Home Habari ng’ombe wawili wamponza kamanda wa polisi

ng’ombe wawili wamponza kamanda wa polisi

1716
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

Ng’ombe wawili wanaodaiwa kutolewa na wafanyabiashara wa kahawa ya magendo nchini Uganda kwa baadhi ya maofisa wa polisi wilayani Kyerwa wanatajwa kuwa miongoni mwa sababu za kusimamishwa kazi kwa vigogo wa jeshi hilo, mkoani Kagera.

Katika siku za hivi karibuni, jeshi la polisi wilayani Kyerwa limejikuta likiingia kwenye kashfa ya kushiriki kusafirisha kahawa kimagendo, pamoja na kufanya vikao haramu na baadhi ya wafanyabiashara wa Uganda ili kufanikisha magendo hayo.

Madai hayo ya kuwapo kwa baadhi ya maofisa wa polisi wilayani humo kushiriki vitendo hivyo yalitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipkuwa ziarani mkoani Kagera.

Waziri Mkuu Majaliwa, alisema anazo taarifa kuwa Kamanda wa polisi wilaya ya Kyerwa (OCD) Justine Joseph, ambaye tayari amesimamishwa kazi kwa agizo la Rais Dk. John MagufuliWaziri amekuwa akishiriki kwenye kusafirisha Kahawa kimagendo.

Alisema baadhi ya maofisa wa jeshi hilo wamefikia hatua ya kufanya mikutano nchini Uganda na wafanyabiashara wa huko pamoja na kupewa ng’ombe wawili.

“Ile mikutano mnayofanya kule Uganda kule, Mugambo…afu ng’ambo kule kuna mji wa Uganda, unaitwa Kakagate, kile kikao mlichokifanya na wafanyabiashara wa Uganda wakawapa ng’ombe wawili kitawaponza, kitawaponza.”

Katika hotuba yake mbele ya wananchi wa Kyerwa, Waziri Mkuu alishangzwa na jeshi hilo kujiingiza katika kusafirisha kahawa kimagendo, badala ya kuzuia.

“OCD, huku kwako kuna barabara za  Kamisango, Nyakasinga, Chamoshaija, Chebukube na Mwakatome ndiko mnakopitisha kahawa.

“OCD usipowadhibiti, utapoteza kazi, kuna makamanda wako baadhi wanasindikiza kahawa na wengine wanasema na wewe mwenyewe unasindikiza.

“Wameniambia wenzako, ni hatari sana kama jeshi lenyewe linaingia kufanya biashara hiyo hasa Kyerwa, jeshi la polisi Kyerwa limeingia kwenye shutuma hizo, linasindikiza Kahawa, OCD simamia Kahawa.

“Tutakutoa vyeo, utafukuzwa kazi na bado familia yako inakutegemea, ni marufuku kupeleka kahawa kwa mfumo wa wizi.

“Kahawa tunayoitafuta ni hii ambayo itarahisha mkulima kupata hela yake kwa haraka zaidi.

“Jeshi letu hapa halifanyi vizuri, nina orodha ndefu, hamfanyi vizuri, nyie ndio mnashiriki kwenye mutura…, Kyerwa mnasindikiza   badala ya kuzuia, mjipange vizuri na upange makamanda wako….

“Ile mikutano mnayofanya kule Uganda, kule Mugambo…afu ng’ambo kule kuna mji wa Uganda, unaitwa…Kakagate, kile kikao mlichokifanya na wafanyabiashara wa Uganda wakawapa ng’ombe wawili kitawaponza.

“Hiyo itawaangusha RPC simamia jeshi la polisi Kyelwa linafanya kazi ya kufuatilia na kusindikiza magendo kwenda nchi jirani, mkoa huu mnatutia aibu, wilaya hii inatutia aibu….Mheshimiwa mkuu wa Mkoa…shughulika na Kyerwa.

JESHI LA POLISI LANENA

Msemaji wa jeshi hilo ACP Barnabas Mwakalukwa mwanzoni mwa wiki hii alitoa taarifa iliyoonesha kuhamishwa kituo kazi kwa Mrakibu wa Polisi (SP) Joseph kwa kile alichoeleza kuwa ni kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizoelekezwa kwake.

Taarifa ya msemaji huyo wa Polisi, iliweka wazi kuwa Inspekta Generali wa Polisi (IGP) Simon Sirro amesikitishwa na suala hilo na kuwataka askari polisi wote nchini kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za jeshi la Polisi bila kusahau misingi na kanuni za maadili.

UAMUZI WA RAIS

Muda mfupi mara baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo ya jeshi la polisi, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, kupitia kwa Mkrugenzi wake, Gerson Msigwa ilitoa taarifa iliyobainisha kuwa Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi kwa maofisa wa juu wa polisi mkoani Kagera.

Waliosimamishwa kazi ni  Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, SACP Agustine Ollomi, SP Joseph, Mkuu wa upelezi wilaya ya Kyerwa na Mkuu wa Polisi wa kituo cha Kyerwa Robert Marwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika katika magendo ya zao la kahawa.

Mbali na kusimamishwa kazi kwa maofisa hao wa jeshi la polisi, lakini pia Rais amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jen Jacob Kingu na IGP Sirro kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na hatua stahiki zinachukuliwa, endapo watabainika kuhusika kwenye tuhuma hizo na makosa mengine.

Aidha, RAI limedokezwa kuwa uchunguzi huo una nafasi kubwa ya kuondoka na idadi kubwa ya maofisa wakiwamo wale wanaoshughulikia uuzwaji wa kahawa.