Home kitaifa Ni bajeti ya miradi mikubwa

Ni bajeti ya miradi mikubwa

342
0
SHARE

Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

IKIWA zimebaki siku nane kabla ya Serikali kuwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti yake ya mwaka 2019/20, Juni 12, tayari mwelekeo unaonesha maeneo muhimu ambayo yatachukua idadi kubwa ya fedha za maendeleo.

Hii ni bajeti ya nne ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli tangu alipoingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015, ikitanguliwa na ya mwaka 2016/17 iliyokuwa ya Sh trilioni 29.5, 2017/18 Sh trilioni 31.7 na 2018/19 Sh trilioni 32.

Kuwasilishwa kwa bajeti hiyo kuu Jumatano ijayo, ni baada ya kuhitimishwa kwa bajeti za wizara zote zilizoanza kujadiliwa Aprili 2 hadi Juni 3, mwaka huu ambapo Wizara ya Fedha na Mpango iliwasilisha bajeti yake.

Katika wizara zote ambazo tayari zimewasilisha mapendekezo yake, wizara ambayo imeonesha bajeti yake kuwa ni kubwa ni Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyoidhinishiwa Sh trilioni 4.9.

Eneo kubwa ambalo linaonesha kuwa litachukua fedha nyingi ni mradi wa Standard Gauge Railway (SGR), ambapo Bunge limepitisha Sh trilioni 2.5 kwa ajili ya mradi huo.

Mei 9 mwaka huu, wakati akiwasilisha makadirio ya wizara yake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe aliliambia Bunge kuwa Sh trilioni 2.5 ni kwa ajili ya SGR.

 “Kiasi cha Sh trilioni 2.4 ni kwa ajili ya ujenzi wa eneo la Dar es Salaam-Makutupora huku iliyobakia ni kwa ajili ya ujenzi wa Isaka-Rusumo na ile inayopita kutoka Makutupora hadi Tabora na Isaka,” alisema Kamwelwe  ambapo aliomba Bunge kupitisha matumizi ya Sh trilioni 4.9 ya wizara yake.

Katika bajeti ya wizara hiyo, shughuli ambazo zitafanyika 2019/20 zinajumuisha ujenzi wa kilomita 300 ya reli kati ya Dar es Salaam na Morogoro na kilomita 422 ikiunganisha Morogoro na Makutupora.  

Mbali na hilo, Serikali pia itatoa sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali katika ngazi ya Serikali za mitaa huku Bunge likipitisha Sh trilioni 1.693 kwa Ofisi ya Rais (Utawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa). 

Mradi mwingine mkubwa wa Rais Magufuli ikiwa ni ya tatu miongoni mwa maeneo yaliyotengewa fedha nyingi ni Rufiji Hydroelectric Dam ikifahamika zaidi kama mradi wa Stiegler’s Gorge. Wiki iliyopita Bunge limeidhinisha Sh trilioni 1.44 ya mradi huo.  

Elimu, Maji na afya inachukua nafasi ya nne, tano na sita baada ya Bunge kupitisha Sh bilioni 863 (elimu), Sh bilioni 611 (maji) na Sh bilioni 547 (afya).  

Kiasi cha Sh bilioni 500 imepitishwa kwa ajili ya Air Tanzania Company Limited (ATCL) ikiwa ni nia ya Rais Magufuli kufufua shirika hilo.

 Serikali pia imepanga kusambaza umeme vijijini ambapo jumla ya Sh bilioni 360 inatarajiwa kutumika kwa mradi wa Rural Electrification Agency (Rea).     

Kwa upande wa Wizara ya Nishati ambayo imetengewa Sh trilioni 2.142, kati ya fedha hizo Sh trilioni 1.42 zimeelekezwa katika mradi wa kuzalisha umeme wa Stieglers Gorge.

Hoja zilizoibuliwa katika wizara hiyo ni pamoja na umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kuruka vijiji na vitongoji na migogoro ya ardhi.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akiwasilisha hotuba yake alisema miradi mingine ni kusambaza umeme vijijini (Rea III) ambayo imetengewa Sh bilioni 363.11 na mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi 1 Extension Mv 185 utakaogharimu Sh bilioni 60.

Akijibu hoja za wabunge kuhusu kurukwa vijiji au vitongozi, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alisema wameyasikia mawazo ya wabunge na wanahitaji kuyafanyia kazi ili kuunganishia vijiji vyote.

Kuhusu Wizara ya Madini, ambayo imeidhinishiwa Sh bilioni 49.46, akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Doto Biteko alitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa ambao mikoa ambao mikoa yao haijafunguliwa masoko ya madini, kufanya hivyo mara moja.

Mbali na hilo, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilieleza kusikitishwa na utolewaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya wizara hiyo usioridhisha baada ya kupokea chini ya asilimia moja ya fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya 2018/2019.

Akisoma maoni hayo ya kamati, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariam Ditopile alisema kiasi cha fedha za miradi ya maendeleo kilichopokelewa katika kipindi cha kati ya Julai 2018 hadi Februari mwaka huu ni Sh milioni 100 sawa na asilimia 0.5 ya bajeti yote ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2018/2019 ambayo ni Sh bilioni 19.6.

Wakati fedha za maendeleo mwaka 2018/19 zikitolewa Sh milioni 100 pekee, katika bajeti ya 2019/2020 fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo zimepungua kwa Sh bilioni 12.5 ikilinganishwa na mwaka 2018/19.

Akitoa mchanganuo wa bajeti ya wizara hiyo, Biteko alisema kati ya Sh bilioni 49.46 bilioni, bajeti ya maendeleo ni Sh bilioni 7.03 ambazo zote ni fedha za ndani na Sh bilioni 42.42 ni za matumizi ya kawaida ambapo Sh bilioni 16.47 bilioni ni za mishahara na Sh bilioni 25.95 bilioni ni matumizi mengineyo.

Kwa upande wa Wizara ya Viwanda na Biashara, imeidhinishiwa Sh bilioni 100.38 kiasi ambacho ni pungufu ya Sh bilioni 48.88 ikilinganishwa na bajeti iliyopita.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuhakikisha wadau wote wanatoa mchango unaohitajika katika ujenzi wa uchumi wa taifa.

Aliitaja miradi ya kimkakati kuelekea ujenzi wa viwanda mama kuwa ni pamoja na Mchuchuma na chuma cha Liganga.

Alisema miradi hiyo inatekelezwa na Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Limited ambayo ni ya ubia kati ya Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Schuan Hongda Group ya China.

Kipaumbele kingine alikitaja kuwa ni kufufua kiwanda cha matairi Arusha, maarufu General Tyre kilichokuwa GTEA na utafiti wa kina juu ya ufufuaji huo umeshakamilika.

Waziri ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, akiwasilisha bajeti yake aliliomba Bunge liidhinishe Sh trilioni 1.389 kwa ajili ya matumizi ya mwaka 2019/20.

Fedha hizo ni pungufu kidogo kwa asilimia 1.2 ikilinganishwa na makadirio ya Sh trilioni 1.406 ya mwaka wa fedha 2018/19 unaoisha mwezi huu.

Alisema kati ya fedha hizo Sh bilioni 826.71 au zilizobaki zitatumika kwa matumizi ya kawaida.

Hata hivyo, kiasi cha fedha kilichoelekezwa katika miradi ya maendeleo kimepungua kidogo ukilinganishwa na makadirio ya mwaka huu unaoishia Juni ambapo wizara ilitenga Sh bilioni 929.9.. 

Akizungumzia vipaumbele vya wizara yake, Profesa Ndalichako alisema pamoja na mambo mengine wanakusudia kuanzisha mfumo wa usajili shule kwa njia ya kielektroniki (Electronic accreditation system) ambao utasaidia kuboresha ufanisi wa usajili wa shule hizo. 

Wizara ya Maji, nayo imeidhinishiwa Sh bilioni 634.19, ambapo kati ya fedha hizo Sh bilioni 23.72 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 610.46 zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Mei mwaka huu, akiwasilisha bungeni mapendekezo ya wizara yake, Profesa Makame Mbarawa alisema katika fedha za miradi asilimia 57 zitatokana na vyanzo vya ndani na asilimia 43 zitatoke nje.

“Katika fedha za matumizi, Sh bilioni 17.45 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara na chuo cha maji na Sh bilioni 6.26 kwa ajili ya matumizi mengineyo,” alisema Profesa Mbarawa.

MWELEKEO WA BAJETI

Machi 12, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mpango, Dk. Philip Mpango aliwasilisha bungeni Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2019/20 ambapo alisema Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh trilioni 33.1.

Dk. Mpango alisema Serikali Kuu itakusanya Sh trilioni 22.2, kati ya hayo yanayotokana na kodi (TRA) ni Sh trilioni 19.1 na mapato yasiyo ya kodi ni Sh trilioni 3.1.

Alisema mapato yanayotokana na halmashauri katika mwaka huu yatakuwa ni Sh bilioni 765.4.

Waziri huyo alisema mikopo ya ndani na nje itakuwa Sh trilioni 7.27 trilioni ambapo kati ya hiyo Sh trilioni 4.96 ni mikopo ya ndani na ya nje yenye masharti ya kibiashara, inakadiriwa kuwa Sh trilioni 2.31.

Dk. Mpango alisema kati ya fedha hizo Sh trilioni 20.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, matumizi yatajumuisha gharama za uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2020.

DENI LA TAIFA

Dk. Philip Mpango, aliliomba Bunge liidhinishe bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/20  ambapo Sh trilioni 11.94, huku akisema kwa sasa deni la taifa ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Kutokana na mkakati uo, alisema Sh trilioni 9.73 kwa mwaka wa fedha 2019/20 kwa ajili ya fungu 22 (Deni la Taifa).

“Katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo: Matumizi ya kawaida Sh trilioni 9.73 (Kati ya hizo, mishahara Sh bilioni 8.88) na matumizi mengineyo Sh trilioni 9.72,” alisema.

Dk. Mpango akizungumzia usimamizi wa deni la Serikali, alisema hadi kufikia Aprili liliongezeka na kufikia Sh trilioni 51.03 kutoka Sh trilioni 49.86 Aprili 2018.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa jengo la tatu la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, miradi ya umeme, barabara na madaraja makubwa.

DK. SILAS NA BAJETI

Akichambua bajeti hiyo, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Joe Silas alisema katika wizara nyingi zilizowasilishwa bungeni, fedha nyingi zimeelekezwa kwenye miradi mikubwa ya kimkakati.

Dk. Silas ambaye pia ni Mhadhiri wa UDSM, alisema kwa malengo ambayo Serikali imeweka ya ukusanyaji wa mapato kama yatafikiwa na Serikali kukusanya mapato ya kutosha bajeti ijayo, miradi mingi ya maendeleo itatekelezwa.

“Nafikiri kama umezisikiliza bajeti nyingi za mawaziri unaweza ukaona kabisa fedha nyingi itaelekezwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Mfano SGR, REA pamoja na elimu hasa upande wa elimu bure, sasa basi sehemu nyingine ya bajeti ya maendeleo hutegemea michango ya wadau wa maendeleo au wahisani kuchangia.

“Mara nyingi wengi wao wamekuwa hawatekekelezi ahadi zao nah ii husababisha Serikali kushindwa kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo.

“Nafikiri kwa malengo ambayo Serikali imeweka ya ukusanyaji wa mapato kama yatafikiwa na Serikali kukusanya mapato ya kutosha bajeti ijayo, miradi mingi ya maendeleo itatekelezwa,”alisema Dk. Silas.