Home Makala Kimataifa NDOTO YA‘DUNIA BILA NYUKLIA’ NI NGUMU KUTIMIA

NDOTO YA‘DUNIA BILA NYUKLIA’ NI NGUMU KUTIMIA

1542
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Miezi michache tu baada ya kuingia Ikulu kuwa Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama alizungumzia ndoto yake ya kuwa na dunia isiyo na sila za nyuklia.

Katika hotuba yake aliyoitoa huko Prague, Mji mkuu wa Jamhuri ya Czech, Mei 2009 kwa maelfu ya wananchi wa nchi hiyo katika mkutano wa hadhara, Obama alisema Marekani ambayo ni nchi pekee duniani iliyowahi kutumia silaha hizo kwa hasira, inayo majukumu ya kimaadili kuanzisha enzi mpya ya upunguzaji wa mirundikano wa silaha za nyuklia.

Aliongeza kusema kuwa katika kipindi chake atahakikisha nchi yake inazingatia upatikanaji wa amani katika dunia isiyo na silaha za nyuklia.” Ingawa ni kweli katika kipindi chake cha miaka minane hadi anaondoka madarakani hakukutokea matumizi ya zana hizo vitani, lakini ilikuwa dhahiri kauli ile ilikuwa ya kimawazo tu na ni kitu ambacho kisingewezekana kwani kingeweza kuamsha pingamizi kubwa kutoka karibu nchi nyingine nane zinazosadikiwa kumiliki silaha za nyuklia. Nchi hizo ni Uingereza, Ufaransa, Urusi, China, India, Pakistan, Israel na Korea ya Kaskazini. Hata hivyo, umiliki wa Israel wa silaha hizo unafanywa kwa siri kubwa.

Na ingawa Obama alikiri kwa kusema kwamba lengo lake huenda lisikamilike katika kipindi cha uhai wake, kauli yake hiyo ilionekana inasimika sera mpya za nchi yake kwa masuala ya mambo ya nchi za nje na upunguzaji wa silaha hizo hatari ni sera mpya ambayo haijapatwa kutamkwa na kiongozi yeyote wa Marekani kwa miongo kadhaa.

Alisema ataondoa umuhimu wa nchi yake kumiliki silaha hizo katika mpango mzima wa usalama wa nchi hiyo na kwamba atatoa msukumo kwa Bunge la Senate la nchi hiyo mara moja liridhie mkataba mzima wa kimataifa wa upunguzaji wa silaha za nyuklia duniani (wa mwaka 1968), hatua ambayo Marekani ilikuwa bado haijafanya kikamilifu.

Aidha, kauli hii ya Obama iliendana na onyo kwa Korea ya Kaskazini na Iran na pia uwezekano wa nchi nyingine alizoziita za ‘kigaidi’ kumiliki silaha za nyuklia. Alisisitiza kuwa Iran inayo haki ya kuendeleza mradi wake wa nishati ya nyuklia, lakini chini ya usimamizi wa kimataifa.

Miaka minane baada ya kauli hiyo, dunia sasa hivi inashuhudia uwezekano wa matumizi ya zana za nyuklia katika vita, kutokana na majaribio ya urushaji wa makombora yenye zana hizo yanayofanywa na Korea ya Kaskazini pamoja na vitisho vyake vya kuvishambulia Marekani.

Hata hivyo, si wengi wanaoamini utawala wa Korea ya Kaskazini unaweza kweli kukabiliana vilivyo na Marekani pamoja na washirika wake wa dunia ya Magharibi katika vita yoyote ijayo ya nyuklia.

Kama ilivyotajwa hapo mbele, Mkataba wa Upunguzaji wa Silaha za Nyuklia (Nuclear Non-Proliferation Treaty – NPT) ulianzishwa mwaka 1968 wakati wa Vita Baridi na lengo ni kuzuia usambazwaji wa silaha hizo pamoja na teknolojia ya utengenezaji wake.

Pamoja na vipengele vigumu vya mkataba huo, kumetokea ukiukwaji mkubwa tangu wakati huo, ukiukwaji uliotokana na usimamizi mbovu. Mataifa makubwa yamekuwa hayazingatii haki katika usimamizi na migongano ya sera na itikadi imekuwa ikiathiri sana utekelezwaji wa mkataba huo kikamilifu.

Karibu nchi zote tano zenye uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa China na Urusi) zinamiliki silaha za nyuklia na zinatambulika hivyo katika NPT.

Nia hapa, inasemekana ni kwamba nchi zote hizi tano polepole zitapunguza silaha zao kwa matarajio kwamba hakuna nchi nyingine zitataka kumiliki silaha hizo.

Wanaoiunga mkono NPT wanasema mkataba umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwani kusingekuwapo mkataba huo nchi nyingi zingeweza kutengeneza zana hizo hatari na hivyo kumiliki silaha hizo katika kipindi cha miongo mitano iliyopita.

Mataifa makubwa yamekuwa hayatendi haki katika kusimamia NPT na hivyo kuruhusu au kutofanya lolote kwa nchi nyingine zinazomiliki silaha za nyuklia. Kwa mfano, India, Pakistan, Israel na Korea ya Kaskazini hazijatia saini mkataba wa NPT ingawa zinamiliki silaha za nyuklia.

Kuhusu Israel, Marekani imekuwa inapuuzia umiliki wake wa silaha hizo hatari, huku ikiikoromea Iran ambayo daima hujitetea kwa kusema haina silaha za nyuklia, wala haina nia ya kuzitengeneza na kwamba mradi wake wa nyuklia ni kwa ajili ya nishati tu.

Na pamoja na hayo, Iran ilisaini mkataba wa NPT wakati wa utawala wa aliyekuwa mfalme wa nchi hiyo, Shah Mohammed Reza Pahlevi aliyekuwa swahiba mkubwa wa Marekani katika miaka ya 70.

Lakini hakuna Taifa ambalo umilikaji wake wa silaha za nyuklia umeleta utata mkubwa kama Pakistan. Tangu kuundwa kwake mwaka 1948, nchi hii imekuwa haina utulivu wa kisiasa na zaidi ya theluthi mbili ya kipindi hicho imekuwa inatawaliwa kijeshi. Aidha, imepigana vita nne na jirani yake India, mara ya mwisho kabisa ni mwaka 1999.

Miaka michache baadaye nchi hiyo ilikuwa na msukosuko mkubwa kutokana na kuingiliwa kwake na Marekani na kufanywa eneo muhimu katika vita yake dhidi ya ugaidi. Hatua hii iliamsha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na hivyo kuzuka ‘vikundi’ vingi vya kigaidi vilivyokuwa vinapinga ardhi yao kutumika na Wamarekani katika azma hiyo.

Vikundi hivi vimekuwa vikifanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kujitolea mhanga na kusababisha vifo vingi na majeruhi kwa watu wasiokuwa na hatia.

Kuna baadhi ya watu walidiriki kumwambia aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, George W. Bush, kwamba ilikuwa vyema na halali kwa Marekani kuivamia kijeshi na kuikalia Pakistan, badala ya Iraq, kwani Pakistan ilikuwa na silaha za maangamizi (za nyuklia) na kuwepo magaidi kibao, wakati Iraq ilikuwa haina kabisa vitu hivyo wakati inavamiwa kijeshi na Marekani mwaka 2003.

Isitoshe, Pakistan iligundulika kwamba ndiyo nchi iliyoiuzia Korea ya Kaskazini teknolojia ya kutengeneza zana za nyuklia, kitu ambacho si siri baada ya kukiri mwaka 2004 kufanya hivyo kwa mwanasayansi wa nyuklia Mpakistan Abdul Qadeer Khan.

India ambayo pia haijasaini mkataba wa NPT, inazo silaha za nyuklia kwa sababu tu hasimu yake Pakistan inazo. Nchi zote mbili zina uhusiano mzuri na Marekani ambayo imekuwa haitoi msukumo wowote wa kusaini NPT.

Hata hivyo, inasadikiwa kuna jumla ya nchi nyingine 25 duniani ambazo zimejaribu, katika nyakati tofauti, kumiliki zana za nyuklia. Baadhi yao:

  • Afrika ya Kusini: Wakati wa utawala wa Makaburu nchi hii ilitengeneza bomu la nyuklia, lakini baada ya uhuru kwa wazalendo mpango mzima ukafutiliwa mbali katika miaka ya 90.
  • Iraq: Wakati wa utawala wake, Sadaam Hussein alijaribu kuunda bomu la nyuklia lakini alishindwa ki-teknolojia.
  • Libya: Libya, chini ya Muammar Gaddafi iligundulika inanunua vifaa vya kutengeneza silaha za nyuklia kutoka Pakistan na hata hivyo baadaye ikaachana na mpango huo.
  • Japan: Nchi hii inayo vifaa na teknolojia ya kutengeneza zana za nyuklia na inaweza kuunda mabomu hayo kwa haraka sana kama ikitaka.
  • Ujerumani: Vivyo hivyo kama Japan.

Nchi nyingine zinazotajwa kwamba zina silaha hizo ni Brazil, Argentina, Algeria , Saudi Arabia, Syria na Uturuki, ingawa kumekuwa hakuna uthibitisho.