Home Makala NEC na uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura

NEC na uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura

1044
0
SHARE

Barthoromew Wandi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kupewa majukumu mbalimbali ya msingi ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani kwa Tanzania Bara.

Uboreshaji huo wa daftari la kudumu la wapiga kura, kisheria hutakiwa kufanyika mara mbili ndani ya miaka mitano, yaani baada ya uchaguzi mmoja kumalizika na kabla ya unaofuata kufanyika.

Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na madiwani wa Tanzania Bara wa mwaka 2015 umeshamalizika ndiyo maana Julai 18 mwaka 2019, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alialikwa na tume kuzindua  Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa 31 ya Tanzania kwa awamu ya kwanza katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Baada ya uzinduzi huo, uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ulishika kasi katika mikoa mingine ambapo mpaka sasa mikoa 27 tayari imeshaboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Mikoa ambayo mpaka sasa imeshamaliza Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Simiyu, Mara, Mwanza, Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida, Dodoma, Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Lindi na Mtwara.

Mikoa minne iliyobaki kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura, ingawa mchakato wa uboreshaji unaendelea kwenye mikoa hiyo ni Tanga, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Ukiangalia kwenye takwimu hapo juu utaona kuwa tume imeenda kwa kasi sana kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, mikoa mingi zaidi ukilinganisha na iliyobaki pamoja na changamoto za kusimamisha zoezi la uboreshaji kupisha masuala mengine ya kitaifa kama; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Tamisemi), mitihani ya darasa la saba, kidato cha pili na kidato cha nne.

Kutokana na kasi iliyonayo NEC, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mikoa minne iliyobaki linatazamiwa kumalizika Februari mwaka huu.

Awamu ya kwanza itaisha pale tu daftari la awali la wapiga kura litakapowekwa wazi huko kwenye ofisi za kata Machi mwaka huu ili wapiga kura walioandikishwa upya na walioboresha taarifa zao na wengine waliohamisha taarifa zao waangalie majina yao kama hayajakosewa na taarifa zao kama ziko sahihi na pia kuwawekea pingamizi wale ambao wameandikishwa kwenye daftari hilo lakini hawana sifa za kuwemo kwenye daftari hilo.

Watu ambao hawana sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wapya kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ni wale ambao ni raia wa nchi nyingine au ana uraia wa nchi mbili, wana utii wa nchi nyingine, wamethibitishwa na daktari kuwa hawana akili timamu na wamehukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama.

Sababu nyingine ambazo zinaweza kuwakosesha watu wasiandikishwe kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ni kwamba wanatumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita gerezani, wamezuiliwa kujiandikisha kuwa wapiga kura na sheria za uchaguzi ama sheria nyingine kwa makosa yanayohusiana na uchaguzi na hawatakuwa wametimiza umri wa kupiga kura ikifika siku ya uchaguzi.

Watu ambao wana sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wapya kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ni wale ambao ni raia wa Tanzania, wametimiza umri wa miaka 18 na kuendelea au atatimiza umri wa miaka 18 ikifika siku ya uchaguzi na hawajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi au sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge la Tanzania.

Zoezi hili la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa ujumla litawahusu wananchi wote waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawakuandikishwa mwaka 2015, watakaotimiza umri wa miaka 18  Oktoba mwaka huu, waliojiandikisha mwaka 2015 na sasa wamehama kata na jimbo moja kwenda linguine.

Wananchi wengine watakaohusika na zoezi hili ni wale ambao walikosa sifa za kupiga kura mfano kuondoa wale waliofariki dunia au wamepata uraia wa nchi nyingine, wale ambao jinsia zao, tarehe za kuzaliwa na majina yao yalikosewa wakati wa uandikishaji wa mwaka 2015, waliopoteza kadi zao na wale ambao kadi zao za kupigia kura zimeharibika.

Kwa wale ambao waliandikishwa mwaka 2015 na wanazo kadi zao lakini hazijakosewa taarifa zao, hazijafutika maandishi au picha na hawajahama kata au jimbo kwenda kata au jimbo lingine la uchaguzi, hawa hawahitajiki kwenda vituoni kupata kadi nyingine ila wataendelea kuzitunza kusubiria siku ya Uchaguzi Mkuu na chaguzi zingine ndogo zitakazotokea baada ya Uchaguzi Mkuu kupita mwaka huu.

NEC inatumia njia mbalimbali kuwahimiza na kuwahamasisha wananchi wote wanaohusika na zoezi hili la uboreshaji waende vituoni wakajiandikishe na kuboresha taarifa zao ili waweze kushiri Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Njia ambazo NEC inatumia kuwahimiza na kuwahamasisha wananchi waende vituoni ni matangazo kupitia vyombo vya habari, kama Redio na TV, vipindi mubashara kwenye Redio na TV, vya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, gari la matangazo la tume na gari la matangazo la Halmashauri,  asasi za kiraia, kushiriki maonesho mbalimbali ya kitaifa kama Sabasaba, Nanenane, mikusanyiko ya kijamii kama vile masoko, minada, matamasha na mitandao ya kijamii.

Tume inatoa rai kwa namna ya pekee kwa kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura kwenda kituoni mwenyewe akajiandikishe na mwenye kuhitaji kuboresha taarifa zake, naye aende kituoni akaziboreshe ili apate kadi yake kama kauli mbiu inavyosema “kadi yako kura yako, nenda kajiandikishe”