Home Habari Nguo fupi hazihalalishi unyanyasaji wa kijinsia

Nguo fupi hazihalalishi unyanyasaji wa kijinsia

1599
0
SHARE

Na BRIGHITER MASAKI

WATALAAMU wa saikolojia wanakubaliana kwamba unyanyasaji wa kijinsia una madhara makubwa si tu kimwili, bali hata kiakili kwa mwathirika.

Mbaya zaidi, bado elimu juu ya unyanyasaji wa kijinsia si ya kuridhisha kwani wengi wanaamini ni wanawake/wasichana pekee wanaofanyiwa vitendo hivyo, ilihali pia wanaume/wavulana hukumbana navyo.

Miongoni mwa matukio yanayoingia moja kwa moja katika hilo la unyanyasaji wa kijinsia ni ubakaji.

Zipi athari za unyanyasaji wa kijinsia?

Huenda mwathirika akapatwa na changamoto ya afya ya akili, hasa endapo atakuwa ameambukizwa magonjwa ya zinaa, mfano Ukimwi, au kupewa mimba isiyotarajiwa.

Ni kwa kuwa bado mtu wa aina hiyo atakuwa na kumbukumbu ya maumivu au fedheha aliyoipata baada ya kufanyiwa unyama huo, mathalan kubakwa.

Pia, unaweza kuongezea maumivu makali yatokanayo na ukeketaji.

Lakini je, vipi endapo msichana atashindwa kuendelea na masomo baada ya kupachikwa mimba? Hiyo nayo ni athari nyingine kwa mwathirika.

Nguo fupi huhalalisha unyanyasaji?

Ubakaji kamwe si kosa la aliyebakwa, bali aliyebaka. Ni kwa maana hiyo basi, nguo fupi anayovaa msichana haimnyimi kinga dhidi ya ubakaji au aina nyingine ya udhalilishaji, ikiwamo ya lugha za fedheha.

Hata hivyo, ni lazima wanawake/wasichana nao watambue kwamba si tu ni hatari kwao kuwa kwenye mavazi ya aina hiyo, pia ni kinyume cha maadili ya jamii zao.

Ieleweke kwamba zipo sababu nyingi za mwanaume/kijana kubaka, zikiwamo kulipiza kisasi au matumizi ya dawa za kulevya, bangi ikifaa pia kutolea mfano.

Jamii inahusika vipi?

Licha ya kwamba elimu imefanya kazi kubwa katika miaka ya hivi karibuni, ukweli ni kwamba bado zipo jamii zinazoendeshwa kwa mila na tamaduni zilizopitwa na wakati.

Zinazozungumziwa hapa ni zile zisizoamini katika usawa kati ya mwanaume na mwanamke.

Ukiacha matukio ya ubakaji katika maeneo ya aina hiyo, pia wanawake wamekuwa wakikabiliwana na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na ‘sauti’ katika mahusiano ya kimapenzi au ndoa.

Kwao, mwanamke ni kiumbe dhaifu, ambaye jukumu lake la msingi ni kumtumikia mume/mpenzi wake.

“Mfano; sababu nyingine ya ndoa za utotoni ni mtazamo wa tamaduni, mila na desturi baina ya jamii mbalimbali kuhusu miaka ya mtoto wa kike anayetakiwa kuolewa, kuingia unyago, ukeketaji, pamoja na ngoma za asili zinazopelekea watoto wa kike kuolewa mapema,” ilieleza ripoti ya utafiti uliowahi kufanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Ni katika jamii za aina hii unapoweza kukuta utitiri wa ndoa za mitaala, kwa maana ya wanawake kufanywa ‘chombo cha starehe’, wakikeketwa, wakinyimwa haki kumiliki mali.

Hali hii si maeneo ya vijijini pekee, pia inaweza kuonekana mijini, ambako bado wanaume wengi wamekuwa wazito kuwaruhusu wake zao kufanya kazi, wakibebwa na dhana kwamba jukumu lao ni kubaki nyumbani na kulea watoto.

Katika hilo la jamii, utafiti wa mwaka 2013 uliwahi kubaini kwamba vitendo hivyo vya udhalilishaji hufanyika zaidi majumbani (asilimia 46.7), huku pia yakichukua nafasi njiani (asilimia 37.6) na shule na madrasa (asilimia 14.5).

Umasikini una nafasi gani?

Aidha, zipo tafiti zilizowahi kubaini kwamba umasikini ni chanzo kingine cha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia. Kwamba, familia nyingi zilizo kwenye hali mbaya kiuchumi ndizo hutegemea kuozesha mabinti zake ili kupata mahari.

Hilo linawekwa vizuri na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ukieleza: “Utafiti huo ulionesha Mkoa wa Mara, asilimia 59 ya wananchi walikubaliana (umasikini chanzo unyanyasaji kijinsia), Mkoa wa Dar es Salaam ni asilimia 56…”