Home Makala Kimataifa NDOTO YA AFRIKA KUWA TAIFA MOJA HAIJAFIFIA

NDOTO YA AFRIKA KUWA TAIFA MOJA HAIJAFIFIA

1124
0
SHARE

NA MOSES NTANDU

KATIKA jambo ambalo lilionekana kufifia na kuanza kupoteza ladha, ama kutokuungwa mkono na baadhi ya viongozi wakuu katika siasa za bara la Afrika, ni kuundwa kwa Afrika moja kama taifa, yaani kuwa na taifa moja la Afrika.

Ndoto hii inaonekana bado ipo hai kwa baadhi ya mataifa ikiwemo Taifa la Morocco, licha ya Morocco kuwa na wazo la awali kabisa miaka ya 1960 na 1970 ambalo lililenga kuundwa kwa Taifa moja la Afrika na baadaye wazo hilo lilionekana kuungwa mkono na hayati Muamar Gadhafi aliyekuwa rais wa Libya na baadaye wazo hilo kutoweka bila ya mwendelezo wowote.

Katika hali ambayo inaonesha ni harakati mpya na zenye nguvu ni wazo hili kuendelea kuungwa mkono na pia kupigiwa upatu na Taifa la Morocco, ikiwa ni mwendelezo wa kile kinachotajwa kuwa ndio waanzilishi wa wazo hilo toka enzi za kupigania uhuru wa mataifa mengi ya bara la Afrika.

Mfalme wa Morocco Mohamed wa sita (VI), anatoa hotuba iliyojaa maneno ya kuliamsha bara la Afrika ili kuwa imara kisiasa, kiuchumi na pia kidiplomasia, hii ilikuwa ni katika maadhimisho ya miaka 64 ya uhuru wa taifa hilo. Hafla hii imefanyika wiki kadhaa zilizopita huku taifa hilo likisherehekea katika mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo hapa Tanzania kupitia ubalozi wao.

Mfalme anasema kuwa uhuru wa Morocco umekuwa chachu au amani na utulivu barani Afrika, kwani Morocco imekuwa ikifanya mambo mengi kwa ajili ya bara la Afrika, mfano kwa mara ya kwanza Morocco iliweza kutuma vikosi vya kijeshi kwenda kulinda amani nchini Zaire mwaka 1960 kwa wakati huo, ambapo kwa sasa nchi hiyo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Pia Morocco iliweza kuwa mwenyeji wa mkutano wa kwanza barani Afrika wa kamati ya maendeleo ya Afrika (African Development Committee), mkutano ulifanyika Tangier nchini humo mwaka huo huo wa 1960.

Halikadhalika mnamo mwaka 1961, Morocco iliweza kuunda jopo na wizara maalumu ya masuala ya Afrika ili kusaidia na kuchangia kupigania uhuru kwa mataifa ya Afrika.

Michakato wa uratibu wa kusaidia na kuunga mkono juhudi za mataifa ya Afrika kupigania uhuru ziliratibiwa katika Jiji la Casablanca na kupewa jina la mkutano wa Casablanca (The Casablanca Conference 1961) ambao ulizaa na kufanikisha kuundwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (Organization of African Unity OAU) hapo mnamo mwaka 1963.

Mfalme Mohamed VI anasema kuwa taifa lake lina sera nzuri na imara sana katika kulinda na kutetea masilahi ya bara la Afrika na amekuwa akiziboresha kila mara hadi hivi sasa. “Kwa maana hii kujitoa Morocco kwa ajili ya kulinda na kuzitetea nchi za Afrika katika harakati zao za kupigania uhuru na kulinda masilahi ya nchi zao si jipya kwetu hadi sasa, ndio maana ninajiamini na niko kifuambele nikijivunia juhudi zetu,” anasema Mfalme Mohamed VI.

Juhudi za Morocco kuwa na nia ya kulisaidia bara la Afrika si za kubahatisha, kwani hadi sasa bado zipo hai na Morocco inaendelea kuzizingatia na kuziboresha, kwani zinaonesha imani kubwa kwao na uthubutu wao bado unaendelea kuwa imara na wanaamini kuwa siku moja utazaa matunda chanya kwa bara la Afrika kuwa taifa moja imara.

Sera ya Morocco kwa sasa ni kuhakikisha kuwa wanatambua mahitaji ya nchi za bara la Afrika, kwani Mfalme wa taifa hilo amekuwa na jitihada za kutembelea nchi zote za Afrika kwani hadi sasa alikuwa ameshatembelea zaidi ya nchi 29 ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja tu toka Oktoba mwaka jana  hadi sasa, alikuwa ameshatembelea mataifa ya Afrika 14 ili kuimarisha na kuboresha mahusiano na kuwa na miradi ya maendeleo yenye lengo la kufaidika kwa nchi zote za Afrika kwa pamoja na Taifa hilo la Morocco.

Sera hii imara ya Taifa hilo inalenga kuhakikisha kuwa dhima ya kuliunganisha bara la Afrika inafanikiwa, kwani hadi sasa Mfalme Mohamed VI anaeleza kuwa tayari Taifa lake limeshaunganishwa na Taifa la Nigeria kwa ukaribu wa kimahusiano na kiuchumi, kwani hadi sasa kuna bomba la gesi linalounganisha mataifa hayo.

Mfalme Mohamed VI alisisitiza kuwa Moroco ipo tayari kuwa pamoja na wapenda amani na maendeleo kote barani Afrika ili kuhakikisha kuwa mustakabali wa Afrika kwa amani, utulivu na maendeleo vinaboreshwa na kuimarishwa ili Afrika izidi kuwa imara.

“Taifa la Morocco linahusika sana kwa kiwango kikubwa katika kuhakikisha kuwa Afrika mpya ya Amani, utulivu, uchumi na maendeleo inajengwa na jitihada hizi zinaanza sasa na sasa ni muda wa kuongea kwa vitendo tu,” anasema Mfalme.

Pamoja na yote hayo, mfalme anasema kuwa Morocco inaimarisha jitihada zake za ujenzo wa Afrika mpya ambazo ilizihuisha miaka kumi na tano iliyopita, ni kweli taifa hili linaonesha kuamka na kupambana kwa ajili ya kuimarisha mahusiano yake na jumuiya mbalimbali barani hapa.

Hii inadhihirika kwa kuwa Morocco hivi karibuni iliweza kujiunga na kuomba na kukubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za Afrika Magharibi (Economic Commission of West African States – ECOWAS), jambo ambalo linazidi kuimarisha mchango wa Taifa hili katika maendeleo ya Afrika.

Inaelezwa kuwa kwa Morocco kujiunga na jumuiya hii, itaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa sana kuchangia na kuboresha uchumi katika ukanda huo wa Afrika ambao pia utaleta chachu ya maendeleo kwa bara lote la Afrika.

Mfalme anaeleza kuwa taifa hilo linatumia pesa nyingi sana kwenye miradi mbalimbali katika mataifa ya Afrika ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya Afrika yanapatikana.

Hali hii inajidhihirisha kwani taifa hilo lina miradi kadhaa hapa nchini kwani hadi sasa wanajenga uwanja wa soka wa kisasa makao makuu ya nchi huko Dodoma, pia ujenzi wa msikiti mkubwa wa kisasa wa Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata), msikiti unaojengwa Kinondoni, Dar es Salam.

Miradi mingine zaidi ya hii inaendelezwa na taifa hili la Morocco katika mataifa mengine barani humu ili kuhakikisha kuwa Afrika imara yenye nguvu kiuchumi na maendeleo inajengwa.

Mfalme katika hotuba yake alihitimisha kwa kuwapongeza mabalozi wake waliopo katika mataifa mbalimbali barani Afrika na duniani kote kwa kusema kuwa wanaiwakilisha Morocco vyema sana kwa lengo la kulinda masilahi si tu ya Morocco, bali ya bara zima la Afrika duniani kote.

Jitihada hizi zinapaswa kuungwa mkono na wapenda amani, utulivu na maendeleo barani Afrika ili kuweza kutimiza ndoto ya kuwa na taifa moja lenye nguvu la Muungano wa Afrika, jambo ambalo litaiwezesha Afrika kuwa shindani kiuchumi.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba hii 0714840656, mosesjohn08@yahoo.com

ENDS