Home KIMATAIFA Ndoto ya wanawake wanaharakati ilivyozama Sudan

Ndoto ya wanawake wanaharakati ilivyozama Sudan

1342
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU

-MITANDAO

VUGUVUGU la mabadiliko nchini Sudan ambalo liliongozwa na wanawake chini ya uratibu wa mwanaharakati, Alaa Salah (22), ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Sudan (SIU) sasa linaonekana kuchukua sura mpya.

Alaa ndiye aliyeongoza maandamano ya kumng’oa madarakani Rais Omar al-Bashir, ambaye aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1989 na kuiongoza Sudan – taifa lililokuwa kubwa barani Afrika katika zama hizo, hadi mwaka 2011 alipochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Mwanaharakati huyo anasema yeye kama mwanamke anafurahi kwa kutimiza wajibu wake nchini mwake.

Al-Bashir alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan iliyokuwa kwenye mapigano makali ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Kaskazini na Kusini kwa miaka 21.

Hata hivyo mapema wiki hii vuguvugu hilo la mabadiliko limechukua sura mpya baada ya wanajeshi kuwakabili waandamanaji.

Vikosi vya ulinzi vimetumia nguvu kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliokita kambi nje ya makao makuu ya jeshi jijini Khartoum.

Milio ya risasi imekuwa ikisikika na tayari watu nane wameripotiwa kufa na kadhaa kujeruhiwa kwenye rabsha hizo.

Sudan imekuwa chini ya utawala wa Baraza la Kijeshi la Mpito toka Al-Bashir alipoondolewa Aprili, mwaka huu, huku waandamanaji wamekuwa wakilazimisha utawala urejeshwe mikononi mwa serikali ya kiraia.

“Kwa sasa kuna jaribio la kutawanya waandamanaji waliokita kambi,”  imeeleza taarifa fupi kutoka kwa Jumuiya ya Wataalamu wa Sudan ambao ndio waratibu wa maandamano hayo ya kitaifa.

Mashuhuda wanasema kuwa kwa sasa waandamanaji wanachoma matairi na kuweka vizingiti ili kuwazuia maafisa usalama kuwafikia.

Mwanahabari Benjamin Strick, ambaye amebobea katika kusanifisha picha zinazotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, alituma video kadhaa za kile kinachoendelea kwa sasa katika Jiji la Khartoum.

Jeshi la Sudan hadi sasa bado lipo kimya juu ya kinachoendelea huku waandamanaji wakipiga kambi mbele ya makao makuu ya jeshi tangu Aprili 6, mwaka huu, siku tano kabla ya Bashir kupinduliwa na jeshi.

Mwezi uliopita, viongozi wa waandamanaji na majenerali wa jeshi walitangaza kuwa wamefikia mwafaka wa muundo wa serikali ya mpito ya miaka mitatu ambayo itaandaa uchaguzi wa kiraia.

Lakini wanasema bado wanatakiwa kufanya maamuzi ya nani aingie kwenye baraza huru ambalo ndilo litakuwa na maamuzi ya mwisho kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitatu.

Hadi sasa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa kuhusu upande upi baina ya raia na wanajeshi uwe na wawikilishi wengi kwenye baraza hilo.

RAMADHANI  ILIVYOIMARISHA HARAKATI 

Sasa ni zaidi ya mwezi mmoja baada ya majeshi nchini Sudan kuuondoa madarakani utawala wa Bashir, umati mkubwa wa watu umeendelea kupiga kambi usiku na mchana mbele ya makao makuu ya kijeshi katika mji wa Khartoum.

Wanahisi kuwa utawala wa mpito unaoongozwa na Baraza la Jeshi hautaki kuhamisha madaraka kwa utawala wa kiraia.

Wamejitolea kufanya hivyo licha ya kuwa wanaendelea na mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Nguvu ya uwepo wao katika eneo hilo inadhihirika wakati wanapokuja pamoja kufuturu jua linapotua.

Punde baada ya wao kusali na kufuturu waandamanaji wanaanza kuimba kwa pamoja: “Utawala wa kiraia ama mageuzi ya daima”.

Wengine wanajibu kwa kufuatilia na maneno haya : “Sitarudi nyuma, Nina mahitaji”.

Maelfu ya watu huanza kufika huku wengine wakiwa wamebeba vyakula vyao pamoja na maji kutoka nyumbani na wengine huamua kupika pamoja katika eneo lililotengewa waandamanaji.

Vyakula pia hutolewa na wanawake ambao wanawaalika watu waliojitolea kuunga mkono maandamano hayo kupitia mitandao ya kijamii kwenda majumbani mwao kuchukua vyakula.

Taasisi mbalimbali zimejitolea kuwapelekea maji ya chupa na vyakula kwa kutumia magari makubwa ili kuhakikisha hakuna mtu anayeshiriki maandamano hayo anaumia kwa njaa au kiu wakati huu wa Mfungo wa Ramadhani.

Viongozi wa kijeshi Sudan wamesitisha kwa muda wa siku tatu mazungumzo na waandamanaji juu ya kubuniwa kwa baraza huru la mpito.

HARAKATI ZA VUGUVUGU

Desemba 9, 2018: Maandamano yanalipuka baada ya bei ya mafuta na mkate kupanda.

Desemba 20, 2018: Waandamanaji jijini Khartoum waanza kuimba nyimbo dhidi ya Serikali wakitaka “uhuru, amani, haki”

Februari 22, 2019:  Rais Omar al-Bashir atangaza hali ya hatari na kuvunja Baraza la Mawaziri.

Februari 24, 2019: Maandamano yanaendelea licha ya vyombo vya ulinzi kutumia silaha za moto kutawanya waandamanaji 

Aprili 6, 2019: Wanaharakati waanza kukita kambi mbele ya makao makuu ya jeshi wakiapa hawataondoka hadi Bashir ang’oke madarakani .

Aprili 11, 2019: Majenerali wa jeshi wanatangaza kuwa Bashir ameng’olewa uongozini lakini waandamanaji wasalia wakitaka Serikali ya kiraia. 

Aprili 17, 2019: Bashir alipelekwa jela jijini Khartoum.

Aprili 20, 2019: Mazungumzo baina ya viongozi wa kijeshi na wawakilishi wa waandamanaji yalianza. 

Mei 13, 2019: Shambulio la risasi nje ya Makao Makuu ya Jeshi linasabisha watu sita kuuawa.

Mei 14, 2019: Majenerali na viongozi wa raia watangaza mapatano ya kuunda Serikali ya mpito ya miaka mitatu.

Mei 16, 2019: Mazungumzo yanaahirishwa baada ya jeshi kutaka baadhi ya vizuizi kuondolewa.