Home kitaifa Ndugai awashangaza wasomi

Ndugai awashangaza wasomi

1302
0
SHARE

MWANDISHI WETU

MWENDELEZO wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwafikisha baadhi ya viongozi mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, pamoja na kuwatishia polisi umeonekana kuwashangaza baadhi ya wasomi. RAI linaripoti.

Katika siku za hivi karibuni, Spika Ndugai ameshawafikisha mbele ya Kamati hiyo, baadhi ya wabunge kutokana na kudaiwa kufanya makosa mbalimbali.

Hata hivyo, viongozi walioibua mjadala baada ya kuagizwa na Spika kufika mbele ya Kamati hiyo na kama wasingefanya hivyo wangefikishwa kwenye kamati hiyo chini ya ulinzi wa Polisi ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Mussa Assad na sasa mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika, Stephen Masele.

Masele ameingia kwenye kadhia hiyo baada ya kudai kuwa anasimamia haki ndani ya PAP kwa kuunda Tume ya kumchunguza Rais wa Bunge hilo Roger Dang.

Utetezi huo ulionekana kutofua dafu mbele ya nia ya Spika Ndugai, ambaye aliagiza mwanasiasa huyo kijana arejee nyumbani haraka sanjari na kusitisha ubunge wake ndani ya PAP kwa kile alichodai kuwa ni kufanya mambo ya ovyo ovyo, pamoja na kugonganisha mihimili ya dola.

Kwa kuzingatia taratibu za kiongozi Masele ambaye alisema anaheshimu miiko ya uongozi na hajawahi kukurupuka na kwamba hajafanya kosa lolote la utovu wa nidhamu katika Bunge hilo la PAP, zaidi alikuwa anasimamia misingi ya hakiza binadamu, mwanzoni mwa wiki hii alifika mbele ya Kamati hiyo, jijini Dodoma.

Kutokana na hatua hiyo ambayo imeibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii,  baadhi ya wasomi waliliambia RAI kuwa wanashangazwa na hatua ya Spika wa Bunge kuutumia muda wa Bunge la Bajeti kushughulika na watu badala ya masuala muhimu yanayogusa maslahi ya wengi.

Badala yake wamemshauri Spika kuepuka kufanya uamuzi kwa jazba, hatua inayomfanya kuonekana kama ana chuki binafsi kwa anaowataka wafike mbele ya Kamati hiyo.

Aidha, walimwomba ajitahidi kushauriana na viongozi wenzake na hasa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kabla ya kutangaza maamuzi yoyote ili kuondoa maswali yasiyojibika.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala, alisema hamwelewi na anamshangaa Spika Ndugai… na kuongeza kuwa haelewi ni Spika wa aina gani kwa sababu anaonekana ni mtu mwenye jazba.

Alitolea mfano mvutano kati yake na CAG na kubainisha kuwa halikuwa saula la msingi la kupambana na Prof. Assad kiasi kile.

“CAG alitamka maneno yale kama kulikosoa Bunge, jambo ambalo si dhambi na kwamba katika mfumo wowote kukosoana ndiyo msingi wa maendeleo, lakini Spika Ndugai alilishughulikia kwa jazba kwelikweli, hata hivyo naamini baadae yeye ndiye ameonekana ni tatizo siyo CAG.

“ Kauli ya CAG ilisababisha wabunge ambao walitoa matamko kwa kum- quote  (nukuu) CAG nao wanasimamishwa ubunge. Sasa hii ya Masele mimi nilikuwa namfuatilia sana kule Afrika Kusini, yale anayoyazungumza mle kwenye Bunge unasema kweli Tanzania tuna mwakilishi kwenye Bunge la Afrika.

“Alikuwa anazungumza mambo ya busara kabisa, sasa alivyoibuka Spika na kusema mambo ya ovyo ovyo ni mambo gani ya ovyo ovyo aliyoyafanya kule, mimi ninasema Spika wetu wa sasa nadhani tuna matatizo naye,” alisema.

Aliongeza kuwa kiongozi wa Bunge anatakiwa kutambua kuwa Bunge ni chombo cha wawakilishi wa wananchi, ni chombo kikubwa.

“Lazima wafanye kazi ya kuwawakilisha wananchi, kujadili mambo, sheria na sera za kuwakomboa wananchi na wahakikishe kwamba Bunge linai-control Serikali katika misingi ya kisheria, lakini sasa badala ya kufanya hayo utakuta yuko kwenye malumbano aidha na wabunge wenzake au na watu wa Serikali, jazba jazba mimi sielewi.”

Aidha, Prof. Mpangala alimshauri Spika Ndugai ashauriane kwanza na wenzake na kupata ushauri kabla ya kuchukua maamuzi.

Hoja hiyo pia imeungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk. Benson Bana ambaye alisema wapiga kura wasingependa kuona mazingira ya aina hiyo yakijitokeza katika mhimili huo ambao ndiyo unaowakilisha wananchi.

“Sifurahii kuona mbunge wangu akipewa adhabu ya kutohudhuria vikao… unamwadhibu yeye mmoja, lakini sisi wananchi maoni yetu hayafiki bungeni na hatuna mbadala kwa hiyo ni adhabu ya mbunge lakini kwa mtazamo mpana inakwenda mpaka kwa wananchi wa jimbo lile ambao wamemchagua hilo si jambo jema.

“Lema anakosekana bungeni, na sisi watu wa huku Boko na Bunju tunamkosa Halima Mdee,  sasa hilo nalo kwa upande wangu ni tatizo, labda kanuni za Bunge wangeliangalia upya, ni vema hata ukampa adhabu ya kumkata mishahara miwili kuliko kumzuia kabisa asiwepo, kwa sababu hiyo adhabu inawaathiri wale waliomchagua, maoni yao hayafikishwi bungeni,” alisema.

Hata hivyo, aliwashauri wabunge kusimamia  viapo vya ubunge wao kwa kufuata kanuni na sheria.

Pamoja na kutofurahishwa na baadhi ya maamuzi ya Spika, Dk. Bana alisema anaamini maamuzi yonayotangazwa na Spika bila shaka ni ya Kamati zilizozopo kisheria, hivyo kuna haja pia ya kuliangalia hilo.

“Lakini Spika anatangaza maamuzi ya kamati husika na Bunge zima aidha litayaafiki ama litayapuuza, nalo pia hilo tulitilie maanani, maana inaonekana lawama kubwa zinakwenda kwa Job Ndugai kama Spika,” alisema na kuongeza kuwa.

Spika Ndugai ana Kamati ya maadili, ambayo haipaswi kubinafsishwa na kuyafanya kuwa mambo ya Spika ila ni mambo yanayokwenda mezani kwake kwa kuwa yeye ndiye msemaji wa Bunge.

Aidha, alikwenda mbali zaidi kwa  kushangazwa na vitendo vya wabunge kushindwa kujadili hoja zinazowasilishwa bungeni badala yake wanajikita katika kuwajadili Lema na Masele au CAG Assad na Spika Ndugai.

“Nadhani ifike wakati Bunge lijitathmini kwanini kila siku tunajadili bajeti yenye hoja ni zile zile… bajeti ya maji iongezwe nk. ukisoma vitabu vya Bunge vya mwaka uliopita, ikija kwenye bajeti ya kilimo mambo ni yale yale na hoja ni zile zile. Inatakiwa mtu anaposema bajeti ya maji iongezwe aseme wapi ipunguzwe,” alisema Dk. Bana.

Kauli za wasomi hao zinawiana na ile ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, aliyoitoa mkoani Kilimanjaro wakati wa shughuli za mazishi ya mfanyabiashara Reginald Mengi kwa kumtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kutenda haki na kufanya maamuzi ambayo yana masilahi kwa wananchi wanaowawakilisha bungeni.

Dk. Shoo alitoa onyo hilo wakati akiendesha ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Usharika wa Moshi Mjini Mei 9, mwaka huu.

Katika mahubiri yake alitumia nafasi hiyo kumtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kutenda haki na kufanya maamuzi ambayo yana masilahi kwa wananchi wanaowawakilisha bungeni.

“Ndugai leo upo hapa, nasema mnapokaa bungeni na kuamua mambo, mtende haki na mfanye maamuzi yenye masilahi kwa wananchi,” alisema.

Masele

Mvutano kati ya Spika na Masele uliibuka rasmi  Mei 16 mwaka huu baada kumtaka mbunge huyo arudi haraka nchini ambako pia alibainisha kuwa atafikia mikononi mwa Kamati za maadili za Bunge na chama chake (CCM) kwa kuwa amekuwa akifanya mambo kinyume na utaratibu na kugonganisha mihimili ya dola.

“Amefanya mambo ya utovu wa nidhamu huko na taarifa tumezipata na hata kwenye mitandao imeonekana, sasa tumemtaka arudi lakini amegoma hivyo tumeamua kusimamisha kwa muda ubunge wa mheshimiwa huyu hadi tutakapotoa taarifa nyingine,” alisema Ndugai.

Akijibu madai ya Spika Ndugai, Masele alisema msimamo wa kuunda Tume ya uchunguzi dhidi ya Dang aliyetuhumiwa kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ndiyo.

Wakati wa uchunguzi huo, tayari Masele alikuwa akikaimu nafasi ya Rais wa Bunge hilo, akisema ripoti imeshakamilika na inaonesha Dang alikuwa na kesi za kujibu.

CAG

Spika Ndugai na CAG Assad waliingia  katika mvutano ambao ulianzia mwishoni mwa mwaka jana baada ya Ndugai kulieleza Bunge kuwa maelezo ya Prof. Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.

Aidha, baada ya Prof. Assad kuripoti mbele ya kamati hiyo na kujieleza na baadaye Bunge kuazimia kutofanya kazi naye, Ndugai aliongeza kuwa CAG anafaa kujitathmini na kuchukua uamuzi wa kujiuzulu.

Pia alidai Assad “anampatia wakati mgumu” rais John Magufuli, na kumtaka aende mbele yake (rais) kujieleza.

Mvutano huo ulianza baada ya CAG kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

Sakata la CAG lilisababisha baadhi ya wabunge wa upinzani kuadhibiwa kutokana na kumuunga mkono Prof. Assad.

Miongoni mwa wabunge walioadhibiwa ni Godbless Lema (Chadema-Arusha Mjini), na  Halima Mdee (Chadema-Kawe).