Home Habari Nenda Dk. Mengi, nenda haraka!

Nenda Dk. Mengi, nenda haraka!

1802
0
SHARE

NA NASHON KENNEDY

DUNIA ni sehemu nzuri na muhimu ambamo viumbe huja ndani yake kustawi na bila shaka na kuondoka. Hakuna taarifa ya binadamu kuja duniani, hadi anapokuja kweli kwa maana ya kuzaliwa na mama mmoja anayejulikana na asiyejulikana!

Kuondoka kwa binadamu duniani hufanana sana na kuja kwake, isipokuwa kwa mambo mawili ambayo ni sherehe na furaha wakati wa kuja kwake duniani, majonzi na huzuni wakati wa kuondoka kwake na hii ndiyo kanuni tena kanuni ya kudumu.

Dunia hii kwa siku za karibuni imekuwa na viongozi walioacha alama ya kukumbukwa (Legacy) kwa wema wao, ubunifu, ujasiri, uzalendo, uadilifu na kujali kwao jamii inayowazunguka na kuamua kwa makusudi kuwa majawabu ya utatuzi wa maswahibu yanayoisibu jamii katika nchi zao na maeneo mengine jirani kama vile umaskini, maradhi, ujinga, dhuluma na ubaguzi wa kila aina.

Watu wenye sifa hizo kwa desturi huwa ni wachache kwani viongozi na wanajamii waliofanikiwa kwa kiasi kikubwa huwa ni wabinafsi waliojaa wivu usio wa kimaendeleo na wanaopenda kudumu katika kilele cha mafanikio lakini bila kukaribiwa au kujongelewa kisifa na kimtazamo na wale walio chini yao.

Miongoni mwa viongozi hao ni Mahatmaghadhi, George Washingtone, Christopher Churchill, Nkwame Nkurumah, Ahmed Benbella, Juma Abdelnaser, Mwl Julius Nyerere, Patrice Lumumba bila kumsahau Nelson Mahlalah Mandela na hawa wote wametangulia mbele ya haki, orodha ni ndefu!

Hapa kwetu Tanzania kwa miaka kama mitatu iliyopita, nchi yetu imeshuhudia watu wenye sifa kama hizo nilizozitaja wakija na kuondoka, lakini wakienda haraka mara tu baada ya manufaa ya uwepo wao yanapoanza kudhihirika kwa jamii! Mifano ni mingi lakini Mwl Julius Nyerere na Edward Moringe Sokoine wanatosha kuiwakilisha orodha hiyo.

Wakati wa maombolezo ya kifo cha Mwl Nyerere, wasanii wa bendi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Mwenge Jazz Band walitunga wimbo uliokuwa na kibwagizo cha “ Nenda Mwalimu na wala usiogope,” ! Hivi karibuni wala siku hazijawa nyingi taifa limepata simanzi baada ya kupatikana taarifa za kifo cha ghafla cha mfanyabiashara, mwalimu, mwekezaji, msomi, mshauri, mlezi na mzalendo wa kweli katika taifa letu, Mzee wetu Dk. Reginald Mengi.

Mengi kama lilivyo jina lake amefanya mambo mengi yaliyochangia kwa kiasi kikubwa hamasa ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa ndani na nje ya nchi imeongezeka  na pia amefanya mengi kuitanabaisha serikali juu ya mashaka yanayotokana na maamuzi mabaya pindi inapoingia kandarasi na makampuni ya kigeni lakini pia kuishauri serikali juu ya hila za makampuni ya kigeni na siasa za biashara za kimataifa!

Dk. Mengi kama mfanyabiashara mzalendo alitumia jukwaa la kibiashara kuisaidia serikali na wakati mwingine kusafisha uso wa serikali mbele ya Jumuiya za kimataifa kuhusu masuala ya biashara na fedha. Ametumia jukwaa la mikutano ya biashara ya kimataifa kuitangaza Tanzania kibiashara na kisiasa na hivyo kushawishi uingizaji wa mitaji mipya, ongezeko la watalii katika taifa letu na kwa kutumia vyombo vyake vya habari amefanikiwa kupambana na makampuni ya nchi jirani ambayo kwa makusudi kwa madhumuni ya kupata faida katika ushindani usio halali wa kibiashara, yalikuwa yakichafua sifa njema ya uwezo wetu wa kuzalisha kwa ubora bidhaa tunazouza katika masoko mbalimbali.

Kimsingi juhudi za Dk. Mengi na makampuni yake lukuki zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa taifa letu, kututetea kibiashara na kuionyesha thamani ya mtanzania nje ya taifa letu, ni kazi njema bila shaka maana imeandikwa katika vitabu vitakatifu kwamba mwenyezi Mungu alipoumba mbingu na dunia alisema hakika hii ni kazi njema! Aliyoyafanya Dk. Mengi katika uhai wake ni mengi lakini ni darasa maridhawa likifuatiliwa kwa umakini kuanzia kujitambua kwake, kuchukia umaskini kwa vitendo, kuchagua njia ya kujinasua na umaskini, kufanya maamuzi sahihi na kujitoa mhanga kwa ajili ya jamii na taifa lake, lakini pia kusimamia alichokiamini kama ndiyo njia sahihi ya mapambano yake.

Mengi kafanya mengi na mengi aliyoyafanya yamewasaidia watu wengi na watu wengi waliosaidiwa na mengi ni vigumu kuhesabiuka katika hesabu za kawaida kwa wingi wao na bila watu wengi watamuombea dua Dk. Mengi. Kifo cha ghafla kimetunyang’anya mtu muhimu sana na kwa wakati muhimu sana, Mwenyezi Mungu halaumiwi, hapangiwi wala hashauriwi, tunachoweza kukifanya pekee ni kumuombea Dk Mengi na kumuomba mwenyezi Mungu kwa heshima ampeleke na kumpa makazi ya kudumu katika eneo na mahala panapomstahiki!

Japokuwa ingekuwa tuna utashi na uamuzi sisi kama binadamu pengine tunemtamfutia kasiri njema kwenye bustani yenye mito mingi na hitaji la kila aina na kumuweka humo, lakini uwezo huohatuna! Mchango wa makampuni yake ya IPP utakumbukwa na kuenziwa kwa muda mwingi wa kizazi chetu, makampuni haya ya kizalendo yamekuwa kwa kiasi kikubwa chanzo cha ajira cha vijana wetu wasomi na wenye elimu ya kawaida.

 Makampuni yake yamekuwa chuo cha kujifunza jinsi ya kusimamia, kutetea na kuongoza watu wengine, yamekuwa sura ya uwekezaji makini kwa serikali nyingi za nje na ndio maana makampuni mengi ya kibiashara na taasisi za kijeshi kutoka nje ya nchi yanapofanya ziara nchini Tanzania hayaachi kuyatembelea makampuni ya IPP na kuzungumza na Dk. Mengi, lakini pia kushangaa ni kwa jinsi gani yeye na timu ya watalaam wa makampuni yake wameweza kuendesha kwa mafanikio makubwa biashara mbalimbali pamoja nauzalishaji unaofanywa na viwanda vinavyomilikiwa na IPP Limited!

Katika uwanja wa diplomasia ya kimataifa, Dk. Mengi alifanikiwa vikubwa katika uwakilishi wa matakwa, maoni na mtazamo wa wananchi juu ya sera za biashara na mikakati ya kimataifa katika kupambana na umaskini(Pooverty alleviation struggle), amemwakilisha vizuri na kutafasiri vyema falsafa za Profesa De-Suto. Katika kutekeleza vizuri dhana ya serikali ya kupambana na umaskini, Dk. Mengi ametoa kama msaada au mchango wake wa mamilioni ya fedha kwa mtu mmoja mmoja lakini vikundi mbalimbali vya vijana, makundi ya watu wenye uhitaji maalum kwa kufadhili matibabu yao nje ya nchi kwa gharama zake, taasisi za kidini tena bila ubaguzi, tukishuhudia akisaidia taasisi za kiislamu na kikristo bila kuchoka kila alipoombwa na kuguswa na shughuli yenye manufaa kwa jamii inayosimamiwa na taasisi za dini hizo.

Watanzania wengi mbali ya kupenda siasa (homo-politicus), wana uchumi (homo-economicus) pia ni wana michezo na katika michezo hiyo, mpira wa miguu unaongoza kwa kuwa na wapenzi wengi. Dk. Mengi aliamini na amekufa akiamini kwamba binadamu baada ya kufanya kazi nzito za uzalishaji, anahitaji wasaa wa kuburudika kwa kushiriki michezo mbalimbali kwani michezo ni furaha na Dk. Mengi alitamani watanzania kufurahi. Katika jitihada hizo, Dk. Mengi alishiriki ana alifadhili vilabu mbalimbali lakini hasa timu ya Dar –Young African na pia kusaidia timu za vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20, zijulikanazo kama Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys, lakini Pia timu ya taifa Taifa Stars, atakumbukwa kwa mengi Dk Mengi kwani amefanya mengi!

Katika kuhamasisha njia njema ya kuwahifadhi wasichana wetu wanaoshiriki mashindano ya urembo, Dk. Mengi hakuwa nyuma kwani alichagua njia bora ya kuhifadhi urembo kwa kumuoa na kuishi na mrembo wa zamani Jacklin Ntuyabaliwe-Kylin. Katika kuonyesha umuhimu wa kusoma na kuandika, pamoja nakutunza kumbukumbu ya hazina ya fikra kuelekea mambo fulani ya msingi kama njia za kufanikiwa katika maisha kibiashara na kuhamasisha uthubutu Dk Mengi ametunga kitabu alichokipa jina la “I can, I must, I will kitabu hicho kina lengola kumpa kijana wa Tanzania na Afrika msukumo wa kutokata tamaa katika kutafuta maisha bora na kuyafikia malengo.

Kwa upande wa elimu, Dk. Mengi amejenga shule nyingi za msingi na sekondari lakini pia uchangiaji katika shule zilizokwama umaliziaji na vyama vya walimu nchini havikuacha kwenda kumuona kuomba msaada ama wa mali ama ushauri. Ameshiriki kikamilifu katika suala zima la uhifadhi wa mazingira katika nchi yetu kwa kuhamasisha upandaji wa miti na uhifadhi wa vyanzo vya maji ukiwemo Mlima Kilimanjaro.

Katika tasnia ya afya, Dk. Mengi mbali ya kuchangia fedha taslimu katika kampeni mbalimbali za chanjo na kinga, lakini pia vyombo vyake vya habari (ITV na Radio One) vimetoa mchango mkubwa wa matangazo(elimu) ya uhamasishaji na ufafanuzi juu ya mashaka waliyokuwa nayo watu juu ya operesheni hizo za serikali, zikiwemo kampeni maalum ya kutibu saratani ya matiti na kizazi kwa wanawake na tezi dume, kampeni maalum ya kuzuia ajali za barabarani, zikiwa kama mfano wa michango mingi ya Dk. Mengi kwa siha za jamii.

Kwa mengi haya aliyoyafanya Dk. Mengi, ni vyema kusema “ Nenda Dk. Mengi tena nenda haraka, tena nenda haraka kwa mola wako ili wenye hila wasije wakageuza juhudi zako na wema wako kuwa laana na msiba kwa watu, kwani watu hawana wema, waswahili husema, “ Fadhila mfadhili mbuzi, binadamu ana maudhi”