto wa masikini aweze kufika chuo kikuu.

Nimeanza kukaa na walimu na nitafika ninapotaka kufika hadi sasa ninashule zaidi ya 10 na lengo langu ni kuzimaliza shule zote za Jiji la mbeya.

Nitajenga academy ya michezo mbeya, nimekaa na shule tayari kuandaa mashindano ya wilaya, lazima tujenge utamaduni wa kuwakutanisha vijana ili kupata vipaji, mbalimbali na hii ndio ndoto yangu mimi, nitafurahi kuona mtoto anasoma, anaimba, na kucheza.

Lazima tuwajenge vijana kwa kuwaondoa kwenye mawazo ya fedha za haraka na kuwa na mawazo ya fedha za matarajio, ukiwa na kitu cha matarajio lazima utafanikiwa tu, na hili tutaenda hadi kwa waandishi wa habari.

Lazima hamsha hamsha ya maendeleo Mbeya ifanyike na ifanikiwe.