Home Habari kuu Ndugai abeba maridhiano

Ndugai abeba maridhiano

1231
0
SHARE

Na Mwandishi Wetu-DODOMA

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, sasa anatazamwa kama kiongozi aliyebeba jukumu la maridhiano ya kisiasa ndani na nje ya Bunge, RAI linachambua.
Anatazamwa kwa sura hiyo kutokana na kauli zake za hivi karibuni za kutaka amani, umoja na mshikamano vitawale ndani ya Bunge.

NDANI YA BUNGE

Katika mazungumzo yake na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge, Ndugai alisema si jambo la busara kwa Wabunge kutukuza watu wengine huku wengine wakififishwa.

Spika alikemea tabia ya baadhi ya Wabunge kuwatukuza baadhi watu huku wengine wakionekana si lolote mbele ya jamii.
Amesema anahitaji kujenga Bunge moja ambalo lilionekana kumeguka vipande viwili, hasa baada ya Wabunge wa Kambi ya Upinzani kususia vikao vyote vilivyokuwa vinaendeshwa na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson.

Uamuzi wa Ndugai kusaka maridhiano umeonekana dhahiri kwenye kikao chake cha kwanza cha Mkutano wa Nne wa Bunge, ulioanza juzi.

Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na Wabunge wote wa upinzani wakiwa wamevalia mavazi meusi, hali ilikuwa shwari, tofauti na ilivyokuwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Bajeti, lililokuwa chini ya Dk. Tulia.

Katika Bunge la Bajeti, kuliibuka mgawanyiko uliowahusisha Wabunge wa Upinzani walio chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa upande mmoja, na Naibu Spika, Dk. Tulia kwa upande wa pili.

Sababu zilizoibua mgawanyiko huo, zilidaiwa kuwa ni hatua ya Dk. Tulia kushindwa kuendesha vikao vya Bunge kwa usawa, pamoja na kuchochea migogoro, mvutano, matumizi ya polisi ndani ya Bunge, kuwasimamisha baadhi ya Wabunge wa Upinzani na kauli za kejeli za mara kwa mara zilizokuwa zikitolewa na pande zote mbili.

Dk. Tulia ambaye ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais, alikuwa akilalamikiwa mara kwa mara na Wabunge hasa wa upinzani, kuwa alikuwa na tabia ya kukandamiza hoja zao, huku akizikubali hoja na kauli za kuudhi za Wabunge wa chama chake.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika huyo, ambaye alidaiwa kukalia kiti hicho kimkakati, amekuwa akitazamwa kama mtu anayeoongoza mhimili huo wa pili wa dola kwa nia ya kuilinda Serikali.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ni miongoni mwa Wabunge wenye mtazamo huo, ambapo kwenye ukurasa wake wa Twitter, aliwahi kuandika ujumbe uliobeba dhana hiyo.

Zitto aliandika: Hata Nyerere hakuwahi kujaribu kuleta Spika wake au Naibu Spika wa mfukoni mwake. Alipomteua Chief Adam Sapi Mkwawa kuwa Waziri, aligomewa na Wabunge (wakati wa chama kimoja), akamrudisha kwenye nafasi yake ya Spika, nafasi aliyokalia hadi alipostaafu tena kwa kumtungia Sheria ya Ustaafu (wakati wa Mwinyi).

“Unapoona Rais anajaribu kulazimisha Kiongozi wa Bunge anayemtaka, mjue huko mbele ya safari, Bunge litafanywa kibogoyo. Kwa mfano, hakuna Naibu Spika yeyote katika nchi hii, ambaye hakuwahi kuwa Mbunge wa Jimbo. Nawakumbusha tu kwamba; Bunge huendeshwa kwa kutumia Katiba, Sheria, Kanuni na desturi au maamuzi yaliyokwishafanywa.”

Zitto alikwenda mbali zaidi kwa kumnyooshea kidole Rais magufuli kuwa kwa sasa yeye ndio analiendesha Bunge kwa ‘remote control’.
“Rais Magufuli tunakuunga mkono kwa dhati kupambana dhidi ya ufisadi. Tunakupinga kwa nguvu zote kupambana dhidi ya demokrasia. Kuanzia mwanzo tumekuunga mkono dhidi ya ukwepaji kodi, ubadhirifu, uvivu na uzembe.

“Tangu mwanzo tulionya kuwa ni lazima udhibitiwe na Bunge ili ufanye kazi kwa mujibu wa Katiba. Hivi sasa wewe Rais ndio unaendesha Bunge kwa ‘remote control’. Tunakupinga kuturudisha nyuma. Hutafanikiwa kamwe kubomoa misingi ya taasisi za uwajibikaji tulioanza kuzijenga.

“Narudia nukuu muhimu sana ‘ukitaka kutawala tawala peke yako. Ukitaka kuongoza ongoza na wenzako’ Rais Magufuli Tanzania inataka uongozi madhubuti na si wa kiimla. Huko tumeshatoka na Watanzania hawatakubali kurudi huko.”

Mnyukano huo wa maneno, sasa unakila dalili ya kumalizwa na Ndugai, ambaye kwa namna moja au nyingine, anaonekana kukubalika na pande zote mbili.

Kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge, Ndugai pia alipata nafasi ya kukutana na baadhi ya viongozi wa kisiasa nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam mara baada ya kurejea nchini mwishoni mwa Julai akitokea nchini India kwa matibabu.

AGOSTI 3

Mara baada ya kurejea nchini, Ndugai alikutana na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe hata hivyo mazungumzo yao hayakuwekwa wazi zaidi ya kuelezwa kuwa Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alikwenda kumjulia hali.

AGOSTI 13

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi –CUF, Maalim Seif ambaye anatazamwa kama mpinzani mkubwa wa siasa za Zanzibar, akiwa na ujumbe wake alimtembelea Ndugai nyumbani kwake, Salasala.
Kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine, mazungumzo ya Maalim Seif na Ndugai hayakufahamika wala kuwekwa wazi.

AGOSTI 15

Wiki mbili baada ya kuonana na Mbowe, Ndugai alipata nafasi ya kuonana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva ambaye alimtembelea nyumbani kwake kwa maelezo kuwa nae amekwenda kumjulia hali baada ya kurejea kutoka nchini India alikokwenda kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo Jaji Lubuva akiwa nyumbani kwa spika pamoja na mazungumzo yao ambayo pia hayakuwekwa wazi, alimkabidhi ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015 na kumueleza kuwa kukamilika kwa ripoti hiyo ndio hitimisho la Uchaguzi Mkuu na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Kwa upande wake Ndugai aliipongeza hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya kuweka mikakati ya kushiriki katika maonyesho mbalimbali yakiwemo yale ya biashara SabaSaba na Nanenane katika kutoa elimu kwa wananchi.

AGOSTI 16

Siku moja baada ya Jaji Lubuva kumtembelea Spika Ndugai, Rais John Magufuli nae alifanya hivyo akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli.

Pamoja na mazungumzo yao ambayo pia hayakuwekwa wazi Rais alimwombea Spika kwa Mwenyezi Mungu apone na kupata nguvu haraka ili waweze kuendelea na majukumu yake ya kawaida katika ujenzi wa Taifa.

Katika ziara hiyo Ndugai alishukuru kutembelea na Rais na kumjulia hali na kufuatilia afya yake kwa ukaribu wakati wote alipokuwa akipata matibabu nchini India hadi aliporejea hapa nchini.

NJE YA BUNGE

Busara hizo za Ndugai ndani ya Bunge, zinamfanya kuwa mmoja wa viongozi wachache ndani ya Dola, kuwa na ushawishi mbele ya wanasiasa wa pande zote mbili nje na ndani ya Bunge.
Kwamba anao uwezo wa kuzisuluhisha kisiasa pande zinazosigana, kutokana na hatua yake ya awali ya kumaliza msigano usio na tija ndani ya Bunge.

Wanaobeba hoja hiyo wanamtazama Ndugai kama mwanasiasa na kiongozi shupavu wa moja ya mihimili mitatu ya dola, mwenye kauli zenye kubeba dhana ya demokrasia, tofauti na ilivyo kwa baadhi yao, ambao hutumia kauli nzito na maneno makali na ya vitisho. Kiongozi mzuri husikiliza hoja na kufanya uwamuzi wa busara kwa lengo la kutuliza mihemuko ya kisiasa.

Akizungumzia hatua hiyo ya Ndugai Msemaji wa chama cha ACT Wazalendo, Abdallah Khamisi, alisema Spika ameonesha ukomavu kisiasa kwani siasa inahitaji maridhiano na si vitisho wala ubabe kama inavyofanywa na baadhi ya viongozi.

“Suala la maridhiano ni jambo la msingi kwani jambo lolote lisilokuwa na maridhiano mwisho wake huwa ni mbaya,”alisema.
Aliongeza kuwa hatua ya Spika Ndugai kuwaunganisha wabunge wote linapaswa kuungwa mkono na watu wote na kwamba maridhiano hayo yawe ya vitendo ili ifikie wakati kila mmoja akubali kupoteza baadhi ya vitu kwa masilahi ya Taifa.

“Jambo alilolifanya Spika kutafuta mwafaka wa kuwarudisha wabunge wa upinzani bungeni ni jambo la zuri na liwe mfano kwa yule aliyesababisha mgogoro huo kwamba kila jambo analolifanya liongozwe na busara.

“Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson hakutaka kujishusha na kuamua kuwa na kiburi hivyo kusababisha wabunge wa Upinzani kutoka bungeni na kumuacha aongoze Bunge mwenyewe. Sitaki kuamini kuwa kiburi hicho kimetoka na kuingia bungeni kwa namna aliyoingia.

“Mtu wa namna hiyo ambaye hana taadhari ya kufanya jambo ni sawa na yule anayejitoa muhanga kwa jambo fulani ili mradi atimize malengo yake,” anasema Khamisi.

Aliongeza kuwa hali hiyo ya kubeba maridhiano inamfanya Ndugai kuwa miongoni mwa viongozi wachache wanaoweza kuondoa mkwamo wa kisiasa uliotawala nje ya Bunge kwa sasa.