Home Makala NGUVU YA KUKUSANYA KODI IENDE SAMBASAMBA NA ELIMU

NGUVU YA KUKUSANYA KODI IENDE SAMBASAMBA NA ELIMU

692
0
SHARE
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

NA FARAJA MASINDE


 

ENEO la ukusanyaji kodi wa kiwango cha juu ni moja ya jambo ambalo kwa miezi kadhaa sasa limekuwa likiijengea sifa kubwa katika Serikali ya awamu ya tano chini ya, Rais John Magufuli.
Ndiyo, sifa hii ilikuwa ikichangizwa na kiwango kikubwa cha mpato ambayo Serikali ilikuwa ikikusanya kwani ilikuwa ni kiwango cha juu mno cha mapato kuwahi kukusanywa ikilinganishw ana miaka ya nyuma.
Mafanikio hayo ya ukasanyaji mapato kwa kiwango cha juu yalichangizwa hasa na kugusa kila nyanja inayopasa kulipa kodi balabala tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya mapato hayo yalikuwa yanatoka kwa wananchi wenyewe kupitia shughuli zao mbalimbali pamoja na mali wanazomiliki ama kusafirisha.
Tumeshuhudia chini ya Serikali hii TRA ikikusanya kiwango cha Sh trilioni 1.5 kiwango ambacho ni cha juu zaidi kushinda hata malengo ya mamlaka yenyewe.
Mamlaka zinazohusika na ukusanyaji huo zimekuwa zikifanya kila linalowezekana katika kuhakikisha kuwa ukusanya kiwango chote cha kodi kinachostahili kuchukuliwa na Serikali.
Tumeshuhudia mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kupitia mashine za elekroniki za (EFDs) ukianza kufanya kazi kwa nguvu zote na hivyo kuwa chachu ya ongezeko la mapato.
Hata hivyo, mfumo huo na mamlaka nzima zinazohusika na ukusanyaji mapato ni kama unaonekana kuwa mwiba kwa wale wanaostahili kulipa kodi hiyo ama kwa lugha nyingine unaweza kusema kuwa ni ‘paka na panya’.
Ni lazima tukubali kuwa bado kuna changamoto kubwa katika mfumo huu mzima wa ukusanyaji kodi kwani bado watu wanaolipa hiyo kodi hawajajengewa mazingira rafiki jambo ambalo linafanya wafanyabiashara wengi kukwepana na TRA.
Kwa kawaida tafsiri ya ukusanyaji mkubwa wa mapato inatakiwa ionekane kupitia maisha ya wananchi wenyewe ikiwamo kulipwa mishahara mizuri kwa wafanyakazi pamoja na mazingira rafiki kwa wananchi ambao ndio walipa kodi tofauti na ilivyo hivi sasa.
Hata hivyo, hii imekuwa ni kinyume chake kwani wananchi wanaolipa kodi ndio wameendelea kuumia zaidi kutokana na kutokuwapo kwa mazingira bora kwa wao kufanya kazi.
Hii inatokana na kukamuliwa vya kutosha kwenye eneo hili la kodi bila kuzingatia tahamani ya biashara yenyewe, lakini pia nguvu kubwa ambayo imekuwa ikitumika kukusanya kodi kuliko kutoa elimu.
Ufinyu huu wa elimu kwa wafanya biashara kuhusu kulipa kodi ndio unafanya leo tunashuhudia biashara nyingi zikifungwa kutokana tu na kile wanachoeleza kuwa kodi imekuwa kubw akuliko kinachopatikana.
Wapo wanaofungwa wenyewe lakini pia wapo wanafunzi au hata kutoza kiwango kikubwa cha kodi kwa wafanywa biashara wanaoenenda kinyume jambo ambalo linapelekea kupungua kwa walipa kodi.
Sidhani kama kuna uhalali kwa mamlaka kumfungia mtu biashara kwa kigezo cha kutokutoa risiti ama hata mashine ya kutolea risiti EFD, je, hivi ni kweli kwamba mfanyabiashara huyu hataki kutoa risiti ama kuchangia kodi Serikali yake? Hapa kuna mamabo mawili ambayo ni lazima TRA iyafanyie kazi kama mkweli tunahitaji watu walipe kodi bila kusukumwa.
Binafasi siamini katika hili ila ninachokiamini ni kwamba bado hakuna mazingira mazuri yanayotengenezwa na mamlaka husika ikiwamo Serikali kwa ajili ya kuwasaidia walipa kodi hawa kutimiza wajibu wao bila kusukumwa.
Tunashuhudia biashara nyingi zikiendelea kufungwa kwenye maeneo mbalimbali hasa Dar es Salaam, hii pia inasababishwa kiwango kikubwa cha kodi ambacho wafanyabiashara hawa wamekuwa wakilipa ilihali hakuna uuwiano na kile wanachokiingiza kwenye biashara zao za kila siku.
Ingekuwa busara kama TRA ingeweka viwango vya ulipaji kodi kwa kuzingatia thamani ya biashara, hivyo wengi wanajikuta wakilipa kiwango kikubw acha kodi tofauti na kile wanacho kiingiza matokeo yake ni nini?
Matokeo yake ni kuongeza bei ya bidhaa wanaweza kuuza na hivyo kujikuta kwamba hakuna wateja wanaomudu tena kununua bidhaa zao matokeo yake ni kufungwa tu kwa biashara yenyewe au kushindwa kulipa kodi.
Lakini pia eneo jingine ambalo TRA bado hawajalifanyia kazi kisawasawa ni juu ya utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara walio wengi kwani kutokuwa na elimu ndiko kunakochangia wengi kushindwa kulipa kodi na hatimaye kufanya kazi kiujanja ujanja matokeo yake ni kufungwa kwa biashara yenyewe.
Lakini vipi kama huyu mtu mngempatia elimu mapema juu ya ulipaji kodi?.
Changamoto hizi ndizo tunashuhudia sasa mapato yanayokusanywa na TRA yakianza kuporomoka kadri siku zinavyosonga na hii inachangizwa hasa na kuendelea kupungua kwa biashara nyingi nchini huku Serikali ikilazimika kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Lakini pia kama hiyo haitoshi bado kuna ukakasi kwenye hili la ulipaji kodi kwani kumekuwa na mamlaka mbili tofauti ambazo ni Manispaa pamoja na TRA ambazo kila mmoja amekuwa akikusanya mapato kwa wakati wake jambo ambalo ni changamoto kwa wafanyabiashara.
Jambo hili ni vyema vikawekwa sawasawa ili kuondoa ukakasi huu ambao umekuwa ukiwakuta baadhi ya wafanyabiashara.
Lakini pia eneo la mashine hizi za EFD halina budi kuangaliwa upya na Serikali kama siyo TRA wenyewe, na hii inasababishwa kwamba gharama za upatikanaji wa mashine bado ziko juu kwani siyo jambo rahisi kwa mfanyabiashara anayeanza biashara kumudu kununua mashine ya Sh 700,000.
Hii inamlazimu mtu anayetaka kufanyabiashara ni lazima awe na mtaji wa Sh milioni 3.7 kwaajili ya kumudu kupata EFD.
Ili kuendana na kasi hii ya Dunia tuliyonayo hatuna budi kuhakikisha kuwa mamlaka zinatoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara juu ya ulipaji kodi kwa taifa lao kama kweli tunania ya kukusanya mapato ya uhakika kupitia eneo hili.
Hii itasaidia kuinua uchumi wa taifa kwani kamwe hatuwezi kufikia malengo ya ukusanyaji mapato ikiwa hatutatoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara na kuweka viwango vya kodi vunavyoendana na tahamani halisi ya biashara.
Ni lazima tukubali kuwa kila siku kuna wafanyabiashara wapya wanaoanza biashara huku wengine wakifunga biashara tofauti hapa ni ndogo tu kuwa ni ukosefu wa elimu itakayowasaidia kutambua umuhimu wa kulipa kodi.
Tuwahamasishe Watanzania kulipa kodi ikiwamo ni pamoja na kuwekeza kwa lengo la kukuza uchumi wetu lakini bilakusahau kutoa elimu inayohusu kodi hii itasaidia kufufua tena kiwango cha juu cha mapato ambacho kwasasa kimeshuka kutokana na biashara nyingi kufungwa lakini pia hali ngumu ya biashara inayowakabili wafanyabiashara kutokana na kukosa wateja kwa kupandisha bei ya bidhaa ili kufidia pengo kubwa la kodi.
Naamini hatua hii itakuwa na faida kubw akatika kuongeza mapato ya Nchi, tutumie changamoto hii ya kushuka kwa mapato kutoka Trilioni 1.5 hadi bilioni 700 kurekebisha mahala ambapo bado kuna ukakasi.
Kama ambavyo tumeweza kujipanga vyema katika kuimarisha eneo la Bandari na nayanja nyingine za uchukuzi basi tutumie nguvu hiyo hiyo katika kutoa elimu kwa wananchi wetu kwenye hili la ukusanyaji kodi ambalo ndilo kitovu cha uchumi, naamini kabisa kuwa tunaweza kulikabili balabala.