Home Habari NGUMU KUJENGA, RAHISI KUBOMOA

NGUMU KUJENGA, RAHISI KUBOMOA

4748
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


KWA waliopata bahati ya kujenga, ujenzi wowote bila kujali ni wa aina gani watakubaliana nami kuwa si kazi rahisi kutekeleza tendo hilo.

Ugumu zaidi unakuja pale unapotaka kujenga mjengo bora na mzuri wenye kumvutia kila mtu mwenye utimilifu wa akili na mwili.

Ili kulifanikisha suala hilo kikamilifu na kwa ufasaha, itahitajika ubunifu, muda, fedha na utayari.

Mambo yote manne niliyoyaanisha hapo juu kwa maana na ubunifu, muda, fedha na utayari yanagharama zake, kuzidadavua gharama hizo itanihitaji kurasa nyingi zaidi ya uga nilionao kwenye ukurasa huu.

Ukweli huo unanilazimisha kuamini kuwa si jambo rahisi kujenga chochote kilicho bora. Hivi ndivyo ilivyo hata katika ujenzi wa nchi.

Ili kufanikisha ujenzi wa nchi bora yenye utulivu na utuvu, ni gharama mno, nchi zote zenye utulivu leo, zimetumia muda mwingi kuujenga na kuulinda utulivu huo.

Hakuna jambo rahisi kama kubomoa chochote kile bila kujali ni nyumba, nchi ama ndoa. Ukiamua kubomoa ni suala la dakika moja tu, kila kitu kinakuwa shaghalabhaghala.

Tanzania ya leo yenye umri wa miaka 57 haikufika hapa ilipofika kirahisi, imewagharimu baadhi ya watu, muda, ubunifu, utayari na fedha.

Wapo walioridhia kupoteza muda wao ili kuipigania Tanzania ya leo, wapo waliokuwa na utayari wa kubuni njia na mbinu mbalimbali za kujenga nchi yenye amani na utulivu isiyomwaga damu.

Wapo waliokuwa tayari kutoa fedha zao hata zile za kulisha familia zao ili kuhakikisha mipango ya kujenga nchi huru haikwami, lakini pia wapo waliokuwa na utayari wa kutoa chochote ikiwezekana hata uhai wao ili kufanikisha ujenzi wa Tanganyika na baadae Tanzania imara na yenye heshima kubwa.

Katika kuendeleza mema haya, kamwe Watanzania wa leo hatupaswi kuwa wa kwanza kushika marungu, nyundo na shoka kwa ajili ya kuibomoa nchi hii.

Haitatugharimu chochote kama tutakuwa wa kwanza kutaka kubomoa, kitakachotugharimu ni nguvu zetu tu, zipo baadhi ya nchi zilizojengwa kwa miaka mingi, lakini zilibomolewa kwa muda mfupi sana.

Kamwe hatupaswi kuwa na fikra hizo, tunachopaswa kukifanya ni kukosoana na kuelekezana kwa dhamira ile ile ya kujenga kwa kukarabati mahala ambapo huenda pana ufa ama nyufa.

Binafsi yangu nafurahishwa na mwenendo wa kiutendaji na kimazungumzo wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Majaliwa amekuwa mstari wa mbele kuhubiri kile kinachohimizwa na Rais Dk. John Magufuli cha kutaka Watanzania wafanye kezi.

Hamasa hii imebebwa vema na mjasiriamali na mfanyabiashara mzalendo, Allex Msama.

Mtanzania huyu ameamua kulijenga Taifa lake kwa vitendo, pamoja na mambo mengine, lakini mara nyinbgi amekuwa mstari wa mbele kupigania wavuija jasho wanaonyonywa na mabwanyenye wachache.

Mwenendo wake huu unaniaminisha kuwa Msama ameamua kuwa muumini wa kweli wa kauli mbiu ya hapa kazi tu, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Katika siku za karibuni, Msama amekuwa mstari wa mbele kuzalisha ajira kwa vijana wa rika na kada zote, hii inamaanisha dhamira njema ya kulijenga Taifa na si kulibomoa.

Mara kwa mara unapozungumza nae, kamwe si mtu wa kulalamika ama kusononekea viongozi, badala yake amekuwa akizungumzia namna sahihi ya kutoka hatua moja kwenda nyingine bila kumnyooshea mtu kidole.

Mwenendo kama huu unapaswa kuigwa na Watanzania wote, hatupaswi kuwa walalamishi na wakosoaji wa viongozi hasa wa kisiasa pasi sisi wenyewe kusaka suluhu.

Mafanikio yoyote yale hayaji kwa kulalamika, tunapaswa kuwa wa kwanza wa kusaka suluhu ya changamoto zinazotukabili. Kulalamika na kusononeka kutazalishia fikra ovu zinazoweza kuvunja kuta imara za nchi yetu zilizojengwa kwa gharama kubwa.

Tuwe na utayari wa kuwa wa kwanza kuwakemea watu wenye nia ovu ya kutaka kuvunja chema cha nchi yetu, tusikubali kudanganywa, badala yake tuwe wa kwanza kuambizana ukweli.

Ni vema tukawatumia watu aina ya Msama katika kumuunga mkono Rais na serikali yake kwa vitendo ili tusiwe wa kwanza kuibomoa nchi hii, maana kubomoa ni rahisi kuliko kujenga. Tusiruhusu kujazwa chuki dhidi ya tuliowapa dhamana, tushindane kujenga nchi, tusishindane kubomoa, tutakaoumia ni sie wanyonge.