Home Habari NEC YAMALIZA UTATA JIMBO JIPYA IFAKARA

NEC YAMALIZA UTATA JIMBO JIPYA IFAKARA

3183
0
SHARE
NA GABRIEL MUSHI  |  

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeweka hadharani sababu za kushindwa kulitangaza rasmi jimbo jipya la Ifakara kutokana na hatua ya Serikali kuchelewa kuitangaza Ifakara kuwa Halmashauri.

Jimbo hilo ambalo sasa liko chini ya mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema) ni moja ya majimbo mapya ambayo yalipaswa kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kabla ya ufafanuzi wa NEC, kulikuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanasiasa hasa wa vyama vya upinzani kuwa tume hiyo imeacha kulitangaza jimbo hilo kwa makusudi licha ya kutimiza vigezo vyote.

Julai 9 mwaka 2015 Serikali ilitangaza mikoa, wilaya na tarafa mpya Tanzania ikiwamo wilaya ya Ifakara ambayo ilitoholewa kutoka katika Wilaya ya Kilombero iliyopo mkoani Morogoro.

Hata hivyo, siku nne baadae (Julai 13) Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza majimbo mapya 26 ya uchaguzi na kuliweka kando jimbo la Ifakara hivyo kulazimu Kilombero kubaki kuwa jimbo moja pamoja na Ifakara.

Akizungumza na RAI hivi karibu Afisa Habari Mwandamizi wa NEC, Clarence Nanyaro alisema licha ya kwamba kisheria na kiutaratibu eneo lolote likishatangazwa kuwa halmashari linatakiwa kuwa jimbo la uchaguzi, tume ilishindwa kufanya hivyo kwa Ifakara mwaka 2015 kwa kuwa ilichelewa kutangazwa kuwa Halmashauri.

Alisema madai ya kwamba NEC ilifanya makusudi kutoitangaza Ifakara kuwa Jimbo la uchaguzi si ya kweli kwa kuwa NEC haina upendeleo wa aina yoyote.

“Kwa mfano katika uchaguzi wa mwaka 1995 hadi 2000 kulikuwa na jimbo moja huko Mtwara ambalo lilikuwa na tarafa mbili zilizoko wilaya mbili tofauti ambazo ni Kitangari, Newala na Ihuta, Tandahimba, zilikuwa zinampa shida sana Mbunge wa jimbo hilo kutekeleza majukumu yake kama ilivyo kwa Lijualikali.

“NEC ilichukua hatua na mwaka 2000 ikafuta jimbo moja hilo la Nikema na kubakiza 231. Hivyo si mara ya kwanza ndio maana tume husisitiza jimbo moja lisiwe katika halmashauri mbili kwani utekelezaji wa majukumu huwa magumu.

“Kwa hiyo wasiojua sheria ndio hutumia siasa kupiga kelele, wakati Tume inatumia ibara ya tatu kutekeleza jukumu hilo, kwa mfano ukiangalia orodha ya majimbo yaliyoongezwa tangu mwaka 1995 ni kama ifuatavyo, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 kwenda 2000 yaliongezwa majimbo 52, mwaka 2005 liliongezwa jimbo moja na kuwa 232, mwaka 2010 yaliongezwa saba na kufikia majimbo 239, mwaka 2015 yaliongezwa majimbo 25 na kuwa majimbo 264,” alisema.

ACT-WAZALENDO WATOA NENO

Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo, Yeremia Maganja alisema Tume ya uchaguzi haipo tayari kushauriwa ndio maana ilikwepa kutangaza Ifakara kuwa jimbo la uchaguzi.

“NEC inafanya kazi kwa kuongozwa na CCM, kwa sababu Ifakara ninayoijua CCM haiwezi kupata kura hata tano kwa porojo zao. Watu wa kule wanajua kila kitu na wanaelewa CCM ipo vipi, ndio maana hakuna shinikizo la jimbo kugawanywa.

“Hawakutaka kutangaza kwa sababu hata sasa hawana uhakika wa kushinda, hata kama wakitumia jeshi la polisi au mkurugenzi hawana uhakika kama watashinda. Ukifuatilia sana Kilombero na Ifakara na kwingine Morogoro kuna ushindani mkubwa sana ni eneo ambalo wananchi wanaelewa kesho yao,” alisema.

LIJUALIKALI AIKOSOA NEC

RAI lilizungumza na Lijualikali ambaye pamoja na mambo mengine alisema NEC wameudanganya umma kuhusu muda ambao Serikali ilitangaza kuigawanya Kilombero.

RAI: Je, unafahamu kuwa Ifakara ilipaswa kuwa jimbo la Uchaguzi tangu mwaka 2015?

LIJUALIKALI: Ndio nafahamu, natambua NEC walifanya makusudi tu kutolitangaza katika ule uchaguzi wa mwaka 2015. Na kwa hali iliyopo sitashangaa hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 wasipolitangaza.

NEC wanasema eti halmashauri ya Ifakara iligawanywa baada ya majimbo mapya kutangazwa, si kweli ni waongo hao.. nakumbuka vizuri aliyekuja kuchukua maoni ya wadau alikuwa ni Mwenyekiti wa Tume wakati huo Jaji Damian Lubuva mwenyewe.

Alikuja kwenye kikao akaita wadau, wanachama wa CCM wakakataa kusiwe na jimbo la Ifakara, akawashangaa na kuwaambia kuwa mbunge wenu atapata shida kwa sababu haiwezekani kuongoza halmashauri mbili, atafanya kazi vipi!

Lakini tukashangaa kwanini hakutangaza jimbo la Ifakara, sasa kauli ya kwamba halmashauri iliundwa baada ya NEC kutangaza majimbo mapya ni uongo. Na hilo ndio lilisababishwa hata nihukumiwe kifungo cha miezi sita kwa sababu baada ya uchaguzi mimi kama Mbunge nina halmashauri mbili kwamba kata 10 zipo Kilombero na tisa zipo Ifakara.

Sasa wakati wa kupiga kura walinizuia nisiingie Ifakara kupiga kura wakanilazimisha kupigia Kilombero jambo ambalo niliwakatalia.

RAI: Ni changamoto gani unazokutana nazo katika kutekeleza majukumu yako hasa ukizingatia jimbo la Kilombero lipo ndani ya wilaya mbili tofauti?

LIJUALIKALI: Hakika ni changamoto nyingi, ila kubwa ziko mbili. Kwanza ni mgawanyo wa fedha za mfuko wa jimbo kwani zinaingia kwenye halmashauri nyingine na inabidi zitoke ziende pia kwenye halmashauri nyingine. Yaani zinaingia Kilombero zinagawanywa na kupelekwa pia Ifakara.

Kutokana na hali hiyo hakuna usimamizi thabiti wa fedha kwa sababu Mkaguzi wa Hesabu za Serikali akija anakagua halmashauri ya Kilombero hawezi kwenda kule Ifakara.

Pili ni vikao vya baraza la madiwani, unakuta Ifakara kuna vikao na wakati huohuo Kilombero kuna vikao, nashindwa kujigawa kama Mbunge wao. Vilevile nashindwa kuhudhuria vikao vyote vya kamati za fedha..

Lakini pia kwenye mfuko wa jimbo ni shida kwani sheria inataka upate mtendaji mmoja, afisa mipango mmoja, madiwani watatu, sasa kwa upande wangu inanilazimu kuwa watendaji wawili kila halmashauri vivyo hivyo kwa upande wa maafisa mipango.

RAI: Una ushauri gani kwa viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi?

LIJUALIKALI: Nafahamu kuwa sasa hawawezi kuitisha uchaguzi mdogo katika jimbo mojawapo, labda waje waniulize nataka nibaki jimbo gani. Licha ya kwamba sheria hairuhusu kutangaza uchaguzi mdogo nawahisi ifikapo 2020 watangaze Ifakara kuwa jimbo la uchaguzi haraka. Nahisi wanaweza kusita kutangaza kuwa jimbo kwa sababu hali iliyopo humu pande zote itawawia vigumu sana CCM kupenya hivyo sitashangaa wakiacha kuyagawa majimbo haya vilevile kama walivyofanya 2015.