Home Makala Ndimbo diwani anayepigania ndoto za Rais Magufuli

Ndimbo diwani anayepigania ndoto za Rais Magufuli

2229
0
SHARE

Akiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Kihagara.

Markus Mpangala

SIFA za kiongozi wa ngazi yoyote ni pamoja na kutambua na kuwafanya watu anaowaongoza kuwa washiriki wa michakato na mipango ya maendeleo katika eneo lake, kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata, tarafa, Wilaya, Mkoa, Kanda na taifa.

George Ndimbo ni miongoni mwa vijana wa kitanzania ambao wamejitolea kwa hali na mali kuhakikisha wananchi wanasimamiwa, kuhamasishwa, kushirikishwa pamoja kufurahia matunda ya juhudi zao za kujiletea maendeleo.

Ndimbo ni diwani wa Kata ya Kihagara iliyopo tarafa ya Ruheheki katika jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma. Ni msomi ambaye ameamua kuanzia ngazi ya chini ili kuwatumikia wananchi wa Kata ya Kihagara. Katika mahojiano haya anaeleza mbio za udiwani na mikakati ya maendeleo. Fuatilia….

SWALI: Tueleze historia yako kwa ufupi.

NDIMBO: Asante sana. Mimi nimezaliwa miaka 29 iliyopita katika Kijiji cha Kihagara. Jina la Kijiji hicho ndio la Kata yetu, yaani Kata ya Kihagara katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma. Nilisoma shule ya msingi Kihagara na sekondari ya Mtakatifu Paulo iliyopo mjini Liuli wilayani Nyasa. Nimehitimu elimu ya sekondari mwaka 2007. Baadaye nilichaguliwa kwenda mkoani Tabora kuendelea na elimu  katika sekondari ya Milambo High school.

SWALI: Ni muda huo uliingiza kwenye siasa?

NDIMBO: Kwanza, nilikwenda masomoni katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Pale nimehitimu shahada ya kwanza katika fani ya Takwimu. Kwa sasa nipo mkoani Morogoro kujiendeleza kielimu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe ambako nachukua shahada ya uzamili ya Usimamizi na tathmini ya huduma za afya.

SWALI; Uko masomoni na wakati huo unawakilisha wananchi wa Kata ya Kihagara?

NDIMBO; Kila kitu ni ratiba. Ratiba yangu kwa sasa ni kwenda katika eneo langu la kazi, baada ya muda nitaendelea na jukumu jingine masomoni. Msingi wa uongozi katika Kata yetu ya Kihagara ni kuamini kuwa unapotatua matatizo ya watu ndipo tunapata kuishi. Watu waliofanikiwa wengi ni wale waliotatua shida za wengine.

Sisi katika Kata yetu kwa tunashikiriana na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Nyasa na wa kisiasa. Lengo letu ni kuhakikisha watu wanapata matunda ya uongozi na ushiriki wao wa maendeleo ya Kata yote, halafu yaje kwenye wilaya, na baadaye katika mkoa wa Ruvuma na taifa. Kila upande upiganie maendeleo ya eneo lake na taifa lote.

SWALI; Wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 ulikuwa na umri wa miaka 26 tu. Nimepata habari kuwa hadi sasa wewe ndiye diwani mwenye umri mdogo katika jimbo la Nyasa?

NDIMBO; Hii ni habari ya kweli, nilikuwa mgombea mdogo sana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, inasemekana kwa mkoa wa Ruvuma, mimi ndiye diwani mwenye umri mdogo zaidi. Japo inasemwa hivyo na watu wengi bila kufanya tafiti. Ila sidhani kama kuna diwani yeyote ninayemzidi Umri katika majimbo yote ya uchaguzi ya mkoa wa Ruvuma.

SWALI: Kwanini hukuwaachia wakubwa wagombee?

NDIMBO; (kicheko) Kwa mazingira ya wilayani kwetu Nyasa au niseme mkoa wa Ruvuma kuna dhana ya tuwaachie wakubwa. Mimi nilikataa dhana hii, nikajitosa mwenyewe bila kushawishiwa na mtu.

Kwa kweli haikuwa rahisi, kama nilivyokuambia kuwa hata ndugu waliniambia kuwa hawatanipigia kura. Ilionekana kama kijana msomi anapoteza muda na mwelekeo kujiingiza kwenye kinyang’anyiro cha udiwani, ambayo ni ngazi ya nchi. Lakini sikukata tamaa.

Bahati nilipata sapoti ya aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Nyasa, Stella Manyanya, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.

Mbunge wangu huyu ni mwanachama mwenzangu wa CCM, aliamini na alibaini uwezo wangu, alinisapoti kipindi chote na hakika sina cha kumrejeshea zaidi ya kumshukuru. Nitashirikiana naye na chama chetu cha CCM kulijenga jimbo, mkoa wa Ruvuma na taifa letu. Hii ni zawadi pekee muhimu kwake na kwa wanachama wenzengu wa CCM.

SWALI: Nini kilitokea baada ya msimamizi kutangaza umeshinda?

NDIMBO; Aaaah! (kicheko) yote yaliyotokea ni historia kwa sasa. Nilishangiliwa sana, ukizingatiwa sikutegemewa kutokana na umri ule. Nadhani sasa wanaelewa kuwa nia yangu ilikuwa thabiti kuwatumikia wananchi wa Kata ya Kihagara, bila shaka nikiwa hai watanipigia kura katika uchaguzi mkuu mwaka 2020 kwa shangwe. Kuona ni kuamini, ingawa twaenenda kwa imani.

SWALI: Utagombea tena katika uchaguzi ujao au utajikita katika taaluma?

NDIMBO: Lengo langu ni kuendelea kuwatumikia wananchi wa Kata ya kihagara, nimesema kama nitakuwa hai, sijasema kama mwaka 2020 nitagombea nafasi hiyo. Nina malengo madogo na makubwa lakini yenye manufaa ya kuijenga Kata yetu na Halmashauri ya Nyasa kuanzia sekta ya afya, elimu na mengine.

Kikubwa tunachotarajia mimi na chama changu CCM ni kuongeza nguvu kuwatua ndoo akina mama. Kero ya maji safi na salama ni changamoto ambayo natakiwa kuondoa katika Kata yangu. Ingawaje tunalo ziwa Nyasa, lakini wananchi wanatakiwa kuwa na maji safi na salama ya bomba.

SWALI: Kwahiyo umepanga kumkabili Katibu wa Wizara ya Maji, juu ya suala hilo?

NDIMBO: Zipo njia za kukamilisha kabla ya kufika huko wizarani, makao makuu Dodoma kwa Profesa Kitila Mkumbo. Iwapo nitakutana na Katibu wetu wa wizara ya Maji naweza kumweleza hali hiyo, lakini lazima sisi kama Kata ya Kihagara, Halmashauri ya Nyasa na mkoa wa Ruvuma tufanye kitu cha kuwatua ndoo za maji akina mama. Tunatakiwa kuhakikisha wanaondokana na maji ya visimani.

SWALI: Mbali ya hilo ni mambo gani yamefanikiwa katika Kata ya Kihagara?

NDIMBO; Kata ya Kihagara tulikuwa na shauku ya kupata angalau kituo cha Afya, sasa tunacho. Kama unavyojua mazingira yetu nchini suala la afya ni muhimu mno, na linatufanya tuhangaike huku na huko kuhakikisha mambo ya afya kwanza yanakaa vizuri. Tumepata majengo ya kisasa ya kuweza kutolea huduma za Jamii kama vile shule, zahanati, kituo cha Afya.

Kwenye elimu  tumejenga majengo matatu kwa ajili ya kuwapokea kidato cha kwanza mwaka 2019 katika shule ya sekondari Mango. Tunawashukuru wananchi wa Kata ya Kihagara kwa michango yao ya mali na matofali kwa ajili ya ujenzi wa sekondari hiyo.

Tunamshukuru pia Mbunge wetu Injinia Stella Manyanya kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Project ambalo limekuwa msaada mkubwa sana kwa shule zetu za jimbo la Nyasa. Shirika hilo limechangia pakubwa kukamilisha majengo,kutoa vifaa vya viwandani na mambo mengine.

Vilevile tunamshukuru Mama Salome Nkondora wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco) kwa kuwezesha upatikanaji wa mbao zote za kuezekea moja ya majengo ya sekondari ya Mango, pamoja na ofisi yangu kama diwani na Afisa Maendeleo wa Kata yetu, Bertha Patricky kwa kuwahamasisha wananchi waishio ndani na nje kuchangia ujenzi na ufanisi wa Sekondari ya Mango. Bila kuwasahau wenyeviti wote wa vijiji vya Kata ya Kihagara wanaotekeleza ilani ya CCM.

Mpango wangu kwa mwaka 2019 ni kuboresha shule ya msingi ya Songambele. Jitahada kubwa zinafanyika ili kuifanya shule hii iendane na Mazingira ya sasa. Tunawashukuru wananchi wa Songambele kwa michango matofali kwa ajili ya ujenzi. Pia tunamshukuru Mbunge Injinia Stella Manyanya kuwezesha upatikanaji wa mbao zote za kuezekea jengo jipya pamoja malipo ya fundi wa kupaua.

Tumeshirikiana pia na shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Project ambalo limekuwa msaada mkubwa sana kwa shule zetu za jimbo la Nyasa. Bado tuna mpango wa kujenga tena jengo lingine la madarasa matatu. Watoto wetu wanatamani wangesomea mazingira mazuri, tunachukua hatua.

Kwa sasa tunalo jengo la Maabara ya kisasa katika Shule ya Secondari Mango. Limejengwa kwa nguvu za wananchi na ushiriki wa mbunge Stella Manyanya na Halmashauri ya Nyasa. Tunaamini yote yaliyobaki tutakamilisha.

SWALI: Umeajiandaaje kukabiliana na upinzani  wako mwaka 2020?

NDIMBO: Wapinzani wangu? (kicheko), nipo tayari kwa mpambano, niliwashinda nikiwa mdogo sana, na sasa nimeongeza uzoefu. Kama nilivyosema, nikiwa hai mwaka 2020, kwa sababu sijui nini kitatokea kuanzia sasa hadi wakati huo.